Apr 20, 2011

Wasanii kukubali kutumiwa kisiasa ni kujimaliza wenyewe

 Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF), 
Simon Mwakifwamba

 Msanii maarufu na Mbunge wa jimbo la Mbeya Mjini,
Joseph Mbilinyi maarufu kwa jina la Sugu

HISTORIA huwa haina haja na wale wote wenye kushindwa, labda tu kunukuu tarehe walizokutwa na umauti wao... na hii kidesturi huwa ni katika kila fani.” Ni msemo nilioufahamu miaka mingi iliyopita, na ninaamini una maana kubwa mno kwa yeyote anayejiita mwanaharakati.

Tasnia ya filamu hapa Tanzania ilikuwa ikipiga hatua siku hadi siku, lakini kwa siku za karibuni imeonekana kudorora. Kiukweli sanaa hii ipo chumba cha wagonjwa mahututi ikisubiri kupelekwa mochwari hasa kwa hiki kinachojitokeza sasa ambacho kwangu ni kama mazingaombwe.

Ule msemo kwamba wasanii wa Tanzania hawakwenda shule ndiyo maana upeo wao ni mdogo siupendi japo unaweza kuwa na maana katika jambo nililokusudia kulieleza. Fikra iliyojengeka kwamba Sanaa ni kipaji ni jambo ambalo nakubaliana nalo kwa asilimia zote, lakini ieleweke kuwa mbali ya kuwa ni kipaji, Sanaa ni taaluma pia.

Sanaa ya filamu hapa Tanzania kwa miaka mingi imekuwa ni kati ya fani zisizo na vigezo vya kupima utaalam na ubora, kwa maana nyingine haichukuliwi kama taaluma, nadhani ndiyo maana serikali imekuwa haiipi umuhimu unaostahili.

Inasikitisha sana pale maisha ya Wasanii yanapokuwa ya neema kwa muda fulani tu, hasa pale wanapotumiwa na wanasiasa kwa maslahi ya wanasiasa katika kufanikisha jambo lisilowahakikishia uhakika wa soko la kazi zao, wakati ambapo mipango mingi isiyotekelezeka hujitokeza, na kwa sababu wasanii hawajui nini wanachokihitaji na muda upi, hujikuta wakinasa kwenye chambo.

Kwa miaka miwili iliyopita kulikuwa na vuguvugu kubwa la wanaharakati wa filamu kupigania haki yao ili soko la filamu liweze kuleta tija miongoni mwao. Katika harakati hizo ambazo mimi nilikuwa Katibu Mkuu, hatimaye tulifanikiwa kuanzisha shirikisho la filamu (TAFF), lililoonekana kuwa mkombozi wa matatizo ya wasanii na watengeneza filamu nchini.

Wakati huo tulisukumwa na uzalendo wa kutaka kuliokoa soko letu na majangili wa kazi za sanaa, lakini hadi sasa soko bado ni kitendawili. Inasikitisha kuona mtu anatengeneza filamu lakini anaishia kulandalanda na filamu yake mkononi huku wasambazaji wakiwa hawaitaki kwa kuwa tu hakuchezesha wanaoitwa ma-
SuperStar bila kujali ubora wa filamu husika.

Ninachokiamini katika ukombozi wa wasanii ni kuwa na Umoja wa kweli, wenye nguvu utakaohakikisha kilichokusudiwa kinafanyika huku wanaoongoza wanakijua na kunakuwepo mikakati endelevu katika ustawi na maendeleo ya sanaa. Lakini badala yake kumekuwepo chuki, majungu na ubinafsi miongoni mwao.

Kwa muda mrefu nimekuwa nikijaribu kuipigania sanaa hii irasimishwe, wasanii watambulike na wawezeshwe, lakini inakuwa vigumu kwa fani yoyote kukua kama hakuna vigezo vya upimaji wa ubora. Mchakato wa kurasimisha tasnia siyo jambo gumu, kinachotakiwa ni nia na uelewa wa wadau wa sanaa wakiongozwa na viongozi wa serikali ambao wamepewa jukumu la kufanikisha kile kinachoitwa maisha bora kwa kila Mtanzania.

Nimewahi kuiandikia serikali kuhusu mambo muhimu ya kuzingatia kama kweli ina nia ya dhati kuiboresha tasnia ya filamu. Ukweli unabaki palepale; kazi yoyote ya sanaa inahitaji mazingira bora ili iweze kustawi, mazingira bora kwa msanii ni ulinzi wa kazi zake, kuwezeshwa ili afike anapohitaji, soko la uhakika pamoja na kuthaminiwa. Tasnia hii inakabiliwa na matatizo makubwa ikiwemo kudhulumiwa, kuibiwa, kupata fedha kiduchu baada ya mauzo ya kazi, Serikali kutoweka mazingira mazuri ya kuwasaidia kuishi na ukosefu wa mitaji.

Hata hivyo hali ya kutokuwepo vigezo vya kupima utaalam wa fani kunafanya wasanii waendelee kuwa duni, wasiothaminika na kubaki katika sekta isiyo rasmi ambayo haiwezi kuchangia maendeleo ya taifa. Urasimishaji wa tasnia ya burudani utabaki kuwa ndoto ya mchana kwa wasanii, lakini kwa wafanyabiashara ni neema kwani hali hii inawapatia faida kubwa bila jasho.

Ni wazi hakuna taaluma isiyo na muongozo, mipaka, miiko na maadili katika utendaji. Sanaa ni moja ya taaluma ingawa si hivyo kwa Tanzania.

Mapema wiki hii kulikuwa na mkutano mkubwa wa kibiashara kwa nchi za Afrika Mashariki, mkutano ulioandaliwa na Baraza la Biashara la Jumuiya ya Nchi za Madola kwa kushirikiana na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC).

Mkutano huo na mikutano mingine mingi imekuwa inafanyika, lakini hakuna wasanii waliowahi kuhusishwa katika kujadili fursa za soko la filamu au muziki. Au tasnia ya burudani haiwezi kuchangia ukuaji wa pato la nchi kama zilivyofanikiwa nchi nyingine? Sijui kama serikali inatambua kivitendo mchango wa sanaa ya filamu, licha ya kuwa imeshatoa ahadi nyingi za kuisaidia iweze kukua.

Hivi sasa wale wanaharakati waliojizolea umaarufu kipindi kile cha kupigania uundwaji wa shirikisho, wengi wao wamegeuka kuwa wasaliti wa shirikisho wakiongozwa na chuki binafsi dhidi ya kiongozi aliyepo madarakani.

Hali hii ilianza mara tu baada ya uchaguzi uliowaweka madarakani rais wa shirikisho hilo, Simon Mwakifwamba na wenzake huku baadhi ya waliokuwa wakishikilia nafasi kubwa ndani ya shirikisho hilo (nikiwemo mimi) kukosa nafasi katika uongozi mpya.

Hali hii iliamsha makundi, uhasama, majungu na fitina. Mambo yaliharibika zaidi baada ya mechi ya hisani iliyochezwa Uwanja wa Taifa kuchangia waathirika wa mabomu ya Gongolamboto, kati ya wasanii wa filamu na wasanii wa muziki. Uhasama ukishinikizwa na watu fulani (majina ninayo) kuigeuza ajenda ya ukombozi wa wasanii kuwa vita dhidi yao na msanii mmoja maarufu ambaye kwa sasa ni Mbunge wa jimbo moja.

Inashangaza kuona wasanii wanaacha kupigania haki zao ikiwa ni pamoja na soko la bidhaa zao na kujiingiza kwenye masuala tofauti kama soka, ingawa naamini mazoezi ya mpira yanayoendelea ni kiinimacho tu, kwani kuna ajenda muhimu inayozungumziwa kila wakutanapo.

Inaaminika kuwa kauli ya mbunge huyo kuwataka Watanzania kuwahukumu wasanii ambao walikipigia debe chama tawala, kwa kutoingia kwenye matamasha yao imegeuka mwiba kwa baadhi ya watu.

Mbunge huyo ambaye ameshawahi kuigiza katika filamu ya Bifu aliyasema hayo alipozungumza na halaiki ya watu waliojitokeza kwenye maandamano makubwa ya chama chake huko Kanda ya Ziwa. Binafsi siwezi kumlaumu kwa kuwa hakuna mwanasiasa yeyote anayeweza kukiunga mkono chama anachopingana nacho.

Hatua ya wasanii kuchangisha pesa (fund raising) kwa kile wanachodai dhamira yao ya kutangaza Amani ndani ya nchi ina jambo nyuma ya pazia. Kuhimiza amani nchini ni jambo jema sana lakini si kutumika kupambana na msanii mwenzao kwa maslahi ya kisiasa jambo ambalo nalitafsiri kama kutoitendea haki tasnia ya burudani.

Wasanii ni kioo cha jamii, wanao uwezo mkubwa wa kufikisha ujumbe kwa jamii moja kwa moja kwa njia ya maigizo na kazi nyinginezo. Lakini, kutumika kwa mambo yasiyo na tija kwa taifa ni jambo nitakalolipinga hata kama litayagharimu maisha yangu.

Katika masuala ya jamii na pale wanapohitaji msaada, wasanii wanapaswa watafute njia sahihi na si kushabikia kulinda maslahi ya baadhi ya watu. Kufuatia mikakati na harakati walizonazo sasa utatambua kuwa wanaowaongoza pia hawajui wanahitaji nini?

Wasanii wanapaswa kupima faida za kujipendekeza kwa wanasiasa, wanapaswa kuwa makini sana la sivyo watajikuta wanapandikiza mbegu za kujimaliza. Hivi kweli hii ni sahihi wasanii kujadili jinsi ya kuwaangamiza wasanii wenzao? Au ndiyo hadithi ya mpini kutumika kwenye shoka kukata miti mingine?

Baada ya kupata shirikisho, nilitegemea wasanii wangeanza juhudi za kujikomboa lakini badala yake imekuwa mwanzo wa makundi, fitina, matusi, chuki na hata ukiukaji wa sheria na taratibu za utendaji kazi, vikiongozwa na walioukosa uongozi ambao wanadhani wanayo hakimiliki ya kuwa viongozi.

Hivi sasa wasanii wamekuwa watu wa kujikomba na kubembeleza ufadhili na wakati huohuo kulaumu kutothaminiwa na serikali. Vyama vya kisanii vimekuwa vikisajiliwa na kufa na kwa mwendo huu hawataweza kuifikisha sanaa mahali popote pa kuthaminiwa kwani ndani yake kumejaa unafiki na kutoambiana ukweli.

Na hata pale baadhi ya wasanii walipojitokeza kuwaambia ukweli wamechukiwa, kutukanwa na kutengwa, hali inayoashiria mgawanyiko mkubwa katika tasnia. Wasanii wamebadilisha ajenda, badala ya kupigania maslahi ya tasnia ya filamu sasa wanapanga kuzunguka nchi nzima kumpiga vita msanii mwenzao!

Hii si haki hata kidogo.

No comments: