Oct 21, 2015

WITO KWA WASANII: Kuna maisha hata baada ya uchaguzi

Baadhi ya wasanii wa Filamu wakiwa kwenye uzinduzi wa Kampeni za mgombea Urais wa Chadema anayeungwa mkono na UKAWA, Edward Lowassa
MWAKA HUU ninashuhudia mihemko ya ajabu ya kisiasa kwa wasanii kushabikia siasa na wanasiasa! Kwa mara nyingine tena nashuhudia namna wasanii wa fani mbalimbali wanavyodhihirisha umuhimu wao katika kipindi hiki cha uchaguzi mkuu, wakihusika katika kampeni za vyama, na kwa wagombea wa ngazi tofauti.

Nilipoona mihemko hii nilijiuliza kama kuna manufaa yoyote wanayopata kwa kushiriki kampeni hizi? Jibu likawa, yapo, kwani hiki ni kipindi cha mavuno kwa wasanii.
Baadhi ya wasanii wa filamu wanaomuunga mkono mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli
Hakuna kosa kwa wasanii kushiriki kampeni, wala sioni tatizo msanii kuonesha utashi wake juu ya mgombea fulani, lakini tahadhari ya hali ya juu inahitajika katika hili. Kampeni za mwaka huu zimetawaliwa na matusi na vijembe vya kila aina kuliko kipindi chochote kile, hivyo, msanii yeyote anayejitumbukiza kwenye matumizi ya lugha za matusi, vijembe na maneno ya kifedhuli anaonesha amesahau kuwa kuna maisha baada ya uchaguzi.

Najua kuwa kuna wakati rika fulani huibuka na mihemko inayofanana kwa muda wa wakati wao kushabikia au kuiga na kufanya jambo fulani linalofanana, lakini rika la wakati wao likipita kila kitu hupita kisha huja rika jipya na mihemko yao mipya juu ya kitu kipya.

Nimewahi kusoma machapisho fulani kuhusu falsafa ya mihemko ya uhitaji wa rika, ambapo zaidi ya asilimia 60 ya kada hiyo hushabikia kitu cha aina moja, rika hili nalo hupita na huja rika jipya lenye mihemko ya uhitaji wake pia. Ukomo wa rika huja tu pale tabia zenye kufanana miongoni mwa rika hilo huanza kuhama na kila mmoja kufuata njia yake kimawazo na kifikra, hakuna ukomo wa umri katika tabia za uhitaji wa rika.

Mwandishi wa falsafa hii anaandika: “Tukumbuke miaka ya 1998-2006 enzi za kuibuka kwa makundi ya muziki wa kizazi kipya Tanzania kama vile; Kwanza Unit, Salehe Jabir (mwanzilishi wa rap ya Kiswahili), 2 Proud (kwa sasa Sugu, aliyeufanya muziki huu kupiga hatua ya kuanza kuuzwa), Wababe Crak, Gorilla Killers, HBC (Nigga Jay, Terry na Fanani), Diplomats (Saigoni na wenzake) nk.

“…Makundi na wasanii wa muda mrefu kidogo walikuwa na dhamira kubwa ya wazi ya kuona muziki wa kizazi kipya Tanzania unakuwa imara na wenye tija, baadaye kizazi kile cha muziki uliokuwa wa dhamira ya kutengeneza mfumo wa muziki kilipita. Kikaibuka kizazi cha rika la wasanii wa upepo wanaoenda na matukio walioamini si muda wa kuimba matatizo ya jamii bali ni muda wa kuburudika tu na watu wasahau shida zao kwa muda. Miaka hii tunakumbuka kulikuwa na mihemko ya vijana wakiibuka na kufanya muziki wa kizazi kipya (kwa sasa Bongo Fleva).”

Inabainishwa kuwa kwa sasa kila mkoa, kila wilaya, kila kata, kijiji na pengine karibia kila kaya huwezi kukosa mtu anayejiita msanii (wa muziki au filamu), anayesuka nywele bila kujali jinsia yake, anayevaa jeans kwa mtindo wa ‘Kata K’, na hata wanaovuta bangi siyo kwa sababu ya asili yao bali kwa sababu ya mihemko ya kudhania kuwa, kuwa msanii lazima uvute bangi.

Katika kipindi hiki cha kampeni za Uchaguzi Mkuu zinazohitimishwa Jumamosi wiki hii, hali ya vuguvugu la kisiasa limekuwa kubwa katika jamii yetu kiasi kwamba kila mmoja anazungumza kuhusu siasa, hasa upinzani mkubwa uliopo kati ya vyama vinavyounda Ukawa na Chama Cha Mapinduzi.

Kumekuwepo mihemko mikubwa kwa wasanii, ambapo wamegawanyika (au wamegawanywa pasipo kujijua) katika makundi makubwa mawili, kila kundi linaonesha jinsi gani siasa inavyolihusu na linavutia upande wake kwa nguvu zote. Bahati mbaya, wasanii hawa wameamua kuonesha tofauti zao katika hali ya uadui, kwa sababu tu wana mitazamo tofauti!

Hili ni kosa kwa sababu katika siasa, hatuwezi kufanana, lazima tutofautiane na ndiyo maana halisi ya vyama vingi. Hata hivyo, hali hii haiwezi kupita pasipo kuisemea kwani siasa, hasa wakati kama huu ambao nchi yetu bado haikupata kushuhudia mihemko, ushabiki, upinzani na tambo za aina hii baina ya vyama kama ilivyo hivi sasa.

Uadui wa waziwazi umejitokeza na ulianza baada ya baadhi ya wasanii kugomea kuhudhuria ile hafla ya kuagana na Rais Jakaya Kikwete katika Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam, ambayo pia ilikusudia kumuunga mkono mgombea wa CCM, Dk. John Magufuli.

Baadaye akina mama wafuasi wa Chadema walifanya mkutano wao wa ndani katika Jengo la Millennium Towers, Kijitonyama jijini Dar es Salaam, tukio ambalo mgeni rasmi alikuwa Edward Lowassa. Mkutano huu ulihudhuriwa na wasanii kadhaa wa filamu na muziki.

Baadhi ya wasanii wa filamu waliohudhuria tukio hilo ni, Chuchu Hans, Jacqueline Wolper, Aunt Ezekiel, Shamsa Ford na wengineo, ambao walijipambanua kuwa wao ni ‘Ukawa damu’. Siku chache baadaye CCM nao walifanya kitu kama hicho, kilichopewa jina la ‘Mama Ongea na Mwanao’, katika Hoteli ya Hyatt Regency Kempinski, ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais Jakaya Kikwete. Kama ilivyokuwa kwa Chadema, huku nako waigizaji wa filamu walikuwepo na kutangaza ukereketwa wao.

Lakini kwenye hafla ya ‘Mama Ongea na Mwanao’, Chuchu Hans alikuwepo kuthibitisha yeye ni chama tawala, kitendo kilichosababisha kutupiana maneno ya kejeli na wenzake aliowaacha Ukawa.

Baadaye tukasikia tetesi kuwa kuna vitisho na harakati za chini kwa chini zinazoongozwa na mmiliki mmoja wa chombo cha habari anayesimamia wasanii, kuhakikisha wasanii walio upande wa Ukawa hawapati fursa zozote za kisanii kama njia ya kuwakomoa!

Sina uhakika kama ni matunda ya harakati hizo au ni mapenzi tu vilivyowafanya kina Vincent Kigosi (Ray), Anti Ezekiel, Juma Nature na wengineo kuamua kujiengua Ukawa na kurudi CCM wakidai kuwa kule walikokuwa awali hakujakidhi vigezo vyao, ingawa kuna hisia kuwa huenda walipata ushawishi wa ziada kuweza kuhama chama ndani ya muda mfupi tu.

Ama kweli ‘siasa inaweza kuwa mchezo mchafu’, muda mfupi tu unaweza kubadili kila kitu. Unaweza kuona kitu kidogo, lakini kuna watu wengi wamepoteza maisha yao kwa sababu ya siasa, hasa unapokuwa mtu mwenye wafuasi kama ilivyo kwa wasanii hawa wenye mihemko na wanaowekeana uadui kwa sasa. Huu ni mchezo hatari hasa kwa wakati huu! Wasanii hawa wanatumika na kusahau kuwa mambo haya mwisho wake ni Jumapili.

Wasanii wanapaswa kujua kuwa wana mashabiki kutoka pande zote, kwa kila chama, kwa kila mgombea na hivyo wanastahili kuhakikisha hawapotezi mashabiki wao kwa kujiingiza katika mihemko na kampeni chafu. Ingawa wapo wasanii wanaoona msimu wa kampeni ndiyo msimu wa kutoka kimaisha na hivyo wako tayari kujilipua kwa aina yoyote ile ili mradi wapate dili za kushiriki kampeni.

Ni vema aina hii ya wasanii wakajua kuwa kuna maisha baada ya uchaguzi na kwamba baada ya hapo watalazimika kurejea tena kwa wateja wao ambao ni wapiga kura. Kumtusi mgombea au chama ni sawa na kumtusi mfuasi wa mgombea au mfuasi wa chama, kitakachofuata baada ya hapo ni chuki itakayodumu milele.

Tunaweza kufanya utani katika masuala mengine lakini siyo siasa, hasa kama hizi za kwetu ambazo tunaambiwa zimejaa matumizi makubwa ya fedha kutoka kwa wanasiasa. Watu wamewekeza na wapo katika hatua za mwisho kuona zinawasaidia kufikia malengo yao.

Uadui wa wasanii umekuwa mkubwa kiasi cha wengine kujikuta wakiambulia matusi mazito kutoka kwa wenzao, kisa kikiwa ni kuonesha mapenzi yao kwa mgombea fulani wa urais, kama ilivyotokea kwa Jacqueline Wolper, aliyeporomoshewa matusi mazito na msanii mwenzake, Isabela Mpanda, kisa mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa.

Inasemekana matusi hayo yalimnyima raha Wolper, kiasi cha kujuta kuonesha mapenzi yake kwa Lowassa. Najua kuwa si dhambi mtu kuwa na upande, tena unaofahamika. Ni afadhali mtu akakuchukia lakini ukawa na msimamo wako, kwa sababu kutofautiana katika siasa ni jambo lililo wazi. Watu wote hatuwezi kuwa na itikadi moja.

Katika siasa za sasa za dunia yote, wala siyo Tanzania tu, mihemko ya uhitaji wa rika imetia fora. Lakini wasanii wanapaswa wajitambue na wasisukumwe na mihemko hii, japo ni mizuri endapo wataitumia vizuri, wakadumu nayo kwa ari waliyonayo kwa mwelekeo wenye dira na ndoto sahihi kwa Taifa letu.

Lakini sidhani kama wasanii wana dira zaidi ya mihemko na tamaa ya pesa. Wanadhani siasa ni burudani kama ilivyokuwa sanaa, na kusahau kuwa siasa ni zaidi ya mfumo wa kutengeneza Taifa imara, hivyo, tutofautiane kifikra, kimtazamo na kiitikadi lakini tusitofautiane kwenye lengo kuu.

Wapo wasiojua tofauti ya vyama vya siasa na Taifa au Serikali, hawa wapo tayari hata kupinga Jakaya Kikwete kuitwa Rais, wapo pia wanaodhani tofauti ya itikadi ndiyo tofauti ya malengo makuu ya siasa za nchi (wanahitaji kupelekwa shule). Siasa haiko hivyo bali tunasimama leo kwa ajili ya kesho, na siyo kusimama asubuhi ya leo kwa ajili ya jioni ya leo, ‘mobb politics’ huvuma kwa wakati wa rika na huisha rika linapokwisha!


Alamsiki.

No comments: