Apr 27, 2011

Tutumie watunzi wazuri wa stori kuboresha filamu zetu

 Marehemu Hammie Rajab

 Marehemu Hammie Rajab akiongoza upigaji picha za filamu

ALHAMISI ya Aprili 21, 2011 saa tatu asubuhi, nilipokea ujumbe mfupi kwenye simu yangu uliotoka kwa Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania, Simon Mwakifwamba, akinijulisha kuhusu kifo cha mmoja wa watunzi mahiri wa vitabu na muongozaji wa filamu nchini ambaye nchi hii imepata kumshuhudia, Hammie Rajab.

Mwakifwamba alinijulisha kuhusu msiba huo ambao umeacha pigo sio tu kwa wapenzi wa riwaya bali kwa tasnia nzima ya filamu nchini.

Hammie Rajab alifariki dunia usiku wa kuamkia Alhamisi ya wiki iliyopita katika Hospitali ya Amana, Ilala jijini Dar es Salaam na taarifa zake kusambaa haraka sana. Marehemu alikuwa akisumbuliwa na vidonda vya tumbo kwa muda mrefu lakini pia alikuwa na Malaria.

Binafsi nilimfahamu mzee Hammie Rajab tangu nikiwa mdogo sana kupitia hadithi zake, historia yake inaonesha kuwa alianza kazi ya uandishi kwa kuandika visa katika magazeti mbalimbali hapa nchini. Nilipopata uwezo wa kusoma nilipenda sana kusoma hadithi za watunzi mahiri waakiwemo Eddie Ganzel, Shaaban Robert, Agolo Anduru sambamba na hadithi za Hammie Rajab, na watunzi hawa ndiyo walionivutia sana kupenda kuandika.

Kifo cha Hammie Rajabu kinaongeza idadi ya watunzi mahiri walioaga dunia ambao binafsi naomba nikiri kuwa walikuwa hazina bora kwa taifa hili na naamini nchi hii haiwezi kupata mfano wao, wengine waliotangulia ni pamoja na Shaaban Robert, Eddie Ganzel, Agolo Anduru, Ben R. Mtobwa, Elvis Musiba, Kassim Chande, Rajabu Mbega na John Rutayisingwa.

Historia fupi ya marehemu Hammie Rajab inaonesha kuwa alizaliwa mwaka 1936 mkoani Morogoro, ameacha mke, watoto 14 na wajukuu 14.

Wakati nikiwa bado kwenye simanzi ya kupotelewa na mtu huyu muhimu sana ambaye tumewahi kufanya kazi kwa ukaribu zaidi, msomaji mmoja ambaye hakutaka kujitambulisha jina lake kwangu alinipigia simu akionekana kutofautiana kidogo na makala yangu ya wiki mbili zilizopita; “Tatizo kubwa kwenye filamu zetu ni kukosa waongozaji,” akisema kuwa pamoja na kwamba niligusia matatizo mawili katika filamu zetu: uongozaji na uandishi lakini nikajikuta nikiegemea upande mmoja tu katika kuwakosoa waongozaji pekee huku nikiwatetea waandishi.

Msomaji alinieleza kuwa hao wanaojiita waandishi wa miongozo ya filamu wengi wao anawafahamu na anaamini kuwa hawana uwezo wa kuandika stori nzuri, na uandishi wao umeegemea katika kunakiri hadithi nyingine na kupelekea kukosa mvuto, mara nyingi inavyoonekana ni waongozaji ndiyo wanaofanya kazi kubwa kuziboresha hadithi hizo ili angalau zivutie na kuwa nzuri.

Sikutaka kupingana na msomaji wala kumjibu kwenye simu lakini nilimshauri kuwa asome makala ya wiki hii ambayo natumaini itakidhi kiu yake na hata wengine katika kutaka kujua mengi kuhusu waandishi wa stori na umuhimu wa stori nzuri katika filamu zetu. Ningeweza kuandika kuhusu uongozaji na utunzi/uandishi wa stori kwa wakati mmoja lakini naamini kuwa ninapozama kuchambua jambo huwa nina mambo mengi sana ya kuzungumzia na bahati mbaya nafasi huwa haitoshi kuyaeleza yote kwa wakati mmoja.

Nakubaliana na msomaji kuwa tatizo lingine kubwa lililopo kwenye filamu zetu ni kuwa na stori mbovu ambazo nyingi zinafanana. Kama nilivyodokeza kwenye makala ya
“Tatizo kubwa kwenye filamu zetu ni kukosa waongozaji;” kuwa stori mbovu haiwezi kutoa filamu mzuri hata kama wachezaji wa filamu hiyo watakuwa magwiji wa filamu kutoka Hollywood.

Kosa kubwa linalofanywa na watayarishaji wa filamu hapa nchini ni kudhani kuwa kila mtu anaweza kuwa mtunzi mzuri au mwandishi mzuri, wakasahau kuwa tuna hazina kubwa ya watunzi wazuri ambao hatuwatumii, tunasubiri waage dunia tuishie kuwasifia.

Nakumbuka siku moja nilikuwa nikiongea na mtunzi mwingine mahiri hapa nchini, mzee Faraji H. Katalambula, aliyekuwa akilalamikia kitendo cha watayarishaji wa filamu zetu kutowatumia watunzi wa vitabu kama yeye ambaye ana hadithi nzuri sana ambazo zingeweza kuchezwa kwenye filamu zetu.

Nilikubaliana naye kwa kuwa namfahamu siku nyingi na nilikuwa mpenzi mkubwa wa hadithi zake, lakini nilimtahadharisha kuwa watayarishaji wengi wa filamu hapa nchini ni wabinafsi, ukisubiri wakutafute ili kununua stori yako unaweza kufa njaa, kwani kila mmoja siku hizi anadhani yeye ni mtunzi mzuri.

Tasnia yoyote ya filamu katika nchi zilizoendelea hupenda kuwatumia watunzi wazuri, hivyo tusijaribu kuwakwepa watunzi hawa kwa kisingizio kwamba bajeti haituruhusu kuwatumia, kwani naamini wao ni binadamu wanaoelewa hali halisi ya soko letu na sidhani kama wanaweza kutudai mamilioni kwa kazi ya bajeti ndogo. Pia kitendo cha kuwashirikisha watunzi hawa peke yake kitaonesha namna tunavyowaenzi na kuwathamini.

Pamoja na kuondokewa na watunzi kadhaa mahiri, lakini bado tunayo hazina ya watunzi kadhaa wazuri waliobaki ambao tunapaswa kuwatumia ili kuboresha filamu zetu. Watunzi kama Beka Mfaume, Hussein Tuwa, Hamisi Kibari, Faraji Katalambula, Juma Mkabarah, Adam Shafi, Jackson Kalindimya, Amri Bawji, Chris Magori na wengineo.

Naamini kuwa utunzi wa stori unahitaji kipaji zaidi kuliko vinginevyo. Ni rahisi kumfundisha mtu kuwa mwigizaji na akawa mwigizaji mzuri sana lakini ni vigumu kumfundisha mtu kuwa mtunzi na akawa mtunzi mzuri.

Kwa kawaida uigizaji unahitaji Ubunifu + Kipaji lakini utunzi wa stori unahitaji Kipaji + Lugha + Ubunifu + Msuko. Mwalimu wangu wa kwanza katika uandishi, marehemu Eddie Ganzel, aliwahi kuniambia kuwa kwa asili watu wote ni watunzi, lakini ili uwe mtunzi/ mwandishi mzuri unahitaji kuwa na kipaji, kuijua vizuri lugha, kuwa mbunifu na kuwa na inspiration.

Katika filamu zetu, stori ndiyo ramani kama ilivyo kwenye ujenzi wa nyumba, na script ni msingi kama ulivyo msingi wa nyumba. Ili kujenga nyumba nzuri unapaswa kuwa na msingi imara uliotokana na ramani nzuri. Na ili kuwa mwandishi mzuri wa stori/script unapaswa kuwa na sifa kuu tisa:
-Analytical ability: Lazima uwe na uwezo wa kuchambua habari, kuyagusa mahitaji halisi ya walengwa na uwezo wa kutofautisha mambo muhimu na yasiyo muhimu.
-Interest in diverse topics: Mwandishi mzuri anahitaji kufanya utafiti wa kina na makini katika kile anachokiandikia.
-Organizational skill: Lazima uwe na uwezo wa kukusanya taarifa, kuandaa taarifa zenye mantiki kuhusiana na kisa.
-Empathy for your audience: Lazima uwe na uelewa mkubwa kuhusu kile watazamaji wako wanachokitaka, lazima uzame ndani ya mitazamo ya watazamaji wako, vitu wanavyovipenda, mitindo yao, na matamanio yao.
-Writing skill: Lazima uwe na uwezo wa kuandika kwa uwazi na kwa ufupi, na lazima uwe na uwezo mzuri katika matumizi ya sarufi.
-Ability to think visually: Lazima uwe na uwezo wa kuwasilisha taarifa/ mawazo yako sambamba na picha, na si maneno tu.
-Creativity: Lazima uwe mbunifu katika kufikiri unachokihitaji kwa ajili ya kuandika stori nzuri.
-Presentation and selling skills: Lazima uwe na uwezo wa kuwasilisha mawazo yako kwa ufanisi kwa wateja wako na uwezo wa kuuza kazi yako.
-Ability to work on a team: Kiutendaji utajikuta ukifanya kazi na watu kadhaa wenye kazi tofauti, hivyo uwe na uwezo wa kufanya kazi katika kundi.

Pia ieleweke kuwa uzuri wa stori yoyote ile unatokana na msuko mzuri wa matukio. Msuko wa matukio unahitaji sana
creativity na inspiration. Unapotunga stori yoyote inayohitaji msuko mzuri wa matukio unahitaji sana 'meditation' na kufanya utafiti wa kina wa kile unachokiandikia. Katika utunzi, inafika wakati mtu unakwama na kujikuta ukiwa huna kitu cha kuandika.

Mtunzi mzuri akishaona hana kitu cha kuandika ataacha kuandika kwa muda na kuzama katika tafakuri (meditation) ili apate kitu bora cha kuendelezea stori yake badala ya kukurupuka tu mradi amalize. Watunzi wa filamu zetu wengi wanakosa uvumilivu na hawana muda wa kutafakari kwa kina au kufanya utafiti na matokeo yake huishia kukopi stori za wengine na kubadilisha mtazamo kidogo tu, hivyo kukosa msuko mzuri wa matukio.

Elewa kuwa msuko mzuri wa matukio katika stori yako ndiyo utakaomfanya mtazamaji wa filamu au msomaji wa hadithi apate hamu ya kuendelea mbele zaidi ili kujua kitakachotokea.

Stori iliyopwaya inaleta filamu mbovu hata kama waigizaji wataakuwa wazuri kiasi gani. Stori iliyosukwa vizuri inazalisha filamu itakayovutia kutazamwa, hata na watu wasiojua lugha iliyotumika kwenye filamu husika. Mfano mzuri ni sisi tunaovutiwa kutazama sinema za Bollywood wakati hatuijui lugha la Kihindi inayotumika kwenye filamu zao. Ndiyo maana nasisitiza umuhimu wa kuwatumia watunzi wazuri wa stori.

Watengenezaji wa filamu wa Tanzania waache ubinafsi kama wanataka kuboresha kazi zao na wanapaswa watafute watu wenye uwezo mzuri wa kutunga stori watakaoisuka stori vizuri kuliko kulazimisha kufanya kazi hiyo wao wenyewe kwani endapo yatakosekana niliyoyainisha lazima filamu itapwaya, na ndo haya tunayoyashuhudia kila siku kwenye filamu zetu.

Alamsiki

No comments: