Mar 25, 2014

MATOKEO YA UBINAFSI NA UMIMI: Msanii awabeza wasanii wenzake...

*Haya ni matokeo ya kupoteza dira kama Taifa
Viongozi wa Mashirikisho la Sanaa wakiwa pamoja na Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Paul Mtendah (wa pili kushoto) na Maria Sarungi (wa tatu kushoto), kwenye hoteli ya Dodoma, kabla ya vikao vya Bunge kuanza


WIKI iliyopita kwenye gazeti moja litolewalo kila siku (ambalo limetoka kifungoni hivi karibuni) kulikuwa na makala ya mwandishi mmoja ambaye pia ni msanii aliyesomea taaluma ya sanaa katika Taasisi ya Sanaa Bagamoyo, iliyobeza juhudi zinazofanywa na wasanii hivi sasa kupigania kutajwa kama mojawapo wa kundi muhimu kwenye Katiba ya nchi. Makala hayo yaliyojikita katika kile ambacho mwandishi huyu (nitamtaja zaidi kama msanii) alidai kuwa wasanii wenzake wamekumbuka shuka wakati kumekucha, kiasi cha kuzua mjadala mkubwa kwenye mtandao wa kijamii wa facebook.

Ukisoma kwa umakini makala ya msanii huyu utagundua kuwepo kwa mambo makuu matatu: ukosefu wa taarifa, umimi na kukurupuka kuongelea jambo bila utafiti, ili mradi aonekane anajua kusema!

Msanii huyu ambaye hupenda kuponda (yeye huita kukosoa) kazi za wenzake pasipo kuonesha jinsi ya kuboresha ameona kuwa juhudi zinazofanywa hivi sasa na Shirikisho la Filamu Tanzania na Mtandao wa Wanamuziki Tanzania kupigania mambo mawili yaingie kwenye katiba ya nchi ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu. Eti hawajafuata ushauri wake!

Mambo ambayo wasanii wanataka yaingizwe kwenye Katiba ni kulitambua kundi la wasanii kama mojawapo ya makundi muhimu, kama ambavyo imetambua uwepo wa makundi ya wakulima, wavuvi, wafanyakazi, wafugaji nk.

Wasanii ni kundi kubwa sana linaloyazidi makundi mengine huku likizidiwa na wakulima, pia ni kundi linalochangia uwepo wa ajira kwa vijana wengi, kutolitambua ni kosa. Kwa mujibu wa utafiti wa WIPO wa Septemba 2012, sekta ya sanaa inachangia kwenye pato la Taifa kwa asilimia 4.275. Kutokutambuliwa kwa kundi hili kunafanya pato litokanalo na sanaa kupotelea katika mifuko ya watu na kuwakosesha wasanii na Taifa pato kubwa.

Jambo la pili ni kuwa kutajwe ulinzi wa Miliki Bunifu (Intellectual Property) katika Katiba na hivyo kuwezesha sheria bora kutungwa na pia utekelezaji wa ulinzi wa kazi kama ilivyo katika mali nyingine za wananchi wengine. Kwenye Rasimu ya Katiba imetajwa ulinzi wa kazi zinazohamishika na zisizohamishika lakini mali zisizoshikika (za ubunifu) hazikutajwa. Kwa msanii huyu haya yanayopiganiwa ni upuuzi (sijui kwa kuwa hajashirikishwa kama anavyodai?) na kwamba hayatafanikiwa.

Sanaa zetu zimekuwa hazilindwi, hazikuzwi, hazitangazwi, hazitambuliki na wala hazipewi umuhimu unaostahili. Jambo muhimu na la msingi ni kuzingatia, kuzikuza, kuzitambua na kuzilinda sanaa zetu ili zisipoteze uasili wake pamoja na wimbi la mabadiliko ya wakati na mazingira ya sasa ya utandawazi na biashara huria. Ieleweke wazi kwamba sanaa ni kazi ya ubunifu tena yenye ufundi na mvuto kama sumaku, kazi nzuri ya sanaa ni ile iliyo na ubunifu, uasili na inayotumia mbinu bora ya uwasilishwaji wa ujumbe kwa hadhira.

Kwa kuwa mawazo haya yametoka kwa wasanii ambao hawajaenda shule ni ndoto kufanikiwa! Ila kama yangetoka kwa wasomi isingekuwa shida kwa msanii huyu. Anaposema ‘wasanii wamekumbuka shuka kumekucha’ maana yake, hawapaswi kupigania haki yao kikatiba ila waendelee kulalamika tu?

Msanii huyu badala ya kuungana na wenzake ili kuhakikisha mambo haya yanapitishwa yeye anaendeleza mambo yaleyale kama ilivyo kwa viongozi tuliowapa dhamana ya kutuongoza kwenye masuala ya sanaa na utamaduni kushindwa kusimamia, kutudharau (eti hatujasoma) na kutukatisha tamaa kiasi kwamba hadi leo tumeshindwa kuthamini tamaduni zetu.

Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kutamka kuwa Utamaduni ni kiini na roho ya Taifa, na kwamba nchi inayokosa utamaduni wake ni sawa na mkusanyiko wa watu usiokuwa na roho na hivyo kukosa sifa ya kuitwa taifa kamili. Hii ilikuwa wakati wa kuunda Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana, mwaka 1962.

Kupuuzwa kwa tamaduni kumekuwa ni suala linalojitokeza katika nyanja mbalimbali hapa nchini. Kati ya mambo ambayo binadamu hana budi kuyazingatia ni uhusiano wake na mila na desturi alizotunukiwa na jamii yake. Ni katika kuzingatia hilo tu ndipo binadamu anapata uwezo wa kukua na kujichotea utajiri mkubwa unaotolewa na tamaduni za jamii yake.

Hii imesababisha hata sera ya utamaduni kutokupewa nafasi katika serikali hii tangu ilipoanzishwa wizara inayoshughulikia masuala ya sanaa. Naamini kuwa hali ya mtu kujitenga na tamaduni asilia kunaweza kuwa tishio katika kupokea hata imani ya kidini. Hii inatokana na ukweli kwamba imani ambayo mtu aipokeayo kama zawadi toka kwa Mungu ina msingi wake katika mila na desturi tuziishizo. Hakuna uwezekano wa kuwa na imani ya kidini iwapo mtu hakujengeka katika utamaduni wa kweli. Ni katika tamaduni zetu ndipo tunapata maana ya utu, upendo na kadhalika.

Hatari kubwa ya kupotea kwa tamaduni asilia inatukumba sana vijana ambao bila kujua huwa tunajikuta katika utamaduni hasi unaotusukuma kudharau tamaduni zetu na kujiingiza katika mienendo ambayo kwa kiasi kikubwa si tamaduni ila vurugu zinazotokana na kukosekana kwa tamaduni.

Hii inajionesha katika sanaa zetu tunazoziandaa ambazo nyingi zinajengwa katika misingi isiyo na maana katika jamii. Uigaji usio na uchambuzi umetupelekea kukosa kabisa vipaumbele katika maisha yetu, na kubaki kuwa bendera kufuata upepo.

Sijui kama msanii huyu anajua kuwa sanaa ni zao la matokeo ya juhudi za wasanii katika kutoa ujumbe, kukidhi matumizi na mahitaji ya binadamu, na jambo hili linaonesha umuhimu wa utamaduni si kitu kilichoibuka tu. Hivyo inapaswa kupiganiwa kwa gharama yoyote iingizwe kwenye katiba mpya.

Hakuna heshima kubwa kama mtu kutambulika kuwa ni sehemu ya utamaduni fulani, utamaduni unaoweza kutupatia urithi usiofutika. Yale tunayoyaonesha katika maisha yetu ya kawaida, hayaishii hapo tu bali yanaathiri hata maisha yetu ya kiimani.

Kama Taifa tumepotea na tumechanganyikiwa. Tumekumbatia baadhi ya tamaduni za wengine na kuzigeuza kuwa zetu bila kujali kama zinaakisi jamii husika. Hakuna heshima kubwa kama mtu kutambulika kuwa ni sehemu ya utamaduni fulani, utamaduni unaoweza kutupatia urithi usiofutika. Yale tunayoyaonesha katika maisha yetu ya kawaida, hayaishii hapo tu bali yanaathiri hata maisha yetu ya kiimani.

Labda nimuelimishe msanii huyu kuwa Korea Kusini imekuwa Taifa kubwa na tishio Barani Asia kwa sababu tu ya kulitambua kundi la wasanii na ulinzi wa Miliki Bunifu kwenye Katiba yake. Nchi zingine za Asia (China, Japan, Philippines, Indonesia, nk) zimeipa jina la Marekani ya Asia.

Korea imefanikiwa sana kueneza utamaduni wake katika nchi zingine za Asia, na walitumia fursa ya mtikisiko wa kiuchumi uliozikumba nchi za Asia mwaka 1997, ambapo wao waliamua kuwekeza katika sanaa na utamaduni kwa lengo la kuzalisha na kuuza nje kama bidhaa. Hata Rais wa wakati huo, Kim Dae-jung, alipenda kujiita Rais wa Utamaduni na alianzisha mradi huo na kutenga dola za Kimarekani milioni 148.5.

Mwaka 2005 serikali ya Korea iliweka lengo la kuhifanya nchi hiyo miongoni mwa nchi tano bora katika uuzaji wa sanaa na utamaduni. Baadhi ya maeneo ambayo serikali iliwekeza ni pamoja na kusaidia usambazaji na masoko ya nje na kusaidia uzalishaji kupitia vifaa na mitaji. Serikali pia ilihakikisha vyombo vya habari vya ndani vinarusha kwa kiasi kikubwa vipindi vinavyozalishwa ndani.

Kutokana na kutambuliwa kwa sanaa katika Katiba, kuwa na sera sahihi na uwekezaji mkubwa, nguvu ya serikali, ubora wa kazi za sanaa na utamaduni ukapanda, uzalishaji ukawa rahisi huku msisitizo mkubwa ukiwekwa katika ubunifu lakini juu ya msingi wa utamaduni wa Korea na hivyo kufanya kazi ya kuakisi uhalisia wa maisha ya watu.

Ndiyo maana Marekani imeendelea kuwa Taifa kubwa na lenye nguvu kubwa, nguvu ambazo hazitokani tu na uchumi imara na mabavu ya kijeshi bali nguvu za kiutamaduni. Hebu angalia nchi kama China japo ina idadi kubwa ya watu (bilioni 1.5), bado kiutamaduni hawana ushawishi kama walionao Wamarekani hata katika eneo lao la Asia Mashariki. Ni Wakorea peke yao wanaoshindana na Marekani katika soko la sanaa na utamaduni katika nchi za Asia. Kwanini? Kwa sababu wamelitambua kundi la Wasanii na ulinzi wa Miliki Bunifu katika Katiba yao.

Inashangaza pale msanii wa Kitanzania, kwa kuwa tu kapata jukwaa (gazeti) anapotumia nafasi hiyo kuwaponda na kuwakejeli wasanii wenzake badala ya kuwatia moyo na kuisuta serikali kwa kuwa imeitelekeza sanaa na utamaduni wa nchi na hivyo kushindwa kuenzi asili yetu.


Tukutane wiki ijayo.

No comments: