Jul 7, 2015

Mabanda ya Video: Tutazame upande wa pili wa shilingi

Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Bi. Joyce Fissoo

Mjumbe wa Bodi ya Filamu, Dk. Vicensia Shule (kushoto), akizungumza katika kikao na wafanyakazi wa kampuni ya usambazaji ya Proin Promotion. Katikati ni Bishop Hiluka na kulia ni Mzee Silvester Sengerema (Kaimu Mwenyekiti Bodi ya Filamu)

INGAWA nchini Tanzania televisheni imekuwapo tangu mwaka 1973 (Zanzibar), Tanzania Bara televisheni imeanza mwanzoni mwa miaka ya 1990. Hadi 1996 kulikuwa na vituo vitatu tu vya televisheni: CTN, DTV na ITV. Kupingwa kwa televisheni Tanzania Bara na kuwapo kwa Radio moja (RTD) tokea miaka ya baada ya uhuru ulikuwa mkakati wa serikali kujenga utamaduni wa Umoja, Udugu na Utanzania.

Enzi hizo (nilikuwa bado mdogo) watu walikuwa wanakwenda kwenye majumba maalum ya sinema kuangalia sinema kwa wakati maalum na masharti maalum. Majumba haya yalikuwepo katika kila mji-makao makuu ya mkoa na baadaye katika wilaya, na idadi yake ilitegemea ukubwa wa mji.

Dar es Salaam kulikuwa na majumba kama Drive Inn (sasa kuna Ubalozi wa Marekani – hili lilikuwa ni eneo la watu matajiri zaidi, waliruhusiwa kuingia na magari yao kwenye ukumbi, watu wakikaa ndani ya magari na kuangalia filamu huku wakiburudika na vinywaji), Odeon (sasa kuna DTV/Channel Ten), New Chox (sasa kuna Continental Hotel), Empire (nadhani kuna makao makuu ya NMB), Avalon (lilianza kutumika na madhehebu ya kilokole kufanyia ibada zao, na sasa ni eneo la ofisi mbalimbali), Empress (zipo ofisi za BMT), na Cameo (sina uhakika linatumika kufanya nini kwa sasa).

Baadaye likaibuka jumba la Starlight (kuna hoteli ya Starlight), lililokuwa na uwezo wa kuingiza watu wengi sana. Na walalahoi pia walikuwa na mahali pa kwenda kutazama sinema, Amana Social Hall, eneo la Ilala. Nakumbuka pale Drive Inn, ilikuwa kama huna pesa ya kuingilia, basi unaangalia sinema bubu – kwani mnalazimika kukaa nje na kutazama sinema kwa mbali lakini hamsikii sauti.

Tanga kulikuwa na Majestic, Novelty, Regal na Tanga Cinema. Mwanza kulikuwa na Liberty na Tivoli, Mji Kasoro Bahari kulikuwa na Shani na baadaye ikaja Sapna. Arusha ilikuwepo Metropolitan. Vivyo hivyo na miji mingine.

Enzi hizo, nakumbuka kulikuwa na mabingwa wa kusimulia sinema hata kama mliiona wote, basi mtaanza kusimuliana tena na tena, hata kama kimombo hukijui, utasimulia yote waliyokuwa wanasema kwenye hiyo sinema. Wakati wa sinema yenyewe watu watapiga makelele, “angalia nyuma wewe… Jamaa anataka kukuua!” Au pale Drive In kwa nje, jamaa anakusimulia utadhani anasikia vile!

Ilikuwa raha mstarehe, enzi hizo tukiwa wadogo basi ikatokea kama kuna sinema maarufu mjini wenzako wanaweza kukusimulia mwanzo hadi mwisho bila kukosea (na kuongezea chumvi kidogo) ingawa hawajaiona ila wamesimuliwa. Ama kweli siku hazigandi!

Kwa sasa ukiwaona watu (hasa Dar es Salaam) wakiingia kuangalia sinema pale Century Cinemax–Mlimani City, Cineplex–Quality Centre, au Century Cinemax–Oyster Bay, unaweza kudhani kuwa huu ni utamaduni mpya. Kumbe kabla na baada ya Uhuru kwenda Sinema ilikuwa ni jambo la kawaida na kitu kilichoweza kukuletea mapenzi na heshima kubwa kwa familia yako, rafiki au mpenzi wako, kwa wakati ule.

Hivi sasa katika ulimwengu huu wa utandawazi na soko huria, hasa baada ya ujio wa televisheni nchini, majumba ya sinema yamefungwa kutokana na kukosa wateja – sijui nani kasema mkiwa na televisheni nyumbani basi majumba ya sinema si muhimu? Badala yake majumba ya sinema yamehamia kwenye nyumba zetu na vichochoroni kulikochipuka mabanda ya kuonesha video kama uyoga ambayo siyo rasmi.

Mabanda ya video (maaruf vibanda-hasara) yamechukua nafasi ya majumba rasmi ya sinema yaliyofungwa au kugeuzwa kuwa ya kufanyia huduma nyingine za kijamii. Mabanda haya mengi yamejengwa kwa mabati, mbao au mifuko ya sandarusi na kukosa mvuto, yamekuwa mbadala wa kuonesha sinema zikiwemo zile chafu maaruf kama ‘Pilau’, ‘Kachumbari’, ‘Kuchikuchi Hotae’, ‘Yale mambo yetu’, ‘Picha la ukweli’, ‘Ubwabwa’ na majina mengine ambayo kwa mtu wa kawaida si rahisi kujua maana yake.

Mabanda haya (mengi hayastahili kuitwa Kumbi za video) yana ukubwa tofauti kutegemeana na sehemu lilipo, lakini yenye kuingiza watu 20 hadi 50 kwa wakati mmoja wanaojazana kuangalia sinema. Hutoza kiasi cha shilingi 200 hadi 500 kwa onesho. Baadhi huonesha hadi maonesho 10 kwa siku.

Tafiti zinaonesha kuwa asilimia 60 ya wakazi wanaoishi mijini na vijijini wanapenda kuangalia filamu kwenye kumbi za maonesho – ikiwemo mabanda ya video – ingawa wengi wao, wanawakatishwa tamaa na kutokuwepo kwa miundombinu sahihi. Takwimu ya waangaliaji sinema inatofautishwa kulingana na umri: Asilimia 50 ya watazamaji hawa ni wenye umri kati ya miaka 6-24, asilimia 30 ni wenye umri kati ya miaka 25-34, asilimia 15 ni watu wenye umri wa miaka 35-49 na asilimia 5 tu ya watu wenye umri zaidi ya miaka 50 ndiyo hupenda kuangalia filamu hizi.

Dar es Salaam ndiyo mji unaoongoza kuwa na idadi kubwa ya watazamaji wa filamu ikichukua asilimia 35. Hata hivyo, vijana wadogo ndiyo wenye mazoea ya kwenda kwenye kumbi za video kuangalia sinema.

Kumbi za video zinawavutia vijana wengi hasa wa vijijini. Filamu za mapigano na mara nyingine hata za ngono (Blue films) zinaoneshwa kwa viingilio vya bei rahisi kwenye kumbi/mabanda yaliyopo sehemu za vijiweni karibia kila kitongoji.

Mwaka 2010 Serikali ilipiga marufuku uoneshaji wa sinema kwenye mabanda ambayo hayajakidhi vigezo vinavyotakiwa kisheria. Kwa mujibu wa Kanuni za Sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza za Mwaka 2011, Sehemu ya V, kanuni imetamka wazi kabisa masharti ambayo yanatakiwa kutekelezwa ili mtu aweze kuonesha na kujenga mahali pa kuonesha sinema.

Kwa kuwa kuna uhitaji mkubwa wa watu kutaka kuangalia sinema (na hapa ndipo panapoonekana umuhimu wa kurejeshwa kwa vituo vya kijamii “Community Centres” ili kuwezesha wananchi wote nchini kujumuika pamoja na kuweza kupata habari), hali hii inawafanya wamiliki wa kumbi/mabanda ya video kufanya shughuli zao kwa njia za wizi, wakiwa hawana leseni na wala hawaingizi pato lolote kwa Taifa. Wazazi wengi wanakerwa na jambo hili na kuilalamikia Serikali kwa kushindwa kuyafunga mabanda haya.

Hali hii imewafanya baadhi ya mgambo wa halmashauri na askari kuyatumia mabanda haya kama sehemu ya kujipatia kipato, kwani huwakamata waoneshaji video na kuwatisha ili wapatiwe “kitu kidogo”. Kumekuwepo uadui kati ya waendeshaji wa mabanda haya na serikali kwa upande mmoja, na waendeshaji wa mabanda na jamii kwa upande mwingine.

Tupende tusipende, mabanda haya yapo na yataendelea kuwepo, hakuna nanma ya kuyaondosha kabisa. Dawa si kuyapiga marufuku, bali kutafuta njia nzuri ya kuyarasimisha (kwa yale yatakayokidhi vigezo vinavyokubalika), ili yaweze kuchangia pato la Taifa, na pia yatumike kama mtandao wa usambazaji (maonesho ya sinema) kabla hazijatolewa rasmi kwa matumizi ya nyumbani.

Kwa wenzetu, usambazaji filamu huanzia kwenye “Box Office” – uoneshaji wa sinema ndani ya kumbi za sinema – na baadaye hurushwa kwenye vituo vya televisheni za kulipia, kwenye mtandao wa internet, kisha katika televisheni za umma, na hatimaye kutolewa kama bidhaa rasmi (DVDs) kwa matumizi ya nyumbani.

Ili kupitia mchakato hapo juu Serikali (kupitia Bodi ya Filamu) inaangalia namna ya kuyarasimisha mabanda haya – yatakayokuwa yameboreshwa na kukidhi vigezo – ili yatumike kama “box office” zetu (sehemu ya maonesho/uzinduzi wa sinema). Hii itaongeza kipato kwa wasanii wetu, na hata kupunguza uchafu huu tunaoushuhudia sasa wa mabanda kutumika kama sehemu ya maficho ya vibaka na upotoshaji badala ya kuelimisha.

Kwa kuwatumia Maafisa Utamaduni wa Wilaya na Manispaa, kupitia Wizara ya Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), tutaweza kupata takwimu sahihi za idadi ya mabanda, kuyakagua na kuyapa leseni yale yote yatakayokidhi vigezo, jambo litakalosaidia pia kuongeza ajira, pato la wasanii na Taifa, na hata kupunguza uhalifu, kwani yatatumika kisheria kuliko ilivyo sasa.

Hatuna tena muda wa kulalamikia mabanda bali tuchukue hatua stahiki, mahitaji ya kumbi za video yameonekana si kwa mijini tu hata vijijini, licha ya kuwepo kwa utandawazi lakini kuna baadhi ya jamii na hasa za vijijini bado hazipati taarifa sahihi za mambo mbalimbali yanayoendelea katika ulimwengu huu. Hii inatokana na njia zinazotumika kutowafikia wengi kama inavyodhaniwa na hivyo bado kuna haja ya kurasimishwa na kurejeshwa vituo vya kupashana habari kama ilivyokuwa zamani.

Miaka ya nyuma, nakumbuka kulikuwa na siku na sehemu maalum, hasa vijijini, watu walikuwa wanakutana na kuangalia sinema mbalimbali ambazo zilikuwa maalum kwa kufikisha ujumbe fulani kwa jamii. Lakini hayo siku hizi hakuna, hivyo, nashukuru kwa Bodi ya Filamu kuliona hili na kuangalia namna nzuri ya kurudisha burudani hizi.


Alamsiki.

No comments: