May 14, 2014

Kwa hili la kukaa mezani na kuutazama upya mfumo unaofaa, naipa tano Serikali

Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, akizungumza Bungeni


KATIKA jitihada za kuhakikisha kuwa wasanii hapa nchini Tanzania wanatengenezewa mazingira mazuri zaidi ya kufaidika na kazi wanazotengeneza, Serikali imetoa maagizo kwa Chama Cha Hatimiliki Tanzania, COSOTA na Mamlaka ya Mapato nchini, TRA, kukutana ndani ya siku tano za kazi kuanzia sasa. Mpango huu ni kwa ajili ya kutengeneza makubaliano juu ya mfumo utakaofaa kwa ajili ya kukusanya na kudhibiti mapato ili kuboresha faida kwa wasanii na serikali.



Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Mwigulu Nchemba, alitoa kauli hiyo bungeni ambapo alitaka waangalie namna ya kuboresha stempu/stika zinazobandikwa katika kazi za wasanii ili badala ya kutumika kukusanya ushuru peke yake zitumike pia kulinda kazi za wasanii hao.



Kwa hili naipa tano Serikali kwani itasaidia kuondoa sintofahamu kuhusiana na stempu za TRA, ambapo serikali kwa kupitisha sheria ya stempu za TRA imekuwa ikijigamba kuwa imezirasimisha sekta za filamu na muziki. Nimekuwa nikisisitiza kuwa hakuna 'excuse' yoyote kwa wasanii katika kukuza pato lao, kuondokana na umaskini na hata kushindana kimataifa kama hawataingizwa kwenye mfumo rasmi ambao utawafanya watambulike ndani na nje ya nchi ili kujenga mazingira ya wao kuweza kukopesheka, kupata fursa za kikazi na kukuza kazi wanazozifanya. Katika mataifa mengine wasanii wako rasmi na wameweza kuvuma na kupaa kiuchumi.



Lakini urasmishaji ninaoukusudia si huu ambao tumekuwa tukiushuhudia wa kutubandikia stempu za TRA zitakazotumika kabla kazi hazijaingia sokoni. Inawezekana kabisa serikali ilikuwa na nia nzuri lakini bila kujua ikataka kutumia mfumo ambao si mzuri na imegundulika kuwa serikali kwa mfumo huu “ilishaingia mkenge” na kukosa nia ya dhati ya kumkomboa msanii, hii imethibitishwa na kauli ya Naibu Waziri, Mwigulu Nchemba, alipokiri kuwa ni kweli kuweka stempu za TRA kwenye kazi za wasanii hakulengi kulinda kazi za wasanii zaidi ya kukusanya mapato ya serikali.



Mpango huu unaodaiwa ni wa kurasimisha sekta hii ili kuiboresha umekuwa na maswali mengi mno bila majibu, hasa kutokana na kile kinachoonekana kuwa upande wa serikali (kupitia taasisi zake) hauelewi upande wa pili unatendaje kazi zake, unataka kuchukua haki ya upande wa pili na kutokana na upya wa dhana yenyewe pande zote hazielewi nini kinatakiwa.



Pamoja na TRA kujidai kuwa wamefanya utafiti wa kutosha kabla ya zoezi zima za urasimishaji lakini ukweli hakuna utafiti wowote wa kitaalam uliofanyika, hii inathibitishwa na majibu ya viongozi wa maamlaka wenye dhamana pale wanapobanwa kwa maswali, na mara nyingine walifikia hatua ya kutaka kufunika kombe mwanaharamu apite kwa kutoa majibu mepesi lakini wakisisitiza kuwa wao wanachotaka ni kukusanya kodi tu na hawatarekebisha chochote bali kukazia, masuala mengine hayawahusu!



Kuna wakati katika mkutano mmoja kati ya mamlaka za serikali zenye dhamana kuhusiana na sekta ya filamu na muziki ikiwemo TRA na wasanii kulitokea mtafaruku baada ya maofisa wa TRA walipoulizwa kwanini wanadai TRA inawalinda wasanii wakati ni wazi katika hili kazi yake ni kukusanya kodi kutoka kwa wasambazaji, jambo ambalo halina tija yoyote kwa wasanii binafsi? Majibu yaliyotolewa yalileta mvurugano mkubwa kati ya mamlaka za serikalai na wasanii.



Sielewi ni kwanini serikali imekuwa ikidharau tafiti zinazofanywa na wadau mbalimbali zinazoegemea kwenye hali halisi, tafiti ambazo zimekuwa zinakuja na muarobaini wa kutatua mambo. Mimi pia nimewahi kufanya utafiti kuhusiana na filamu ikiwemo urasimishaji, nikagusia mfumo unaotumika Afrika Kusini ambao ungetufaa sana.



Kama serikali wameliona hili itakuwa vyema maana wengine tulishafikia hatua ya kutaka “kuingia msituni” ili kupigania uwepo wa mfumo sahihi badala ya hiki tulichokiona cha serikali kupitia TRA kuhitaji kodi tu kutoka kwa wasanii lakini ikiwa haina mpango wa dhati kuhusu wasanii, tulitaka tupiganie haki hadi kieleweke, hasa baada ya mfumo uliopo kuonesha kushindwa hata kabla haujaanza.



Kama nilivyowahi kushauri mwaka juzi kuwa ili kuleta ufanisi katika sekta hii serikali inapaswa kuziagiza mamlaka husika kuandaa takwimu za kina kuhusu soko la filamu na kuzitazama fursa zilizopo kabla ya kuamua chochote. Na yote haya yatategemea sera nzuri ya filamu itakayokuwa imeanzishwa. Sera ya filamu ndiyo hati pekee yenye kueleza kwa ufasaha uwezekano mbalimbali katika kuandaa mazingira mazuri kwa ajili ya uzalishaji wa filamu.



Sera hii inapaswa iende mbali zaidi ikizingatia mchakato wa utoaji wa filamu na uanzishwaji wa haki za usambazaji wa miliki. Katika mchakato huu, wasambazaji wenye leseni watatarajiwa kuwasilisha ripoti ya kila wiki ya kisheria katika shughuli zao za usambazaji ambayo inaweza kutumiwa katika kutathmini utendaji wa kifedha wa filamu.



Kwa mfumo uliopo sasa, nimekuwa nikijiuliza maswali mengi yasiyo na majibu. Hivi ni kweli stampu za TRA pekee zinatosha kuleta ufanisi katika soko la filamu bila hata kuijua nguvu ya soko? Mbali na stampu hizi je, kuna mikakati gani katika kudhibiti kazi zisizo na stempu? Je, mlaji atatofautisha vipi stempu halali na batili? Hivi zoezi hili litafanikiwa kweli pasipo elimu kwa walaji?



Sikuishia hapo bado niliendelea kujiuliza maswali lukuki: ni 'mechanisim' gani itakayotumika kuweza kutekeleza hilo na je, msanii atahakikisha wapi kipato chake? Kwenye stampu au wapi? Je, kuna mpango gani katika kuandaa miundombinu ya soko la filamu ili wasanii na watengeneza filamu pia wafaidi jasho la kazi zao tofauti na ilivyo sasa? Je, Serikali ikisharasimisha sekta hii, itawekeza au ndiyo itaingia kwenye mpango wa kuvuna pasipo kupanda? Maswali haya yalikuwa yakinijia kichwani kwa kuzingatia kuwa mfumo wa biashara ya filamu nchini umekaa kienyeji sana. Sidhani kama ni busara kwa serikali (kupitia Mamlaka ya Mapato) kukusanya mapato wakati haijengi miundombinu ya soko, haijengi shule zitakazowasaidia wadau wa filamu, wala haisaidii katika kutafuta soko!


Hapa hata mkikusanya kiasi gani, bado haitatusaidia kama elimu kwa wasanii na wadau wengine haitatolewa. Hivi kuna vyuo vingapi vinavyofundisha filamu? Kwa sheria iliyopo inambana msambazaji/muuzaji kuhakikisha analipa kodi lakini haimsaidii mtayarishaji/msanii ambaye anaendelea kunyonywa kama kawaida.



Kwa mfumo huu serikali bila kujua ilikuwa inatengeneza bomu kwa tasnia ya burudani, bomu ambalo limeleta mgogoro mkubwa katika nchi ya Ghana sababu ya msingi ikiwa ni ndogo tu, kazi ya Mamlaka ya Mapato si kulinda haki za wasanii bali ni kukusanya kodi. Kazi ya kulinda haki hizi iboreshwe katika vyombo vya wasanii husika na Chama Cha Hakimiliki ili TRA iweze kupata takwimu sahihi za kukusanya kodi.



Naomba katika kikao watakachokaa Cosota na TRA wajaribu kuangaalia ni namna gani wataweza kuwa na mfumo wenye kuleta tija, ikiwa ni pamoja na kuangalia kama tunaweza kuwa na chombo chenye mfumo ambao utaweza kudhibiti aina na aina ya wasambazaji, kutoa miongozo kwa ajili ya usajili na leseni ya wasambazaji (ambayo ada fulani wanatarajiwa kulipwa), na kubainisha aina ya haki za usambazaji ambayo wasambazaji katika ngazi mbalimbali wataendelea kumiliki pamoja na udhibiti ili kuhakikisha kuwa haki hizi zinalindwa.



Chombo hiki kiambatane na kuwepo kwa sera mpya itakayoonesha pia sifa zinazopaswa kuchukuliwa katika mkataba halali wa usambazaji ambao pamoja na mambo mengine, utalazimisha wahusika kuandikisha filamu zao kama miliki bunifu (intellectual property). Moja ya masuala ya ubunifu wa sera ya uzalishaji wa fedha na ulinzi ambayo nadhani sera inayopaswa kuwepo ni ya kutoa ufadhili kwa wamiliki wa haki za filamu.



Alamsiki…

No comments: