Nov 26, 2014

Uandishi bora wa Filamu: Tuanze kuwafundisha watoto jinsi ya kuandika script

Magdalena Hiluka, akiwa na miaka 4 wakati huo. Inashauriwa 
kumpa hamasa mtoto katika umri mdogo ili kujenga kipaji chake 


Tangazo (poster) la filamu ya Mke Mchafu.

NIANZE makala yangu kwa kumpongeza Mtayarishaji na Muongozaji wa filamu nchini, John Lister Manyara, kwa sinema yake “MKE MCHAFU” ambayo ni sinema pekee ya Tanzania iliyokubalika kuoneshwa kwenye ndege za Shirika la Ndege la Emirates. Haya ni mafanikio makubwa. Sinema hii imewashirikisha waigizaji maaruf wa Tanzania; Zuberi Mohammed (Niva), Hisan Muya (Tino) na Blandina Chagula (Johari) na wengineo, imeongozwa na John Lister na mimi (Bishop Hiluka) ndiye niliyeiandika. Mafanikio ya sinema hii yananihusu kwa kiasi kikubwa.

Haikuwa kazi rahisi kuiandika, hasa kutokana na mazingira niliyokuwa nayo na katika muda mfupi sana. Lakini kwa kutambua ugumu wa kazi ya uandishi wa filamu na umuhimu wa script kama kipengele muhimu sana katika uandaaji wa filamu, ilibidi nivae viatu vya watazamaji wangu kujua wanataka nini. Uandishi wa filamu ni kazi ngumu sana inayohitaji weledi wa hali ya juu.

Ili kupata waandishi wazuri, wakati mwingine tunatakiwa kuwaandaa waandishi wakiwa katika umri mdogo kwani akili zao bado zinakua na hawana msongo wa mawazo, hii inasaidia kupata waandishi wenye ubunifu. Mwandishi mzuri anahitaji kuwa na kipaji, kujenga tabia ya kujifunza, kutafuta taarifa na ubunifu. Inamsaidia kujenga taswira akilini mwake ya kitu anachotaka kukisimulia katika hali kama vile anaangalia sinema, kama ilivyo kwangu.

Nilikuwa na mazoea ya kufuatilia mambo katika umri mdogo kitu kilichonifanya nipende kuandika na kuufanya uandishi kuwa sehemu ya maisha yangu. Nilipenda kuandika tangu nilipojua kusoma na kuandika, nilipenda kufanya utafiti na kufuatilia mambo. Nilikuwa tayari kusamehe chakula kama angetokea mtu akaanza kusimulia hadithi au kisa cha aina yoyote. Nilijikuta najenga taswira ya kitu kilichosimuliwa akilini mwangu na kukiona kama vile naangalia sinema jambo lililonifanya nianze kupenda kujisomea na kuandika visa mbalimbali tangu nikiwa mdogo.

Kwa sasa mfumo wa maisha yangu umetawaliwa na uandishi: nilalapo, niamkapo, nitembeapo na chochote nifanyacho nafikiria kuandika tu. Uandishi ni sehemu ya maisha yangu. Hivyo, nashauri tufikirie sana kuwapa hamasa watoto na kuwafundisha kuandika jambo litakalowasaidia kujenga taswira akilini mwao na kuwafanya kuwa waandishi wazuri baadaye.

Mwandishi mzuri lazima awe na kipaji na uwezo wa kuandika. Kipaji mtu huzaliwa nacho au hukipata (adapt) katika umri mdogo kutokana na mazingira anayokulia. Uandishi mzuri wa filamu huanzia katika kuwa na uwezo wa kuumba maneno ambayo yatakuwa rahisi kueleweka pindi mtu akiyasikia. Wakati unaandika ni muhimu sana kuzama ndani ya akili za walengwa wako ujue wanataka nini. Pia unapaswa kuifahamu bajeti ya sinema unayoiandikia. Hii itakusaidia usiandike vitu vinavyoweza kuongeza bajeti na kukuharibia kazi.

Mwandishi mzuri ni yule anayefahamu ni maudhui gani yanayofaa katika kizazi cha leo yanayokwenda sambamba na watazamaji ndani ya akili zao na kuihusisha jamii moja kwa moja. Mafanikio yanayotokana na maudhui yanategemea sana mmenyuko wa watazamaji, na kujenga maudhui yaliyo kwenye mstari na mwelekeo wa watazamaji na matarajio yao. Inahitajika kwa waandishi kujihusisha moja kwa moja na mtazamo wa watazamaji katika mazingira waliyomo. Kwa matokeo haya, utafiti ni suala la kupewa umuhimu mkubwa kabla ya kuandaa kazi husika.

Bila uelewa mzuri wa maudhui ni sawa na kufunga safari kwenda sehemu bila kufikiria jinsi ya kufika huko. Kumbuka, unachokiandika si kwa ajili yako, ni kwa ajili ya watazamaji na hadithi zao! Kama mwandishi, usipende kuingiza kila taarifa ukasahau kuwa unaandika kwa ajili ya jicho (kuonekana) na sikio (kusikika).

Suala la uzoefu halijitokezi kama hutaandika kwa muda mrefu, ndiyo maana husemwa kuwa uzoefu ni mwalimu mzuri kwa ajili ya kujua kama stori unayoiandika ni bora, hafifu, au mbaya, na huwezi kupata uzoefu kama hujengi tabia ya kuandika muda wote bila kuchoka.

Kama tutawekeza kwenye akili za watoto wadogo na wakapenda kuandika, tutakuwa tumejenga msingi imara sana kwa mustakabali wa tasnia ya filamu na waandishi wa baadaye, kwani mtoto akishajenga tabia ya kuandika na kuuchukua uandishi kuwa sehemu ya maisha yake hatachoka kuandika na kupitia maandishi yake kuangalia kama kuna makosa. Kisha atakaa chini na kuandika upya. Kumbuka, uandishi hautaki mwandishi awe mvivu wa kufikiri.

No comments: