MUZIKI ni chombo ambacho
kimewavutia wanadamu. Katika kutumia nyimbo, waimbaji wameweza kuhifadhi
historia na utamaduni wa jamii zao.
Muziki umekuwa ukitumika kama
njia mojawapo ya kujifundisha utamaduni na aghalabu hutumiwa katika kumwelezea
mtu, mazingira yake na jinsi anavyoweza kuyatumia na kuyatunza vilivyo.
Kama chombo ambacho hutumiwa
kuelezea historia ya jamii, muziki hutumiwa kupasha ujumbe maalumu kwa
wanajamii hasa kutoka kizazi kimoja hadi kingine na hutumiwa hasa kuelezea
historia, imani, itikadi na kaida zajamii.
Nyimbo kama zao la mazingira ya
jamii, zinaweza kufananishwa na mtoto ambaye hufinyangwa na mambo mengi katika
historia ya jamii yake.
Hata hivyo, muziki ni zaidi ya taaluma kama zilivyo
taaluma zingine za sheria, uhandisi, udaktari, usimamizi wa fedha, biashara na
kadhalika. muziki ni kipawa ambacho mtu hutunukiwa na Mungu.
Kipawa hiki
ni uwezo wa kiasili ulio ndani ya mtu katika maumbile, nafsi na roho yake. Kipawa
hiki kinatoka ndani yake. Ni tunu au zawadi mahsusi kutoka kwa Mungu, ambayo
hakuna anayeweza kumnyang’anya au kumuibia mpaka anapokufa.
Kwa
kawaida kila mtu ameletwa duniani kwa kusudi maalumu na la kipekee. Ili
kutekeleza kusudi hilo, Mungu kamjaalia kila mmoja kipawa chake, wengine
wamepewa vipawa vya uimbaji, uigizaji, ufundi, uchoraji, uchongaji, ususi,
uchezaji muziki, uchekeshaji, uchezaji michezo mbalimbali, ujasiriamali,
utabibu, ualimu, uongozi katika jamii, ugunduzi, uandishi n.k.
Unapovamia kipawa ambacho si cako
kwa vyovyote hutoweza kufika mbali, utakwama tu. Ndiyo maana wapo wanamuziki
wengi ambao wamewahi kutamba kwa muda mfupi kisha wakapotea, wapo walioimba
wimbo mmoja tu au nyimbo mbili na kupotea na wengine wakafanikiwa kutoa albamu
moja tu kisha wakapotea kwenye gemu.
Ila wengine wameweza kudumu kwenye gemu kwa muda wote bila kuchuja, na wengine wanawika hadi
leo hata baada ya vifo vyao miaka mingi iliyopita.
Mmoja
wa wanamuziki mashuhuri ambao wameweza kudumu kwenye gemu la muziki ni Aretha
Franklin, aliyejulikana kama ‘Malkia wa muziki wa taratibu Soul’, ambaye
amefariki dunia siku ya Alhamisi.
Aretha
Franklin alikuwa mwanamke wa kwanza kuchaguliwa katika Rock na Hall of Fame
amefariki dunia huko Detroit akiwa na umri wa miaka 76.
Mwanamuziki huyo alikuwa
anasumbuliwa na ugonjwa wa saratani ya kongosho tangu mwaka 2010 na alitangazwa
kuwa anaumwa mwaka jana wakati alipoamua kustaafu rasmi muziki.
Muziki wake ambao ulijulikana
zaidi ulikuwa ni 'Respect and Think' ambao ulikuwa katika nyimbo 20 bora
zilizopendwa zaidi nchini Marekani kwa miongo saba.
Aretha aliweza onesho lake la
mwisho mwezi Novemba mwaaka jana katika gala iliyoko mjini New York akiwa amesaidiwa na
taasisi ya Elton John ya ‘Elton John Aids Foundation’.
Hata hivyo, Aretha Franklin aliishi maisha ya ‘mateso ya kimya kimya’ na miongoni
mwa siri za maisha ya Franklin zilizomfanya kupenda kuishi maisha ya “faragha sana,”
ni jukumu lake kama mama, jambo lililokuwa moja ya mambo yaliyomfanya nyota huyo
kuwa na maisha ya faragha sana.
Malkia huyu wa Soul alikuwa na watoto wanne, huku mtoto wake
wa kwanza akiwa amempata akiwa katika
umri wa miaka 12 tu.
“Alikuwa na maisha magumu sana utotoni,” David Ritz, mwandishi
ambaye aliandika wasifu mara nyingi juu ya maisha ya Aretha Franklin
alibainisha hayo kabla ya kifo cha nyota huyo.
Maisha magumu ya utotoni ya mwimbaji huyo wa “(You Make Me Feel Like) A Natural Woman” yalisababishwa
na kutengana kwa wazazi wake, mama yake Barbara na baba yake Clarence LaVaughn,
jina ambalo aliamua kumpa mtoto wake wa kwanza, hii ni kwa mujibu Respect,
kitabu cha Ritz kinachohusu maisha ya Franklin.
Mama yake Franklin aliondoka nyumbani akiiacha familia wakati
mwimbaji huyo alipokuwa na umri wa miaka 6 tu kwa sababu ya kuchukizwa na mumewe
aliyekosa uaminifu.
“Alijaribu sana kuonesha kuwa aliishi maisha ya furaha na
watoto wenye furaha na kila kitu kilikuwa kizuri, na hadithi nyingine zozote
kinyume cha hayo ziliweza kumkasirisha sana,” alibainisha Ritz kwenye kitabu hicho
cha Respect.
Franklin alikuwa hajawahi kuthibitisha hadharani kuhusu baba
wa mtoto wake mkubwa aitwaye Clarence mwenye umri wa miaka 63, lakini Ritz aliweza
kufichua siri hiyo katika kitabu chake kwamba baba wa Clarence, aliitwa Donald
Burke, ambaye walijuana na Franklin tangu shule.
“Aretha alirudi shuleni baada ya kumzaa Clarence,” dada ya nyota
huyo wa muziki, Erma alibainisha kwenye kitabu cha Respect. “Alikuwa mwanafunzi
mzuri ambaye alifanya vizuri katika madarasa yake yote.”
Miaka miwili tu baada ya kumzaa Clarence, Franklin alimpata mtoto
wake wa pili, Edward, ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 61.
Franklin hatimaye akaamua kuacha shule ili azingatie kipaji chake
cha muziki, kilichomfanya kuishi maisha ya “mateso ya kimya kimya,” kama ambavyo
dada yake Erma anaelezea kwenye kitabu hicho.
“Tulikuwa sehemu ya kizazi hicho cha waimbaji wadogo wa kike
ambao kwa hakika walijitolea muda wao pamoja na watoto wetu kuhudhuria kwenye kazi
zetu. Tulifanya hivyo kwa kufahamu,” dada mkubwa wa Franklin alinukuliwa kwenye
kitabu hicho. "Pia tulifanya hivyo tukiwa na hatia.”
Kuwatunza watoto wake wawili ilikuwa ni kazi ngumu sana kwa “Mama
Mkubwa,” yaani bibi wa Franklin, kwa mujibu wa biografia ya mwaka 2015 ya
maisha ya Franklin.
“Nilitamani sana kutoka na kwenda matembezi na rafiki zangu,” Franklin
aliwahi kuliambia jarida la Ebony mwaka 1995 kuhusu umama wake katika umri mdogo.
“Nilitaka kuwa katika sehemu mbili kwa wakati mmoja. Lakini
bibi yangu alinisaidia sana, na dada yangu na binamu yangu. Walijitahidi kuwalea
watoto wangu ili nipate nafasi ya kutoka mara kwa mara.”
Akiwa na umri wa miaka 19, Franklin aliolewa na Ted White, na waakapata
mtoto wa kiume aliyempa jina la Ted “Teddy” White, Jr., ambaye sasa ana umri wa
miaka 54.
Ted na mwimbaji huyo wa soul waliachana mwaka 1969 baada ya
taarifa za unyanyasaji wa ndani kufichuka, kwani mwaka 1968 makala ya jarida la
Time ilielezea jinsi ambavyo Ted “alimtendea visivyo” mwanamuziki huyo zaidi ya
mara moja.
Ted White, Jr. alijiingiza kwenye muziki na kumpigia gitaa mama
yake, Franklin, kabla ya kuamua kuanzisha muziki wake kwa jina la Teddy
Richards.
Mtoto mdogo zaidi wa Franklin, aitwaye Kecalf mwenye umri wa
miaka 48, alizaliwa mwaka 1970. Jina lake linawakilisha kifupi cha majina
kamili ya baba yake na mama yake - Ken E. Cunningham na Aretha Louise Franklin.
“Tumempoteza bibi, malkia na mwamba wa familia yetu,” familia
ya mwimbaji huyo iliandika katika taarifa rasmi. “Upendo aliokuwa nao kwa
watoto wake, wajukuu, wapwa, na binamu zake haukuwa na mfano.
“Tumeguswa sana na upendo wa ajabu na sapoti ambayo tumeipata
kutoka kwa marafiki wa karibu, wafuasi na mashabiki duniani kote,” familia yake
iliendelea kuandika.
"Asanteni kwa upendo na sala zenu. Tumeuona upendo wenu
kwa Aretha na inatuletea faraja kujua kwamba alama yake itadumu.
Tunapohuzunika, tunawaomba muheshimu faragha yetu katika wakati huu mgumu.”
Aretha alizaliwa Memphis na
alianza kuimba kama muimbaji wa nyimbo za dini na mpiga kinanda na alikuwa
muhubiri katika sherehe za ubatizo.
Franklin alianza kufundishwa
katika umri mdogo kuwa nyota wa muziki wa dini kama ilivyokuwa kwa Mahalia
Jackson na Clara Ward.
Alihangaika sana kupata
umaarufu katika umri mdogo akiwa chini ya rekodi za Columbia ambazo
zilijitahidi kuondoa aibu aliyokuwa nayo na kuiweka sauti yake inayovutia
kuweza kung'ara duniani.
Mwanamuziki Elton Jon ameandika
salamu zake za pole katika ukurasa wa instagram na kusema kuwa kifo cha Aretha
Franklin kimeshtua kila mmoja anayependa muziki wa kweli.
“Sauti yake ilikuwa ya kipekee,
jinsi alivyokuwa anapiga piano kwa ufanisi... nilimpenda na nilikithamini kipawa
chake. Mungu ambariki na salamu zangu za pole kwa familia," aliandika Elton
Jon.
No comments:
Post a Comment