Sep 9, 2015

Tuache utengenezaji sinema wa kulipuwa


SEKTA YA FILAMU nchini imekuwa inakua kwa kasi na kuwa kimbilio la vijana wengi, hata wale walioshindwa (failures) katika sekta zingine. Ukuaji wake umeambatana na changamoto nyingi katika kufikia ubora unaokubalika kimataifa kwenye filamu zetu.

Filamu ni nguzo muhimu sana ya Utamaduni wa nchi. Filamu zimeibuka kuanzia karne ya ishirini na baadaye kuwa kishawishi kikubwa na mawasiliano ghali katika karne ya ishirini na moja. Hakuna aina nyingine ya sanaa ambayo imesambaa kwa ufanisi na kuonekana kuvuka mipaka ya kiutamaduni katika mataifa mengi kama hii.


Lakini kwa miaka ya karibuni filamu zetu – zilizoanza kututangaza nje ya mipaka yetu – zimeanza kukosa mwelekeo, na zinatupeleka kusikojulikana. Filamu zetu nyingi kwa muda mrefu zimekuwa ni za kulipuwa tu huku hadithi zikiwa si za asili yetu bali tunanakili kwa wenzetu zenye vitendo na maudhui ya jamii za nje!

Watayarishaji wetu wa sinema wanalipua kazi; waigizaji hawalipwi vizuri; utengenezaji sinema unafanywa haraka haraka. Sinema zinatengenezwa kwa wiki moja hadi mbili na zinatolewa ndani ya mwezi mmoja tu. Haraka haraka… Halafu tunataka kujilinganisha na tasnia za filamu zilizoendelea, kama Hollywood, Bollywood nk.

Katika miongo kadhaa iliyopita sinema nyingi zenye mafanikio zimetolewa huko Hollywood. Hilo limekuwa na uvutano mkubwa ulimwenguni pote kwani sinema nyingi za Marekani hutazamwa katika nchi nyingine majuma machache au hata siku chache tu baada ya kuoneshwa kwa mara ya kwanza nchini Marekani.

Sinema fulani hata zimeoneshwa kwa mara ya kwanza tarehe ileile duniani kote. Rais wa usambazaji wa filamu nchini Marekani wa shirika la Warner Brothers, Dan Fellman, anasema: “Soko la ulimwenguni kote la uuzaji wa sinema linazidi kukua nalo linasisimua sana, kwa hiyo tunapotengeneza sinema, huwa tunaitengeneza kwa ajili ya soko la ulimwenguni kote.” Sasa kuliko wakati mwingine wowote, kile kinachotendeka huko Hollywood huathiri biashara ya sinema ulimwenguni.

Lakini kupata faida kutokana na sinema si rahisi kama tunavyodhani. Sinema nyingi zinahitaji kiasi kikubwa mno cha pesa ili kulipia gharama ya kuzitengeneza na kuziuza. Na kufanikiwa kwake kunategemea watazamaji ambao mtu hawezi kutabiri watapendezwa na nini. Huwezi kujua ni lini jambo fulani litawavutia au kuwasisimua watazamaji.

Kwa hiyo watengenezaji wa sinema huongezaje uwezekano wa sinema yao kufanikiwa? Ili kupata jibu, tunahitaji kuelewa mambo machache ya msingi yanayohusika katika utengenezaji wa sinema.

Mara nyingi, matayarisho yanayofanywa kabla ya upigaji picha ndiyo sehemu muhimu zaidi ambayo huchukua muda mrefu katika utengenezaji wa sinema. Kama tu ilivyo na mradi wowote mkubwa, mafanikio yake hutegemea sana matayarisho. Inatumainiwa kwamba pesa zozote zinazotumiwa wakati wa matayarisho zitapunguza sana gharama za kutengeneza sinema yenyewe.

Kutengenezwa kwa sinema huanza na hadithi fulani ambayo huenda ikabuniwa au ikategemea matukio halisi. Mwandishi huandika hadithi hiyo kwenye hati (script). Hati hiyo inaweza kufanyiwa marekebisho mengi kabla ya rasimu ya mwisho kupatikana.

Rasimu hiyo ya mwisho huwa na wahusika pamoja na maelezo mafupi kuhusu kitendo kitakachofanywa. Pia hutoa maagizo mengine kama vile mahali ambapo kamera zitakuwa na mabadiliko yatakayofanywa katika kila onesho.

Hata hivyo, ili sinema iweze kukidhi mahitaji hati hiyo hutegemea inatolewa msimu gani na imekusudiwa kuwalenga watu gani zaidi. Ila watayarishaji wengi hupendezwa hasa na sinema ambayo itawavutia zaidi vijana. Hati inayofaa hata zaidi ni ile itakayowavutia watu wa umri mbalimbali.

Mtayarishaji akiona kwamba hati inaweza kuwa sinema nzuri, huenda akainunua na kumpa muongozaji na mwigizaji maarufu. Kuwa na mwongozaji na mwigizaji maarufu kutafanya sinema hiyo ivutie sana wakati itakapotolewa. Hata katika hatua hii ya kwanza, waongozaji na waigizaji maarufu wanaweza kuwavutia wawekezaji wanaohitajika ili kugharimia utayarishaji wa sinema hiyo.

Hatua nyingine ya matayarisho ni kutengeneza michoro mbalimbali ya filamu hiyo hasa ile inayohusisha mapigano. Michoro hiyo humwongoza mpiga-picha za sinema nayo husaidia kupunguza wakati unaotumiwa kupiga picha. Hakuna jambo baya zaidi kama kupoteza wakati wa kupiga picha kwa sababu tu ya kutojua mahali ambapo kamera inapaswa kuwa.

Kuna mambo mengine mengi muhimu yanayopaswa kushughulikiwa wakati wa matayarisho. Kwa mfano, picha zitapigiwa wapi? Je, itakuwa lazima kusafiri? Je, kuna picha zitakazopigwa ndani ya nyumba, nayo itapambwaje? Je, mavazi maalum yatahitajika? Ni nani atakayeshughulikia mwangaza, kupamba na kutengeneza nywele za waigizaji? Na vipi kuhusu sauti, madoido, na yule atakayeigiza sehemu hatari badala ya mwigizaji mkuu?

Hayo ni baadhi ya mambo yanayohitaji kufikiriwa hata kabla ya kupiga picha za filamu. Ukitazama majina yanayooneshwa mwishoni mwa sinema inayotazamiwa kuleta faida kubwa, huenda ukaona kwamba mamia ya watu walihusika kuitayarisha! Hii inamaanisha kua ni watu wengi sana huhusika katika kutengeneza filamu nzuri.

Kupiga picha za sinema kunaweza kuchukua wakati mwingi, kunaweza kuchosha, na pia kunaweza kugharimu pesa nyingi. Kwa kweli, kupoteza dakika moja tu kunaweza kugharimu maelfu ya dola. Nyakati nyingine inabidi waigizaji, wafanyakazi, na vifaa visafirishwe hadi sehemu ya mbali. Hata hivyo, haidhuru picha hizo zitapigiwa wapi, lazima pesa nyingi sana zitatumika kila siku.

Watu wanaoshughulikia mwangaza, wale watakaowapamba na kuwatengeneza nywele waigizaji huwa kati ya watu wa kwanza kufika mahali ambapo picha zitapigiwa. Kila siku ya kupiga picha, waigizaji wakuu hupambwa kwa saa kadhaa. Kisha picha hupigwa kwa siku nzima.

Mwongozaji husimamia kwa uangalifu kupigwa picha kwa kila onesho. Inaweza kuchukua siku nzima kupiga picha za onesho fupi sana. Picha za maonesho mengi katika sinema hupigwa kwa kutumia kamera moja, kwa hiyo, onesho moja linaweza kupigwa picha kadhaa kutoka pembe tofauti-tofauti.

Isitoshe, huenda onesho lilelile likapigwa picha mara kadhaa ili kupata picha bora zaidi au kurekebisha tatizo la kiufundi. Ikiwa onesho ni refu, huenda picha 50 au zaidi zikapigwa! Kwa kawaida, mwishoni mwa kila siku, mwongozaji huchunguza picha zote na kuamua ni zipi zitakazotumiwa. Kazi ya kupiga picha inaweza kuchukua majuma au hata miezi kadhaa.

Baada ya upigaji picha ndipo hatua ya kuunganisha sinema iliyotengenezwa huanza. Katika hatua hii, picha zilizopigwa huboreshwa na kupangwa zinavyopaswa kufuatana. Kwanza, muziki utakaotumiwa huambatanishwa na sinema hiyo. Kisha, mhariri huunganisha sehemu za sinema hiyo na kufanyiza nakala ya kwanza isiyo kamili.

Madoido ya sauti na picha pia huongezwa katika hatua hiyo. Nyakati nyingine kompyuta hutumiwa kutia madoido hayo katika hatua hii ambayo ni mojawapo ya sehemu ngumu zaidi za utengenezaji wa filamu. Kazi inayofanywa katika hatua hii inaweza kuifanya sinema ivutie na ionekane kuwa halisi.

Muziki uliotungwa hasa kwa ajili ya sinema hiyo huongezwa katika hatua hiyo, na jambo hilo ni muhimu katika filamu za leo. Kwa watengenezaji wa sinema makini hutaka muziki uliotungwa hasa kwa ajili ya sinema, nao hawataki muziki wa dakika ishirini tu au vipindi vifupi vya muziki, bali wao hutaka muziki utakaochezwa kwa muda unaozidi saa nzima.

Nyakati nyingine filamu iliyoboreshwa huoneshwa watu wachache ambao wanaweza kuwa rafiki wa mwongozaji au wafanyakazi wengine ambao hawakuhusika katika kutengeneza filamu hiyo. Ikitegemea jinsi watakavyoitikia, mwongozaji anaweza kupiga picha upya maonesho fulani au kuyaondoa kabisa. Katika visa fulani, umalizio wote wa filamu ulibadilishwa kwa sababu watu walioitazama kwanza hawakuupenda.

Hatimaye, filamu iliyokamilika huoneshwa kwenye majumba ya sinema na kabla kuuzwa kama bidhaa kwa ajili ya kutazama nyumbani (DVD). Ni wakati huo tu ndipo inaweza kujulikana ikiwa sinema hiyo itafanikiwa au haitafanikiwa, au itakuwa ya wastani.

Lakini mambo mengi yanahusika kuliko kupata faida. Sinema kadhaa zikikosa kufanikiwa zinaweza kuharibu sifa ya mwongozaji na matarajio ya mwigizaji kupata kazi.

Kwa watengenezaji wetu wa filamu wanapaswa kujua kuwa watu wanaotafuta sinema, kwa ujumla hawafikirii ikiwa watengenezaji wa sinema hiyo watapoteza kazi zao au la. Wao hujiuliza yafuatayo: Je, nitafurahia sinema hii? Je, inafaa nitumie pesa zangu ili kuitazama? Je, sinema hii itanivutia au itanichukiza? Je, inawafaa watoto wangu? Hivyo, watengenezaji sinema wanapaswa kuwafikiria zaidi wateja wao kuliko kujifikiria wao.


Alamsiki.

No comments: