Apr 30, 2014

Nollywood na mchango wa uchumi Nigeria, Tanzania na upuuzaji wa sekta ya hakimiliki

Desmond Eliot, msanii wa Nollywood

HIVI karibuni Nigeria imetangazwa kuwa ndilo Taifa lenye uchumi mkubwa barani Africa na kuipita Afrika Kusini. Pato Ghafi la Ndani (Gross Domestic Product ‘GDP’) la Nigeria limefikia Dola Billion 509 huku lile la Afrika ya Kusini likifikia Dola Bilioni 322.

Kwa mujibu wa Idara ya Takwimu ya Nigeria, Nigeria imekuwa Taifa lenye uchumi mkubwa Afrika baada ya wanauchumi wa nchi hiyo kuziongeza sekta za Mawasiliano na Filamu (Nollywood) kwenye takwimu. Ni dhahiri kuwa soko la Filamu la Nigeria linatoa mchango mkubwa mno katika ukuaji wa uchumi wa nchi hiyo. Kabla ya hapo Nigeria ilionekana kama taifa linalotegemea zaidi uuzaji wa mafuta na ilikadiriwa kuwa pato la mafuta lilichangia asilimia 32 kwenye GDP lakini ripoti ya wanauchumi hivi karibuni imeonesha sasa pato la mafuta huchangia Asilimia 15 tu ya pato ghafi la ndani.


Haikuishia hapo, ripoti imeonesha pia utegemezi wa kilimo katika kuchangia pato la Taifa nchini Nigeria umepungua. Kwa wanataaluma wa uchumi wanaelewa kuwa kupungua kwa utegemezi wa sekta ya kilimo katika ukuaji wa uchumi maana yake uchumi unapiga hatua. Ili mjitoe katika nchi tegemezi na kuingia kwenye nchi za daraja la kati ni lazima mtegemee zaidi sekta ya viwanda kwa ukuaji badala ya kilimo, wakati nchi zilizoendelea hutegemea sana huduma.

Kwa hali hiyo, kuna nafasi kubwa ya masoko ya Nigeria kuvutia mitaji ya uwekezaji kutoka ndani na nje ya nchi na kupunguza nakisi kubwa ya bajeti (budget deficit) jambo litakaloongeza pia tija, uchumi kupaa na ushawishi wa nchi hiyo katika diplomasia na siasa za kimataifa utaongezeka.

Wakati Nigeria wakijitoa kwenye kutegemea kilimo na kuigeukia sekta ya filamu kama chanzo muhimu cha kichumi (new sector with economic potential), sisi Tanzania tunafanya mzaha. Bado tunang’ang’ana kwenye kilimo cha jembe la mkono huku tukibadili misamiati kila mwaka: Kilimo cha kufa na kupona, Siasa ni kilimo, Kilimo ni uti wa Mgongo, Kilimo Kwanza n.k. na kuzipuuza sekta ambazo zingeweza kuwa mchango mkubwa katika kuliletea Taifa pato. Au basi tungeboreshaa kilimo chetu.

Nollywood ndiyo sekta ya pili kwa kutoa ajira katika nchi ya Nigeria baada ya sekta ya kilimo, na mchango wake kwa Taifa ni mkubwa sana kwani ina thamani ya Naira bilioni 853.9 (Dola za Marekani bilioni 5.1). Hii ni ishara ya jinsi gani sekta ya filamu inavyoweza kukuza na kubadili uchumi wa nchi yoyote, kwa njia ya utoaji wa ajira kama itachukuliwa kwa umakini mkubwa. Matokeo ya kukubalika kwa sinema pia huwafanya watayarishaji wa sinema, waigizaji na watendaji wengine kuwa na heshima kwenye jamii na hata kisiasa.

Mfano, wakati wa kuondolewa kwa ruzuku ya mafuta Nigeria miaka kadhaa iliyopita, Rais Goodluck Jonathan alimtuma mwakilishi wake kujadili suala hilo na wadau wa Nollywood kuhusu kupunguza udhibiti wa kibiashara, mkutano ulioandaliwa na kikundi cha Segun Arinze wa Chama Waigizaji wa Nigeria (AGN). Hapa najaribu kuonesha umuhimu wa sekta ya filamu katika kubadilisha sera za kiuchumi katika uhusiano na siasa nchini Nigeria. Si hivyo tu, mwaka jana Rais Goodluck Jonathan alitangaza kutoa Naira bilioni 3 kwenye kuiendeleza Nollywood, jambo linaloonesha kuutambua mchango muhimu wa sekta hii.

Serikali ya Nigeria inaichukulia sekta ya filamu kwa umakini mkubwa. Vipi kuhusu serikali yetu? Na moja ya maendeleo ya kutia moyo sana Nigeria ni uwepo wa sera ya filamu iliyopatikana mwaka 1991 wakati Shirika la Filamu la Nigeria (NFC) lilipoandaa jopo kuangalia kanuni zilizokuwepo kwa lengo la kuoanisha na kuhuisha kiini cha sera ya filamu.

Tanzania tunakabiliwa na changamoto kubwa sana, sekta ya hakimiliki si sekta rasmi kama tunavyoaminishwa, tunaongopewa kuwa tumerasimishwa wakati si kweli, tunachokishuhudia ni kuwekewa stempu za kodi kwenye kazi zetu, basi. Itakuwaje rasmi wakati hatuna hata sera? Hatuna takwimu, hakuna utafiti wowote uliofanywa kuijua nguvu ya soko la filamu, hatujatengenezewa miundombinu ya soko, wala thamani ya mchango wa sekta hii katika uchumi wa taifa hautambuliwi ipasavyo. Halafu tunaambiwa tumerasimishwa!

Pia sanaa zetu zimekuwa hazilindwi, hazikuzwi, hazitangazwi, hazitambuliki na wala hazipewi umuhimu unaostahili kama ambavyo sekta iliyo rasmi inavyopaswa kuwa. Serikali imeshindwa kuitilia maanani, kuchukua hatua stahiki, kutoa takwimu halisi za mchango wa sekta hii kwa uchumi wa taifa pamoja na ukuaji wa kasi wa sekta hii hali inayosababisha ishindwe kupata pato halisi linalotokana na sekta hii.

Shughuli nyingi zinafanyika kiholela bila wahusika kuwa na hakimiliki na sehemu kubwa ya mchango wake kwa pato la taifa haijarekodiwa katika vitabu vya mapato vya taifa. Hii inaonesha kuwa mchango wa sekta hii katika pato la taifa ni mkubwa zaidi kuliko takwimu zinavyoonesha.

Ili tuweze kupiga hatua na kuimarisha sekta ya hakimiliki ni lazima sasa serikali iache porojo ya kutuongopea kuwa wanautambua mchango wetu, bali waelekeze nguvu kuhakikisha tuna sera madhubuti ambazo zitatungiwa sheria na kanuni zinazostahiki ili kuboresha uendeshaji wa sekta hii nchini.

Sera bora zitachochea maendeleo ya kisekta, mazingira ya ubunifu yenye ushindani na salama ambayo serikali itayatumia kuendeleza sekta hii na kutambua thamani ya kazi za ubunifu.

Pamoja na hayo, bado sekta ya hakimiliki nchini mwaka 2009 kwa mara ya kwanza katika pato la taifa, iliingiza Sh676 bilioni ikiwa ni asilimia 4.6 ya Pato la Taifa (GDP), likiwa ni zaidi katika uchumi wa taifa kuliko sekta ya hoteli, migahawa na madini.

Taarifa hiyo ambayo imetolewa hivi karibuni kwa lugha ya Kiingereza ikiwa na jina: ‘The Economic Contribution of Copyright-Based Industries’ kwa mwaka 2012, imebainisha kwamba sekta ya madini imechangia asilimia 2.6 ya GDP wakati hoteli na migahawa imechangia asilimia 4.5, sekta ya hakimiliki imefanya vyema.

Pia sekta hii imeajiri watu wengi zaidi ya wale walioajiriwa na sekta ya afya na ustawi wa jamii, fedha, majumba ya kukodisha, huduma za biashara, ujenzi, usafirishaji, mawasiliano, madini, umeme, gesi na sekta ya maji. Mchango wa sekta ya hakimiliki kwa malipo ya wafanyakazi, ulikuwa Sh 80.474 bilioni sawa na asilimia 5.

Tusiishie kusema tu, tutafute suluhisho kwa kuhakikisha kuwa tunao mfumo wa kutathmini na kuangalia ukuaji wa sekta kwa kuzingatia ukuaji wake ambao kwa sasa unakwenda kasi, kama ambavyo tafiti za WIPO zimebainisha. Ni vyema sasa tukatafuta utaratibu wa kukusanya takwimu na kuzifanyia uwiano kwa kuziunganisha na takwimu za Taasisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA).

Imekuwa ikisemwa kuwa nchi kadhaa ambazo sasa zimeendelea zilikuwa na uchumi sawa na Tanganyika (sasa Tanzania) wakati tukipata uhuru mwaka 1961, nchi hizo ni pamoja na Singapore, Korea Kusini, Thailand, Malaysia na kadhalika, ila kilichowafanya kutuacha kimaendeleo na kupata maendeleo ya haraka ni ulinzi na uendelezaji wa Miliki Bunifu.

Kwa mfano Korea Kusini imekuwa ni Taifa kubwa na tishio Barani Asia kwa sababu tu ya kulitambua kundi la wasanii na kuweka mazingira mazuri ya ulinzi wa Miliki Bunifu kiasi cha kubatizwa jina la Marekani ya Asia.

Korea imefanikiwa sana kueneza utamaduni wake katika nchi zingine za Asia, na walitumia fursa ya mtikisiko wa kiuchumi uliozikumba nchi za Asia mwaka 1997, ambapo wao waliamua kuwekeza katika sanaa na utamaduni kwa lengo la kuzalisha na kuuza nje kama bidhaa. Hata Rais wa wakati huo, Kim Dae-jung, alipenda kujiita Rais wa Utamaduni na alianzisha mradi huo na kutenga dola za Kimarekani milioni 148.5.

Mwaka 2005 serikali ya Korea iliweka lengo la kuhifanya nchi hiyo miongoni mwa nchi tano bora katika uuzaji wa sanaa na utamaduni. Baadhi ya maeneo ambayo serikali iliwekeza ni pamoja na kusaidia usambazaji na masoko ya nje na kusaidia uzalishaji kupitia vifaa na mitaji. Serikali pia ilihakikisha vyombo vya habari vya ndani vinarusha kwa kiasi kikubwa vipindi vinavyozalishwa ndani.


Alamsiki.

No comments: