Oct 26, 2009

Ujio wa Sinema katika bara la Afrika

Waongozaji wa sinema za Kitanzania, Sulesh Marah na Bishop J. Hiluka

Nembo ya soko la Filamu nchini Nigeria

Ieleweke kuwa kwa miaka mingi tu Afrika imekuwa ikiwasilishwa katika uwanja wa filamu kama bara lenye giza na mataifa ya Ulaya na Magharibi. Matamanio ya kueneza propaganda katika kipindi cha vita kuu ndiko kulikosababisha na kuibuka upya kwa ari katika mataifa ya Magharibi, kwa mfano nchini Uingereza walitengeneza sinema kama “FORTY-NINTH PARALLEI (1941)”, “WENT THE DAY WELL? (1942)”, na “THE WAY AHEAD (1944)” zote zikiwa zina lengo lile lile la kueneza propaganda.Miaka ya mwanzo ya kuingia kwa sekta ya filamu Afrika, vitengo vya filamu vya Serikali za kikoloni vilisambaza sinema hapa Afrika zilizokuwa zimetengenezwa Ulaya na Marekani kwa lengo maalum, ndiyo maana sinema zilizooneshwa hapa Afrika zilikuwa zinafanyiwa uhariri mara ya pili (re-edited) chini ya uangalizi wa watu maalum ili kuhakikisha kuwa Waafrika hawaoni mambo ambayo hayakukusudiwa kwao.
Sekta hii ya filamu ilipoingia katika bara hili la Afrika, iligawanyika katika makundi manne kulingana na lugha zilizotumiwa kwenye nchi zilizopo katika bara hili. Anglophone iliwakilisha sekta ya filamu kwa nchi zilizotumia lugha ya Kiingereza. Francophone iliwakilisha nchi zilizotumia Kifaransa, Lusophone iliwakilisha nchi zilizotumia Kireno, na Arabophone iliwakilisha nchi za Kiarabu.  

Nchi za Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania, zilikuwa katika kundi la kwanza (Anglophone), na historia ya sinema kwa Tanzania inaanzia mwaka 1929 ambapo sinema ya kwanza kabisa iliingia Tanganyika (sasa Tanzania).
Kati ya mwaka 1935 na 1936 raia wawili wa Uingereza, Major L.A. Notcutt na Geoffrey Latham waliingia Tanganyika na kuifanya iteuliwe kuwa kituo maalum na baraza la kikoloni ‘International Missionary Council’ kwa ajili ya mradi wa majaribio ya elimu kwa njia ya sinema ‘Bantu Education Cinema Experiment’. 
Mradi huu ulianzishwa kama heshima, tuzo na imani kwa utawala wa Kiingereza katika makoloni yake kwa ajili ya kuinua na kuendeleza sekta ya filamu kwa Waafrika mbumbumbu (illiterate Africans). Elimu iliyotokana na ‘Bantu Education Experiment’ iliwezesha kutengenezwa kwa sinema kama “GUMU”, sinema iliyokuwa ikielezea matatizo na ugumu wa maisha ya mjini, lengo kubwa likiwa kuwahimiza vijana wabakie vijijini badala ya kukimbilia mjini.
G. C. Latham, ambaye alikuwa mkurugenzi wa mafunzo wa ‘Bantu Education Experiment’ aligundua kuwa mazingira na tamaduni za Kiafrika yalikuwa ni mandhali nzuri sana kwa sinema za kuburudisha (entertaining), hivyo alitoa ushauri kuwa baadhi ya sinema zingeweza kutengenezwa kwa kutumia baadhi ya hadithi za mapokeo zilizowahusu mashujaa wa Kiafrika waliokuwa maarufu, moja ya sinema zilizokuja kutengenezwa kutokana na ushauri wake ni “WAKALINDI SAGA”.
Jumla ya sinema 35 zilitengenezwa kwa kutumia kamera ya 16mm hapa Afrika Mashariki, zilipigwa katika maeneo tofauti tofauti zikiwa katika lugha ya Kiingereza na lugha zingine nane za asili ambazo ni Kiswahili, Kisukuma, Kikuyu, Kijaluo, Kiganda, Kinyanja, Kibemba, na Kitumbuka.
Mambo waliyoyatilia mkazo sana katika sinema zao ni pamoja na “Benki ya Posta”, “Mmomonyoko wa udongo”, “Malaria kwa watoto wachanga”, “safura”, “soko la kahawa”, “kodi”, n.k.
Walisafiri maeneo mengi ya Afrika Mashariki na kati kwenye miaka ya 1936 na 1937 na kufanikiwa kuzionesha sinema hizo kwa zaidi ya watu 100,000. Pamoja na kazi hizo lakini Wakoloni hao walijikita zaidi kwenye kuonesha sinema za kipropaganda zaidi kwa Waafrika. Walitufanya tuamini kuwa matambiko yetu ni ushenzi mtupu, ni kutostaarabika kulikopitiliza!
Hadi sasa sinema zao nyingi zimejikita zaidi katika kuonesha matatizo tu ya bara la Afrika na jinsi mtu mweupe akiingia kwenye bara hili anavyokumbana na matatizo na jinsi anavyoyashinda.
Sinema kama: “KING SOLOMON’S MINES”, “TARZAN”, “SAFARI”, “THE APE MAN”, “SNOW OF KILIMANJARO”, “TRADE HORN”, nk. (zote za miaka ya 1980), ni mfano mzuri. 
Notcutt na Latham walipofika mwisho wa mradi wao waliishauri Serikali ya Kikoloni ya Tanganyika ianzishe kitengo maalum cha filamu kitakachofanya kazi za kueneza propaganda kwa maelekezo maalum kutoka London, Uingereza.
Wizara ya Habari ya Uingereza (British Ministry of Information) ikaanzisha kitengo cha sinema kilichojulikana kama “Colonial Film Unit (CFU)” mwaka 1939 kwa ajili ya kutengeneza na kusambaza sinema za kipropaganda. Wizara hiyo pia iliandaa magari maalum (mobile cinema vans) kwa ajili ya kuoneshea sinema hizo na zingine za kuburudisha kwenye maeneo ya vijijini katika Afrika Mashariki.
Serikali ya Uingereza ilianzisha matawi yake katika sehemu mbalimbali za makoloni yake  yaliyotumia lugha ya Kiingereza (Anglophone): kwa Afrika Mashariki matawi hayo yalikuwa Kenya, Tanganyika, na Uganda; Afrika ya Kati matawi yalikuwa Rhodesia (sasa Zimbabwe), na Nyasaland (sasa Malawi); na kwa upande wa Afrika Magharibi waliweka matawi yao Nigeria na Gold Coast (sasa Ghana).
Kwa mujibu wa Jean Rouch, Serikali ya Uingereza ilikuwa imeanzisha vitengo vya filamu ili iweze kuwapata vijana wa Kiafrika kwa urahisi zaidi kwa ajili ya kushiriki kwenye vita kuu ya pili ya dunia (Rouch, uk. 390).
Vita kuu ya pili ya dunia ilitoa msukumo zaidi kwa sekta ya filamu; Serikali ya Uingereza iliichukulia sekta ya filamu si kwa ajili ya kuwaburudisha tu askari wake, lakini pia kama wazo zuri la kueneza propaganda, hasa kwa watu ambao hawakwenda shule (illiterate audiences). Wakoloni walianzisha na vitengo tofauti kulingana na sekta zilizokuwepo ili kuweza kutengeneza sinema kwa uhakika zaidi kulingana na sekta husika.
Wakati wa vita kuu ya pili ya dunia kitengo cha filamu cha Posta “British General Post Office Film Unit” kilionekana kuzidiwa na kupoteza mwelekeo, hivyo shughuli zake kuhamishiwa kwenye kitengo kingine kilichojulikana kama “Crown Film Unit”, huku kikiwa kinakabiliwa na kulemewa na bajeti kubwa sana na wafanyakazi waliokuwa chini ya Wizara ya Habari.
Hatimaye kazi za kitengo hicho zilikabidhiwa kwa kitengo kingine cha “Colonial Film Unit (CFU)” kilichofanya kazi kubwa ya kuwapatia mafunzo Waafrika na baadaye kuvigawa vitengo vya filamu katika kila koloni ili vijiendeshe.
Mwaka 1945, baada ya vita kuu ya pili, uoneshaji na usambazaji wa sinema hizi ulibadilika kidogo kwenye baadhi ya sinema. Kuna sinema kama “MISTER ENGLISH AT HOME” na “AN AFRICAN IN LONDON” zilitengenezwa kwa lengo maalum la kutufundisha mambo na tamaduni za Kiingereza. Hata sinema zilizoanza kutengenezwa Afrika baada ya hapo zilizingatia mambo kadha wa kadha kama; Faida ya dawa (tiba) za Kimagharibi dhidi ya tiba za Kiafrika kwenye kutibu baadhi ya magonjwa kama kifafa (leprosy).

No comments: