Oct 13, 2009

Mafanikio ya Sinema za Hollywood


Watengeneza filamu wa Kimarekani wakiwajibika.


Soko la filamu la Marekani au kama linavyojulikana na wengi ‘Hollywood’, jina linalotokana na eneo la kijiografia lililopo katikati ya California, limeweza kufikia nafasi lilipo sasa si kwa bahati tu, bali lilitokana na jitihada kubwa na mikakati ya dhati iliyofanywa kitaifa. Hollywood imefanikiwa kuzalisha na kusambaza sinema zake nchi zote hadi kufikia kulitawala soko la sinema duniani.
Ieleweke kuwa kukua kwa sekta ya filamu ndiko kulikosababisha uwepo wa nembo mbalimbali katika nchi nyingi zikiwakilisha soko la filamu kwa nchi zao, kama vile: Hollywood (USA), Bollywood (India), Nollywood (Nigeria) na Lollywood (Pakistan).

Pia kuna nembo zingine kama; Tollygunge (Bengali Film Industry), Malluwood (Malayalam Film Industry), Kollywood (Tamil), Sandalwood (Kannada Film Industry) na Tollywood, zote hizi zikiwa katika majimbo mbalimbali ndani ya ardhi ya India.

Ingawa Hollywood ndiyo wameonekana kufanikiwa kwa kiasi kikubwa sana katika sekta ya filamu duniani lakini ni sinema za Kifaransa na Kiitaliano ndizo sinema zilizokuwa maarufu na zenye nguvu sana (most powerful) duniani.
Kabla ya vita kuu ya kwanza ya dunia, Ufaransa ndiyo waliokuwa wakilitawala soko la sinema duniani. Hollywood walikuja kutumia mwanya wa kuanguka kwa uzalishaji wa sinema nchini Ufaransa wakati wa vita kuu ya kwanza na hivyo kujijengea mkakati madhubuti (hegemony) dhidi ya nchi zingine katika soko.Auguste Lumiere, baba wa sinema za Kifaransa

Ikumbukwe kuwa Marekani tayari walianza kukua kwa kasi hadi kufikia wakati wa vita kuu ya kwanza (1914-1918) na kusababisha  kupungua kasi ya soko la filamu zitokazo bara la Ulaya (Europian film industries).
Baadaye Ujerumani ndiyo ikawa nchi pekee duniani iliyoweza kutoa ushindani wa kweli kwa Marekani (Hollywood) katika soko la filamu.

Katika miaka ya 1920, Marekani iliweza kufikia kile ambacho hadi sasa kinajulikana kama zama zake za mafanikio makubwa, iliweza kuzalisha wastani wa sinema 800 kwa mwaka, na kuingiza 82% ya mauzo yote ya filamu duniani (kwa mujibu wa Eyman, 1997).

Sinema za Marekani zikaanza kuwafanya waigizaji wake kuwa maarufu zaidi duniani: vichekesho vya wachekeshaji maarufu duniani Charlie Chaplin na Buster Keaton, “THE SWASHBUCKLING ADVENTURES OF DOUGLAS FAIRBANKS” na “THE ROMANCES OF CLARA BOW”, ni mifano michache ya sinema hizo jinsi zilivyoweza kufanya sura za waigizaji wa Hollywood kuwa maarufu sana katika kila bara la dunia hii.

No comments: