Apr 27, 2011

Ramsey atoa somo kwa waigizaji filamu bongo

 Ramsey Noah katika pozi

Wasanii wa Tanzania wakiwa na muigizaji kutoka Nigeria, 
Ramsey Noah.

MSANII maarufu wa Nollywood, Ramsey Noah Atashirikiana na muigizaji maarufu wa filamu nchini, Steven Kanumba katika filamu ya Devil's Kingdom. Ramsey ambaye yupo jijini, atashiriki katika filamu hiyo ambayo imeandaliwa na Kanumba na kwa sasa iko hatua za mwishoni za maandalizi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana katika mkutano uliofanyika hoteli ya Peacock jijini, Ramsey alisema amefurahishwa kushirikishwa kucheza filamu hiyo na Kanumba kwani anaamini ushiriki wake utakuwa chachu na changamoto kwa wasanii wa hapa nchini.
“Nimefurahi sana, hii itakuwa ni mara ya pili kushiriki na Kanumba kucheza filamu na kwa kufanya hivi kama Waafrika tunapanua wigo wa ubora wa kazi kwani kila mmoja anajifunza kutoka kwa mwenzake.

“Lakini katika soko la filamu pia tunakuwa tumejiongezea watazamaji hivyo kuongeza soko la kazi zetu kwa sababu kila nchi itahitaji kununua kuona kazi za msanii wao na kwa namna hiyo watazamaji wanajifunza mambo mengi mfano lugha za nchi husika kwa sababu hata mimi kuna baadhi ya maeneo nimetumia lugha ya Kiswahili.

“Hii yote ni katika kupanua pia wigo wa lugha, lakini jambo ambalo ningependa kulitoa kama changamoto kwa waigizaji wa bongo ni waendeleze jitihada za kufanya filamu kwa ubora wa hali ya juu zenye hadhi ya Kimataifa zaidi na si ‘Local’ kama ambavyo binafsi naliona hilo ingawa kwa sasa wanajitahidi sana,” alisema.

Naye meneja masoko wa Steps Entertainment ambao ndio wasambazaji wa filamu hiyo, Simbiso Machine aliiomba Serikali kupitia Chama cha Hakimiliki (COSOTA) kusimama kidete kuzuia wizi wa kazi za sanaa hasa hizo za filamu kwani kwa sasa hali ni mbaya.
“Yaani inaumiza, sisi mwezi huu tulikuwa Singida na tulikamata karibu kopi 5000 feki na jambo hili linafanyika bila kificho hivyo kuendelea kuwaumiza wasanii na kuwarudisha nyuma,” alisema Simbiso.

Awali akizungumzia maudhui ya filamu hiyo, mtunzi wake, Steven Kanumba alisema inaelezea namna shetani alivyo na nguvu na ushawishi wa kuwashika watu Duniani hadi baadhi yao kuamini kwamba hakuna Mungu na ndio sababu wengi wanavutwa na kuingia katika ufalme wake inakuwa vigumu kujinasua.

Chanzo: www.newhabari.com

No comments: