Oct 3, 2013

Muziki ni muhimu sana kwenye filamu zetu

  • Watayarishaji wa filamu nchini hawana bajeti ya muziki
  • Wengi huokoteza miziki isiyoendana na maudhui

Kwenye nchi zingine wanamuziki kama hawa (John Kitime), wenye ubunifu huwa wanatumika kunogesha filamu kutokana na midundo ya muziki

WIKI hii nilitembelea ofisi ya watayarishaji wa filamu nchini, John Lister na Paul Mtendah, kwa lengo la kuwajulia hali, niliwakuta wakikamilisha uhariri wa sinema inayotazamiwa kutoka hivi karibuni ya ‘Mke Mchafu’, iliyotokana na mwongozo (script) niliouandika. Nikiri tu kuwa pamoja na kuandika script hiyo, lakini nilijikuta nikiangalia sinema ambayo ni kama vile sikuwahi kuiona hadithi yake kutokana na jinsi sauti na miziki iliyotumika kwenye filamu hiyo jinsi ilivyoleta radha tofauti.

Ingawa nilikuwa na haraka, nilijikuta navutiwa sana kuiangalia sinema kutokana na miziki iliyotumika kwenye sinema hiyo kuendana sana na matukio ya sinema na kukoleza mshawasha wangu wa kutaka kuiangalia hadi mwisho. Niliwadadisi watayarishaji hao kama miziki hiyo ilikuwa imetungwa maalum kwa ajili ya filamu hiyo au imetokea kama ajali (accidentally) tu.

John Lister alinieleza kuwa ilitengenezwa maalum kwa ajili ya sinema hiyo kwani amegundua kuwa muziki, hasa unaoandaliwa maalum kwa kufuata kisa cha filamu huipa filamu yako uzito mkubwa na kuwavutia watazamaji wako waendelee kuifuatilia hadithi hata kama itakuwa na mapungufu fulani. Kwa kiasi kikubwa mno nakubaliana na John Lister.

Mimi ni mtazamaji mzuri sana wa sinema, huwa napenda zaidi sinema zenye hadithi za mikasa au sinema za matukio yanayoduwaza (suspense movies). Miaka kadhaa iliyopita nilikuwa nikijiuliza kwanini ninapoangalia sinema hasa za Kihindi zikiwa na maandishi yenye tafsiri (subtitle) za Kiingereza zenye kuniwezesha kufahamu kinachoongewa, nikiondoa sauti, hasa muziki, hujikuta hisia zangu zinatoweka kabisa kwenye sinema hizo? Na kwanini nikiacha sauti isikike hata kama hakuna ‘subtitle’ huwa nakuwa sehemu ya sinema hiyo japo kinachoongelewa sikijui?

Siku zilivyokuwa zikisonga ndipo nilipofahamu umuhimu wa muziki kwenye filamu. Ukitaka kujua umuhimu wa muziki kwenye filamu hebu jaribu kuiangalia filamu ukiwa umeminya/umetoa sauti. Unaweza kuacha ‘subtitle’ zisomeke kama nilivyokuwa nikifanya ili kujua kinachoendelea, bila shaka utajikuta hisia zote zinatoweka. Mfano mzuri ni kwenye sinema za kutisha. Ondoa muziki, hata mashaka (suspense) pia hutoweka!

Matumizi ya muziki ni muhimu sana katika filamu yoyote. Muziki unaweza kuwa laini wakuvutia na kusikika kwa sauti ya chini wakati wa tukio la kimapenzi (romantic scene) kuwafanya wanawake kutokwa machozi, unaweza kuwa wa sauti kubwa, wenye kuashiria tukio la kutisha, unaotumika kuhamasisha fikra za mtazamaji katika njia zote – muziki ni muhimu katika kuweka mazingira fulani (mood) ambayo yatakufanya uzame wakati ukiiangalia sinema, na kukufanya ujikute ukizama kwenye hisia zaidi kuliko kama isingekuwa na muziki. 

Muziki ni sehemu ya kichocheo. Muziki hukupa mtazamo wenye mbawa za kuruka hadi mbinguni. Amini usiamini, muziki huleta tofauti kubwa katika sinema. Muziki hufanya kazi kama mtengeneza hali ‘mood setter’.

Kwa sinema fulanifulani, muziki hutengeneza mtiririko wa filamu, kwa sinema zingine, muziki upo hapo ili kuwaweka watu katika tahadhari, kutegemeana na hadithi, kwa mfano; matukio ya haraka na ya ghadhabu, msuko wa hadithi unapokosa sifa yoyote ya ukweli, lakini tempo inakuwepo, ikisaidiwa na muziki. Kwa walioziona filamu kama Gladiator, Troy, Kingdom of Heaven na filamu za aina hiyo, watakubaliana nami jinsi hadithi inavyokuondoa, na muziki kukuhadaa. Kisha kuna filamu za kutisha, ambapo muziki huwekwa kusaidia kukujengea mashaka/woga (suspense), au mshtuko.

Hivyo, nadhani kuwa baadhi ya sinema zinahitaji sana muziki kuchochea adrenaline (homoni zinazosababisha woga kwa mtu) za watazamaji kuzalishwa.

Muziki hukufanya kuweka kipaumbele kwenye sinema unayoitazama badala ya kufikiria mambo mengine. Pia inakuwezesha kujua jambo zuri linaloelekea kutokea na jambo baya linalotokea. Kitu kingine muziki unachoweza kufanya ni kukufanya ufikiri kuna kitu kibaya kinaendelea wakati ukweli si hivyo. Hii hukusaidia kuiweka akili yako ililenge moja kwa moja kwenye sinema (kukuteka katika ulimwngu wa sinema). Muziki pia hukupumzisha wakati unaangalia sinema.

Hata katika maisha, muziki una jukumu muhimu sana na ushawishi mkubwa katika maisha yetu tofauti na jamii kwa ujumla. Kila mtu anahusiana kwa namna tofauti na muziki, lakini bado humuathiri kila mtu kwa namna anavyofikiri. Muziki hutumika kwa zaidi ya kusikiliza tu au madhumuni ya kuburudika, unaweza kukubadilisha katika maamuzi yako, unaweza kukupunguzia msongo au kukushawishi, hubadili namna mtu anavyoweza kutambua mambo, hutumika kukirihisha, kutesa na mengine mengi zaidi.

Kuna ushahidi ulio wazi kwamba muziki una jukumu muhimu katika maisha yetu, lakini jambo la kujiuliza; kwanini watayarishaji wengi wa sinema wa Tanzania hawana bajeti kwa ajili ya muziki, au hawadhani kuwa wanauhitaji? Nimekuwa nikishuhudia watayarishaji wetu wa filamu kuokoteza nyimbo zisizoendana na maudhui na kuzitumia kwenye sinema zao jambo linalopunguza utamu wa sinema. Ndiyo maana ni jambo la kawaida kuwakuta watu wakizilalamikia sinema zetu kuwa ‘zinaboa’ mno kuzitazama.

Watayarishaji hawa wa filamu wanasahau kuwa hata kama tukio la sinema limejengwa vizuri sana na ukawatumia waigizaji wazuri bado kama hakuna muziki sinema yako itapungukiwa kitu muhimu, muziki huongeza radha ya tukio. Lakini pia isidhaniwe kuwa nasema muziki ni muhimu katika kila tukio kwenye filamu. La hasha.

Ni wazi, kuna mifano mingi ya jinsi ukosekanaji wa muziki unavyoweza kufanya matukio kuwa makubwa zaidi na kuduwaza. Hata hivyo, ukosefu wa muziki katika filamu nzima unaweza kusababisha kuwepo haja ya kutafuta kitu cha ziada; kitu cha kuusaidia ujumbe na kuibeba script zaidi kuliko uigizaji wenyewe.

Muziki unapochukuliwa kama kitu kisicho muhimu au jambo dogo, pia hupunguza soko lako na humsababishia mtengenezaji wa filamu kukosa fursa kubwa ambayo ingeweza kuifanya filamu yake kutambulika zaidi. Uzoefu unaonesha kuwa muziki ni moja ya zana muhimu sana kimasoko mtu anaweza kuitumia katika sekta yoyote. Mtayarishaji wa filamu anapaswa kuweka bajeti kwa ajili ya muziki kila atengenezapo sinema, ambapo asilimia 10 ya bajeti nzima inapaswa kuwa ya muziki na sauti zingine maalum.

Kumbuka, unaweza kuwa na hadithi nzuri mno na waigizaji wazuri sana, waongozaji, watayarishaji, wahariri, vikorombwezo muhimu (special effects), nk, lakini kama nakshi ya muziki imekosekana kwenye filamu, basi itaishusha filamu yako hadi ‘levo’ ya chini, ambayo inaweza kupunguza mafanikio ya filamu sokoni.

Hapa kuna tofauti kubwa kati ya mtu anayechukua/anayeokoteza vipande vya muziki kutoka maktaba na yule anayemlipa mtunzi ili atunge nyimbo maalum kwa ajili ya sinema fulani, utunzi wa nyimbo huzidisha msukumo kwenye filamu yako, lakini muziki wa maktaba ni kwa kipande cha jina tu (title), lakini huwa tofauti kabisa na mwelekeo wa hadithi yako. Muziki unapotungwa maalum kwa filamu yako, hutengeneza uhusika mwingine zaidi; pamoja na husika zilizotangulia huunda kitu kimoja kilicho kamili. lakini muziki wa kuokoteza siku zote hauna uhusiano wowote na hadithi iliyotumika kwenye filamu.

Ni jukumu la waongozaji wa filamu kuhakikisha wanateka hisia za watazamaji wao. Wana wajibu wa kuhakikisha kunakuwa na watunzi wa muziki wenye ubunifu kwa ajili ya kubuni muziki utakaoongeza radha tofauti katika filamu. Muziki unaweza kutoa tafsiri ya wahusika, kuihamisha hadithi yako kutoka point A kwenda point B, kujenga mazingira ya mvutano (tension), kukoreza uhondo katika mchezo, na kuungisha pamoja dhamira (themes) ambazo humuacha mtazamaji katika hisia kamili zaidi.

Alamsiki.

No comments: