Apr 18, 2018

Sakata la Diamond, Nandy:Tusipojipanga dunia itatupanga

Wanamuziki Nandy na Bill Nass katika pozi
Diamond Platnumz
KAMA mtafiti, mchambuzi, mdau wa sanaa na mwananchi wa nchi hii nimekuwa nikiitahadharisha jamii yangu kuhusu vita vinavyoendelea duniani kati ya mataifa makubwa na mataifa machanga.

Lakini hivi si vita kama vile vinavyoendelea huko Syria, wala si vita vya kupinga ugaidi n.k. la hasha! Bali ni vita vya kiutamaduni, vya kutawalana kiakili.

Vita vya utamaduni huenezwa kupitia vyombo vya habari ikiwemo mitandao, televisheni, redio, magazeti, sinema, muziki n.k. ambavyo ni jukwaa muhimu sana katika kueneza utambulisho, utamaduni na fikra za nchi husika.

Mataifa kama ya India, China n.k. siyo wajinga kuruhusu tamthilia na filamu zao zitafsiriwe Kiswahili (tena kwa gharama zao) na kurushwa bure kwenye vyombo vyetu vya habari. Ni kwa sababu wanajua kuwa dunia sasa ipo kwenye vita ya utamaduni, vya kutawalana kiakili.

Katika kipindi cha wiki mbili wasanii wa muziki wametawala kwenye ‘headlines’ nzito za vyombo vyetu vya habari baada ya kuvuja kwa video zao mtandaoni zinazoelezewa kuwa zinadhalilisha utu wao na wa watu wengine.

Wiki iliyopita video ya utupu ya mwanamuziki nyota wa Bongo Fleva, Faustina Charles maarufu kama Nandy, ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii ikimuonesha akiwa na mwanamuziki wa kiume, Bill Nass, wakiwa kwenye nguo yake ya ndani sambamba na mwenza wake kitandani.

Inasemwa kuwa video hiyo ya utupu iliaza kusambaa mtandaoni siku moja baada ya Nandy kumtakia heri ya siku ya kuzaliwa Bill Nass na kuachia picha hizo ambazo hazikuwahi kuonekana hapo awali zikiwaonesha wakiwa karibu zaidi.

Kama hilo halitoshi, wiki hii mwanamziki mwingine maarufu wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul maarufu kama Diamond Platnumz ameingia matatani baada ya video zilizosambaa kwenye kurasa mbalimbali za mitandao ya kijamii zikimuonesha akiwa kitandani akicheza na mzazi mwenzake, Hamisa Mobetto, pia na mwanamke mwingine ambaye hajajulikana, zinazoelezwa kuwa hazina maadili.

Awali serikali ilitaja changamoto kubwa inayolikabili taifa kuwa ni athari ya utamaduni wa nje katika maadili, mila na desturi za Mtanzania kutokana na kuwepo na muingiliano mkubwa wa watu duniani.

Hili la wasanii kujitokeza hadharani (mitandaoni) wakiwa nusu watupu linaendeleza kile ambacho nimekuwa nasisitiza kuwa ‘wasanii ni kioo cha jamii’ japo baadhi ya watu wanadhani kuwa kwa sasa wamekuwa si kioo cha jamii tena.

Maneno ‘wasanii ni kioo cha jamii’ yanayotokana na tafsiri ya maneno ya Kiingereza ‘Artists are the mirror of the society’, usemi uliozoeleka sana katika vyombo vya habari na hata baina ya wasanii wenyewe, na ninaamini kuwa msanii asiyeitafsiri jamii yake hujikuta yuko peke yake akiwa hana wapenzi wala washabiki.

Naamini siku zote wasanii wataendelea kuwa ‘kioo cha jamii’ na haya yote yanayoendelea katika vyombo vya habari, kwenye miziki, filamu na hata kwenye video za muziki yanaonesha zao halisi la jamii yetu ilivyo kwa sasa.

Kitendo chochote cha kuukana ukweli na kuwatupia lawama wasanii peke yao huku tukiwabeza kwa maneno haya na yale ni sawa na kukataa kutumia kioo jambo ambalo si njia ya kubadili ubaya wa sura zetu.

Naamini kuwa tatizo tulilonalo hapa si wasanii kupiga picha chafu wala kazi zao, kwani wao ni sehemu tu ya jamii hii, tatizo lililopo ni mmomonyoko wa maadili katika jamii nzima, kwa kuwa tumeruhusu utamaduni wa nje uingie na kutawala maisha yetu, kwa kisingizio cha utandawazi.

Tumeshafika hatua ya wasanii wengine kuamini kuwa jamii haina tatizo na jambo hilo kiasi cha mtu kukaa mtupu katika jukwaa wakati akiangaliwa na maelfu ya watu, na kwa vile teknolojia imekua, wanapokaa katika hali ya utupu ni sawa na kukaa utupu kwenye macho ya ulimwengu mzima!

Hivi tunaandaa taifa lijalo (kizazi) la aina gani? Kwa mfumo huu kizazi chetu tunakiachia urithi wa aina gani wa utamaduni? Tuamke sasa, tusipojipanga basi dunia itatupanga, kwani huu ni mkakati maalumu wa kujenga jamii itakayobadilisha tamaduni zake na kujifunza tamaduni za nje, na hivyo kutawaliwa kiakili.

Tusipojipanga tutajikuta tunaishia kujenga jamii ya watu waliochanganyikiwa. Tunaweza tusilione sasa ila ni uhakika lina madhara makubwa sana kwa jamii zetu na mustakabali wa nchi yetu.

Inashangaza pale tunapowafungia wasanii wetu kwa kurusha video zisizo na maadili lakini tunaruhusu vichupi kwenye video za miziki zinazotoka nje kuoneshwa kwenye vituo vyetu vya televisheni. Utalindaje maadili kwa kuzuia picha za ndani wakati unarusha video za nje zenye vichupi?

Ukiangalia kwa makini, utagundua hata mfumo wa utangazaji katika baadhi ya vituo vya Redio na Televisheni umeigwa kutoka Magharibi, kitu kinachotoa taswira ya kuua suala la ubunifu na kubaki watupu tusio na kitu chochote.

Bahati mbaya sana katika dunia hii ya vita vya utamaduni, ukitaka kupata fedha nyingi kwa urahisi basi fanya jambo linalodhalilisha utamaduni wako au taifa lako na kutukuza utamaduni wa mataifa ya Magharibi.

Haya yanayoendelea sasa ya kina Nandy, Bill Nass. Diamond na wengineo ni ‘alamu’ kuwa tusipojipanga basi vita vya kiutamaduni havitatuacha salama.
Kutoa wito kwa wasanii kuwa mitandao siyo kokoro la kupeleka uchafu, bila kuweka mikakati thabiti ya kulinda kizazi hiki dhidi ya utandawazi haitatusaidia.

Ni kweli sasa tunayo Sheria ya makosa ya mtandao ya mwaka 2015 iliyotungwa ili kudhibiti matumizi mabaya ya mitandao, kama inavyoainishwa katika kifungu cha 14.-(1) (a) na (b) lakini tusipojipanga dunia itatupanga.

No comments: