Jul 18, 2015

Buhari kuipiga jeki sekta ya filamu NIgeria

Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari

Rais mpya wa Nigeria, Muhammadu Buhari, ameendeleza kile kilichoanzishwa na mtangulizi wake, Goodluck Jonathan, katika kusaidia sekta ya filamu kwa kuapa kuhakikisha anasaidia sekta ya filamu nchini humo kutoanguka kutokana na uharamia wa kazi.

Alisema kuwa sekta ya filamu ya Nollywood inafanya vizuri ila inaweza kuathiriwa na uharamia. Sekta hii ina thamani ya dola bilioni 5 (sawa na paundi bilioni 3), lakini watengeneza filamu bado wanasota kutengeneza faida  kwa sababu ya uharamia.Japo ni sinema zinazotengenezwa kwa bajeti ndogo, visa vya mapenzi, mikasa, usaliti na uchawi ni mambo ambayo yameenea zaidi barani Afrika. Rais Buhari aliagiza taasisi za ulinzi kuwatambua wale wote wanaojiingiza kwenye uharamia wa hakimiliki na kuwafikisha kwenye mikono ya sheria.

Nollywood si sekta pekee inayoathirika na tatizo hili. Mtayarishaji wa Kannywood – sekta ya filamu za lugha ya Kihausa zinazotengenezwa katika jiji la kaskazini la Kano – pia analalamika na amemuomba Rais kuingilia kati.

Rais Buhari amesema atafanya kila awezalo kuilinda sekta ya burudani ya nchi hiyo. “Wameijenga (watayarishaji wa filamu) sekta kwa jasho lao,” alisema. “Tuna dhima ya kuhakikisha tunawaunga mkono.”

Wachambuzi wa sekta ya filamu ya Nigeria wanaamini kwamba Nollywood inatoa sinema 50 kwa wiki. Hata hivyo, nyingi ya sinema hizi zinauzwa moja kwa moja kwenye DVD na watengenezaji bado wanasota kutengeneza faida.


No comments: