Aug 21, 2014

Filamu zetu zinaharibiwa na waongozaji


·         Wengi hawana sifa zinazohitajika na hawataki kujifunza




UKWELI tuna tatizo kubwa kwenye tasnia ya filamu Tanzania kwa waongozaji wengi kudhani kuwa kazi ya uongozaji wa filamu ni kujua: “standby... action... cut!” na kusahau kuwa muongozaji ndiye anayepaswa kumtengeneza muigizaji aweze kuuvaa uhusika ipasavyo kwa kutegemea script ilivyo. Kama muigizaji atashindwa kuvaa uhalisia, mara nyingi hilo siyo kosa lake bali ni kosa la muongozaji kwa kushindwa kumtengeneza, na hutafsiri uwezo wa muongozaji ulipokomea.

Mtazamo wangu, mtu yeyote anayetaka kuwa muongozaji mzuri wa filamu katika tasnia yetu anapaswa kujifunza kwa makini hatua kwa hatua kwa kusoma machapisho na kuhudhuria warsha na mafunzo ya muda mfupi — si kwa ajili ya kujifunza njia nzuri ya utengenezaji wa filamu, bali kwa ajili ya kupata msukumo wa kufuatilia masuala muhimu ya uumbaji wa kisanii kwa bidii na kwa umakini.

Miezi michache ijayo nitazindua vitabu viwili nilivyoandika, kimojawapo kikiwa ni “Uongozaji wa Filamu – Sifa, Misingi na Kanuni za Uongozaji.” Nimeandika kitabu hiki nikijaribu kutoa mchango wangu kwa kile ninachokijua ili kuwasaidia waongozaji wa filamu katika nchi hii, nikiamini kuwa tatizo kubwa kwenye filamu zetu ni kukosa uongozaji makini.

Methodolojia ya kitabu changu ipo katika msingi mkuu wa pendekezo ambalo kitabu hiki ni kama mwongozo wa filamu unaoelezea kile ambacho muongozaji anatakiwa kukifanya. Nikilenga zaidi kwenye maeneo ya lugha ya filamu, mbinu za kuwaongoza waigizaji, misingi ya uongozaji, na maswali ambayo muongozaji anapaswa kujiuliza.

Kuna dhana sababishi nyingi ambazo ni za lazima sana kwa muongozaji mzuri wa filamu: ubunifu, msimamo, elimu/ufahamu kuhusu sanaa, ufahamu kuhusu watu, uwezo wa kufanya kazi na wengine, utayari katika kuyakubali majukumu, ujasiri, ustahimilivu, na nyingine nyingi. Lakini dhana sababishi iliyo kuu kabisa, ambayo ikikosekana itatangua mengine yote, ni ubayana (clarity) — ubayana kuhusu hadithi na jinsi kila kipengele ndani yake kinavyoweza kuchangia kwenye hadithi nzima, na pia ubayana kuhusu kile kinachowasilishwa kwa watazamaji.

Kwa waliosoma lugha ya filamu watakubaliana name kuwa filamu ni taaluma inayozungumza kwa kutumia picha na vitendo zaidi, hivyo, haihitaji mtazamaji kufahamu lugha iliyotumiwa ili afahamu maudhui na ujumbe unaowasilishwa na kazi husika ya filamu, ndiyo maana kuna watu wanaangalia filamu za Kihindi au Kikorea na wanaburudika na kuelewa kinachoendelea.

Msingi mkuu wa hadithi katika sinema ni kuwa, filamu ni zaidi ya kiwanda (sekta), ni zaidi ya onesho linalowakutanisha nyota. Filamu ni lugha. Utengenezaji wa filamu una lugha yake. Kwa hiyo, filamu ni lugha inayotumika kusimulia hadithi, na sauti inayotumika kusimulia hadithi hiyo ni kamera, wakati muongozaji wa filamu ndiye msimuliaji wa hadithi hiyo.

Muongozaji wa filamu ni mtu ambaye huwa anaongoza utengenezaji wa filamu. Kwa ujumla, muongozaji wa filamu hudhibiti masuala ya kisanii na kimchezo katika filamu, na kutengeneza taswira kutoka kwenye script wakati wa kuwaelekeza watendaji wa kiufundi na waigizaji katika kutimiza dira ya filamu. Muongozaji huwa ana jukumu muhimu katika kuchagua waigizaji, wabunifu wa uzalishaji, na masuala ya ubunifu katika utengenezaji wa filamu. Katika baadhi ya nchi za Ulaya, muongozaji hutazamwa kama ndiye mtunzi (author) wa filamu au mmoja wa watunzi.

Muongozaji wa filamu hutoa mwelekeo/maelekezo kwa waigizaji na watendaji katika kutengeneza dira (vision) kwa njia ambayo filamu hatimaye itaonekana. Waongozaji huhitaji kuwa na uwezo wa kupatanisha panapokuwa na tofauti katika ubunifu na kusimamia katika mipaka ya bajeti ya filamu. Kuna njia nyingi ya kuwa muongozaji wa filamu. Baadhi ya wongozaji wa filamu walianza kama waandishi wa filamu (screenwriters), wahariri wa filamu au waigizaji. Waongozaji wengine wa filamu wamesoma katika shule za filamu.

Waongozaji hutumia mbinu mbalimbali. Baadhi huelezea kwa muhtasari (outline) kisa chote na kuwaachia waigizaji kufanya faraguzi kwenye mazungumzo yao, wakati wengine hudhibiti kila nyanja, na kuhitaji waigizaji na wafanyakazi wengine kuyafuata maelekezo kwa usahihi. Baadhi ya waongozaji pia huandika miongozo (screenplays) yao wenyewe au kushiriki katika kuandika na washirika wao wa muda mrefu katika uandishi. Baadhi ya waongozaji hupenda kuhariri au kuonekana katika filamu zao, au kutunga muziki kwa ajili ya filamu zao.

Muongozaji wa filamu ana kazi nyingi zisizokuwa na mwisho, lakini kazi iliyo muhimu zaidi ni ile ya kuwaongoza waigizaji na kuhakikisha kuwa anapata zao bora kabisa litakaloonekana kwenye televisheni. Kumekuwa hakuna ushauri wa kutosha unaotolewa kuhusu jinsi ya kuwaongoza waigizaji wanapokuwa kwenye eneo la upigaji picha. Binafsi nimewahi kusoma vitabu na machapisho kadhaa kuhusu uongozaji, na kitabu kimojawapo kikiwa ni ‘Directing Actors’ (Kuwaongoza Waigizaji), kilichoandikwa na Judith Weston.

Pengine hiki ni kitabu kilichowahi kunivutia zaidi ambacho kinaelekeza nguvu katika kipengele hiki maalum cha namna ya kuwaongoza waigizaji. Hata watu wengi waliokisoma niliowahi kukutana nao wanakisifia kitabu hiki, lakini kwa mtazamo wangu nadhani kuwa kinayafanya mambo haya kuwa ngumu kwa kuwa hakijikiti zaidi katika jinsi ya kuongoza – pale unapozungukwa na shinikizo au matatizo mengine mengi – nimegundua kwamba ushauri ambao machapisho na watu wengi wamekuwa wakiutoa kwenye kuwaongoza waigizaji ni ule ambao mara nyingi usiotekelezeka.

Muongozaji wa filamu ni kiongozi wa timu katika uzalishaji wa filamu na msimulizi wa hadithi kwa kutoa picha halisi. Muongozaji mzuri ni yule anayehakikisha kwamba sehemu zote za filamu zimeandaliwa katika hali ya ubunifu na kuletwa pamoja: ndiye mbunifu na kiungo muhimu kati yake na timu ya uzalishaji, anayeutafsiri mwongozo wa filamu kutoka kwenye karatasi na kuuhamishia katika taswira halisi yenye sauti kwenye video, na ndiye anayeiona taswira halisi na kutafsiri mtindo na muundo wa taswira hiyo. Pia ana wajibu katika masuala ya masoko na kuelewa changamoto za filamu katika muda na bajeti.

Nafasi ya muongozaji katika mchakato wa filamu kijadi inatofautiana sana na ni ngumu sana. Muongozaji wa filamu huonekana kama kiongozi wa timu ya wafanyakazi wengine, na hutoa aina fulani ya nguvu ya kuongoza. Kwa mujibu wa mtazamo huu, matokeo ya mwisho hayaamuliwi na mahitaji ya mwongozo wa filamu, upigaji picha, uigizaji, au uhariri; muongozaji wa filamu ndiye huandaa mazingira ya picha kwa ajili ya matokeo ya mwisho.

Ikiwa waongozaji wanataka kuijua misingi na kanuni za kuwa muongozaji wa filamu lakini hawana elimu rasmi ya uongozaji, wanapaswa kuwa watu mwenye nia ya dhati ya kupenda kujifunza na kufuatilia sinema na wenye kipaji kikubwa cha sanaa kama sharti kuu.

Inavyoonekana, kila sinema inayozalishwa ina muongozaji wa filamu nyuma yake. Huyu ni mtu anayesimamia masuala ya ubunifu na ya kiufundi ya uzalishaji wa sinema, kama vile usaili, usanifu, na taa. Mtu yeyote mwenye shauku katika masuala ya sinema na mwenye kujitoa kwa dhati anaweza kuongoza filamu, lakini tu atafanya vizuri zaidi kama ana jicho la kisanii katika kuyaona matukio yenye kusisimua katika mchezo. Ili kufanikiwa katika sekta hii yenye ushindani, unapaswa kuthibitisha kwamba una utaalam unaotakiwa ili kutengeneza sinema itakayofanya vizuri sokoni.

Alamsiki.

No comments: