Oct 1, 2009

Sera ya Habari na Utangazaji Tanzania

 Ramani ya Tanzania

 Mwandishi Bishop J. Hiluka

Sera ya Habari na Utangazaji Tanzania inabainisha wazi kuwa ni haki ya msingi ya kila raia kupata au kutoa habari kama inavyotamkwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Ibara ya 18 ya Katiba inasema:
"Kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta, kupokea na kutoa habari na dhana zozote kupitia chombo chochote bila ya kujali mipaka ya nchi, na pia ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa kati. Pia kila raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali nchini na duniani kote ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia juu ya masuala muhimu kwa jamii."

Aidha, kutoa na kupokea habari kunatambuliwa duniani kote kuwa ni moja ya haki za binadamu. Umoja wa Mataifa, na Umoja wa Afrika zina matamko rasmi ambayo Serikali imeridhia kuhusu haki ya kupokea na kutoa habari. Haki hii, kama zilivyo nyingine zote, hutolewa kwa kuzingatia wajibu wa kila raia kwa jamii na uhuru binafsi wa binadamu.

Blog hii imeanzishwa kwa madhumuni yaleyale ya kupashana habari kuhusu yaliyojiri na yanayoendelea kutokea katika ulimwengu wa filamu (film industry).
Ili sekta ya filamu iweze kukamilika ni lazima iwe imetimiza hatua tano muhimu ambazo hujulikana kitaalam kama: Development, Pre-production, Production, Postproduction, na Distribution.

Sekta ya filamu nchini Tanzania huwa haifikiriwi sana kuwa ni taaluma adimu ndiyo maana imekuwa haipewi kipaumbele katika kamati za mipango Serikalini. Lakini bado, sekta ya filamu kama mwasilisha taarifa yaweza pia kuwa mwangamizaji na mchochezi mkubwa katika jamii ya kidemokrasia na pengine kuwa mwasilisha taarifa potofu.
Tuna mifano mingi tu kuhusu sekta hii kutumiwa kwa ajili ya uchochezi au propaganda na mataifa makubwa ya Magharibi. Nitakuwa nikizijadili sinema kadhaa ambazo zimewahi kutumiwa kwa ajili ya propaganda na uchochezi katika makala zangu zinazokuja.
Pia sekta hii imekuwa ikitumika kutoa taarifa potofu, kuficha ama kufichua uovu. Moja ya sinema ya mfano iliyowahi kutumika kutoa taarifa za kupotosha inaitwa "DARWIN'S NIGHTMARE (2004)" ambayo iliichafua sana Serikali ya Tanzania katika uso wa dunia hii.

Hubert Sauper, mzaliwa wa Australia anayeishi Ufaransa ndiye mtunzi na mtoaji wa sinema tashtiti ya mapanki (Darwin's Nightmare). Aliiandaa, kuiongoza na kuitoa filamu hiyo yenye kejeli iliyomfedhehesha Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mh. Jakaya Kikwete pamoja na umma wote wa Watanzania. 
Nina hakika kabisa kuwa sinema hiyo ni matokeo ya Serikali ya Tanzania kujiweka mbali na sekta ya filamu. Serikali inapaswa kuwa imepata onyo kupitia filamu hiyo na kuwa karibu zaidi na wadau wa sekta hii hasa katika zama hizi za utandawazi.

Tanzania haipaswi kuibeza sekta hii ya filamu kwani kuna mengi yanayoweza kufanywa katika kukuza utalii na kuliletea taifa mapato kupitia filamu, pia sekta hii ikitumika vizuri itasaidia kufichua mambo yanayoweza kusababisha madhara na upotoshaji kwa jamii (mfano; tohara kwa wanawake, uchunaji ngozi, mauaji ya vikongwe, maalbino, nk.).

No comments: