Apr 13, 2011

Tatizo kubwa kwenye filamu zetu ni kukosa waongozaji

 Quentin Tarantino, mmoja wa waongozaji filamu 
wa Hollywood wanaoheshimika duniani

 Steven Kanumba, mmoja wa waongozaji filamu Tanzania

WIKI iliyopita msomaji mmoja wa makala zangu alinitumia ujumbe kupitia baruapepe akitaka kujua mtazamo wangu kuhusu mapungufu yaliyopo katika filamu za Kibongo, huku yeye akitupia lawama moja kwa moja kwa waigizaji na waandishi wa muswaada andishi (scriptwriters) kwa kutokuwa na uwezo.

Msomaji huyo aliyejitambulisha kwa jina la Masengwa, mkazi wa Kazima, Tabora alisema kuwa waigizaji wengi wa filamu za Kibongo wamekuwa wanashindwa kabisa kuuvaa uhalisia wanapoigiza! Akitolea mfano wa filamu moja (anaitaja jina) ambapo ilionekana mwigizaji akiigiza analia lakini uso wake ulikuwa umebeba tabasamu la chati!

Na kuongeza kuwa, kwenye filamu zetu si ajabu kuona tukio la utekaji nyara katika filamu huku mtekwaji akionesha dalili zote za kukaa tayari kwa kutekwa!

Msomaji huyo pia alitaka kujua nini maoni yangu kuhusu uandishi mbovu wa miongozo ya filamu hasa kwa kuwa mimi mwenyewe ninajitambulisha kama mmoja wa waandishi, ingawa yeye hakuficha hisia zake kwa kusema kuwa uandishi limekuwa tatizo kubwa kwenye filamu zetu, akisema kuwa stori mbovu kamwe haiwezi kutoa filamu nzuri hata kama wachezaji wa filamu hiyo watakuwa ni magwiji wa filamu kutoka Hollywood!

Nakubaliana naye kwa kiasi fulani japo mimi ninaweza kuwa na mtazamo tofauti kidogo. Kwa kifupi mimi hupenda kuiangalia filamu na kuupima uzuri wake kwa kuangalia mambo makuu matano: Mwongozo mzuri (script), Waigizaji wazuri, Wapigapicha wazuri, Muongozaji mzuri na Mhariri mzuri.

Naamini kuwa mwongozo mzuri wa filamu ni sawa na msingi imara wa nyumba unaotokana na ramani nzuri (stori). Kama mwongozo hautakuwa mzuri naamini hata filamu haiwezi kuwa nzuri kabisa, hii inamaanisha kuwa kwa script mbovu hata ukimleta Denzel Washington hawezi kucheza katika kiwango tulichozoea kumuona akicheza.

Waigizaji ni sawa na matofali yanayotumika katika ujenzi wa nyumba, huku wapigapicha nikiwafananisha na simenti na maji kwa ajili ya kujengea nyumba. Muongozaji ndiye fundi mjenzi, anayepaswa kuchanganya vizuri simenti, maji na mchanga ili kupata kile kinachotakiwa, hivyo bila kuwa makini nyumba haiwezi kuwa imara.

Bahati nzuri tasnia yetu imebarikiwa kuwa na waigizaji wengi wazuri, wapigapicha wengi wazuri na hata wahariri wengi wazuri, lakini inakosa waandishi wazuri wa script na waongozaji wazuri wa filamu.

Hii haimaanishi kuwa hakuna kabisa waandishi au waongozaaji wazuri hapa nchini, wapo wengi tu wenye uzoefu na elimu ya kutosha katika uandishi na uongozaji wa filamu, tatizo ni mfumo uliopo unaowafanya kutupwa nje ya ulingo wa soko la filamu kwa kuwa hawathaminiki, hawatumiki wala hawapewi heshima inayostahili.

Ile hoja ya kuwa uandishi wa script ni tatizo kubwa kwenye filamu zetu, ina mantiki hasa kwa kuwa mwongozo wa filamu ni moja ya vipengele muhimu sana katika uandaaji wa filamu na michezo ya kuigiza na dhana ya kuwa script ni hatua ya mwanzo, ni ramani ya kutuongoza kutoka kwenye wazo (concept) hadi kazi inapokamilika (final edit).

Lakini watazamaji walio wengi hukimbilia kumlaumu mwandishi wa script pindi filamu inapokuwa mbaya, ikisababishwa na kutoelewa nani hasa mwenye jukumu la kuhakikisha filamu inakuwa nzuri. Hapa ndipo script inapokuwa chanzo cha mahusiano mabaya (a hate relationship) kati ya mwandishi na muongozaji wa filamu.

Uhusiano mbaya huja pale muongozaji wa filamu anapoamua kubadili baadhi ya matukio ndani ya script, wakati mwingine hubadili sehemu kubwa ya script bila hata kumshirikisha mwandishi na hivyo kuvuruga mtiririko mzima wa stori. Kitendo hiki kinaweza kusababisha kuzalishwa hadithi tofauti kabisa na iliyoandikwa mwanzo ingawa jina la mwandishi litabaki lilelile. Haya yamekuwa yakitokea sana, binafsi yamenikuta na nimeshawahi kushuhudia yakitokea hata kwa waandishi na waongozaji wakubwa duniani.

Mwandishi ndiye mtu wa kwanza anayeiona sinema wakati akiandika, muongozaji huiona pale anapopitia script ili kuongoza upigaji picha (
shooting). Tatizo linakuja pale muongozaji anapoiona kwa jicho tofauti. Filamu ikiwa mbaya lawama humwangukia mwandishi kama ambavyo msomaji ameelekeza lawama zake.

Kwa kawaida filamu ni zao la muongozaji na wala si la mtayarishaji, mwandishi au muigizaji kama ambavyo wengine wanadhani. Katika makala ya leo nitajaribu kujikita zaidi katika kumwangalia muongozaji wa filamu na mchango wake katika kufanikisha kazi nzima.

Hoja ya kwamba waongozaji wa filamu za Kibongo hawakusoma ndiyo maana wanashindwa kuongoza inaweza isiwe sababu ya msingi, kwani hata Hollywood kuna waongozaji ambao hawakusoma kabisa lakini bado wamekuwa waongozaji wazuri na wanaoheshimika sana duniani.

Waongozaji ambao hawakwenda shule ni pamoja na; Steven Soderbergh, Robert Rodriguez, Quentin Tarantino (pichani), Richard Linklater, Spike Jonze...

Muongozaji wa filamu anapaswa kuwa mbunifu na kiungo muhimu kati yake na timu ya uzalishaji. Muongozaji anawajibika katika kutafsiri script iliyoandikwa kwenye karatasi na kuihamishia katika picha halisi na sauti kwenye skrini – na anapaswa kuiona taswira halisi na kutafsiri mtindo na muundo wa filamu, na hivyo kufanya kazi zote mbili kama kiongozi wa timu na msimulizi kwa kutoa picha halisi.

Tatizo kubwa lililopo kwenye tasnia ya filamu hapa Tanzania ni kwa waongozaji wetu wa filamu kudhani kuwa kazi ya uongozaji wa filamu ni kujua: “standby... action... cut!” na kusahau kuwa muongozaji ndiye anayepaswa kumtengeneza mhusika kwa kutegemea muongozo unasemaje. Kama muigizaji atashindwa kuvaa uhalisia, hilo sio kosa lake ni kosa la muongozaji na hutafsiri uwezo wa muongozaji ulipokomea.

Binafsi siwezi kumlaumu muigizaji anapochemsha, huwa namtupia lawama muongozaji wa filamu, kama muongozaji ni mzuri hawezi kukubali kuona muigizaji anashindwa kuvaa uhalisia kwa kuwa atamharibia kazi.

Nimewahi kuwauliza baadhi ya watazamaji wa filamu za nje (Hollywood au Bollywood) kuwa ukiona filamu ambayo mhusika mkuu ni mtoto mdogo, ambaye amefanikiwa sana kuvaa uhalisia kiasi kwamba unaweza kudhani hakuwa akiigiza, ina maanisha nini, ana akili nyingi kuwazidi watu wazima waliopo kwetu?

Kwa swali hilo utagundua kuwa muongozaji kafanikiwa kumtengeneza, kitu ambacho kinakosekana kwa waongozaji wetu wanaodhani ukijua kusema “action... cut... utakuwa umefuzu kuwa muongozaji wa filamu.

Muongozaji anapaswa kuwa na uelewa mkubwa katika kuitafsiri script na kuihamishia katika picha halisi na hata kupendekeza sauti zitakazotumika kwenye skrini, pia anapaswa kuangalia mtu anayefaa kuigiza, ndiyo maana mojawapo ya majukumu ya muongozaji ni pamoja na kufanya usaili (casting).

Wakati masuala muhimu katika utayarishaji wa filamu, kama vile fedha na masoko, hubakia mikononi mwa Mtayarishaji wa filamu (producer), Muongozaji anapaswa pia kuwa na ufahamu wa bajeti inayotumika kwenye filamu anayoiongoza na kujua ratiba. Katika baadhi ya filamu, Waongozaji huhodhi majukumu mengi kama Muongozaji/Mtayarishaji au Muongozaji/Mwandishi, jambo ambalo halikatazwi kama atakuwa na uwezo wa kuyatenda kwa ufanisi.

Sifa nyingine ya mtu kuwa muongozaji wa filamu ni kuwa na uelewa wa kina wa jinsi sinema inavyotengenezwa, kuwa na ubunifu mkubwa (creative vision), ufahamu wa namna ya kuandika script na kujitoa kwa dhati (commitment) katika kufanikisha. Muongozaji anahusika moja kwa moja kwenye mafanikio yoyote ya kisanii, mafanikio ya kibiashara au kushindwa kwa filamu katika soko.

Muongozaji anaweza kuandika script ya filamu au kusimamia uandikwaji baada ya rasimu ya awali ya script kukamilika. Baada ya kupata waigizaji, muongozaji husimamia mazoezi (rehearsals) na upigaji picha wa filamu (shooting). Muongozaji pia anapaswa kusimamia masuala ya kiufundi ya sinema, ikiwa ni pamoja na kamera, sauti, taa, ubunifu na kadhalika.

Wakati wa uhalili (post-production), Muongozaji hufanya kazi kwa ukaribu na Wahariri katika mchakato wa kiufundi wa uhariri, hadi kufikia mwisho wa kazi. Katika hatua zote, Muongozaji anawajibika kuhamasisha timu yake kutayarisha kazi bora. Muongozaji pia anapaswa kuyafahamu mahitaji na matarajio ya soko la filamu.

Mwisho, muongozaji awe na uwezo wa kufanya mawasiliano (communication skills) na watu wengine katika kufanikisha.

No comments: