Aug 12, 2018

Hatuwezi kuitenganisha sekta ya sanaa na utalii


TANZANIA ni moja ya sehemu bora kabisa duniani ambazo msanii atafurahia kutengeneza filamu yake au kupigia picha za video kwa muziki wake, historia, utamaduni na wanyamapori.

Kuna hali ya hewa nzuri na watu wakarimu ambao wako tayari kumkaribisha mgeni katika mtazamo wa Kitanzania.

Imekuwa inashangaza kuona wasanii wetu wanakwenda kufanya video zao Afrika Kusini na Kenya, wakati Tanzania inashika nafasi ya pili duniani, nyuma ya Brazil, kwa kuwa na vivutio vingi vya utalii huku nchi ya Afrika ya Kusini ikishika nafasi ya 14.


Hii ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Shirika la Habari la CNN la Marekani. Hata hivyo, kulingana na utafiti huo, Tanzania katika mapato na miundombinu yanayotokana na sekta ya utalii inashika nafasi ya 110 kati ya nchi 133 duniani!

Tujiulize, ni kwa namna gani sanaa inaweza kuitangaza nchi? Hebu tuchukulie mfano wa Nigeria… tuanzie kwenye filamu zao, zimeweza kuwatangaza kwa kiasi gani? Tutapata jibu la haraka kwamba taifa hilo limetangazika kwa kiwango ambacho siyo cha kawaida wala cha chini.

Kama filamu za Nigeria zimeweza kuteka soko la Afrika na dunia, haiwezi kutufanya tuumize kichwa sana kujua kwamba taifa hilo limeweza kupata matangazo mengi kupitia sanaa ya maigizo, na zaidi kuvuta watalii kutoka pande mbalimbali za dunia.

Baada ya hapo, fikiria ni kwa kiasi gani kundi la muziki la P-Square limefanikiwa kuifanya Nigeria kuwa taifa linalotajwa mara nyingi na watu mbalimbali duniani kila yanapoibuka mazungumzo au majadiliano ya kukua kwa muziki barani Afrika? Je, tunaweza kuona matunda ya wanamuziki kufanikiwa?

Tangu mwaka 1983, Nigeria ilishaanza kung’ara kimataifa kupitia sanaa. Kuchomoza kwa mwanamuziki Sunny Ade, kisha kampuni kubwa ya muziki duniani ya Island Records kubeba jukumu la kutangaza muziki wa staa huyo, kuanzia albamu yake “Synchro-System” hadi ziara zake, kulifanya watu wa mataifa mbalimbali kuanza kuifuatilia Nigeria.

Ongezea mafanikio ya wanamuziki wa kizazi kipya: 2face Idibia, D’Banj, Davido, Wizkid, Iyanya na wengine wengi. Utapata jawabu ni kwa kiasi gani, sanaa imeiweka Nigeria kwenye ramani ya dunia.

Mamilioni ya watu huingia Nigeria kila mwaka kwa shughuli mbalimbali za utalii lakini zaidi kuona na kujifunza namna wasanii wa nchi hiyo wanavyofanya sanaa za filamu na muziki.

Juni 2000, Benki ya Dunia kwa kutambua umuhimu wa sanaa na nguvu yake kwa ukombozi wa kiuchumi kwa vijana wenye vipaji, ilifanya kongamano la kujadili njia za kusaidia maendeleo ya muziki kwa nchi sita za Bara la Afrika: Afrika Kusini, Zimbabwe, Ghana, Nigeria, Senegal na Mali.

Kwa nyongeza tu hapo ni kuwa nchi zote ambazo zimetajwa, kutoka mwaka 2000 hadi 2010, kila moja imetengeneza wanamuziki ambao, uwezo wao wa kifedha kwa kulinganisha na sarafu ya Tanzania, ni haki kuwaita mabilionea.

Swali; Kama Benki ya Dunia inaweza kuwekeza kwenye sanaa Afrika kwa kuamini inaweza kuwa mkombozi wa kiuchumi katika uwanja mpana, ni kwa nini Tanzania mpaka leo, hatujaifanya sanaa kuwa sekta rasmi ili itumike katika mageuzi ya kiuchumi?

Tangu mwaka 2000 baada ya kongamano la Benki ya Dunia, Ghana imefanikiwa kuingiza fedha nyingi katika Pato la Ndani la Taifa kupitia sanaa, hasa baada ya wanamuziki wake kufanikiwa kupenyeza kazi zao katika mataifa mbalimbali duniani. Afrika na nje ya Bara ya Afrika.

Ushuhuda mkubwa ambao Ghana inao kupitia maajabu ya sanaa ni kutanuka kwa sekta ya Utalii baada ya wasanii wa nchi hiyo kufanikiwa kutamba kimataifa.

Leo hii, Ghana inapokea mamilioni ya wageni wanaotembelea vivutio mbalimbali, ikiwemo sanaa, lakini sababu kuu ni kwa kuvutiwa na kazi za wasanii.

Kwa mujibu wa kitabu cha ‘Ghana and the World Music Boom’, kilichoandikwa na John Collins, mkufunzi katika Shule ya Sanaa za Maonesho katika Chuo Kikuu cha Ghana, yameelezewa mafanikio ya Ghana kiutalii, baada ya wasanii wa Ghana kufanikiwa kutamba nje ya mipaka ya nchi hiyo.

Mwaka 2003, Ghana ilianza kuwa na ingizo kubwa la wageni, hivyo kuinufaisha sekta ya Utalii. Jumla ya watu 550,000 waliingia Ghana, ikiwa ni mara mbili zaidi ya kabla sanaa haijawa na umaarufu wa kimataifa.

Taarifa imeongeza kuwa mwaka 2004, idadi ya watalii ilipanda kwa 100,000 zaidi hadi kufikia 650,000. Yaani kadiri sanaa ya Ghana ilivyokuwa inavuma kwenye soko la kimataifa, ndivyo na wageni walivyomiminika nchini humo kushuhudia “yaliyomo”, hivyo kuwa na matokeo mazuri katika ingizo la pato la kigeni.

Kwa mujibu wa Collins, hivi sasa Ghana inapokea mamilioni ya wageni kila mwaka kutokana na mchango mkubwa wa sanaa. Na inatambulika rasmi kwamba sanaa nchini Ghana inawezesha sekta ya Utalii kushika nafasi ya tatu kwa kuingiza fedha za kigeni baada ya dhahabu na mbao.

Kabla ya sanaa kuchukua nafasi pana, mpaka mwaka 2000 sekta ya Utalii ilikuwa na wastani wa kuingiza dola za Marekani milioni 350. Mwaka 2004 baada ya mwamko mkubwa wa sanaa, Utalii ulifikisha ingizo la dola milioni 800.

Kwa sasa utalii kila mwaka unatengeneza wastani wa zaidi ya dola bilioni 3 ambazo ni sawa na shilingi trilioni 6.7.

Hiyo ni tathmini ya Ghana. Ni wazi kwamba hapa Tanzania inawezekana kabisa kufikia hatua nzuri zaidi na kuona matokeo ya faida ya sanaa katika Utalii kama tutakuwa na nia ya dhati.

No comments: