Aug 26, 2015

Je, tunaweka mipaka kwa watoto kutazama televisheni/filamu?

Watoto wanaangalia televisheni

MAJUZI jirani yangu mmoja (ambaye amenunua kisimbuzi hivi karibuni) aliniita nyumbani kwake na kuniomba nimsaidie kuweka namba za siri (password) kwenye baadhi ya chaneli za televisheni yake ili kuwadhibiti watoto wake wasiweze kuangalia sinema na vipindi visivyo na maadili. Aliamua kufanya hivyo baada ya kugundua uwepo wa chaneli zinazoonesha mambo yenye ukakasi.

Kwa sasa ni jambo la kawaida sana kwa watoto wengi kutazama filamu, televisheni, video, kucheza michezo (games) ya kompyuta, na kutumia Intaneti. Kulingana na makadirio fulani, watoto na vijana hutazama na kuvitumia vyombo vya habari kati ya mara 20 au 30 zaidi ya wakati wanaotumia kufanya mambo na familia zao. Jambo hilo huwafanya watoto wapate habari nyingi zenye kudhuru.


Televisheni huwa kama “mhadithiaji mkuu, mlezi wa watoto na kifaa kinachoathiri maoni ya umma,” inabainisha ripoti ya Not in the Public Interest—Local TV News in America, iliyokusanywa na shirika moja linalochunguza habari huko Marekani.

Televisheni iko kila mahali. Imeenea sana kama moshi wa sigara hewani. Kutazama vipindi vya televisheni kwa muda mrefu bila kuwa mteuzi husababisha madhara kama vile kuvuta moshi wa sigara ulio hewani — hasa watoto.

Kuhusu uhalifu na jeuri kwenye televisheni, ripoti hiyohiyo yasema kwamba “uchunguzi chungu nzima umeonesha kwamba kutazama picha za jeuri huathiri sana kusoma, makuzi na hisia za watoto.”

Katika miaka ya hivi karibuni, watu wamekuwa na maoni mbalimbali kuhusu kuongezeka kwa ngono, jeuri, na lugha chafu katika sinema au televisheni. Mambo hayo ni muhimu kwa wazazi na wote wanaothamini sana viwango vya maadili kuwa na tahadhari nayo.

Mwanadada mmoja aliwahi kulalamika: “Ninapopuuza dhamiri yangu na kurudi kutazama sinema fulani, huwa nahisi vibaya sana. Mimi huona aibu kwa ajili ya wale waliotengeneza sinema hiyo mbovu na kwa ajili yangu mwenyewe kwa kuitazama. Ni kana kwamba kutazama sinema hiyo kumenishushia heshima.”

Ninachowashauri wazazi, hawapaswi kulalamika tu bali kuwapa watoto wao mwanzo mzuri maishani. Tukumbuke pia televisheni inaweza kuwa kifaa kizuri sana cha kujifunzia. Hata hivyo, akili na miili ya watoto inaathiriwa kwa kutumia muda mwingi kutazama televisheni, na hivyo kuwanyima nafasi ya kushiriki utendaji unaowasaidia kuwa wabunifu, kujifunza, na kuchangamana na watu.

Kuna ripoti moja ya uchunguzi baada ya kuchunguza mazoea ya kutazama televisheni ya watoto 2,500, watafiti katika Hospitali moja ya Watoto nchini Marekani walitambua kwamba kadiri watoto walio na umri wa kati ya mwaka mmoja hadi miaka mitatu walivyotazama televisheni sana, ndivyo hatari yao ya kukosa kuwa makini ilivyoongezeka walipofikia umri wa miaka saba.

Watoto hao walikuwa wajeuri kupita kiasi na hawakuwa watulivu na waliweza kukaza fikira kwa muda mfupi tu. Wazazi wengi ambao watoto wao walikuwa na matatizo ya kukaza fikira walitambua kwamba hali hiyo ilibadilika na kuwa nzuri baada ya kuwazuia watoto wao kutazama televisheni.

Kama wazazi tunapaswa kutafuta namna ya kufanya ili kupunguza muda ambao watoto wanatumia kutazama televisheni. Ripoti ya watafiti katika Hospitali ya Watoto inatoa mapendekezo yafuatayo:

Weka mipaka kuhusu ni wakati gani na kwa muda gani watoto wako wanaweza kutazama televisheni kila siku. Epuka kutumia televisheni kuwa mlezi. Badala yake, mhusishe mtoto wako katika kazi nyingi iwezekanavyo za nyumbani. Chagua vipindi ambavyo mtoto wako anaweza kutazama, na uizime televisheni baada ya vipindi hivyo kwisha. Inapowezekana, tazama vipindi ulivyochagua pamoja na mtoto wako na mzungumzie kuhusu mambo mnayotazama. Mwishowe, weka mipaka kuhusu muda ambao wewe mwenyewe unatumia kutazama televisheni.

Hata hivyo, ieleweke kuwa kulalamikia mambo yanayooneshwa katika sinema si jambo jipya. Wakati sinema zilipoanza kutengenezwa, watu walikasirika sana walipoona sinema zilizokazia zaidi mambo ya ngono na uhalifu. Hatimaye, katika miaka ya 1930, sheria ambazo ziliweka mipaka kuhusu mambo ambayo yangeweza kuoneshwa katika sinema zilitungwa nchini Marekani.

Kulingana na machapisho ya The New Encyclop√¶dia Britannica, sheria hizo mpya “zilikandamiza sana, na kuzuia kuoneshwa kwa jambo lolote ambalo linahusiana na mambo ambayo hufanywa na watu wazima. Zilikataza kuoneshwa kwa ‘mambo yoyote ya kimahaba’ na uzinzi, ngono haramu, utongozaji, na ubakaji wala mambo hayo hayakupaswa kutajwa isipokuwa tu iwe ni lazima kabisa kwa sababu yalihusiana na hadithi inayosimuliwa, na waliofanya mambo hayo waadhibiwe kufikia mwisho wa sinema hiyo.”

Kuhusiana na jeuri, filamu “hazikupaswa kuonesha au kuzungumzia silaha zilizokuwa zikitumika wakati huo, kuonesha uhalifu ukitendeka, polisi wakiuawa na wahalifu, ukatili au uchinjaji mwingi, au kuonesha uuaji kimakusudi au kujiua, isipokuwa mambo hayo yawe ya lazima kwa hadithi hiyo. Haikuruhusiwa kuonesha kwamba uhalifu ulifaa chini ya hali zozote zile.” Kwa ufupi, sheria hizo zilisema kwamba “hakuna picha itakayooneshwa ambayo itashusha viwango vya maadili vya wale wanaoitazama.”

Kufikia miaka ya 1950, watayarishaji wengi wa filamu huko Hollywood walikuwa wakipuuza sheria hizo wakihisi kwamba zilikuwa zimepitwa na wakati. Hivyo, mnamo 1968, sheria hizo ziliondolewa na badala yake viwango vya sinema vikawekwa. Hata hapa kwetu tunayo Bodi ya Ukaguzi wa Filamu na Michezo ya Kuigiza, inayoshughulikia viwango na kupanga madaraja ya sinema.

Kwa sababu ya viwango na madaraja hayo, sinema inaweza kuonesha wazi mambo yasiyofaa, lakini inatiwa alama kuwaonya watu kwamba inapaswa kutazamwa tu na “watu wazima.” Lengo kubwa likiwa ni “kuwaonya wazazi ili waweze kuamua sinema ambazo watoto wao wanaweza kutazama na zile ambazo hawapaswi kutazama.”

Nchi nyingi ulimwenguni zina mfumo kama huo ambao alama fulani hutiwa kuonesha sinema fulani inapaswa kutazamwa na watu wa umri fulani. Kwa kuongezea, huenda viwango vya sinema vikatofautiana katika nchi mbalimbali. Huenda sinema inayoonwa kuwa haiwafai vijana katika nchi moja ikaonekana kuwa inafaa katika nchi nyingine.

Katika nchi nyingi, wenye mamlaka hujaribu kuweka sheria na viwango kuhusu umri ambao mtu anaruhusiwa kuona filamu fulani. Hata hivyo, kulingana na ripoti mbalimbali, si nyakati zote ambazo watoto na wazazi huelewa viwango hivyo, au wao huzipuuza. Pia, inajulikana kwamba majumba mengi ya kuoneshea filamu na maktaba za kukodi mikanda ya video hupuuza sheria zilizowekwa kuhusu umri. Isitoshe, programu fulani na filamu hazina viwango vya umri.

Michezo mingi ya video, ya kompyuta, na hata vibonzo vilivyotayarishwa hasa kwa ajili ya watoto, huwa na mambo ambayo yanaweza kudhuru.

Ripoti moja inasema kwamba kila familia “ina wajibu wa kuamua filamu na programu ambazo watoto watatazama.” Lakini swali muhimu la kujiuliza: “Je, sisi watu wazima tuna nia, uwezo, na njia ya kuwalinda watoto kutokana na madhara ya vyombo vya habari?”

Nikiwa mzazi huwa nawajibika kusoma maoni ya wachambuzi au kutazama sehemu ndogo ya sinema ambazo zitaoneshwa kwenye televisheni kabla ya kuwaruhusu watoto wangu kuangalia. Pia hutafuta habari kuhusu sinema hiyo kwenye Intaneti. Na kama nikihisi kwamba sinema hiyo haifai, hutoa sababu kwa watoto kwanini sitaki waangalie sinema hiyo.

Haya yanapaswa kufanywa kwa uwazi na kueleza sababu zitakazowasaidia watoto kuelewa, ieleweke kuwa kama wazazi wakiwakataza watoto wao vitumbuizo fulani na kukosa kuwapa vitumbuizo vinavyofaa, huenda watoto hao wakajaribu kutosheleza tamaa zao kwa siri.


Alamsiki.

No comments: