KAMA wewe ni msanii, iwe wa uimbaji, uigizaji, uchoraji,
uchezaji muziki, uchekeshaji, uandishi n.k., amini usiamini hakuna mtu ambaye
ana kila kitu ulicho nacho wewe.
Hata kama binadamu ni wawili wawili, basi anaweza akatokea mtu
mmoja tu kati ya watu maelfu ndiyo akakufanana kwa vitu vingi: sura, rangi,
uzungumzaji, uwezo wa sanaa, mvuto n.k.
Kitu ambacho pengine hukijui ni kwamba mamilioni ya watu
duniani wametafuta msanii kama wewe, mwenye sifa kama zako ili wamtumie kwenye
matangazo, kwenye video za muziki, kwenye filamu, kwenye mfululizo wa sinema au
michezo ya kuigiza maarufu kama series n.k.
Au pengine wamekutafuta ili watumie kazi zako za sanaa
unazoziandaa, watumie script zako, ubunifu wako na hata kipaji chako ulicho
nacho, na walikuwa tayari kukulipa kiasi kizuri cha pesa, lakini walikosa mtu
kama wewe (kwa kuwa hukujionesha ukafahamika), hivyo wakampachika mtu tu
ilimradi wafanikishe kazi yao.
Kwa kuwa unacho kitu cha pekee ulichojaaliwa kuwa nacho, usije
ukafanya kosa kubwa la kujaribu kuwa mtu mwingine, kwa maana ya kutaka kumuiga mtu
mwingine ambaye ana vitu tofauti na wewe, na usiruhusu kulalamikiwa au
kulaumiwa kuwa huna ubunifu.
Kila mtu ana upekee katika jamii kupitia kipaji chake, na kila
mtu ameletwa duniani kwa kusudi maalumu na la kipekee.
Suala ni kwamba kama kipaji unacho kwanini ubaki unakufa na njaa?
Fahamu kuwa unaweza kufanya biashara ya kipaji ulicho nacho kwa kujiweka sokoni
wewe mwenyewe uonekane na wale wanaokuhitaji.
Kama msanii unapaswa kufanya
juhudi za kukuza kipaji chako cha usanii ndani ya nafsi yako. Msanii ni yule aliyejaaliwa
kipaji cha sanaa, na neno sanaa lina maana ya kile kitu ambacho kinatokana na
mawazo huru ya mwanadamu.
Kwa kuwa kiini cha sanaa ni “ubunifu” nina
kila sababu ya kuamini kuwa kila binadamu ni msanii.
Tofauti huwa iko katika aina za sanaa anazohusika nazo mtu mmoja na
mwingine kwani hakuna binadamu anayeweza kujihusisha na sanaa za aina zote.
Japo ubunifu mwingine huegemea katika baiolojia na teknolojia, yaani sayansi,
lakini ili ukamilike lazima uhusishe sanaa.
Sanaa ni dhana pana inayohusisha mambo mengi. Zaidi ya asilimia 60 ya
maisha ya kila binadamu huhusishwa na sanaa kwani hata ubunifu anaoufanya
mwanandoa katika ulaji wa ‘chakula cha usiku’ ni sehemu ya sanaa na hata
ubunifu anaoufanya mpishi katika chakula anachopika ni sanaa pia.
Katika muktadha rahisi tunaiweka sanaa katika mambo kadhaa yaliyozoeleka
kuitwa sanaa ambayo ni pamoja na: Michezo; Utunzi; Uandishi; Kuimba; Kuigiza; Ushonaji;
Uchongaji; Uchoraji; Ufinyanzi; Ususi; Kupaka rangi na mengine mengi.
Lengo kuu la sanaa ni kuelimisha, kuburudisha, kuonya na
malengo mengine ni pamoja na kutoa ajira, kuhamasisha na kuendeleza
tamaduni.
Sanaa huboreshwa na ubunifu pamoja na viungo vya sanaa ili iwe
sanaa bora. Viungo vikuu vya sanaa ni taaluma na kipaji, kwa maana kwamba sanaa huanzia kwenye kipaji, kisha mafunzo hufuatia.
Japo mtu anaweza kutumia kimoja kati ya viungo hivi katika kutekeleza
kazi za sanaa akafanikiwa lakini inakuwa bora zaidi pale vinapohusika vyote
viwili kwa pamoja.
Kipaji na taaluma katika sanaa hufanya kazi sambamba sawa na nguzo mbili
zilizobeba nyumba moja kila moja kona yake kiasi kwamba hauwezi kuondoa moja
kati ya nguzo hizo na bado nyumba ikabaki salama.
Japo katika hili naweza kutofautiana na baadhi ya watu wenye dhana kwamba kipaji pekee kinatosha kukufanya kuwa bora, lakini vyote
viwili ni lazima vifanye kazi sambamba.
Ni kweli, sanaa ni kipaji na kama
kuna mtu atabisha kuwa si kipaji atakuwa na matatizo ya kufikiri. Lakini sanaa
ni zaidi ya kipaji, sanaa ni taaluma. Kwa maana kuwa inasomewa.
Ni vigumu kwa fani yoyote kubakia
katika kundi lisilokuwa na vigezo vya upimaji wa ubora. Kusipokuwepo vigezo vya
kupima utaalamu wa fani, sanaa zetu zitaendelea kuwa duni, zisizothaminika.
Hata hivyo, kila msanii peke yake
ni kama dunia nzima na sifa hiyo maalumu ya msanii imo ndani ya nafsi yake.
Kama mtu angelipata fursa ya kudiriki dhati ya wasanii angeliweza kuona shani
za dunia na maajabu yake.
Kwa
kifupi, wasanii wengi wanashindwa kabisa kuvitambua vitu vya kipekee walivyo
navyo ndani yao, wanashindwa kuviendeleza na kuvitunza vitu hivyo.
Unaweza
ukawa unazunguka kila kona kutafuta ajira, kumbe unatembea na ajira au mtaji
wako ambao labda ni kipaji cha uchekeshaji, uchoraji, uandishi au ni sauti yako
nzuri kwa kuimba.
Kama msanii mwenye upekee, hupaswi
kutosheka na daraja ya chini. Msanii mvivu na asiyewajibika ambaye hafanyi bidii
ya kukuza kipaji na kazi zake za kisanii, bila ya shaka yoyote atakuwa hakutekeleza
wajibu wake wa kisanii.
Ni jukumu la msanii kuwajibika na
kufanya juhudi bila kuchoka katika kazi zake.
Inawezekana baadhi ya wakati mtu
akafanikiwa kufikia katika hatua ambayo hawezi kwenda mbele zaidi ya hapo wala
kufanya juhudi zaidi ya hizo zilizo nje ya uwezo wake – hilo si neno – lakini bado
anapaswa kuwajibika na kutimiza wajibu wake.
Uwajibikaji huo hauwezi
kupatikana bila ya kuweko shauku, msukumo na hisia za kuwajibika ndani yake.
No comments:
Post a Comment