May 31, 2014

Kudumaa kwa Sekta ya Filamu Tanzania kunatokana na kukosa muongozo

Naibu Waziri wa Habari Vijana Utamaduni na Michezo, 
Juma Nkamia



Alhamisi wiki hii, Wizara ya habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ilisoma bajeti yake ya mwaka 2014/15 na kuweka vipaumbele vyake. Lakini pamoja na kuigusa sekta ya filamu bado imekuwa haipewi kipaumbele japo imeonekana kuchangia kwa kiasi kikubwa katika ajira na pato la Taifa.

Tanzania ni moja ya nchi chache zenye maeneo mazuri ya kuvutia yanayofaa kabisa kwa kutengenezea filamu, ni nchi yenye wasanii wengi wazuri wenye vipaji lakini waliokosa muongozo. Tasnia ya filamu na muziki nchini ni sekta tajiri sana lakini zisizopewa kipaumbele.

-      Takriban filamu kumi hutengenezwa kila wiki nchini
-      Kila filamu kwa kawaida hurudufiwa katika nakala 100,000
-      Kuna takriban video library 25,000 nchini ambazo kama zingetambulika rasmi zinaweza kabisa kuwa sehemu ya soko na kuchangia mauzo ya nakala 75,000 (kwa nakala tatu tu kila library)

Soko la filamu za Tanzania kwa sasa limekuwa mno hadi kufikia nchi zaidi ya nane likijumuisha pamoja nchi za Afrika Mashariki, Congo DRC, Malawi, na Zambia, likiwa na watazamaji zaidi ya milioni 160.

Lakini bado kumekuwepo na kasumba ya kuendelea kuitambua sekta ya sanaa (copyright-based industries) kama ni sehemu ya utamaduni (kwa ajili ya kujiburudisha) badala ya kuitazama kibiashara na chanzo muhimu cha kichumi (new sector with economic potential).

Kwa mujibu wa utafiti wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) wa mwaka 2006 unaonesha kuwa Tanzania ilikuwa na wasanii milioni 6. Sasa ni miaka nane imeshapita na kwa vyovyote idadi hii itakuwa imeongezeka mara dufu hasa ikizingatiwa kuwa teknolojia imekuwa sana na asilimia 60 ya Watanzania ni vijana. Bahati mbaya sana sekta hii imekuwa ikijienda yenyewe tu bila muongozo wowote kutoka serikalini, hali inayofanya kupoteza pato kubwa

Wasanii ni kundi kubwa sana linalozidiwa na kundi moja tu la wakulima, pia ni kundi linalochangia uwepo wa ajira kwa vijana wengi, hivyo kutotoa kipaumbele ni makosa. Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali zikiwemo za WIPO, ILO na nyingine, sekta hii ilichangia TSH680.990 bilioni kwa mwaka 2010 na kuchangia 5% katika GDP. TSH83.686 bilioni ilikuwa ni income iliyoingia kwenye mnyororo wa thamani, ambayo ni sawa na 5.2% ya national economic value.

Sekta hii pia iliajiri watu 44,331 au 5.7% ya ajira nchini. Kwa maani hii utaona kuwa hii siyo sekya ya kubweza kabisa, kwani ikipewa kipaumbele inaweza kuwa mkombozi wa vijana na kuchangia pato kubwa katika uchumi wa nchini hii.

Changamoto kubwa zilizopo kukosekana kwa sera (muongozo), serikali kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kutoyapa kipaumbele Mashirikisho ya Sanaa yaliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Bunge Na 23. ya 1984 iliyounda Baraza la Sanaa la Taifa. Kwa kweli mashirikisho haya yamenyimwa mamlaka na uwezo (kwa makusudi) ya kuwa vyombo vya juu vya wadau kusimamia masuala ya sanaa, jambo ambalo limekuwa likisababisha kupotea kwa mapato, kupungua kwa maadili, na kuongezeka kwa skendo miongoni mwa wasanii.

Sera ni muhimu sana kwani ndiyo muongozo/mfumo wa kuwatambua wanaoendesha sekta ya filamu, husaidia kuandaa mazingira mazuri ya uzalishaji wa filamu, na husaidia uandaaji wa takwimu za kina. Sera pia huangalia mazingira na ubora wa elimu inayopatikana/inayohitajika, na huangalia masoko.

Kukosekana kwa sera kumezifanya filamu zetu kuwa kama mchezo wa soka bila refa, mkutano bila mwenyekiti, darasa bila mwalimu, au nyumba (familia) bila mzazi, japo tuna watu wengi waliosoma (ukiwemo). Ndiyo maana hata elimu tunayoipata hapa nchini imekuwa haitusaidii sana kutengeneza kazi nzuri badala yake tumekuwa wakosoaji wakubwa.

sera ndiyo iliyoifanya Nigeria leo hii iwe nchi ya mfano barani Afrika. Mafanikio waliyoyapata Nigeria yalitokana na uwepo wa sera ya filamu iliyopatikana mwaka 1991 wakati Shirika la Filamu la Nigeria (NFC) lilipoandaa jopo kuangalia kanuni zilizokuwepo kwa lengo la kuoanisha na kuhuisha kiini cha sera ya filamu. Nigeria kwa sasa imetangazwa kuwa ndilo Taifa lenye uchumi mkubwa barani Africa na kuipita Afrika Kusini. Pato Ghafi la Ndani (Gross Domestic Product ‘GDP’) la Nigeria limefikia Dola Billion 509.

Kwa mujibu wa Idara ya Takwimu ya Nigeria, Nigeria imekuwa Taifa lenye uchumi mkubwa Afrika baada ya wanauchumi wa nchi hiyo kuziongeza sekta za Mawasiliano na Filamu (Nollywood) kwenye takwimu. Ni dhahiri kuwa soko la Filamu la Nigeria linatoa mchango mkubwa mno katika ukuaji wa uchumi wa nchi hiyo. Kabla ya hapo Nigeria ilionekana kama taifa linalotegemea zaidi uuzaji wa mafuta na ilikadiriwa kuwa pato la mafuta lilichangia asilimia 32 kwenye GDP lakini ripoti ya wanauchumi ya hivi karibuni imeonesha sasa pato la mafuta huchangia asilimia 15 tu ya pato ghafi la ndani.

Nollywood ndiyo sekta ya pili kwa kutoa ajira katika nchi ya Nigeria baada ya sekta ya kilimo, na mchango wake kwa Taifa ni mkubwa sana kwani ina thamani ya Naira bilioni 853.9 (Dola za Marekani bilioni 5.1). Hii ni ishara ya jinsi gani sekta ya filamu inavyoweza kukuza na kubadili uchumi wa nchi yoyote, kwa njia ya utoaji wa ajira kama itachukuliwa kwa umakini mkubwa.

Na hata Korea Kusini (ambayo nchi zingine za Asia huiita Hollywood ya Asia) imefanikiwa sana kueneza sanaa zake katika nchi zingine za Asia na Afrika kwa sababu ya sera madhubuti, na walitumia fursa ya mtikisiko wa kiuchumi uliozikumba nchi za Asia mwaka 1997, ambapo wao waliamua kuwekeza katika sanaa na utamaduni (kama sera ilivyotaka) kwa lengo la kuzalisha na kuuza nje kama bidhaa. Hata Rais wa wakati huo, Kim Dae-jung, alipenda kujiita Rais wa Utamaduni na alianzisha mradi huo na kutenga dola za Kimarekani milioni 148.5.

Nawasilisha.

No comments: