Aug 12, 2018

King Majuto atabaki kuwa nembo ya tasnia ya ucheshi nchini



WASANII wakongwe na mahiri nchini wa sanaa ya maigizo, hususan wa vichekesho wanazidi kupukutika, na kuwaacha wasanii wachanga wakiwa katika mkanganyiko.

Nawakumbuka wasanii ambao walikuwa mahiri sana katika sanaa ya maigizo na vichekesho enzi za uhai wao na sasa hatupo nao ni pamoja na Ibrahim Raha (Mzee Jongo), Fundi Said (Mzee Kipara), Rajab Kibwana Hatia (Mzee Pwagu) na Ali Said Keto (Pwaguzi).

Wengine ni Hamis Tajiri (Janja au Meneja Mikupuo) Tunu Mrisho (Mama Haambiliki), Branco Minyugu, Bartholomew Milulu (Masawe), Said Ngamba (Mzee Small), Said Maulid Banda (Max) na wengine.

Wasanii hawa waliifanya sanaa ya maigizo, hususan ucheshi (comedy) kujizolea umaarufu mkubwa nchini na hivyo kuwafanya vijana wengi nchini kuingia kwenye sanaa ya vichekesho.

Rais John Magufuli alipokwenda kumjulia hali King Majuto katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili

Nakumbuka nikiwa mdogo tulizowea kusikiliza kipindi cha Mahoka, na vichekesho vya Pwagu na Pwaguzi vikirushwa Redio Tanzania (RTD), hakuna shaka kuwa hawa jamaa walikuwa vinara wa vichekesho kwa jinsi walivyoweza kupangilia vituko vyao japo tulisikia sauti tu.

Na hata waliokwenda kwenye kumbi mbalimbali za burudani, hasa jijini Dar es Salaam na miji mikubwa, walishuhudia burudani kutoka katika vikundi vya sanaa kama DDC Kibisa, Muungano Cultural Troup, Mandela Theatre, Bima Modern Taarab, Super Fanaka, Reli Kiboko Yao, JWTZ, Tancut Almasi, UDA, Urafiki n.k.

Kwa kweli kila mtu aliyekwenda kwenye kumbi za burudani alifurahia sana vichekesho vya kina King Majuto, Mzee Small, Branco Minyugu, Bartholomew Milulu, Mzee Jangala na wengineo.

Wiki hii tasnia ya vichekesho imepata pigo, tena ni pigo kweli kweli kwa msiba uliowagusa na kuwashtua wengi sana, wafuatiliaji na wasio wafuatiliaji wa sanaa ya vichekesho, hasa kutokana na kifo cha gwiji wa vichekesho ambaye umahiri wake ulikuwa wa hali ya juu.

Ni msanii mkongwe na maarufu nchini Tanzania na Afrika Mashariki, Mzee Amri Athuman maarufu kama King Majuto, aliyefariki dunia wakati akipokea matibabu kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam, majira ya saa 2 usiku wa Jumatano Agosti 8, 2018.

Mchekeshaji huyo veterani alikuwa amelazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili katika chumba cha wagonjwa mahututi kabla ya kufariki kwake.

Baada tu ya kifo chake watu maarufu ndani na nje ya Tanzania walituma salamu za rambirambi kwa familia yake kupitia mitandao ya kijamii, miongoni mwao akiwa Rais wa Tanzania, John Magufuli.

Rais Magufuli alisema kuwa King Majuto atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa na wa muda mrefu alioutoa kupitia sanaa ya uigizaji na uchekeshaji, ambapo alishiriki kuelimisha jamii, kuendeleza na kukuza sanaa na kuunga mkono juhudi za Chama Cha Mapinduzi na Serikali katika kuhimiza maendeleo.

Kwa kweli King Majuto alikuwa mfalme katika tasnia ya maigizo ya uchekeshaji nchini Tanzania na Afrika Mashariki, aliweza kujizolea umaarufu mkubwa kupitia namna ambavyo alikuwa akiigiza na kuwa miongoni mwa watu wenye mvuto mkubwa miongoni mwa wasanii.

Niliwahi kufanya kazi na King Majuto, iliyotufanya kuwa karibu sana kwa kipindi kirefu, ulikuwa mradi wa ‘Pamoko One Love’, uliohusu uelimishaji kuhusu watu wanaoishi na ualbino ukisimamiwa na Shirika la Under The Same Sun.

Katika kazi hiyo iliyowahusisha pia wasanii Chausiku Salum maarufu kama Bi Chau, Mrisho Mpoto na wanamuziki Khadija Shaban (K-Sha) ambaye wengi humwita Keisha na Faridi Kubanda maarufu kama Fid Q.

Katika mradi huo uliotufanya kuzunguka takriban mikoa kumi na mbili tukielimisha, kuonya na kuburudisha, mimi nilifanya kazi kama mtaalamu wa sauti.

Katika kipindi hicho nilijifunza mengi kutoka kwa King Majuto, hasa ucheshi, busara na namna alivyoweza kucheza na hadhira kiasi cha kuwa na mvuto wa aina yake.

Afya ya King Majuto ilizorota zaidi mwaka huu ambapo alipelekwa nchini India kwa matibabu baada ya Rais John Magufuli na wapenzi wa sanaa ya King Majuto kumchangia ili kunusuru uhai wake kabla ya baadaye kurejea nchini Tanzania.

Wiki chache zilizopita taarifa za uongo za kifo chake zilisambaa mitandaoni kabla ya familia yake kukanusha mara kwa mara.

Majuto aliyezaliwa mkoani Tanga Kaskazini mwa Tanzania mwaka 1948 alianza kuigiza akiwa na umri wa miaka tisa. Amecheza kwa mafanikio makubwa kwenye filamu mbalimbali zilizozidi kumpa umaarufu mkubwa, japo alikuwa maarufu hata kabla ya ujio wa televisheni nchini.

Kabla ya kifo chake tayari alikwisha wasamehe baadhi ya waandaaji na wasambazaji ambao inasemekana walikuwa wamemdhulumu mamilioni ya fedha baada ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe kutishia kuwashitaki watu hao.

Kwa kweli nilistushwa sana na msiba wa nguli huyu wa sanaa ya vichekesho ambaye kwangu alikuwa rafiki, nikiri kuwa japo binadamu tumeumbiwa kifo lakini mshtuko nilioupata hauelezeki.

Umati uliojitokeza siku ya Alhamis wakati wa kuagwa kwake pale katika ukumbi wa Karimjee na baadaye nyumbani kwake Tanga wakati wa mazishi yake ni ushuhuda tosha kwamba mzee huyu alikuwa kipenzi cha watu na alistahili kuitwa ‘King’, na tasnia ya filamu na maigizo ni sekta yenye nguvu kubwa sana, kama ingetumiwa vizuri ingeweza kuchangia pato kubwa mno.

Japo makala yangu ya leo imetokana na kifo cha King Majuto lakini hailengi kuzungumzia jinsi nilivyomfahamu nguli huyu bali kuangalia undani wa tasnia ya maigizo na vichekesho na mustakabali wake.

Kwa kweli wachekeshaji ni wasanii wenye umuhimu wa aina yake katika jamii. Ndiyo hutufanya tusahau uchungu wa maisha kwa jinsi ambavyo wanatuvunja mbavu tukiwasikiliza redioni, kuwaona kwenye televisheni au hata kukutana nao mitaani.

Miaka ya 1990 baada ya kuanzishwa vituo vya televisheni nchini, viliibuka vipindi vya ucheshi vya kina Mzee Small, King Majuto n.k. ambao nikiri kuwa walituburudisha sana.

Baadaye wakaibuka Max na Zembwela na 'Mizengwe' yao na kuendelea kutupa burudani kulingana na wakati. Kisha likaibuka kundi la Ze Comedy (EATV) lililosheheni wachekeshaji vijana waliouteka umma wa Watanzania kwa vichekesho vyao na staili ya aina yake.

Kuanzia hapo kukaibuka wasanii na vikundi vingi walioanza kuigiza kwenye runinga na kutoa filamu kila kukicha ingawa wengi wao walichoigiza ilikuwa ni mizaha na wala si vichekesho kama walivyotaka kutuaminisha.

Sanaa ya ucheshi ni sanaa yenye lengo la kufurahisha, kufundisha na kuburudisha watazamaji, katika televisheni, filamu, na kwenye majukwaa. Unapocheka ndivyo maisha yanavyokuwa bora zaidi!

Ucheshi ni mwanga unaouangazia moyo, ni igizo lililobuniwa kuchekesha, kuburudisha, na kumfanya mtu astarehe. Muundo wa ucheshi ni kuzidisha hali ya mambo ili kuleta uchekeshaji, kwa kutumia lugha, matendo, na hata wahusika wenyewe.

Ucheshi huhoji na kufuatilia yalipo mapungufu, makosa au hitilafu, na vitu vinavyokatisha tamaa ya maisha, na kuleta uchangamfu na wasaa wa kufurahia maisha.

Sanaa ya ucheshi kwa kawaida imegawanyika katika mifumo ya aina kuu mbili: comedian-led (wachekeshaji), kwa kutuletea vichekesho vilivyopangiliwa vizuri, utani au michoro na situation-comedies (sit-com) ambayo huelezea kisa kilichomo ndani ya hadithi inayosimuliwa.

Vipengele vyote vya ucheshi vinaweza kuonekana kwa pamoja na/ au kuingiliana. Pia kuna mfumo wa ucheshi unaojulikana kama 'Comedy hybrids' ambapo huenda pamoja na aina nyingine: musical-comedy (ucheshi kwa njia ya muziki), horror-comedy (ucheshi wa kutisha), na comedy-thriller (ucheshi wa kusisimua).

King Majuto aliweza kufiti kwenye aina zote hizi za ucheshi, kuanzia ucheshi wa papo kwa papo jukwaani hadi ucheshi wa kwenye runinga, kwa kuwa alikuwa na kipaji cha aina yake tofauti na wengine ambao hulazimisha kutuchekesha badala ya kutufanya tucheke.

Kwa mfano, niliwahi kushuhudia jinsi wasanii fulani wa vichekesho walivyokuwa wakihangaika kuchekesha papo kwa papo pale kwenye ukumbi wa Starlight!

Aina hii ya ucheshi wa papo kwa papo inahitaji kipaji na uelewa mkubwa sana wa jambo unalotaka kuliigiza ili lichekeshe, kwani kichekesho kinategemeana sana na tukio la papo kwa papo au lililotokea!

Hii ni kwa sababu sisi Waafrika kwa sehemu kubwa hutumia ishara, mifano katika hadithi na matukio ya kuchekesha. Ucheshi kwa kawaida huwa na mwisho wenye kufurahisha, ingawa wakati mwingine unaweza kuegemea mambo yanayosisimua au mabaya.

Sikatai, bado tunao baadhi ambao ni wachekeshaji wazuri sana lakini wengi wao wamekosa mwongozo na sidhani kama walipata nafasi ya kujifunza kwa hawa wakongwe ambao sasa wametutoka.

Wachekeshaji wetu walipaswa kujifunza kwa King Majuto ili kujua kilichomfanya abaki kwenye chati kwa miaka yote tangu alipoanza kuchekesha, na pia waongeze wigo wa ubunifu na kujifunza zaidi kama wanataka kuendelea kutusisimua.

Aidha nawashauri wajifunze kwa wenzetu, wawashirikishe wengine, wabadili mfumo, watafute maoni, watumie lugha sanifu, wazame ndani ya akili za watazamaji kujua mahitaji yao na wasome alama za nyakati.

Kinachoua sanaa ya ucheshi ni pamoja na kukosa ubunifu, dharau, kukosa malengo, kutojua watazamaji wanataka nini, na kulewa umaarufu.

Ndiyo maana nasema kuwa King Majuto atabaki kuwa nembo ya tasnia ya uigizaji wa vichekesho nchini Tanzania hata baada ya kifo chake.

No comments: