Jan 1, 2015

Mwaka 2014 umeshuhudia vifo mfululizo vya wasanii

* Wapo waliohusisha vifo hivi na kafara

Marehemu George Otieno Okumu "Tyson"

Marehemu Adam Phillip Kuambiana
 TUMEINGIA mwaka mpya 2015 tukitaraji mafanikio makubwa zaidi na tukiuaga mwaka 2014 uliokuwa wa simanzi kwa tasnia ya filamu tulipokumbwa na taharuki kufuatia vifo vilivyotokea mfululizo vya wasanii wa filamu vilivyotokea katika muda mfupi mfupi. Kufuatia vifo hivyo tetesi zilienea mitaani kwamba vifo hivyo vilitokana na kutoana kafara!


Tetesi hizi zilinilazimu kufanya utafiti ili kujua nini maana ya Kafara, na kama kweli kuna kafara katika vifo hivi. Inasemwa kuwa kafara ni kitendo cha kutoa damu ya mnyama, ndege au mtu kama sadaka kwa mzimu ili kupata upendeleo maalumu kutoka kwa mzimu huo. Upendeleo huo unaweza kuwa ni utajiri, mali, mafanikio katika biashara, uongozi, kazi, mapenzi, ulinzi wa kishirikina, nguvu za kishirikina na kadhalika.

Kwa lugha nyingine kafara ni mabadilishano ya vitu kati ya mtoa kafara na mzimu au muungu ambao unapokea kafara hiyo.

Wataalamu wanatueleza kuwa zipo aina mbalimbali za kafara, lakini zilizo kuu ni mbili: Kafara ya Damu; ambapo mtu hutakiwa kutoa kafara ya mnyama aliye hai, ndege au hata mtu. Na kafara ya kutoa kiungo cha mwili; hii ikimaanisha kuwa mtu hutakiwa kutoa kiungo chake cha mwili ili aweze kukidhi matakwa ya kafara. Hii inawahusu zaidi wanaume, na mara nyingi huambiwa watoe uanaume wao (kuhasiwa) au kuondolewa uwezo wa kumzalisha mwanamke. Vitu vyote hivi hufanyika kichawi.

Hebu tuziangalie aina hizi mbili kwa kina zaidi ili kulinganisha na vifo vilivyotokea mfululizo vya wasanii wetu kama mazingira yanafanana. Je, kwanini mizimu  hutaka kafara ya damu?

Kwa mujibu wa mtaalam mmoja Mungwa Kabili, aliyejitambulisha kama mtaalam wa kafara anasema kuwa zipo sababu mbalimbali kwanini mizimu huomba kafara ya damu, lakini kubwa kuliko zote ni hii kwamba mizimu huwa hailipwi kwa pesa, bali kwa damu. Kwa lugha nyingine, damu ya wanyama katika kafara hutumika kama fedha ya kununua upendeleo (privilege) kwa mzimu.

Mtaalam huyu anabainisha kuwa kafara za damu nazo zimegawanyika katika makundi makuu mawili: damu ya mnyama asiye mwanadamu na damu ya mtu. Kafara ya damu ya mtu hutolewa kwa njia za kishirikina. Mtu aliyetolewa kafara anaweza kufa kifo cha kawaida kabisa kama vifo vingine, lakini kiukweli anakuwa ametolewa kafara kishirikina. Kwa mfano mtu anaweza kuugua ghafla, au kupata ajali nk. Wakati mwingine kafara aina hii inaweza kuhusisha kundi kubwa la watu. Mara nyingi hutokea katika ajali nk.

Lakini bado tuna swali la kujiuliza, je, vifo mfululizo vya wasanii wa filamu vilivyotokea mwaka 2014 vimetokana na kafara? Mtaalamu huyu anasema si kweli kuhusu dhana potofu iliyosambaa miongoni mwa jamii kwamba, eti vifo mfululizo vya wasanii wa filamu vilitokana na kafara inayofanywa na watu waliomo ndani ya Tasnia ya Filamu kwa lengo wanalolijua.

Hata wataalam wengine waliobobea katika masuala ya “ulimwengu usioonekana”, wamebainisha kuwa vifo mfululizo vya wasanii waliofariki mwaka 2014 havikutokana na kafara kwa sababu haviendani na “sifa ya kafara inayolenga watu waliopo katika jamii moja kama vile wanafunzi katika shule ama chuo fulani, wanafamilia fulani ama wana ukoo fulani!”

Kafara inayowalenga watu waliopo katika jamii moja, huwa na sifa zifuatazo: kwanza aina za vifo hufanana. Kama ni wanafunzi ama wanafamilia ama wanaukoo ama wafanyakazi wa kampuni au taasisi fulani, basi wote watakuwa wanakufa vifo vya aina moja. Vifo hivyo vinaweza kuwa kufa kwa ajali ya aina moja tena katika mazingira yanayofanana, au kuanguka chooni, au kufa kwa kuugua kichwa nk.

Hivyo, ukiangalia vifo vya wasanii vimetofautiana, Adam Kuambiana alikuwa anasumbuliwa na kisukari na vidonda vya tumbo kwa muda mrefu, Recho Haule alifariki wakati akijifungua, George Otieno “Tyson” alifariki kwa ajali ya gari, na Mzee Small alikuwa akisumbuliwa na kiharusi. Hivyo, kwa mujibu wa wataalam wa masuala ya kafara wanabainisha kuwa vifo hivi haviwezi kuwa vimetokana na kafara!

Pili; aina ya watu wanaofariki kwa sababu ya kafara hufanana, hii inamaanisha kuwa vifo huwalenga waliopo kwenye kundi moja na huwa na sifa zinazofanana na kushabihiana Inaweza ikawa ni wanawake tu au ikawa ni wanaume tu. Kwa mfano kama kafara imewalenga wanafunzi wa shule fulani, basi watakaokufa lazima watakuwa wa jinsia moja na vifo vyao vitafanana sana.

Ikitokea wamekufa wanafunzi, basi huwa ni wanafunzi tu, haiwezi kuwalenga na walimu kwa wakati mmoja. Kama ni kwenye shule ya watu wa jinsia moja, basi wahanga watakuwa ni watu wenye sifa zinazofanana, kwa mfano wanaweza kuwa viranja tu, au mamonita wa madarasa tu.

Hivyo, kwa sababu hiyo, vifo vya wasanii haviwezi kuwa vimetokana na kafara, kwa sababu walio fariki hawana sifa zinazofanana na kushabihiana hata kidogo. Licha ya kwamba wanatoka katika jinsia tofauti lakini pia walikuwa na majukumu tofauti katika tasnia ya filamu. Kama ingekuwa ni kafara lazima ingelenga watu ambao roles zao katika filamu zinaendana, kwa mfano waongozaji wa filamu, watayarishaji, waigizaji nk!

Tatu; mazingira ya vifo vya kafara hufanana. Hii maana yake kuwa vifo vya kafara iliyolenga watu walio katika tasnia moja au jamii moja hufanana na kushabihiana kwa asilimia mia moja. Sasa hapa ukitazama mazingira ya vifo vya mfululizo vya wasanii waliofariki mwaka 2014 hawa hayafanani wala kushabihiana kwa lolote lile. Kwa kuwa tarehe za vifo huwa na alama au utata wa kinyota unaofanana na kushabihiana kwa kiasi kikubwa sana: Hebu tazama tarehe za vifo vya wasanii hawa wanne wa filamu.

Katika uchambuzi na hesabu za kinyota, ukitaka kujua kama vifo vya wasanii hawa vimetokana na kafara unaweza kuangalia mifano hii inayobainishwa na wataalam wa masuala ya kafara. Marehemu Adam Kuambiana ambaye alifariki alfajiri ya tarehe 17/05/2014, hivyo kwa kubainisha hesabu za kinyota, chukua 17 ambayo ndiyo tarehe aliyofariki Adam kisha jumlisha 05 ambao ndiyo mwezi aliofariki. Hesabu itakuwa kama ifuatavyo: 1+7+0+5=13. Kwa kuwa jibu linatakiwa liwe kati ya 1 hadi 9, jumlisha 1 na 3 ambapo jibu lake litakuwa ni 4.

Rachel Haule alifariki usiku wa kuamkia tarehe 27-05-2014. Kwa hesabu za kinyota, tarehe 26 mwezi wa 05: 2+7+0+5=14. Hivyo, 14 =1+4 = 5. George Tyson alifariki tarehe 31-05-2014. Kwa hesabu za kinyota, tarehe 31 mwezi wa 05: 3+1+0+5 = 9. Na Mzee Small alifariki usiku wa tarehe 7 mwezi wa 06: Kwa hesabu za kinyota 7+0+6=13. Hivyo 1+3=4.

Ukiangalia namba hizi utagundua kuwa kama wangekuwa wametolewa kafara basi kungekuwa na utata wa kinyota unaofanana sana. Namba za mwisho lazima zote zingefanana.

Kwanini lazima kuwe na ufanano? Jibu ni moja tu, nalo ni kwa sababu mauaji ya kishirikina hufanywa na kitu kimoja kwa sababu moja. Kila mzimu, pepo au muungu huwa una njia zake na namna zake za kufanya mambo yake. Kila roho itendayo kazi kishirikina huwa na mipaka yake ya utendaji kazi. Kwa mfano, mzimu fulani unaweza kuwa na uwezo wa kuwasaidia watu matatizo ya uzazi lakini watu hao lazima wawe wanawake au wanaume tu.

Mzimu au pepo fulani linaweza kuwa na uwezo wa kuua watu lakini ili watu hao wauawe ni lazima wawe ndani ya maji kama mtoni, baharini au ziwani, au ni lazima wawe chooni, nje na maeneo hayo mzimu huo unakuwa hauna nguvu. Mzimu fulani unaweza kuwa na uwezo wa kuua biashara fulani, lakini ni lazima ufilisi biashara hiyo kwa njia ya ajali ya moto au chumaulete nk.

Hivyo, mzimu huo unapokuwa katika kutimiza lengo la kutoa kafara za watu walio katika jamii moja ni lazima watu hao watakuwa wenye sifa zinazofanana, na vifo vyao vitakuwa vya aina moja.

Vifo vilivyotokea mfululizo vya wasanii Adam Kuambiana, Rachel Haule na George Tyson na Mzee Small havikutokana na kafara. Ni vifo vya kawaida kama vifo vingine, ilitokea tu kama “coincidence” kwa vifo vinavyowahusu watu maarufu na ambao wapo katika tasnia moja. Wasanii wasimtafute mchawi. Waendelee kulisukuma mbele gudurudumu la tasnia ya filamu ambalo limeendelea kutengeneza maelfu ya ajira kwa vijana nchini Tanzania.

No comments: