Jan 8, 2014

Sawa tunaibiwa, je tunaibiwaje?

* Hivi tunamjua mwizi wetu?


Wasanii wa filamu wakionesha kazi bandia za filamu zinazouzwa mtaani


MWAKA uliopita 2013 kwa tasnia ya filamu nchini tuliuaga kwa pilikapilika mbalimbali, mojawapo ikiwa ni mkutano mkubwa wa wadau wa filamu na muziki uliofanyika 30 Disemba 2013 kwa kuandaliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kushirikiana na Cosota, Bodi ya Filamu, Basata, Shirikisho la Filamu (TAFF) na Shirikisho la Muziki (TMF). Pia kulikuwepo maandalizi ya chinichini ya wasanii/watayarishaji kuandaa maandamano makubwa ya kuishinikiza Serikali ichukuwe hatua dhidi ya maharamia wa kazi za sanaa.

Isingekuwa busara za uongozi wa Shirikisho la Filamu Tanzania inawezekana hivi sasa kungekuwa na tafrani, kwani wasanii/watayarishaji hawa walikuwa kwenye shinikizo kubwa kutoka kwa msambazaji wa filamu kuwa endapo hawatafanya hivyo, yeye atajitoa kusambaza filamu, jambo lililowatia hofu wasanii hawa na aliwapa masharti kuwa ili aendelee kusambaza kazi zao ni lazima wafanye maandamano yenye kulaani na kuishinikiza serikali kabla ya tarehe 1 Januari 2014.

Iliundwa kamati ya kuratibu zoezi zima, kuchapisha fulana na kuandaa mabango yenye jumbe mbalimbali za kulaani, lakini walijikuta wakikwama kwa kuwa taasisi pekee inayotambulika ni Shirikisho la Filamu Tanzania, hivyo, hawakuwa na uchaguzi ila kuufuata uongozi wa shirikisho kwa ajili ya kuomba sapoti.

Niweke wazi tu kuwa kwa kiasi fulani nakubaliana nao kuhusu kukithiri kwa wizi unaodumaza ubunifu na pato la wasanii, lakini napingana nao kwenye aina ya malalamiko wanayotaka kuyawasilisha, na niweke wazi tu kuwa binafsi sipendi kutumiwa kama ngazi na wafanyabiashara ambao hukutumia kwa kipindi fulani, kisha wanakutupa wakishafanikiwa.

Hapa tujiulize, hivi wale wote wanaotaka kuandamana ni kweli wanamjua mwizi wao? Kama wanamjua ni nani? Je, wanazo takwimu/ushahidi wowote unaoonesha wanaibiwaje, wanapoteza kiasi gani kutokana na wizi huo, na serikali inakosa pato kiasi gani kwenye wizi huo? Nijuavyo, unapotaka serikali ichukuwe hatua ni lazima uoneshe kwenye malalamiko yako mambo hayo, hasa ukikazia kwenye suala la kiasi gani serikali inapoteza pato, vinginevyo watakusikiliza kisha malalamiko yako yatafungiwa kwenye makabati, na mchezo utaishia hapo.

Hivi kati ya wasanii/watayarishaji wanaotaka kuandamana, ni nani anayemiliki kazi (filamu)? Hakuna! Wote walishauza kazi zao kwa msambazaji. Sasa wanapotaka kuandamana eti tunaibiwa, mwizi wetu ni nani? Yule tuliyemuuzia kazi au nani? Maana hatuna kazi sisi! Anayepaswa kulalamika kuibiwa ni yule mmiliki wa kazi.

Sasa hapa jambo la kushangaza na kujiuliza, kwanini mmiliki wa kazi hataki kujitokeza kulalamika au kuandamana na badala yake anajificha kwenye mgongo wa wasanii kwa kututaka sisi tuandamane na kulalamika kwa niaba yake? Kuna nini hapa kinaendelea? Nawashauri wasanii kabla hatujataka kuandamana ni bora tukarejea kwenye mikataba yetu na msambazaji ili tujiridhishe kama ni sisi ndiyo tunaoibiwa, na tunaibiwaje ili tusije tukaingizwa mkenge.

Vinginevyo tungeandamana na kulalamika kuhusu mikataba hii ya kinyonyaji inayotufanya kudhulumiwa haki zetu, lakini si kwa sababu ya wizi wa kazi zisizokuwa zetu ambao wala hatuna takwimu zozote kuhusu kiasi cha kazi kinachouzwa, pato la shilingi ngapi linaingia, au kiasi gani kinapotea kutokana na wizi huo.

Ninatambua wazi kuwa katika biashara yoyote ile siku zote, katika makubaliano ya kazi, ni muhimu sana pande zote kuwa na haki na wajibu wa kila upande katika mkataba wa makubaliano wanaoingia baina ya pande mbili. Katika jambo hili, umakini wa hali ya juu huwa unahitajika sana ili kuepusha upande mmoja kuumizwa.

Inafahamika wazi kwamba katika suala la mikataba ni vyema kushirikisha wanasheria ambao ndiyo wataalam wa mikataba ili kuepuka kudhulumiwa, lakini pia kutokana na viwango vya elimu vya wasanii wengi katika nchi hii, ni muhimu kuwa na wasimamizi (mameneja) wanaoelewa masuala ya mikataba.

Ni vyema wasanii wakatambua kuwa kilio wanacholia cha kuibiwa si kweli, wengi wanaingia kwenye mkumbo wa wachache wanaotumiwa na wasambazaji (ambao walishawauzia haki zote) ili ionekane kuwa biashara ya filamu si nzuri na kuleta punguzo la kodi kwa wasambazaji hawa. Na hata kama kuna wizi unaaofanyika, wasanii hawaibiwi bali mikataba wanayoingia ndiyo inayowaponza.

Ili kutatua changamoto hii kwanza wakubali mapungufu yao na pindi wanapoona mikataba kwa lugha ya Kiingereza ambayo inawapa tabu walio wengi, basi ni vyema wakaikataa mikataba hiyo au kuipeleka kwa watu wenye utaalam na lugha hiyo, hasa wanasheria, wasipende kuendekeza njaa.

Aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa, Ghonche Materego, aliwahi kusema kwamba ni vyema vyama vya sanaa na mashirikisho kuwa na wanasheria ambao watasimamia shughuli za wasanii wao, ikiwemo kuwaongoza katika kuingia mikataba. Ghonche aliamini kuwa kwa kufanya hivi, wasanii wataweza kujiamini katika utendaji wa kazi zao, kwani hawatakuwa na wasiwasi wa kunyanyasika pindi washirika wao katika mikataba watakapoonekana wanakengeusha mambo.

Nakubaliana kabisa na Mzee Ghonche lakini sijui kama anafahamu kuwa wasanii wetu wamekuwa hawashauriki, wenye kupenda njia za mkato ili kufanikisha mambo na wanaendekeza njaa, hasa pale wanapotajiwa pesa ambazo wanaamini zitawasukuma kwa wiki kadhaa. Taarifa nilizonazo ni kwamba Cosota na Bodi ya Filamu wana wanasheria waliojitolea na wako tayari kupitia mikataba ya wasanii lakini hakuwa hata msanii mmoja aliyewahi kujitokeza japo hata kuomba ushauri wa kisheria.

Wasanii wengi wamejikuta wakidhulumiwa au kupata malipo madogo kutokana kuendekeza njaa na kuwa na uelewa mdogo katika kuingia mikataba na baadhi ya watayarishaji/wasambazaji wa filamu hapa nchini. Suala la mikataba limekuwa likipuuzwa sana na Watanzania wengi (si wasanii tu), hasa linapokuja suala la kusoma vipengele na kuelewa vinamaanisha nini. Wengi hukimbilia kuangalia sehemu inayotaja pesa tu na wakiona pesa nyingi basi husaini bila hata kujali maeneo mengine muhimu.

Hali hii imemkumba jamaa yangu siku za hivi karibuni ambaye aliamua kuja kuniona ili kupata usaidizi baada ya kulizwa na kampuni moja kubwa ya usambazaji wa filamu. Amejikuta akiingia mkataba mbovu ambao sijawahi kuushuhudia katika maisha yangu. Mkataba wake alionionesha ambao ni wakusambaza kazi yake moja, kwa kuuangalia tu niligundua kuwa ulikuwa umetengenezwa na mwanasheria wa msambazaji huyo kwa jinsi ulivyokuwa umepangiliwa kitaalam lakini katika namna ya ujanja ujanja, tena kwa lugha ya Kiingereza. Kibaya zaidi alipopewa alitakiwa kuusaini palepale na wala hakuruhusiwa kutoka hata nao nje kabla hajausaini, ingawa alipewa nakala ya mkataba huo baada ya kusaini. Hili limekuwa ni tatizo ambalo wasanii wote wanatakiwa kulitatua wenyewe, na wala si suala la kuilalamikia serikali.

Mikataba ya aina hii imesababisha vilio, malalamiko na kesi za ajabu ambazo kimsingi zingeweza kuepukika endapo kungekuwa na umakini kabla ya kuingia mkataba husika.

Bahati mbaya wasanii wetu wamekuwa hawajifunzi kabisa kutokana na makosa ya wengine, kwani inapotokea mwenzao kaingia mkataba wa aina hii utashangaa hata watu wake wa karibu nao hurudia makosa kama hayo, kiasi kwamba suala hili limekuwa kama ni desturi kwa wasanii wetu.

Inakuwa vigumu kuelewa kama wanafanya shughuli zao kwa mazoea na si kitaalam, kwa maana ya kuifanya kazi yao kama ajira yao rasmi ambayo inawaingizia kipato kwa kujikimu na kuendesha maisha yao ya kila siku. Kukubali mikataba isiyo na maslahi kwao imekuwa ni sawa na kujimaliza wenyewe.

Kuhusu maisha duni na kudhulumiwa kwa haki zao, kunasababishwa na ubinafsi, kutokuwa na umoja katika kushinikiza haki zao, kutumia vibaya kile wanachokipata kwa anasa na kutotaka kujifunza juu ya haki zao mbalimbali kutokana na kulewa umaarufu na kukimbilia mafanikio ya haraka haraka.

Wasanii wachache wenye maendeleo ni wale wenye kupenda kuingia mikataba ambayo ama wameipitia kwa umakini au wamepata ushauri wa kisheria kutoka kwa wataalam wa sheria, na huingia mkataba hiyo kwa kila kazi wanazofanya na huwa na nakala za mikataba hiyo. Na ni vizuri zaidi mkataba huu ukawa umepitia mikononi mwa watu wanaoweza kuutafsiri.

Jambo jingine la ajabu ni pale wasanii wengi wanapodai kuwa na mikataba lakini wao wenyewe huwa hawana nakala za mikataba hiyo, na hasa mikataba inayohusu usambazaji wa kazi zao, kuna aina ya ujanja ujanja ambao hufanyika ambapo wasanii wengi huambiwa waache mkataba kwa wasambazaji ili ukasainiwe na mwanasheria na baada ya hapo wengi huwa hawauoni tena mkataba wao.


Tafakari…

No comments: