Jan 1, 2014

Tutafute fursa za masoko ya filamu zetu nje ya nchi


Wasanii wakifuatilia jambo kwenye moja ya vikao


MAJUZI nilijikuta nipo kwenye kikao kimoja cha wadau waliojiita wenye uchungu na tasnia ya filamu nchini, nilikuwepo hapo si kama mchangiaji bali kama msikilizaji wakati baadhi ya wadau hao walipokuwa wakijadili kuhusu mfumo unaofaa kwa ajili ya kusambaza na kuuza filamu zetu. Katika kikao hicho ambacho naamini hakikuwa rasmi bali kilichokuja baada ya mjadala mrefu ulioibuliwa kuhusu makato ya kodi ya asilimia tano wanayodai kukatwa na msambazaji wa filamu kwa kisingizio kwamba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeagiza kukwatwa kwa kodi hiyo.

Kikao hiki kimekuja siku mojua tu baada ya mkutano mkubwa wa wadau wa filamu na muziki uliofanywa na TRA ukizihusisha pia taasisi zingine kama Bodi ya Filamu, Baraza la Sanaa la Taifa, Chama cha Hakimiliki na Hakishiriki Tanzania, Shirikisho la Muziki Tanzania na Shirikisho la Filamu Tanzania. Mamlaka ya Mapato nchini walitola ufafanuzi kuwa asilimia tano haikupaswa kukatwa kwenye bidhaa kama ambavyo watayarishaji hawa wa filamu wamekuwa wakikatwa, bali kusudio lake ni kukatwa kwa ajili ya huduma.

Baada ya kupewa ufafanuzi huo ndipo lilipoibuka kundi la wadau linalotaka kumfikisha kwenye vyombo vya sheria msambazaji huyo mwenye tabia ya kuwakata asilimia tano ili arudishe pesa zote alizokuwa akiwakata, na pia wadau hao walikuwa wakijadili kuhusu mfumo mzuri unaoweza kuwasaidia katika kusambaza kazi zao, hasa baada ya kuonekana wakitishiwa kunyimwa mikataba ya kusambaziwa filamu kwa kisingizio kuwa msambazaji huyo anapata hasara kutokana na uharamia wa kazi za sanaa kukithiri.

Ndipo wadau hao walipojaribu kuja na wazo la kufikiria kusambaza kazi zao wenyewe kwani kuendelea kuwategemea wafanyabiashara wenye asili ya Kiasia ambao kiukweli wamekuwa wakiwanyonya imeonekana ni sawa na kutegemea jua lichomozee magharibi.

Japo sikuwa nimealikwa kwenye kikao hicho, lakini niliomba kutoa maoni yangu yaliyojikita kwenye kujaribu kuzitazama fursa za masoko ya filamu zetu si ndani ya nchi tu bali hata nje ya nchi. Kwani watayarishaji wengi wa filamu nchini wamekuwa wakiliangalia soko moja tu, linalomilikiwa na wafanyabiashara hao wenye asili ya Kiasia, na kushindwa kuziangalia fursa zingine.

Siku za hivi karibuni uzalishaji kwa kutumia kazi za sanaa nchini, hususani filamu umekuwa ukichukuliwa kama kimbilio kwa wasiojiweza au walioshindwa katika fani zingine kama njia ya kujikwamua kiuchumi na kuendeleza utamaduni. Jambo hili limekuwa likisababisha kuwa na watendaji wasio na taaluma na hatimaye kuzalishwa kwa kazi mbovu zisizokidhi viwango.

Niliwakumbusha wadau hao wa filamu kuwa hata pale tunapojadili kuhusu mfumo wa usambazaji wa filamu zetu tujaribu pia kujikita katika kuangalia ni fursa zipi za masoko ya filamu nje ya nchi. Lakini nikatoa angalizo kuwa kazi mbovu haziwezi kuuzika hata kama tutaandaa mfumo mzuri kiasi gani.

Kuboresha mfumo wa usambazaji tunahitaji pia kuboresha kazi zetu sambamba na kubadili mtazamo/ dhana iliyojengeka miongoni mwetu kuwa sanaa ya filamu ni kimbilio la wasiojiweza kiuchumi. Tunapaswa kutambua kuwa sanaa hii ni kazi kama kazi zingine ambayo inahitaji ubunifu, akili, maarifa na ni muhimu katika kuinua pato la mtu husika na taifa kwa ujumla kwani inatoa fursa mbalimbali kama vile: Ajira na kuendeleza biashara ndani na nje ya nchi na kukuza pato la taifa kwa ujumla.

Hali ya uzalishaji wa filamu nchini umekuwa ukiongezeka siku hadi siku na kuwavutia wengi ingawa bado kuna changamoto mbalimbali zinazoikabili tasnia hii. Pamoja na umuhimu mkubwa uliopo wa kazi za filamu, bado soko la bidhaa za filamu za Kitanzania limeendelea kuwa duni/ dogo kwa walio wengi katika soko la ndani kiasi cha kutokuwa na tija ya kuongeza kipato cha wasanii na watayarishaji wa filamu, na hata maendeleo ya jamii kwa ujumla.

Hata hivyo, kuna changamoto mbalimbali zinazosababisha soko la ndani kwa bidhaa za sanaa, hususani filamu kuwa duni na kusababisha wanaojihusisha na kazi hizo kuendelea kuwa na kipato duni kinachodidimiza maendeleo binafsi na jamii kwa ujumla. Miongoni mwa changamoto hizo ni kama zifuatazo: kukosa fursa za kupata mikopo kwenye asasi za kifedha, kukosa sera zinazosimama katika misingi ya utendaji, kukosa elimu, ubinafsi na kutokuwa na malengo.

Ukosefu wa fursa za kupata mikopo kwenye asasi za kifedha pia ni tatizo kubwa mno, kwa kweli serikali inapaswa kuyasaidia mashirikisho ya sanaa ili kuinua ubora wa kazi za sanaa na kufikia malengo katika suala la masoko na usambazaji maana ndipo lilipo tatizo. Wazalishaji wa filamu na wasambazaji wa ndani wapewe nafasi ya kuomba ufadhili kutoka kwenye taasisi ya serikali kama misaada au mikopo kwa ajili ya soko na kutangaza bidhaa.

Serikali inapaswa kusaidia juhudi za wasanii katika masoko na usambazaji kwa ajili ya filamu ambazo ni kwa maslahi kwa watazamaji wa Tanzania. Iwekwe maanani kuwa watakaotuma maombi wawezeshwe ili kuzitangaza kazi za Tanzania kwenye matamasha ya filamu ya kimataifa na masoko ya filamu na watazamaji wa ndani walio katika maeneo ambayo uwezo wa vyombo vya habari kupenya ni mdogo.

Wakisaidiwa naamini wataboresha kazi zao kwani filamu nyingi zimekuwa hazina ubora unaohitajika na watumiaji wa bidhaa hizo. Wazalishaji wengi wamekuwa hawaangalii watumiaji wanahitahi nini, bali wamekuwa wakizalisha filamu na kupeleka sokoni bila kujali ubora wa bidhaa yenyewe. Hii inasababisha filamu kukosa soko la kimataifa kwa sababu wazalishaji hawafanyi tafiti za masoko na kujua ni bidhaa ya ubora gani ipelekwe sokoni kwa wateja waliokusudiwa (targeted market).

Wazalishaji wengi wameshindwa kuongeza ubunifu zaidi na badala yake wameendelea kuzalisha vitu kwa kuiga. Ubunifu unasaidia kumtofautisha mzalishaji mmoja na mwingine, hivyo inamfanya mzalishaji kuwa wa pekee katika soko na kuwafanya watumiaji wa bidhaa kuwa tayari kupokea bidhaa za kipekee kutoka kwa mzalishaji hivyo kumsaidia kuwa mshindani katika soko.

Siku zote nimekuwa nikiamini kuwa mafanikio ya filamu yoyote nzuri hutegemea ubunifu katika masoko na promosheni. Sote tunapaswa kuangalia ni namna gani tunaweza kupata msaada watengenezaji filamu na wasambazaji waweze kutangaza bidhaa zao kwa ufanisi kwenye masoko ya filamu na hata matamasha.

Kuwe na taasisi za fedha zinazotoa mikopo yenye masharti nafuu hasa riba nafuu, na kusiwe na mlolongo mrefu katika suala zima la kutoa mkopo ili kumrahisishia mzalishaji kufanya kazi kwa haraka kutokana na muda na soko kwa ujumla kwani mahitaji ya soko yanabadilika mara kwa mara na kwa haraka sana. Pia hii itasaidia kuzalisha kwa wingi na kutumia vifaa bora vya uzalishaji.

Katika uhamasishaji wa soko la ndani, kuwe na juhudi endelevu ya kuhamasisha Watanzania kuwa wazalendo na kununua kazi halisi (original) za Tanzania. Hiyo itasaidia kuinua soko la ndani litakalomsaidia mzalishaji wa kazi za sanaa kupata kipato cha kutosha kitakachomuwezesha kuzalisha bidhaa nyingi na zenye ubora zitakazomsaidia kuwa na uwezo wa kuuza hata katika soko la nje na kuifanya Tanzania itambulike kwa uzalishaji wa bidhaa bora kimataifa.

Kabla sijaanza kuandika makala hii nilifanya utafiti mdogo kwenye baadhi ya taasisi za fedha ili kujiridhisha, ambapo nimegundua mambo kadhaa na nadhani tunapaswa kuyatatua kwanza kabla hatujakimbilia kuyalalamikia mabenki kwamba hayatukopeshi.

Inaeleweka kuwa hakuna ambaye anaweza kuwekeza pesa zake mahala ambapo hana data sahihi japo anasikia ama anaamini kuwa anaweza kufanya biashara inayolipa. Katika utafiti wangu nilikutana na maswali ambayo benki yoyote ingehitaji kupata majibu yake kabla haijajitumbukiza katika kusaidia sekta ya filamu nchini:

• Tasnia ya filamu nchini ina thamani kiasi gani kwa sasa?
• Je, gharama kiasi gani inatosha kuzalisha filamu nzuri?
• Je, nini wastani wa mauzo ya kila mwaka ya uzalishaji wa filamu?
• Je, makampuni ya filamu katika sekta ya filamu yana dhamana gani kwa ajili ya kupata mikopo?
• Je, hesabu za makampuni ya filamu katika tasnia ya filamu zinafanyiwa ukaguzi?
• Je, makampuni ya filamu katika tasnia yana miundo rasmi?

Pia mabenki kwa kawaida hayawezi kuwa na uhusiano wa kibenki na makampuni au wasanii kama hawatakuwa rasmi na wanaotambulika kisheria. Sekta ya filamu Tanzania inapaswa kuboreshwa zaidi, na kuanza kudumisha kumbukumbu sahihi na akaunti, kushiriki huduma ya wakaguzi na kuwa na miundo rasmi ya shirika.

Mambo haya yanaweza kutusaidia katika:

• Kujifunza kuhusu mienendo ya sekta ya filamu;
• Kuwatambua watu wanaoendesha sekta ya filamu,
• Kupewa mikopo kwa urahisi katika mfumo wa mikopo kwa sekta ya filamu;
• Kupewa huduma za ushauri wa kifedha na kadhalika.


Naomba kuwasilisha.

No comments: