Jan 26, 2011

Nini mustakabali wa usambazaji filamu Tanzania? (2)

Cover ya sinema ya Pastor Myamba

Wakati wa upigaji picha za sinema

*Kuhodhi mitandao kama Facebook, Myspace, Youtube, Vimeo ni njia za kujitangaza kwa haraka

WIKI iliyopita nilidokeza kuhusu umuhimu wa maudhui katika filamu, lakini ieleweke kuwa haitoshi tu kuwekeza nguvu kwenye maudhui yanayofaa kama hakuna Jukwaa la Uwasilishaji.
Jukwaa la Uwasilishaji:
Siku hizi, watazamaji wanahitaji pia majukwaa ya habari kama wanavyojali kuangalia maudhui. Falsafa hii ni muhimu wakati unaposhughulikia maudhui yanayowafaa watazamaji. 
 
Binafsi nilipoanza kuhudhuria Jukwaa la Sanaa pale Basata sikuwa naelewa hasa maana ya jukwaa la uwasilishaji, lakini baada ya kufanya utafiti nikagundua kuwa ni njia nzuri sana siyo tu kupashana habari bali hata katika biashara ya usambazaji wa kazi za sanaa.

Maudhui ya jukwaa la uwasilishaji katika dunia ya kisasa ya filamu hayaishii tu kwenye kazi ya usambazaji, yanakwenda ndani zaidi ya kile hasa soko la filamu lilivyo leo. Jukwaa litasaidia kuwasilisha mawazo kwa watu katika njia itakayojumuisha mitazamo yao. 
 
Ufanisi katika uwasilishaji unachangia utoaji haki ya kuchagua; kuyaleta maudhui kwa watazamaji katika dunia yao wenyewe. Kulingana na uwezo mkubwa wa soko la Tanzania kama litawezeshwa (ndani na nje ya bara la Afrika), jukwaa muafaka litamfanikisha kwa urahisi mtengenezaji wa filamu kuendana na ushindani wa soko.

Mustakabali wa biashara ya usambazaji wa filamu na masoko Tanzania unatokana na watazamaji vijana. Watoaji filamu wanatakiwa kuandaa kwa uangalifu takwimu (
demography) hii ya watazamaji na kukutana nao katika dunia yao. Dunia hiyo hustawi kwenye kundi la kweli la teknolojia ya digitali. 
 
Katika hatua hii itakuwa vizuri pia kuuchunguza mfumo wa usambazaji ili kupata ufumbuzi wa kutangaza na kusambaza (promotion and distribution solutions) ambao umesaidia kurekebisha tasnia katika nchi nyingine, ili uigwe katika sekta ya filamu Tanzania. Filamu ni nembo (Film is a brand), kama zilivyo nembo/ bidhaa nyingine, kuzitangaza na kuzisambaza ni vitu vyenye umuhimu sawa. 
 
Lazima tuweke mkakati wa kujitangaza kwenye mitandao ya intaneti. Hii itaongeza mipaka katika utekelezaji wa kampeni ya kuzitangaza kazi. 
 
Lakini tuna tatizo kubwa hapa kwetu kwamba Tanzania bado haina kiwango kikubwa cha watu wanaotumia intaneti ukilinganisha na nchi zingine katika Afrika, ni asilimia ndogo sana ya wananchi wanaotumia mtandao. Taasisi ya Mawasiliano ya Kimataifa (International Telecommunications Union “ITU”) katika ripoti yake inaonesha kuwa kati ya watu takriban milioni 42 waliopo nchini, kuna watumiaji wa intaneti 676,000 (asilimia 1.6). Watumiaji wa facebook 141,580 (asilimia 0.3). 
 
Idadi hii inaifanya Tanzania kuwa nchi ya tatu katika Afrika Mashariki nyuma ya Uganda yenye watu milioni 33 ambayo ina watumiaji wa intaneti 3,200,000 (asilimia 9.6), Watumiaji wa facebook 196,000 (asilimia 0.6). 
 
Kenya yenye watu milioni 40 ina watumiaji wa intaneti 3,995,500 (asilimia 10.0), watumiaji wa facebook 864,760 (asilimia 2.2). Rwanda yenye watu milioni 11 ina watumiaji wa intaneti 450,000 (asilimia 4.1), watumiaji wa facebook 52,520 (asilimia 0.5).
Burundi yenye watu takribani milioni 10 ina watumaji 65,000 (asilimia 0.7), facebook 6,740 (asilimia 0.1).  Takwimu za Agosti 31, 2010 kutoka www.internetworldstats.com/africa.
Ili tuweze kupiga hatua kwenye suala hili tunahitaji nguvu kubwa kuielimisha jamii faida za kutumia mitandao ya jamii inayoweza kusaidia utoaji habari za filamu na kujenga jamii yenye wafuasi, na humo, mijadala inaweza kujadilika, kipengele muhimu kabisa cha kuleta ufahamu au kampeni ya kujitangaza. Jumuiya hizi ni maeneo ambayo watu wanaotembelea wanaweza kupata habari zaidi, kushiriki katika mijadala, kujiunga na majarida, na kubadilishana ujuzi na mawazo na watu wengine, kwa lengo la kupanua wigo mkubwa wa watazamaji. 
 
Katika miaka michache iliyopita, mitandao imesaidia sana kufanya uwepo wa gharama nafuu katika kutangaza na kuuza kazi (promotion and marketing) kwa watengeneza filamu na hata kwa studio. Katika baadhi ya tasnia za filamu za nchi zilizoendelea, ni nadra na kosa kubwa kutokuwa na tovuti ya kutangaza filamu kabla haijaoneshwa kwenye majumba ya sinema. 
 
Kwa takwimu za ITU zinazoonesha Tanzania kuwa na idadi ndogo ya watumiaji wa intaneti, tunahitaji kuelekeza namna nzuri mitandao ya jamii inavyoweza kusaidia na kufanya kampeni yenye kuleta mwamko wa namna ya kujitangaza kwa ajili ya watoaji filamu. Njia ya haraka na madhubuti ya kujenga jamii ya watazamaji kupitia vyombo vya habari za mtandao ni kutengeneza tovuti za filamu wakfu (dedicated website) ili kutoa makala, vipande vifupi vya filamu (film clips) kwa ajili ya kuangalia bure, ku-downloads picha, miziki, sauti (soundtrack), picha za mabango (wallpapers), na kadhalika. 
 
Pia kuwapa mashabiki fursa ya kupata habari kuhusu maudhui/hadithi, wasifu wa waigizaji, na kuchangia maoni yao na hata kuonesha matamanio (interest) yao katika filamu kwa jumla kutasaidia kuenea kwa taarifa au tetesi za filamu. 
 
Mbali na kuwa na tovuti ya kujitolea, Kuweka filamu yako kwenye mitandao ya kijamii iliyopo ni njia nyingine nzuri ya kuongeza jamii ya watazamaji/wafuatiliaji wa filamu. 
 
Katika kuhodhi mitandao kwenye intaneti kama vile Facebook, Myspace, Youtube, Vimeo na kadhalika, maeneo ambapo wadau wanaweza kuwa na mahusiano au mawasiliano na watumiaji kitendo kinachoweza kufanywa kuwa chaguo bora. Siku hizi, facebook-Twitter-youtube ni njia za kujitangaza kwa haraka, watayarishaji lazima waangalie namna ya kuongeza tovuti zao na kuongeza matangazo na taarifa zao muhimu. 
 
Matangazo ya kulipia kwenye televisheni, radio, magazeti, majarida, na majarida ya kitaaluma (professional journals) ni muhimu pia.

Mtayalishaji wa filamu anaweza kuwa na ukurasa wake wa uchapishaji kwa habari za filamu, ambapo taarifa mbalimbali kuhusiana na filamu na maendeleo yake zitapatikana kwa wasomaji kwa kipindi cha muda fulani. Kutokana na uwezo wake wa kuonesha filamu kwa watazamaji wengi kwa haraka, kutoa habari za nyota wa filamu, vipande vya filamu (trailers), mahojiano na muongozaji wa filamu na kadhalika, vinaweza kuwekwa kwenye maonesho ya televisheni, au vipindi vya habari za burudani.

Matangazo ya filamu yaliyoandaliwa vizuri (Advance trailers) na picha zinazoonesha yaliyofanyika nyuma ya pazia (behind-the-scene footage) pia vinaweza kuwekwa kwenye vipindi maalum (documentary) kwa ajili ya vituo vya televisheni na kuvutia watazamaji kuitafuta sinema husika. 
 
Kuzionesha filamu kwenye matamasha ya filamu pia ni jambo zuri sana ambalo linaweza kusaidia kuongeza wigo wa taarifa. Matamasha ya filamu husaidia kueneza taarifa miongoni mwa wakosoaji wa filamu na watazamaji, na inaweza kuongeza umaarufu wa filamu na watazamaji kuwa wengi kama mapitio yake yalikuwa ya kuvutia. 
 
Wakati sisi tukiendelea kukaa katika ulimwengu wetu wa 'uvivu wa fikra' sehemu nyingine ya dunia inasonga mbele kwa kasi zaidi kuliko tunavyodhani. 
 
Pamoja na ongezeko kubwa la idadi ya mitandao na kunyonya filamu (film downloads) ambapo mauzo na usambazaji wa DVD na video yanaendana na mahitaji ya teknolojia yatabadilisha mkondo wa mapato, watengeneza filamu wataweza kupanua njia yao ya wigo wa usambazaji kwa idadi kubwa ya watazamaji (limitless pool of audiences), hasa vijana, ambao wameonekana kuwa na msisimko mkubwa na teknolojia hii. 
 
Mchanganyiko wa vyombo vyote vya habari hutoa fursa ya kipekee kwa watengeneza filamu, tofauti na mfumo uliozoeleka wa usambazaji. Kutokana na mipango madhubuti, mtengenezaji wa filamu anaweza kusambaza filamu yake mwenyewe na kupata faida nzuri. 
 
Katika jitihada za kibiashara, kutafuta masoko ni uwanja wa vita (marketing is a battle-field), na biashara ya filamu haiwezi kukwepa hili. Baadhi ya njia makini zinaweza kutafsiri upya mfumo na kuweka kiwango kipya. Kwa mfano, filamu inaweza kutolewa kwenye vyombo vyote vya habari kwa wakati huohuo, ikiruhusu watazamaji tofauti kuchagua lipi jukwaa linalowafaa.
Je, watazamaji wa Kitanzania wapo tayari? 
 
Kumbuka kuwa: Hivi sasa, mipango ipo njiani kwa nchi kuhama kutoka matangazo ya kizamani ya Analogia ya televisheni kwenda kwenye mfumo mpya wa digitali – kunakoongeza mahitaji makubwa ya vituo vya televisheni; hii inatoa nafasi kubwa ya kuingia.

Jambo la muhimu zaidi, mfumo huu mpya unaweza kuwa majibu ya Mungu dhidi ya uharamia wa hakimiliki (intellectual property) katika Sekta ya Filamu Tanzania.

Utekelezaji wa sheria ya kupambana na uharamia ni vuguvugu na ushiriki wa serikali katika vita hii hauendi zaidi. 
 
Kwa hiyo kama nilivyouliza, nini mustakabali wa mafanikio ya usambazaji katika sekta ya filamu Tanzania? Inapitia katika mawimbi ya njia iliyopo - njia iliyoitoa sekta hii mbali – njia ya ufumbuzi na ubunifu ili kuzalisha na kutafuta masoko ya filamu zetu kwa watazamaji na mtazamo wake.
Pia hii ni njia yenye kuleta faida kama tunaweza kuona maendeleo kupitia masoko ya nchi zingine. Uwezo wa kiuchumi ni suala lililo nje ya mtazamo wetu na matarajio ya watayalishaji ni kuendelea kujenga maudhui yatakayoambatana na uelewa huu.

No comments: