Sep 1, 2018

Sanaa hustawisha fikra



SANAA ni hazina muhimu sana inayohifadhi kazi ya uumbaji, ina lugha pana ambayo hakuna lugha yoyote nyingine yenye upana kama huo.

Hii si lugha ya sayansi, wala lugha ya kawaida, wala lugha ya mawaidha yenye upana kama wa lugha ya sanaa. Inapaswa ipewe umuhimu na pafanyike juhudi za kuhakikisha muundo wa kujivunia wa sanaa unatumiwa.

Bila ya kuwepo sanaa, matamshi ya kawaida hayawezi kupata nafasi yake katika akili ya mtu yeyote yule. Sanaa ni ala na nyenzo nzuri sana ya kufikisha na kupanua fikra sahihi.


Sanaa ni ala, ni zana, ni chombo; naam chombo muhimu mno. Hivyo si sahihi kuipuuza sanaa na kudharau wajibu wa kuiendeleza na kuipanua, na si sahihi kudhani kwamba sanaa ni dhambi au kufikiri ni makosa kuwa msanii na vitu kama hivyo.

Kila msanii peke yake ni kama dunia nzima na sifa hiyo maalumu ya msanii imo ndani ya nafsi yake. Kama mtu angelipata fursa ya kudiriki dhati ya wasanii angeliweza kuona shani za dunia na maajabu yake.

Pia wasanii wana dhamana ya kutibu na kuganga madonda yaliyomo ndani ya moyo wa binadamu na hivyo kumkirimia tena: imani na matumaini, hasa kwa wale wanaoishi katika mazingira magumu, ili kwa njia ya kazi ya wasanii, watu hawa waweze kutambua uzuri wa kazi ya uumbaji.

Katika dunia iliyojaa furaha na majonzi, matumaini na wasiwasi ndani yake ni sanaa inayoweza kuvutia nyoyo na macho, kwa sababu sanaa ni kipawa kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Mtaalamu wa sanaa ambaye pia alikuwa Mkurugenzi wa Tume ya Utamaduni na Sanaa (NCCA) nchini Philippines, Malou Jacob aliwahi kuliambia kongamano la kimataifa la sanaa lililofanyika Australia kuwa, pamoja na faida nyingi zinazoletwa na sanaa, pia sanaa ni tiba yenye njia nyingi.

Alitolea mfano kwamba kuna wakati aliwatumia ipasavyo wasanii wa Philippines kuitibu jamii iliyokumbwa na mafuriko nchini humo na kufanikiwa kwa kiwango kikubwa.

Anasema kuwa jamii hiyo ilipona majeraha ya dhiki baada ya mapinduzi mwanzoni mwa miaka ya 2000 kupitia wasanii.

Hapa tunakubaliana bila shaka kuwa wasanii ni nguvu kubwa. Jambo muhimu ni kuwafanya wao wenyewe wajitambue na wajiamini, kisha na jamii yenyewe iwaamini kwamba wakitumika inavyotakiwa katika mambo ya maana, wanaweza kuchagiza matokeo chanya.

Jamii inapaswa kuwatumia wasanii katika kutibu majeraha yaliyopo kwenye jamii hiyo, na msanii kwa upande wake anapaswa kujua kuwa ana jukumu mbele ya uhakika maalumu.

Kuna baadhi ya watu wanasema kwamba kuna ukinzani na mgongano katika maneno yanayounda istilahi ya Sanaa ya Uwajibikaji.

Neno sanaa lina maana ya kile kitu ambacho kinatokana na mawazo huru ya mwanaadamu, wakati neno uwajibikaji lina maana ya mtu kujifunga (commitment) na kile ambacho anapaswa kukitenda.

Sasa maneno hayo mawili yanaweza kuwa na uhusiano gani baina yake? Wako watu wenye mawazo hayo na wanaoona haiwezekani maneno hayo mawili kukutana.

Lakini ni wazi kwamba mawazo hayo si sahihi na ni makosa kufikiria hivyo. Jukumu la kuwajibika msanii liko juu ya mabega yake kwa kuwa kwake tu mwanaadamu hata kabla ya kufikiria kipaji chake cha kisanii.

Ni wazi kuwa kabla ya msanii kuwa msanii, yeye kabla ya yote ni mwanadamu. Mwanadamu naye hawezi kusema kuwa hana majukumu wala ulazima wa kuwajibika.

Jukumu la kwanza kabisa alilo nalo mwanaadamu linahusiana na wanadamu wenzake, japo kuna majukumu yanayomuhusu mwanadamu kuhusiana na maumbile, ardhi na mbingu, lakini jukumu lake kubwa ni kuhusiana na wanaadamu wenzake.

Msanii ana majukumu katika pande zote, na hapaswi kutosheka na daraja ya chini. Hilo ni jukumu na ni jambo la wajibu.

Msanii mvivu na asiyewajibika na ambaye hafanyi bidii ya kukuza kipaji na kazi zake za kisanii, bila ya shaka yoyote atakuwa hakutekeleza wajibu wake wa kisanii katika kazi yake.

Ni jukumu la msanii kuwajibika na kufanya juhudi bila kuchoka katika kazi zake. Inawezekana baadhi ya wakati mtu akafanikiwa kufikia katika hatua ambayo hawezi kwenda mbele zaidi ya hapo wala kufanya juhudi zaidi ya hizo zilizo nje ya uwezo wake – hilo si neno – lakini mtu anapaswa kuwajibika na kutimiza wajibu wake.

Lakini imekuwa inasikitisha sana kuona kwamba wasanii walio wengi wala hawatambui nguvu kubwa waliyokuwa nayo na hawajiamini zaidi ya kutumika kwa maslahi ya wachache.

Inasikitisha pale unapoyaona maisha ya wasanii yanapokuwa ya kuigiza, wanaonekana kama ni wenye neema, kumbe wanaongoza kwa kuwa na maisha mabaya.

Na hata pale inapojitokeza neema basi huwa ni kwa muda fulani tu, hasa pale wanapotumiwa na baadhi ya wanasiasa kwa maslahi ya wanasiasa katika kufanikisha jambo lisilowahakikishia uhakika wa soko la kazi zao.

Hii inatokana na kwamba wamekuwa wakipewa mipango mingi isiyotekelezeka na kwa sababu wao wenyewe na hata viongozi wa vyama vyao hawajui nini wanachokihitaji na kwa muda upi, hivyo hujikuta wakinasa kwenye mtego wa kutumika.

Hata zile harakati na ajenda ya ukombozi wa wasanii zimekwisha, na sasa kilicho akilini mwao ni jinsi gani wanavyoweza kutumika au kutumia umaarufu wao kuhakikisha mwanasiasa fulani anapata madaraka, kwa kigezo kuwa anajali maendeleo ya vijana.

Inashangaza kuona wasanii wanaacha kupigania haki zao ikiwa ni pamoja na soko la bidhaa zao na kujiingiza kwenye masuala tofauti kama siasa.
Tumefikia hatua mbaya, wasanii wanaunda timu kulingana na wagombea (wakati wa uchaguzi) ili kutumika kuwapigia kampeni wagombea fulani.

Kufuatia mikakati na harakati walizonazo sasa – za kutumika – utatambua kuwa si wao tu hata viongozi wao wanaowaongoza pia hawajui kwanini walianzisha umoja? Hawajui lengo hasa lilikuwa nini? Na hawajui wanahitaji nini?

Hadi leo hawana dira, na malengo yao ni ya muda mfupi tu (kuganga njaa), matokeo yake wamejikuta wakiishia kuilalamikia serikali kwa kukosa fursa za kupata mikopo kwenye asasi za kifedha, na kutothaminiwa.


No comments: