Aug 17, 2018

Tunapomuomboleza King Majuto tusisahau somo alilotuachia

Wachekeshaji mahiri nchini ambao kwa sasa ni marehemu, King Majuto na Sharo Milionea

WIKI iliyopita tasnia ya vichekesho na wapenda burudani tulipata pigo kwa msiba uliogusa na kuwashtua watu wengi sana, wafuatiliaji na wasio wafuatiliaji wa sanaa ya vichekesho, kutokana na kifo cha King Majuto.

King Majuto ambaye jina lake halisi aliitwa Amri Athuman alikuwa msanii mkongwe na maarufu nchini Tanzania na Afrika Mashariki, na gwiji wa vichekesho ambaye umahiri wake ulikuwa wa aina yake.

Majuto alifariki dunia wakati akipokea matibabu kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam, majira ya saa 2 usiku wa Jumatano Agosti 8, 2018 akiwa amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi.

Baada tu ya kifo chake watu maarufu ndani na nje ya Tanzania walituma salamu za rambirambi kwa familia yake kupitia mitandao ya kijamii, miongoni mwao akiwa Rais wa Tanzania, John Magufuli.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe na King Majuto

Rais Magufuli alisema kuwa King Majuto atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa na wa muda mrefu alioutoa kupitia sanaa ya uigizaji na uchekeshaji, ambapo alishiriki kuelimisha jamii, kuendeleza na kukuza sanaa na kuunga mkono juhudi za Chama Cha Mapinduzi na Serikali katika kuhimiza maendeleo.

Kwa kweli King Majuto alikuwa mfalme katika tasnia ya maigizo ya uchekeshaji nchini Tanzania na Afrika Mashariki, aliweza kujizolea umaarufu mkubwa kupitia namna ambavyo alikuwa akiigiza na kuwa miongoni mwa watu wenye mvuto mkubwa miongoni mwa wasanii.

Vyombo vya habari vilipotangaza kuwa King Majuto alikuwa akiomba msaada wa shilingi 500,000 ili kupata matibabu nchini India vilimuibua Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe.

Dk Mwakyembe aliunda kamati ya wanasheria kwa lengo la kupitia upya mikataba ya wasanii ili waweze kulipwa fidia zao na aliweza kukutana na wasanii wa fani mbalimbali nchini kuzungumzia masuala kadhaa ikiwemo wizi wa kazi zao na maslahi yao.

Hata hivyo, kabla ya kifo chake, King majuto aliamua kuwasamehe baadhi ya waandaaji na wasambazaji ambao inasemekana walikuwa wamemdhulumu mamilioni ya fedha baada ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe kutishia kuwashitaki watu hao.

Hili ni somo la kwanza linalotuhusu wote: kusamehe. Haijalishi umeumizwa kiasi gani lakini unatakiwa kusamehe na kuyaacha maisha yasonge badala ya kukumbuka yaliyopita ambayo yanaweza kukuumiza na kukufanya ushindwe kupiga hatua kwenda mbele.

Kwa sasa wasanii wengi wameendelea kubaki wakilaumu tu kuwa wameibiwa sana, wameweka visasi na vinyongo kiasi cha kusahau kuwa wanatakiwa wasahau na kufanya kazi kwa bidii ili kujikwamua katika matatizo waliyo nayo.

Lakini pia wanapaswa watambue kuwa katika biashara yoyote makubaliano ya kazi ni muhimu sana kwa pande zote kuwa na haki na wajibu wa kila upande. Katika jambo hili, umakini wa hali ya juu huwa unahitajika sana ili kuepusha upande mmoja kuumizwa.

Na hili ni somo la pili: mikataba kabla ya kazi. Katika suala la mikataba ni vyema kushirikisha wanasheria ambao ndiyo wataalamu wa mikataba ili kuepuka kudhulumiwa, lakini pia kutokana na elimu ndogo ya wasanii wengi, ni muhimu kuwa na wasimamizi (mameneja) wanaoelewa masuala ya mikataba.

Ni vyema wasanii wakatambua kuwa hata kama kuna wizi wowote uliofanyika, basi hawakuibiwa bali mikataba waliyoingia ndiyo iliyowaponza.
Katika kipindi hiki tunachomuombolzeaa King Majuto ni vyema kutafuta namna ya kutatua changamoto ya kuibiwa, lakini kwanza wasanii wakubali mapungufu yao na pindi wanapoona mikataba kwa lugha ya Kiingereza ambayo inawapa tabu walio wengi, ni vyema wakaikataa mikataba hiyo au kuipeleka kwa watu wenye utaalamu na lugha hiyo, hasa wanasheria, na wasipende kuendekeza njaa.

Lakini pia vyama vya sanaa na mashirikisho yanapaswa kuwa na wanasheria ambao watasimamia shughuli za wasanii wao, ikiwemo kuwaongoza katika kuingia mikataba.

Kwa kufanya hivi, wasanii wataweza kujiamini katika utendaji wa kazi zao, kwani hawatakuwa na wasiwasi wa kunyanyasika pindi washirika wao katika mikataba watakapoonekana wanakengeusha mambo.

Suala la mikataba limekuwa likipuuzwa sana na Watanzania wengi (si wasanii tu), hasa linapokuja suala la kusoma vipengele na kuelewa vinamaanisha nini. Wengi hukimbilia kuangalia sehemu inayotaja pesa tu na wakiona pesa nyingi basi husaini bila hata kujali maeneo mengine muhimu.

Mikataba ya aina hii imesababisha vilio, malalamiko na kesi za ajabu ambazo kimsingi zingeweza kuepukika endapo kungekuwa na umakini kabla ya kuingia mkataba husika.

Bahati mbaya wasanii hawajifunzi kabisa kutokana na makosa ya wengine, kwani inapotokea mwenzao kaingia mkataba wa aina hii utashangaa hata watu wake wa karibu nao hurudia makosa kama hayo, kiasi kwamba suala hili limekuwa kama ni desturi kwao.

Inakuwa vigumu kuelewa kama wanafanya shughuli zao kwa mazoea na si kitaalamu, kwa maana ya kuifanya kazi yao kama ajira yao rasmi ambayo inawaingizia kipato kwa kujikimu na kuendesha maisha yao ya kila siku. Kukubali mikataba isiyo na maslahi kwao imekuwa ni sawa na kujimaliza wenyewe.

Ukiwaangalia wasanii wachache wenye maendeleo utagundua kuwa hawa ni wale wenye kupenda kuingia mikataba ambayo ama wameipitia kwa umakini au wamepata ushauri wa kisheria kutoka kwa wataalam wa sheria, na huingia mkataba hiyo kwa kila kazi wanazofanya na kupewa nakala za mikataba hiyo.

Jambo la ajabu ni pale wasanii wengi wanapodai kuwa na mikataba lakini wao wenyewe huwa hawana nakala za mikataba hiyo, kwani kuna aina ya ujanja ujanja ambao hufanyika ambapo wasanii wengi huambiwa waache mkataba ili ukasainiwe na mwanasheria na baada ya hapo wengi huwa hawauoni tena mkataba wao.

Wakati huu wa majonzi ya kuondokewa na gwiji wa vichekesho wasanii wautumie kutafakari kuhusu mustakabali wa tasnia ya sanaa, hasa wajifunze kuingia mikataba kwa kila kazi wanazofanya. Ni vizuri zaidi mikataba hiyo ikapitia mikononi mwa watu wanaoweza kuitafsiri.

No comments: