Apr 11, 2011

Athari ya filamu za Magharibi katika nchi zinazoendelea

 Original Sin, mojawapo ya filamu maarufu za Kimagharibi zinazoathiri utamaduni wetu

TAFSIRI ya filamu ni mfululizo wa picha zinazoonesha mwendo wa watu au vitu na kuonekana mbele ya watazamaji kwenye skrini. Ni aina ya mawasiliano yanayotumiwa kutolea hadithi au kuwafundisha watu kuhusiana na fikra au mitazamo mipya katika jamii. Wafuatiliaji wa filamu huangalia filamu ambazo zinaelezea hadithi fulani kama njia mojawapo ya kuburudika, kujifunza au kwa sababu ya upenzi tu.

Filamu zilizoibuka kuanzia karne ya kumi na tisa, zimekuwa kishawishi kikubwa na mawasiliano ghali katika karne hii ya ishirini na moja. Hadi sasa hakuna aina nyingine yoyote ya sanaa ambayo imesambaa kwa ufanisi mkubwa na kuvuka mipaka ya kiutamaduni katika mataifa mengi kama ilivyo kwa filamu.

Katika karne ya ishirini na moja teknolojia ya televisheni na maonesho mbalimbali ya wajasiriamali vimeitangaza sana tasnia ya filamu kwa watu wote; watazamaji wa mijini na vijijini katika nchi nyingi zinazoendelea. Hata hivyo, filamu nyingi zinazosambazwa kimataifa na kupenya soko la nchi nyingi ni zile zinazozalishwa nchini Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya. Ukweli huu, pamoja na kutambua nguvu ya filamu “inayoyumbisha mioyo na akili za watu” unaamsha wasiwasi kwa wachambuzi walio wengi.

Tangu miaka ya 1960, mjadala kuhusu filamu kutumika kama chombo cha “ubeberu wa kitamaduni” na nchi za Magharibi umekuwa mkubwa, na umefanikiwa kwa kiasi kikubwa si kinadharia tu.

Filamu pia zimekuwa zikitumika kama njia muhimu ya uchumi, hali iliyopelekea filamu kuwa nyenzo muhimu sana itumiwayo na nchi za Ulaya na Amerika. Marekani ilipata udhibiti wa haraka wa soko la filamu mara tu picha za sauti zilipoanza; nchi nyingine chache sana wakati huo ziliweza kumudu kuwa na vifaa bora vya uzalishaji wao kwa haraka kama ilivyokuwa Marekani.

Mwanzoni mwa miaka ya 1970, dunia ilishuhudia utengenezwaji wa sinema zipatazo 3,500 kila mwaka. Ingawa ni asilimia tano tu ya sinema hizi zilitengenezwa Marekani, lakini filamu za Marekani ndizo zilizochukua asilimia 50 ya muda katika vituo mbalimbali vya televisheni katika kile kinachoitwa “Dunia Huru”. Hali hii haijabadilika sana hata sasa.

Mafanikio ya masoko ya filamu na televisheni ya Marekani kwa kiasi kikubwa yametokana na chombo chao muhimu kinachoitwa Motion Picture Export Association (MPEA), mkusanyiko wa makampuni ya Marekani, Vyama vya Wasanii na Makapuni makubwa ya Universal na Warner Brothers. Nusu ya mapato ya makampuni haya hutoka nje ya Marekani.

Nafasi ya mauzo ya MPEA inatiwa nguvu na rasilimali ndogo ya makampuni ya uzalishaji kutoka nchi zinazoendelea. Gharama kubwa ya kutengeneza filamu imepelekea kwa nchi zinazoendelea kushindwa kuingia kwenye ushindani na nchi za Magharibi na hivyo kuwafanya kuwa waagizaji wakubwa wa vipindi vya televisheni kutoka Marekani au kununua filamu kutoka Marekani kuliko kutengeneza filamu zao wenyewe.

Kwa mfano, nchini vipindi vingi vya televisheni kutoka Marekani ya Kaskazini, na sasa Amerika ya Kusini (Mexico, Venezuela, Brazil na kadhalika) vimekuwa vikinunuliwa sana na hugharimu kati ya dola 1000 hadi 2000, wakati kipindi kimoja kinachozalishwa ndani ya nchi hii hugharimu kati ya dola 800 hadi 2,400. Aidha, kazi za ndani huwa za kiwango na utaalam duni kulinganisha na kazi za nje.

Matokeo yake, watazamaji wa filamu wengi katika nchi zinazoendelea wanavutiwa na mambo ya kitaalam yaliyomo katika filamu za kigeni kuliko zilizotengenezwa kwa kiwango duni za ndani. Filamu za Magharibi hata hivyo zinachukua sehemu kubwa ya muda katika vituo vya nchi kama vile India, Pakistan, Bangladesh, Ufilipino, Uturuki, Thailand, Korea ya Kusini na nchi za Kiafrika.

Nchini Malaysia, filamu za kigeni zinachukua asilimia 99 ya soko. Thailand makampuni ya kigeni yanahodhi sekta ya usambazaji, kwa miaka mingi wazalishaji wa ndani wamekuwa wakilazimika kutoa rushwa kwa wamiliki wa majumba ya sinema ili sinema zao zioneshwe.

Kusambaa kwa wingi kwa filamu zenye maadili ya Magharibi katika nchi zinazoendelea inachukuliwa kama hali ya kutiliwa wasiwasi na makundi mengi, kwamba hatimaye filamu hizo zinaweza kubadilisha hali ya kisiasa na kiuchumi ya nchi zinazoendelea na kubadilisha mitazamo yao ya maisha. Kama mipango madhubuti haitaweza kufikiwa na serikali zetu, hofu za wengi kuhusu ukandamizaji wa kisiasa zitaongezeka.

Filamu huweza kutoa ujumbe tofauti kwa kila mtazamaji na huweza kushawishi na kutoa taswira ya kipekee kwa kila mtu binafsi, hivyo, tunapaswa kuwa makini na kupima matokeo ya athari zinazosababishwa na filamu zinazoweza kupatikana ama kwa mtu binafsi au watazamaji wote.

Mtazamo wa filamu za Magharibi na hasa Hollywood kuhusu nchi zinazoendelea ni wa kisiasa kabisa. Filamu hizo hutengenezwa kwa malengo maalum na huweza kuacha athari za miongoni mwa watazamaji.

Tafiti chache zilizofanywa zimeonesha kuwepo ushawishi mkubwa wa filamu katika majukumu ya kijamii na mahusiano katika jamii ya nchi zinazoendelea, na hata umakini kidogo umetumiwa kama kigezo katika matumizi ya filamu kama njia ya kuchangia au kubadilisha nguvu ya miundo iliyopo ndani ya mataifa haya au kati ya vikundi vya kikabila au makundi ya kisiasa.
Baadhi ya wachambuzi wanasema kwamba kama utamaduni wa asili utaridhia mahitaji ya watu, ni jamii ndogo tu ya watu itakayobaki imara kwenye maadili yanayotishiwa na vyombo vya habari vya kigeni. Nadharia hii haitavutiwa na mawazo ya kigeni ya filamu na televisheni katika jumuiya na nguvu ya matokeo ya filamu vinapowekwa pamoja na mambo mengine ya Kimagharibi, kuanzia kwenye uagizaji vitu hadi kwenye utalii.

Tafiti zingine kuhusu kubadilishana tamaduni zimegundua kwamba yatokanayo na vyombo vya habari vya Magharibi yanaongezeka katika kuleta mafanikio/ athari kwa mtu mmoja mmoja, elimu na kuongezeka kwa uwezo wa uelewa. Utafiti huu ni muhimu; wakati vijiji na miji katika nchi zinazoendelea ikizidi kuwa na mtandao mpana wa upatikanaji wa filamu za Magharibi na video, nchi nyingi za Magharibi wana nafasi finyu sana ya kuona hali halisi ilivyo katika vijiji na miji ya nchi zinazoendelea ili kuwezesha kuwa na uelewa unaofanana.

Filamu za nje zinazopatikana nchini Marekani nyingi hutengenezwa katika nchi za Ulaya, mara nyingi kwa ufadhili wa Marekani yenyewe. Fedha za Marekani hutolewa kwa malengo maalum kwa filamu nyingi zinazoonekana kuwa za Uingereza, Ufaransa, au Italia. 'Kimaono,' hata hivyo, inaonesha dhahiri kuwa hufanywa hivi kwa faida ya nchi za Magharibi.

Wachambuzi wengi wa nchi zinazoendelea wanahofu kwamba nchi zetu sasa zijiandae kupoteza kilicho chao na kupokea mambo na tamaduni za kigeni na kuwa katika hatari ya kuendeleza mazao ya Magharibi badala ya tamaduni zetu.

Kumekuwepo majaribio ya kutaka kuzuia ubeberu wa kitamaduni katika nchi kadhaa zinazoendelea, serikali nyingi za nchi zinazoendelea zimejaribu kuhamasisha tasnia za filamu kitaifa na kutafiti utengenezaji filamu wa ndani kwa ajili ya maendeleo ya taifa na malengo ya kiitikadi. Kuanzishwa kwa vyombo vya kusimamia, ambavyo mara nyingi huitwa 'vyombo vya kitaifa vya utamaduni,' kunaweza kuwa na nguvu ya kukagua mawakala au mambo yasiyoridhisha yanayopaswa kudhibitiwa.

Utamaduni wa nchi ni “kidhibiti mwendo” kinachoongoza mwenendo na tabia za watu katika jamii, ni msingi wa maisha ya mtu binafsi kumuwezesha kujitambua, kuwa na mwelekeo na kujichagulia falsafa sahihi ya maisha yake.

Nchi zinapswa kuanzisha sera muhimu za kulinda haya ili kudhibiti umilikaji wa wageni wa kuagiza vitu toka nje, kupiga marufuku filamu zinazoingizwa kiholela, ukaguzi wa mara kwa mara, udhibiti wa maudhui ya filamu na tamthilia, na kutoa ruzuku kwa watengenezaji filamu wa ndani. Kufuatia sera hizi umma uelimishwe kikamilifu juu ya sera hizi ili uweze kushiriki katika utekelezaji kwa upana wake. Pia ushirikishwaji wa vyombo vya habari katika kusaidia msukumo wa wananchi kuielewa sera ya utamaduni upewe nafasi ya kutosha.

Jambo muhimu na la msingi ni kuzingatia, kuzitambua na kuzilinda sanaa zetu ili zisipoteze uasili wake pamoja na wimbi la mabadiliko ya wakati na mazingira ya sasa ya utandawazi na biashara huria.

Mara nyingi sana, majaribio ya kutaka kudhibiti sekta ya filamu yamethibitisha kushindwa. Ruzuku ya serikali kwa uzalishaji wa ndani ndiyo njia pekee ya kuongeza kiasi cha uzalishaji wa ndani, ingawa inaweza isiongeze ubora wa filamu kama soko la filamu halitadhibitiwa.

No comments: