Mar 5, 2014

KATIBA MPYA: Wasanii kazeni uzi, mmeshatumiwa sana

Kikosi Kazi cha wasanii 12 kilichokwenda Bungeni Dodoma kuonana na Wajumbe wa Bunge la Katiba wakiwa katika picha ya pamoja na Mh. Samwel Sitta

IMEKUWA ni kawaida kila wakati wa uchaguzi kuona wasanii wakitumika kuvuta watu wakati wa mikutano ya kampeni za wagombea urais, ubunge na hata udiwani. Hutumiwa kuwavuta watu ili wafike kwenye mikutano hiyo kabla ya wanasiasa kuanza kampeni zao za kutaka kuungwa mkono.

Pindi wanasiasa wanapopata madaraka wamekuwa hawawakumbuki tena wasanii hadi pale uchaguzi mwingine unapokaribia. Hili ni jambo linalokatisha tamaa, na limeendelea kujitokeza hata sasa wakati tukiwa kwenye mchakato wa kutafuta Katiba mpya itakayotuongoza kwa miaka mingine hamsini baada ya uhuru, ambapo vikao vya Bunge Maalum la Katiba vimeanza mjini Dodoma tangu Februari 18, mwaka huu.

Wanasiana wameonekana kupeleka nguvu zao kwenye masuala ya kisiasa kama muundo wa serikali na masuala yenye maslahi ya kisiasa na kusahau mambo mengine muhimu ya kijamii, ikiwemo suala la wasanii ambao hutumika kama kivutio cha kuwavuta wapigakura kuja kwenye mikutano kusikiliza sera za vyama.

Hivi karibuni timu ya wasanii kumi na mbili ilikwenda Dodoma kuongea na Wajumbe wa Bunge la Katiba ili kuwashawishi kuingiza vipengele viwili muhimu kwenye katiba ya nchi baada ya Tume ya Katiba kuyapuuza maoni yao. Wasanii kupitia Umoja wa Mashirikisho ya Sanaa waliunda Baraza la Katiba ambapo Mashirikisho yalitoa mapendekezo kadhaa yaliyofikishwa kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Pamoja na mapendekezo hayo kupokewa lakini hakukuwepo na jambo lolote lililotokana na mawazo hayo (pamoja na uzuri wake) lililochukuliwa na kuingizwa kwenye rasimu ya Katiba.

Kumekuwepo na kasumba ya kuendelea kuitambua sekta ya sanaa kama ni sehemu ya utamaduni (kwa ajili ya kujiburudisha) badala ya kuitazama kibiashara na chanzo muhimu cha kichumi (new sector with economic potential).

Kwa mujibu wa utafiti wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) wa mwaka 2006 unaonesha kuwa Tanzania ilikuwa na wasanii milioni 6. Sasa ni miaka saba imeshapita na kwa vyovyote idadi hii itakuwa imeongezeka mara dufu hasa ikizingatiwa kuwa teknolojia imekuwa sana na asilimia 60 ya Watanzania ni vijana.

Ninapozungumzia wasanii namaanisha watu wote wanaofanya kazi za sanaa na ubunifu, na si kama wengi wanavyodhani kuwa ni wale wanaoigiza au kuimba tu. Sanaa kwa sasa ni biashara kubwa ambayo ripoti ya Shirika la Hakimiliki la Kidunia (WIPO) ya mwaka 2012 inaonesha kuwa mchango wa mapato uliotokana na shughuli za Hakimiliki ulikuwa ni zaidi ya mchango wa Sekta ya Madini. Pia mchango wa ajira katika kazi zilizotokana na Hakimiliki ulikuwa ni zaidi ya madini, umeme, gesi, maji, usafirishaji, mawasiliano, ujenzi, afya, na ustawi wa jamii. Pia wasanii ndiyo wamekuwa wakilipa jina na utambulisho Taifa hili.

Hivyo, inashangaza kuona kuwa Rasimu ya Katiba imetambua uwepo wa makundi mbalimbali kama wakulima, wavuvi, wafanyakazi, wafugaji nk. lakini ikashindwa kutambua uwepo wa kundi kubwa la wasanii!

Kwa takwimu hizi utagundua kuwa wasanii ni kundi kubwa sana linaloyazidi makundi mengine huku likizidiwa na kundi moja tu la wakulima, pia ni kundi linalochangia uwepo wa ajira kwa vijana wengi, hivyo kutolitambua ni makosa. Kwa mujibu wa utafiti wa Shirika la Hakimiliki la Dunia (WIPO) wa Septemba 2012, sekta ya sanaa inachangia kwenye pato la Taifa kwa asilimia 4.275.

Kwa kutambua jambo hilo, Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) likishirikiana na Mtandao wa Wanamuziki Tanzania (TAMUNET) waliunda Kikosi Kazi cha watu 12 na kwenda Dodoma kupigania mambo makuu mawili.

Kwanza wasanii kutajwa na kutambuliwa katika Katiba mpya kuwa ni kundi rasmi kutokana na ukubwa wa kundi hili nchini, kama yalivyotajwa makundi ya wakulima, wafugaji, wavuvi na kadhalika, pia mchango wake katika ajira ya vijana na ukubwa wa pato linalotokana na kundi hili, ambalo kutokana na kutokutambuliwa linapotelea katika mifuko ya watu na kukosesha wasanii na Taifa pato kubwa.

Kikosi Kazi hiki pia kilitaka ubunifu ulindwe kwanza kwa ulinzi wa Miliki Bunifu (Intellectual Property) kutajwa rasmi katika katiba na hivyo kuwezesha sheria bora kutungwa na pia utekelezaji wa ulinzi wa kazi zao uweko kama ilivyo katika mali nyingine za wananchi wengine. Kwenye Rasimu ya Katiba imetajwa ulinzi wa kazi zinazohamishika na zisizohamishika lakini mali zisizoshikika (za ubunifu) hazikutajwa.

Milikibunifu ni mkusanyiko wa haki mbalimbali anazopewa mbunifu. Wasanii hulindwa na Hakimiliki ambayo ni sehemu tu ya Miliki Bunifu. Kampeni ya wasanii kuhusu hili la Intellectual Property (IP) kutajwa katika katiba ni kuwa katika Katiba kumetajwa ulinzi wa mali zinazohamishika na zisizohamishika, lakini mali zisizoshikika zinazotokana na ubunifu hazikutajwa na ndiyo maana pamoja na sheria kuweko, serikali huzilinda hizo kama fadhila.

Nchi kadhaa hutajwa kuwa zilikuwa na uchumi sawa na Tanzania wakati nchi yetu ikipata uhuru wake mwaka 1961, zikiwamo Singapore, Korea Kusini, Thailand, Malaysia na kadhalika, na kilichowafanya kutuacha kimaendeleo na kupata maendeleo ya haraka ni ulinzi na uendelezaji wa Miliki Bunifu na ndiyo maana leo kuna Samsung, Hyundai, LG, Daewoo nk. Suala hili la Miliki Bunifu ni pana zaidi ya sheria ya copyright ambayo nayo kutokana na spidi ya teknolojia hujikuta ikipitwa na wakati kila baada ya muda mfupi, ni muhimu kuwa katika sheria mama (Katiba) ambayo itaangalia hali leo na miaka 50 baadaye.

Kwa sasa Tanzania imepiga hatua kubwa ya ubunifu katika maeneo nyeti ya kiuchumi kama vile kilimo, kwa hiyo ipo haja ya kuhakikisha uvumbuzi huo unalindwa ipasavyo. Ni muhimu pia kulinda mali asili zetu kama vile utamaduni, na maeneo ya kijiografia. Maeneo mengine yanayohitaji kulindwa ni pamoja na muziki, na sanaa.

Kuwepo kwa kwa sheria ya Miliki Bunifu kwenye Katiba ya nchi kutaleta uhakika wa ulinzi wa haki hizi na kutawezesha kutungwa kwa sheria bora zaidi za ulinzi wa haki ambao matokeo yake katika nchi zilizofuata mfumo huu ni maendeleo makubwa sana katika sanaa na teknolojia.

Wizara ya Viwanda na Biashara umeshaandaa sera ya Taifa ya Miliki Bunifu itakayokidhi mahitaji ya nchi kwa kujenga msingi wa matumizi ya Miliki Bunifu ili kuchangia kikamilifu katika kufikia lengo la Taifa la Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025. Lakini sera hii bila kukaziwa kwenye sheria mama inaweza isipewe uzito unaostahili.

Ieleweke kuwa Ubunifu ni nyenzo muhimu sana ya kuongeza ubora wa bidhaa na huduma zinazozalishwa kwa gharama nafuu. Kutajwa kwenye Katiba ya nchi, Sera ya Taifa ya Miliki Bunifu itasaidia kufikiwa kwa malengo ya 2025 ikiwemo kupunguza umasikini nchini. Kufanikishwa kwa lengo hili la kitaifa kutasababisha ukuaji wa uchumi wetu kwa kiwango kati ya asilimia 8 hadi 10 katika sekta ya kilimo sambamba na sekta ya viwanda inayotegemewa na karibu asilimia 70 ya Watanzania.

Kwa hiyo, hili si jambo linalohusu sanaa peke yake bali ni suala mtambuka kwa maslahi ya Taifa zima. Hii itawezekana tu iwapo itatambuliwa na kusababisha kuwepo maendeleo ya kibiashara na uhamasishaji wa matumizi ya bidhaa zinazozalishwa na viwanda vyetu vya ndani katika masoko ya maeneo EAC na SADC pamoja na masoko mengine ya kimataifa ambako kuna ushindani mkubwa.

Tanzania ni mjumbe wa WTO katika kundi la nchi masikini (LDCs) ambapo inayo fursa ya kufaidika na makubaliano mbalimbali ya kimataifa ambayo hupatikana tu pale ambapo nchi husika itazingatia utekelezaji makini na wa kimkakati wa Sera ya Taifa ya Miliki Bunifu. Ni wakati sasa wa kutambua uhalali wa sanaa na Miliki Bunifu kwa kuviweka kwenye Katiba mpya kwa maendeleo ya nchi.


Alamsiki.

No comments: