Oct 26, 2009

Historia ya Filamu Duniani

Historia ya sinema duniani inaanzia kwa Bw. William Kennedy Laurie Dickson aliyekuwa injinia mkuu wa Edison Laboratories ya Marekani. Huyu Dickson ndiye anayesadikiwa kuwa mvumbuzi na “baba wa filamu duniani”, alivumbua mfumo wa picha unaojulikana kitaalamu kama “Celluloid Strip”, yaani mkanda maalum uliokusanya picha za matukio mfuatano (sequence of images) yaliyopigwa kwa kamera (photographing) maalumu ya picha za matendo (moving images) na kuzionesha kwa njia ya sinema (projecting moving images).


Kinetograph

William K.L. Dickson alizaliwa katika eneo la Minihic-Sur-Rance katika nchi ya Ufaransa kutoka kwa wazazi wenye asili ya Uingereza na Uskochi (English-Scottish parents) mwaka 1860, ingawa baadaye alihamia nchini Marekani ambako alijiunga na kampuni ya Thomas Edison.

Mwaka 1879 akiwa London, Dickson ambaye wakati huo alikuwa amefiwa na baba alisoma habari kwenye gazeti moja zilizomhusu Edison na maabara yake iliyojulikana kwa jina la “Menlo Park Laboratory”. Alivutiwa sana na habari hizo, miaka miwili baadaye alituma “telegram” kwa Edison akiulizia nafasi ya kazi kwenye maabara hiyo.

Edison alimjibu kwa kifupi “hakuna kazi”. Lakini mwaka 1883, Dickson akiwa amefanikiwa kukusanya pesa za nauli aliamua kuelekea Marekani huku akiwa na ujuzi kidogo wa upigaji picha, alipofika Marekani alipata kijinafasi kidogo chini ya paa la kampuni ya Edison na kufanya kazi zake huku akisubiri siku huenda akabahatika kupata nafasi muhimu ya kuajiriwa. Ndipo ikatokea mwaka 1888, alipopewa kazi na Edison ya kufanya utafiti juu ya maendeleo ya mpiga picha Eaydward Muybridge, na wavumbuzi wenzake waliokuwa wakirekodi picha.

Eaydward Muybridge alikuwa mpiga picha ambaye alifanikiwa kutengeneza picha kadhaa za matukio mfuatano (sequential photographs) yaliyohusiana na mwendo wa farasi, mwaka 1877.

Baadaye Muybridge alifanikiwa kuvumbua kifaa kilichoitwa “zoöpraxiscope” mwaka 1879, kifaa hicho kilikuwa kikitumika kwa ajili ya kuonesha na kuzichangamsha (animating) picha za wanyama alizopiga.

Dickson alianza rasmi kazi ya kufuatilia nyendo za Muybridge akiwa na ari kubwa huku akijitahidi kupeleleza na kufuatilia kila jambo aliloona ni jipya kuhusu ugunduzi huo. Alipata wazo la kutengeneza kamera na vifaa vingine vitakavyoweza kumsaidia kuona picha. Hakuwa mwepesi wa kukata tamaa, alijifunza kwa bidii huku akitumia mbinu na nyendo za bwana mmoja aliyeitwa John Carbutt. John Carbutt alikuwa mpiga picha wa Kiingereza aliyehamia Amerika na kufanya tafiti mbalimbali juu ya “Celluloid Photographic Film”.

Kwa kuwa Dickson alikuwa na wazo la muda mrefu la kutaka kutengeneza picha za matendo (sinema), alimweleza bosi wake kuhusu majaribio yake, lakini Edison hakutilia maanani kabisa majaribio (motion picture ideas) aliyoelezwa na Laurie Dickson.

Dickson baada ya kuona anapuuzwa aliamua kujiunga na kampuni nyingine iliyoitwa George Eastman Company ili aweze kukidhi haja yake ya uvumbuzi.

Baada ya muda, Dickson aliamua kumtafuta Hannibal Goodwin, aliyekuwa mchungaji wa kanisa la “Episcopal”, kanisa la asili ya Marekani. Ilisemekana kuwa Goodwin alikuwa amefanikiwa kutumia mafuta maalum mazito (photographic emulsion) kwa kulainishia na kuufanya mkanda wa picha uzunguke. Dickson alimfuata na kumlazimisha akubali utafiti wake huo utumike kwa kampuni ya George Eastman kwa ajili ya uzalishaji.

Dickson “king’ang’anizi” alifanikiwa kuvumbua kamera mnamo mwezi Novemba, 1890 na kuifanyia majaribio kwa kupiga picha (filming) jaribio lake la kwanza aliloliita “MONKEY SHINES” kwa kuhusisha (featuring) mwendo wa msaidizi wake Fred Ott.

Kamera hiyo aliipa jina la “Kinetograph”, na kuionesha kwa Edison, ambaye aliunda timu maalumu iliyofanikiwa kutengeneza  kifaa kingine “Kinetoscope”, kifaa ambacho kilikuwa na tundu (peep-hole) dogo kwa ajili ya kuonea picha ambazo walizipa jina la maajabu ndani ya sekunde tano “five second wonders.”

Uvumbuzi huo haukuwa na ugumu sana kwa upande wake. Mkanda wenye picha kadhaa za matukio mfuatano ulikuwa ukipitishwa mbele ya lenzi yenye kutoa mwanga kwa msaada wa balbu na nyuma yake kulikuwa na gurudumu lenye kuzunguka. Gurudumu hilo lilipozunguka, muonekano wake ulimfanya mtazamaji aone jumla ya picha 46 za matukio tofauti yanayofuatana kwa sekunde moja tu. Mzunguko huo wa picha 46 kwa sekunde uliweza kumfanya mtu anayetazama picha aone matendo halisi (lifelike motion).

Kutambulishwa kwa kifaa cha “Kinetograph” mwezi Oktoba, 1892 ndiyo ikawa chachu na mwanzo wa sekta ya filamu kukua na kufikia hapa ilipo kwa sasa.

Mnamo mwaka 1893, kwenye tamasha la wafanyabiashara la Chicago (Chicago World Fair), Thomas Edison alizitambulisha kwa umma vumbuzi hizo mbili zilizotokana na uvumbuzi wa William K.L. Dickson (Kinetograph na Kinetoscope).


Kinescope

Mfumo wa kinetoscope haukuchelewa kusambaa kwa haraka sana na kwa mafanikio makubwa barani Ulaya.

Mfumo huu wa Kinescope (mkanda wa picha) zilizopigwa na Dickson kwenye studio ya Edison iliyojulikana kwa jina la “Black Maria” ulikuwa wa urefu wa futi hamsini. Picha hizo zilikuwa za matukio mfuatano (sequences) zilizochukuliwa katika sherehe na matukio mbalimbali ya kidunia, mfano “FRED OTT’S SNEEZE (1894)” na picha zingine zilizotokana na burudani mbalimbali kama vile kwenye maonesho ya sarakasi, maonesho ya wanenguaji kwenye kumbi za muziki, na kwenye maonesho ya ngumi.

Hata hivyo Edison hakuwahi kutambuliwa kama mtu muhimu na mvumbuzi aliyekubalika kwa nchi za Atlantiki za bara Amerika, hasa kwa kuwa wao teknolojia hii ilikuwa imewafikia kupitia uvumbuzi na majaribio yaliyotangulia yakitokea Uingereza na bara la Ulaya kwa ujumla.

Juhudi za Dickson zilisaidia sana katika maendeleo ya sekta ya filamu hasa kwa watengenezaji wa kamera na vifaa vingine waliofuatia, mfano mzuri ni kamera iliyotengenezwa na fundi umeme na mwanasayansi wa Kiingereza Robert William Paul na mshirika wake Birt Acres.

Paul aliyekuja na wazo la kutaka kuonesha sinema kwa hadhira (audience), aliona kuwa ni jambo zuri kuionesha kwenye hadhara ya watu kuliko kwa mtu mmoja mmoja, hivyo alivumbua mtambo maalum “film projector” wa kurushia picha na hatimaye alifanikiwa kuonesha sinema kwa mara ya kwanza mwaka 1895.

Mwaka huo huo 1895, nchini Ufaransa ndugu wawili Auguste na Louis Lumière walifanikiwa kuvumbua kifaa cha kupigia picha chenye viambatanisho vitatu ndani yake: camera, printer, na projector.


Kamera iliyovumbuliwa na ukoo wa Lumière

Mwishoni mwa mwaka 1895 jijini Paris, Antoine Lumière ambaye ni baba yao Auguste na Louis alifanya onesho la sinema kwa malipo, huo ndiyo ukawa mwanzo wa kukua kwa sekta hii (kwa mujibu wa Cook, 1990).

Antoine Lumière alizaliwa tarehe 13 Machi, 1840 katika eneo la Haunte-Saone, Ormoy, nchini Ufaransa. Alipofikisha umri wa miaka kumi na nne alifiwa na wazazi na kubaki yatima. Alijifunza useremala na baadaye alianza kujisomea vitabu vya sayansi kabla ya kwenda kujifunza rasmi chini ya mwalimu Auguste Constantin. Baadaye alilitumikia jeshi la nchi hiyo na baada ya hapo alijifundisha upigaji picha.

Alioa mke mwaka 1861 akiwa na miaka 21 na kuanzisha studio yake ndogo ya kupiga picha eneo la Besancon, eneo ambalo wanaye Auguste na Louis walizaliwa.


Hii picha ilichukuliwa wakati wa upigaji wa picha ya 
Workers Leaving the Lumière mwaka 1895

Baadaye alihamia Lyon ambako alimzaa mtoto wake wa tatu, Edward na mabinti wengine watatu. Kutokana na juhudi zao, ukoo wa Lumière walijikuta wakiwa ndiyo wazalishaji (producers) wakubwa wa filamu barani Ulaya. Baadhi ya kazi zao ni kama “WORKERS LEAVING THE LUMIÈRE” na “THE SPRINKLER SPRINKLED” (zote za mwaka 1895).UKOO wa Lumière wakawa ndiyo wazalishaji (producers) wakubwa wa filamu barani Ulaya. Baadhi ya kazi zao ni kama “WORKERS LEAVING THE LUMIÈRE” na “THE SPRINKLER SPRINKLED” (zote za mwaka 1895).
Kutokana na mikakati mizito na changamoto iliyotolewa na ukoo huo kuliifanya kampuni ya Edison kufanya kazi kubwa ili kuukabili ushindani, kwa kumtumia Dickson ambaye alijikita kwenye kutafuta mbinu mpya ili kukabiliana na ukoo wa Lumière na hatimaye alifanikiwa kuvumbua matumizi ya kifaa kijulikanacho kama ‘Vitascope’ ndani ya miezi sita tu.

Baada ya Dickson kuhangaika sana akifanya tafiti na gunduzi mbalimbali hatimaye mfumo wa mwisho wa ‘Vitascope’ ulioneshwa mwaka huo 1895, ilikuwa ni kamera kubwa yenye uwezo mkubwa na mtambo wa kurusha picha na hivyo kuleta mapinduzi halisi ya sinema.

Bahati mbaya mapinduzi hayo yaliipindua pia tamaa ya Edison. Wakajikuta Edison na Dickson wakishindwa kukubaliana kuhusu malengo yao ya baadaye (future) juu ya uvumbuzi huo mpya. Wakatengana kila mmoja akaamua kufanya kazi kivyake.

Dickson akaanzisha kampuni aliyoiita American Mutoscope Company, na kuuendeleza uvumbuzi wake wa Mutoscope kwa nguvu zote na kufanikiwa kutengeneza ‘Mutograph’, kifaa kilichotoa ushindani wa nguvu kwa kampuni ya Edison ndani ya mwaka wa kwanza tu wa historia ya soko la sinema.

Dickson akatoa sinema yake ya kwanza akiwa na American Mutoscope iliyoitwa “EMPIRE STATE EXPRESS (1896)” na hatimaye kuifanya studio yake kuwa moja ya studio kubwa na tishio, na huo ukawa mwanzo wake wa kuibua vipaji vya kina Edwin S. Porter, D. W. Griffith, Billy Bitzer, Mary Pickford, Lilian Gish, na Mack –Sennett.

Dickson hakuishia hapo tu, aliamua kutengeneza kamera na mtambo maalum wa kurushia picha (projector system) aliouita jina la “Biograph”, mtambo huo ulikuwa na uwezo mkubwa kuliko wa Vitascope, lakini bahati mbaya hakuwa na mauzo mazuri katika kampuni yake ya kumwezesha kutoa ushindani wa nguvu kwa kampuni ya Edison.

Dickson akaamua kuuza sehemu ya hisa zake zinazohusu uvumbuzi wa ‘Biograph’ na kuamua kurudi nchi ya mama yake, England, mwaka 1897.
Miaka miwili baadaye, Dickson aliweza kutambuliwa na kupewa heshima na wanahistoria kama ndiye “Baba halisi wa sinema” na ndiye aliyechangia kwa kiwango kikubwa maendeleo na uvumbuzi wa sinema.
Dickson alifariki kwa kansa tarehe 28 Septemba, 1935 katika eneo la Twickenham, Middlesex, England.

Katika kipindi cha uhai wake aliwahi kuoa mara mbili na aliacha mtoto mmoja wa kiume ‘adopted son’ aliyemuasili.

No comments: