Aug 12, 2018

Tujitafakari upya kwenye Bongo Fleva

Wanamuziki Profesa Jay (kushoto) na MwanaFA


MUZIKI kama chombo ambacho hutumiwa kuelezea historia ya jamii, hupasha ujumbe maalumu kwa wanajamii, hasa kutoka kizazi kimoja hadi kingine na hutumiwa kuelezea historia, imani, itikadi na kaida za jamii.

Kwa kawaida nyimbo ni zao la mazingira ya jamii. Zinaweza kufananishwa na mtoto ambaye hufinyangwa na mambo mengi katika historia ya jamii yake.

Hii inamaanisha kwamba muziki hauibuki katika ombwe tupu na hauwezi vilevile kujiundia mazingira yake yenyewe. Mabadiliko na maendeleo ya muziki yamekuwa yakifuatana na historia ya watu wenyewe.

Umuhimu wa muziki unadhihirika katika matumizi ya nyimbo katika wakati maalumu kama njia mojawapo ya kuanzisha mabadiliko katika tabia za jamii au mtu binafsi.


Wanamuziki Diamond Platnumz (kushoto), Aslay (katikati) na Ali Kiba


Muziki hutumika kama njia mojawapo ya kujifundisha utamaduni na aghalabu hutumiwa katika kumwelezea mtu, mazingira yake na jinsi anavyoweza kuyatumia na kuyatunza vilivyo.

Kwa Tanzania muziki umekuwa unabadilika sana, wasanii wengi wamekuwa wakibuni mitindo ya aina mbalimbali ili kuzifanya kazi zao ziende mbali na kuvuta mashabiki wengi wa muziki nchini na duniani kwa ujumla.

Kama ilivyokuwa kwa binadamu wengine, wakazi wa eneo ambalo hatimaye limekuwa nchi ya Tanzania, walikuwa na utamaduni wao. Utamaduni huu ulikuwa ukitofautiana kati ya kabila na kabila. Moja ya vipengele ilikuwa muziki.

Kiasili, hatukuwa na ‘muziki’ katika makabila yetu kabla ya ujio wa wageni, lakini tuliimba, tulicheza ngoma, tulipiga vyombo mbalimbali, ila tulikuwa na utamaduni mwingine kuhusu kitu hiki tunachokiita siku hizi muziki.

Watafiti wanatuambia tulikuwa na ngoma, ambayo tafsiri yake ni kubwa kuliko muziki. Ngoma ilikuwa ni chombo kile kilichotoa muziki, ngoma ilikuwa shughuli yenyewe, kwa mfano ngoma ya mavuno, ngoma ya mashetani na kadhalika, na pia tulicheza ngoma.

Ujio wa wageni ukatuletea muziki wa dansi ulioanza kama klabu za watu walioalikana kucheza aina mbalimbali za muziki wa kizungu (ballroom dancing). Kisha taratibu ukaumbika ukifuata muziki wa soukous kutoka Congo (rumba ya Kikongo) na tokea hapo ikaitwa ‘rumba ya Tanzania’.

Katika wakati huo pia muziki wa taarab, wa Waafrika wa Pwani, haukuachwa nyuma. Ni uimbaji wa mashairi uliofuata muziki wa bendi uliotokana na tamaduni nyingi, hasa muziki wa Waarabu na Wahindi.

Baadaye miaka ya 1990 ukaibuka muziki wa Hip hop, ambao baadaye ukapata jina la Bongo Fleva uliotokana na hip hop kutoka Marekani, ikiwa na ongezeko la athira ya muziki wa reggae, R&B, afrobeat, dancehall, na mitindo ya asili ya Kitanzania kama vile taarab na dansi.

Jina ‘Bongo Fleva’ ni tokeo la matini yaliyoharibiwa kutoka ‘Bongo flavour’, ambapo neno ‘flavor’ linamaanisha ladha na ‘Bongo’ huchukua nafasi ya jina la utani la Dar es Salaam, ambako aina ya mtindo huu inatokea.

Lakini kwa sasa Bongo Fleva inatafsirika kama muziki wa Tanzania kwa sababu hivi sasa neno Bongo limekuwa na maana ya Tanzania.

Hadi hapa sina tatizo na neno ‘Bongo Fleva’, binafsi linanikumbusha mtangazaji Mike Mhagama wa Radio One 99.6 FM mwaka 1996 alipokuwa akijaribu kutofautisha na muziki wa R&B na Hip Hop wa Marekani kupitia kipindi chake maarufu cha redio, 'DJ Show'.

DJ Show kilikuwa kipindi cha kwanza cha redio kukubali wanamuziki vijana wa Kitanzania wenye athira ya muziki wa Marekani.

East Africa Radio nao walikuwa na kipindi cha ‘The Cruise’ ambapo kulikuwa na kipengele cha ‘Bongo Explosion’, wakati Clouds FM walikuwa na kipindi kilichoitwa ‘Fleva ya Bongo’, na Redio Uhuru walikuwa na kipindi cha ‘Deiwaka’.

Vipindi hivyo vyote vilianzishwa kwa sababu muda huo mwamko wa vijana kurekodi nyimbo zilizoonekana za ‘kisasa’ ulikuwa mkubwa.

Hivyo, nyimbo hizo (bila kuzingatia aina ya muziki ambao msanii aliufanya) zikawa nyingi na zikapata wapenzi wengi sana, hii ndiyo ilifanya kuwepo kwa vipindi hivyo vya muziki huo.

Kwa kutokea hapo unaweza ukaona kuwa kumbe ‘Bongo Fleva’ inamaanisha mkusanyiko wa nyimbo za vijana wa Kitanzania, yaani ‘kizazi kipya’.

Kwa mtiririko huo, bado nina shaka kama jina Bongo Fleva linapaswa kuwakilisha aina hii ya muziki unaoimbwa na vijana wa Kitanzania.

Aina fulani ya muziki unatakiwa uwe na sifa za kufanana kimahadhi, vionjo, mpangilio, mirindimo na vitu vingine vyote vinavyoufafanua muziki husika, ndiyo maana hip hop hata iimbwe kona gani ya dunia bado utajua tu hii ni hip hop, kitu hicho hamna kwenye Bongo Fleva yetu.

Japo aina hii imewatangaza wanamuziki wetu kama Diamond, Ali Kiba na wengineo lakini ukweli tunahitaji kuweka sawa vitu kwenye muziki kwa ajili ya utambuzi, hii itawasaidia sana wanamuziki wenyewe, kwani kwa sasa ni kama wanafanya kitu wasichokifahamu hivyo ni vigumu wao kuwa bora sababu hakuna ‘standard’ za kuwapimia, hii nayo inachangia sana wasanii wengi (wa hiyo Bongo Fleva) kuibuka na kupotea.

Bongo Fleva ni kitu tata kidogo, ndiyo maana baadhi yao, hasa wanaojitambua hawapendi uwaambie wanaimba Bongo Fleva. Hata sasa kuna tofauti ya wazi kati ya wanaoimba RnB, Hip Hop n.k.

Swali la kujiuliza: Je, njia tunayoenda nayo katika muziki wetu inatusaidia kujenga juu ya msingi sahihi wa waliotutangulia au tunapotea na wimbi la utandawazi? Kwanini tunakosa alama ya mfano wa muziki wetu?

Kwa kweli fani ya muziki nchini ipo katika hatari kubwa ya kupoteza dira kwani wanamuziki wanaotamba sasa (wa Bongo Fleva) hawafuati miiko katika uteuzi wa maneno katika tungo zao, miundo, mitindo na maudhui kulingana na uasili, mila, desturi, mapokeo, historia na urithi tulioachiwa na waliotutangulia.

Hivyo haya yote yanaashiria hatari ya kuporomoka kwa fani hii. Pengine unaweza kujuliza, tunawezaje kuwa na utamaduni wa muziki mmoja wakati Tanzania kila kabila lina muziki wa asili yake, wenye sauti tofauti?

Kitu kikubwa ni kwamba ngoma ni kitu cha kipekee utakachokikuta kwenye muziki wa asili wa karibia makabila yote. Hivyo, muziki wa Kitanzania usioongozwa na ngoma bado ni vigumu kuuita wa Kitanzania. 

Kwa maana hiyo, hatuna aina yetu ya muziki kama taifa na tusidanganyane, aina ya muziki wa taifa haitungwi kama tunavyotaka kulazimisha kupitia Bongo Fleva bali ni matokeo ya historia yenyewe!

No comments: