Dec 23, 2015

Ni vema kufanya utafiti kabla hujawadharau Wasanii

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Moses Nnauye

WIKI iliyopita kwenye gazeti la Raia Mwema kulikuwa na makala yenye kichwa: “Baraza jipya la mawaziri, mkorogo usio hamasa kwa mabadiliko”, kutoka kwa mwandishi ninayemheshimu, Joseph Mihangwa. Nimekuwa msomaji mkubwa wa Mzee Mihangwa (kwangu ni sawa na baba’angu), kwa miaka mingi, nimekuwa msomaji wake na sijawahi kufikiria kumkosoa. Lakini nadhani ameteleza kidogo kwa kubeza juhudi za wasanii wa nchi hii.


Mzee Mihangwa ameandika, nanukuu: “Hakuna sababu ya kuweka neno ‘Wasanii’, je, kwani hao wanatenda chini ya mwavuli wa utamaduni. Kama hivyo, ndivyo tunaweza kusema pia ‘Wizara ya Uvuvi na Wavuvi?; au Wizara ya Madini na Wachimbaji?
Neno ‘Utamaduni’ lazima litazamwe na kufafanuliwa kwa mapana yote. Rais asiyumbishwe kwa kutaka kulipa ‘fadhila’ kwa Wasanii wa mziki wa ‘kizazi kipya’ pekee walioshiriki Kampeni, akasahau ‘Mkurya’ wa ‘Litungu’ na wengine wanaoendeleza kihalisia mila na utamaduni wa kweli wa Mwafrika unaoharibiwa haraka na ‘kizazi kipya’ kufanya Taifa lionekane kama mti usio na mizizi.
Tuone aibu, Wasanii wetu wa ngoma za jadi kugeuzwa watu wa maonesho na makumbusho kwa mapokezi ya wageni mashuhuri viwanja vya ndege pekee (airport culture) Wasanii hao hutelekezwa ambapo mara tu msafara wa wageni na wenyeji wao unapoanza kuelekea mjini, na zana zao za kisanii, wamesahaulika wakihaha ‘na mimi naomba lifti’ wala wasisikilizwe.
Wizara hii ibakie ya ‘Habari, Utamaduni wa Taifa na Michezo’. Hatuna budi ya kupromoti tamaduni za watu wengine; lazima tutazame nyuma ili kuweza kwenda mbele kwa uhakika…” Mwisho wa kunukuu.

Ukisoma kwa umakini makala ya Mzee Mihangwa, utagundua kuwepo kwa mambo makuu mawili: ukosefu wa taarifa na kuongelea jambo asilolijua bila utafiti. Mwandishi anataka kuturudisha kwenye ile kasumba ya kuendelea kuitambua Sekta ya Sanaa kama sehemu ya Utamaduni (kwa ajili ya kujiburudisha) badala ya kuitazama kibiashara na chanzo muhimu cha kiuchumi (new sector with economic potential). Sanaa ni biashara, lakini Utamaduni hauruhusu biashara.

Wasanii si kundi la kubezwa, hili ni kundi kubwa sana. Kwa mujibu wa utafiti wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) wa mwaka 2006, kulikuwa na wasanii milioni 6. Kwa vyovyote sasa idadi imeongezeka mara dufu hasa ikizingatiwa kuwa teknolojia imekua na asilimia 60 ya Watanzania ni vijana. Kwa takwimu hizi ni wazi wasanii ni kundi kubwa sana linalozidiwa na kundi moja tu la wakulima na linachangia uwepo wa ajira kwa vijana wengi.

Tukizungumzia wasanii tunamaanisha wote wanaofanya kazi za sanaa na ubunifu (filamu, muziki, sanaa za maonesho na za ufundi), na si kama mwandishi anavyodai (ingawa asichojua ni kuwa hata wasanii wengine wakiwemo wa filamu walishiriki kikamilifu kwenye kampeni). Sanaa kwa sasa ni biashara kubwa ambayo ripoti ya Shirika la Hakimiliki la Kidunia (WIPO) ya mwaka 2012 inaonesha kuwa mchango wa mapato nchini uliotokana na shughuli za Sanaa ni zaidi ya mchango wa Sekta ya Madini.

Pia mchango wa ajira katika kazi Sanaa ni zaidi ya madini, umeme, gesi, maji, usafirishaji, mawasiliano, ujenzi, afya, na ustawi wa jamii. Pia wasanii ndiyo wamekuwa wakilipa jina na utambulisho Taifa hili. Kwa mujibu wa utafiti wa WIPO, Sekta ya Sanaa inachangia kwenye pato la Taifa kwa asilimia 4.275.

Mwandishi alipaswa kwanza kuielewa Idara ya Utamaduni anayoipigania kabla hajaandika lolote kuhusu wasanii. Nilidhani angebainisha kuhusu mkanganyiko uliopo wa Maafisa Utamaduni kuwajibika katika Wizara inayohusika na TAMISEMI, badala ya Wizara mama inayobeba Idara ya Maendeleo ya Utamaduni, jambo linalofanya shughuli za pamoja za Kitaifa zinazohusu Utamaduni kuwa ngumu kuzifanya.

Ndiyo maana hata yale Mashindano ya Kitaifa ya kazi za Sanaa hayasikiki tena, hata shughuli zinazohusika na maslahi ya pamoja ya Wasanii kama vile ulinzi wa haki za wasanii (Hakimiliki) umekuwa wa shaghalabaghala, maana hakuna ajenda ya pamoja kwa viongozi hawa wanaotegemewa kuwa karibu kabisa na wasanii.

Sekta ya Sanaa kwa sasa imeporomoka kwa kasi ya ajabu, nguvu kubwa lazima iwekezwe (kama alivyofanya Rais Dk. Magufuli kwa kuipa Sanaa Idara yake kamili badala ya kuiacha kwenye Utamaduni) ili kuhakikisha inakua na kuwa chanzo kikubwa cha ajira na mapato miongoni mwa Watanzania, ikiwa ni pamoja na kulitambulisha taifa katika ngazi mbalimbali za kimataifa.

Miaka ya nyuma Maafisa Utamaduni walikuwa kimbilio la wasanii, waliweza kutafuta vifaa vya muziki kwa wanamuziki, kutafuta maeneo ya kufanyia mazoezi kwa wasanii wasio na nafasi. Hata yale majumba yaliyojengwa karibu kila wilaya maarufu kama ‘Community Centres’ yalikuwa chini ya Maafisa Utamaduni na kuwa mahala ambapo serikali ilipajenga maalum kwa ajili ya shughuli za sanaa.

Community Centres hazipo tena baada ya kugeuzwa aidha kuwa ofisi za Manisipaa au kukodishwa kwa watu binafsi kuongeza pato la Serikali za Mitaa bila kujali vijana waliomo katika Manispaa wanapewa sehemu maalum kufanya shuguli zao za Sanaa. Kukosekana kwa Community Centres na mkanganyiko uliopo ni mambo ambayo yamedidimiza sanaa nchini. Pia ukiangalia Bajeti ya TAMISEMI unajiuliza ni asilimia ngapi ya bajeti hiyo huenda katika shughuli za Utamaduni/Sanaa?

Sekta ya Sanaa ikiendelezwa vizuri ni chanzo kikubwa cha ajira kwa vijana, njia madhubuti ya kukuza utalii na uchumi wa Taifa na wa wananchi kwa ujumla. Sekta ya Sanaa inapotumika vizuri, hufanya kazi kama mhimili huru unaosimamia dola. Katika nchi ambayo Bunge linakosa meno dhidi ya udhaifu wa Serikali, vyombo vya habari navyo vikawa kimya, sekta hii inaweza kuwa nyenzo imara zaidi ya kuwasiliana na jamii na kuieleza jinsi mambo yasivyo sawa. Lakini pia sekta hii ina nguvu kubwa na chanzo kizuri cha kupashana taarifa.

Ni kwa kuwa hatuiangalii sekta hii kwa jicho la tatu. Kuna uchumi mkubwa sana ndani ya Sanaa. Ni vigumu kuuona au hata kuufikia kama tutaichukulia kuwa ni utamaduni au burudani tu. Ni wakati mwafaka sasa itambulike kuwa sanaa ni fedha, ni uchumi, na pia ni tiba yenye njia nyingi. Kwa mfano, Wasanii wa Ufilipino waliwahi kuitibu jamii iliyokumbwa na mafuriko nchini humo na kufanikiwa kwa kiwango kikubwa. Pia jamii ilipona majeraha ya dhiki baada ya mapinduzi mwanzoni mwa miaka ya 2000 kupitia wasanii.

Sanaa pia inatosha kuwa mkombozi wa bajeti za serikali na kutoa mchango wa thamani katika Pato la Ndani la Taifa (GDP) na jumla katika Pato la Taifa (GNP). Biashara ya Sanaa inaposhika nafasi stahiki na kujaa kwenye mifereji yake inaweza kuchangamsha ubunifu kwa watu na kufanikisha kutengeneza ajira, badala ya kufikiria kuajiriwa tu. Mafanikio hasi ya wasanii wa Tanzania, ni sababu ya vipaji vingi kupotea.

Watu wanashindwa kufikiria na kubuni njia ya kutengeneza fedha kupitia sanaa kwa sababu ya kuona jinsi wasanii wanavyoishi kwa taabu. Inahitaji mtu mwenye akili ya uthubutu kama mwendawazimu, ndiye anaweza kuona Sanaa hailipi na imewapotezea dira wengi, kisha naye aifanye kwa kuamini itampa mafanikio.

Ni ndoto ya kila mtu kuwa na maisha mazuri, kwa hiyo watu huangalia maeneo ambayo yanalipa. Mathalan, huko nyuma ilikuwa ndoto ya kila mtoto kuwa daktari, injinia na rubani kwa sababu ilionekana ndiyo mafanikio yanayotazamika na kupigiwa mfano. Siku hizi, vijana wengi wanatamani kuwa wanasiasa au maofisa wa TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania).

Pia mwaka huu tumeshuhudia vijana zaidi ya 70,000, kwenda kufanyiwa usaili Idara ya Uhamiaji. Hiyo ni kuonesha namna gani ajira zilivyo ngumu. Ukweli ni kwamba katika idadi hiyo, wapo wengi wenye vipaji lakini ni ngumu kuvionesha wala kuvitumia kwa mfumo uliopo.

Laiti mwandishi huyo angejua thamani ya Sanaa, angetamani kuona kila msanii mwenye kipaji na aliye na jitihada za kufanikiwa, anafanikiwa na kutengeneza fedha ili kurahisisha mirija mingi ya uchumi kupata mtiririko wenye afya. Sekta ya Sanaa ni kama kichocheo cha ukuaji wa uchumi wa sekta nyingine nyingi. Kwa hiyo, mafanikio ya sekta hii ni msisimko wa Uchumi kwa Taifa.

Biashara ya Sanaa ikifanikiwa na kupita kwenye mkondo wake barabara, husisimua uchumi wa sekta ya Utalii na hata Viwanda na Biashara. Huitangaza nchi na kuchagiza kivutio cha wageni kutembea kibiashara au kitalii, hivyo kuipa nguvu Sekta ya Utalii. Wasanii wanapotajirika, huwezesha kupanuka kwa sekta ya Uwekezaji na kutanuka kwa sekta za Ajira na Elimu.

Hebu tafakari, ni kwa namna gani sekta hii (Nollywood) imeweza kuitangaza vyema Nigeria? Unaweza tu kupata jibu la haraka kwamba Taifa la Nigeria limetangazika kwa kiwango kikubwa hadi kuonekana ni taifa kubwa. Kama Sanaa za Nigeria zimeweza kuteka soko la Afrika na dunia kwa kiasi fulani, haiwezi kukufanya uumize kichwa sana kujua kwamba taifa hilo, limeweza kupata matangazo mengi kupitia sanaa, na zaidi kuvuta watalii kutoka pande mbalimbali za dunia.


Tanzania tunasumbuliwa na ukosefu wa ajira, ni wajibu wetu kuhakikisha Sekta ya Sanaa inakuza ajira na kuwa na faida kubwa kwa Sekta ya Utalii ambayo hatimaye itachangia ukuaji wa uchumi na kuongeza ajira. Biashara katika sekta ya utalii pia inaweza kushuka zaidi katika msimu fulani, lakini Sekta ya Sanaa ni muhimu kupambana na hali hii.

No comments: