Dec 21, 2010

Soko la filamu Tanzania linakua? (2)

Kava la filamu ya Aunt Suzzy, moja ya kazi za Kitanzania

Msanii wa filamu za Kibongo maaruf kama Kishoka

MWAKA 1945, baada ya Vita Kuu ya Pili, uoneshaji na usambazaji wa sinema ulibadilika kidogo kwenye baadhi ya sinema. Sinema kama “Mister English at Home” na “An African in London” zilitengenezwa kutufundisha mambo na tamaduni za Kiingereza. Hata sinema zilizoanza kutengenezwa nchini baadaye zilizingatia mambo kadha wa kadha kama; faida ya dawa (tiba) za Kimagharibi dhidi ya tiba za Kiafrika.

Waafrika katika filamu za Wazungu walifanywa waonekane (na bado wanaonekana) washenzi, watu wa chini, wafungwa, nk. Wakati mwingine walifanywa waonekane wakatili sana na wanaoamini mambo ya kishirikina.
Mwaka 1949, kufuatia ripoti ya John Grierson kwa UNESCO, CFU ilianzisha shule ya filamu mjini Accra, Gold Coast (sasa Ghana).

Grierson aliandika kuwapasha CFU kuwa sinema zilizokuwa zikitengenezwa na “Bantu Film Experiment” na “Colonial Film Unit” hazikuwa zikiwavutia tena watazamaji wa Kiafrika kwa sababu hawakuzielewa. Na hivi ndivyo Grierson alivyoandika (tafsiri yangu):
Natumai kuwa tutaweza kutatua matatizo ya sinema katika makoloni yetu si kwa kuwaongoza kutengeneza sinema za Kimagharibi, bali kwa kuwafanya kutengeneza sinema kwa mtazamo wao ndani ya makoloni yetu” (Van Beaver, uk. 16-17).

Shule ya filamu iliyoanzishwa Accra ilitoa mafunzo kwa miezi sita tu, baada ya hapo wanafunzi walitakiwa kugawanyika kwenye makundi madogo madogo kwa ajili ya kutengeneza sinema za majaribio. Lakini baada ya miezi sita tu ya mwanzo, shule hiyo ilihamia Jamaica, na baadaye London.

Matokeo ya shule hiyo yalikuwa ya kuridhisha sana kwenye sekta ya filamu. “Wanafunzi wa Kiafrika walipewa mafunzo ili wawe wasaidizi wazuri kwenye timu ya uzalishaji iliyopelekwa Afrika Magharibi na makao makuu ya kitengo cha filamu (CFU), London” (Van Beaver, uk. 23).

Bantu Film Experiment na Colonial Film Unit kwa namna fulani waliamua kujitwika “U-baba” kwa kugharamia masuala yote ingawa walitawaliwa na ubaguzi wa rangi (racism). Walikusudia kubadili historia ya filamu kwa kuanzisha aina tofauti ya sinema kwa ajili ya Waafrika badala ya ile iliyotumika Ulaya na Marekani, sababu kubwa ni kwamba waliwachukulia Waafrika kama watu wenye ufinyu wa akili kiasi cha kushindwa kuendana na sinema za Magharibi zilizoendelea.

Kwa maana nyingine walikusudia kuturudisha nyuma ili tusiende na wakati katika historia ya filamu – kwa kutufundisha mfumo wa kizamani (uncut scene).

Mtazamo wao haukuendana kabisa na ukweli halisi kuwa Waafrika walikuwa ni wanadamu waliokamilika kiakili kama wao (Wazungu). Mtazamo huo finyu uliwazuia watengeneza filamu hawa wa Kikoloni kuuona ukweli huu: na sinema zao zikaanza kuchosha na kutovutia tena machoni mwa watazamaji wa Kiafrika.

Mkosoaji wa filamu, J. Koyinde Vaughan aliwahi kuandika haya katika kipindi cha mwaka 1957 (tafsiri yangu): “Ingawa watazamaji (audience) wa sinema wa Kiafrika walikuwa wakiongezeka kila kukicha, lakini walijikuta wakilazimika kutazama ‘sinema zinazochosha’ zilizoandaliwa na ‘CFU’ na kitengo cha mambo ya nje (foreign commercial entertainment film) ambazo zilionekana kushindwa kabisa kukidhi matakwa, licha ya ujuzi katika kazi za sanaa. Katika miji ya Kiafrika kama Freetown, Accra, Kumasi, Lagos, au Nairobi, charles Chaplin na waigizaji wengine maarufu wa Hollywood ndiyo walioendelea kutawala kwenye fikra na midomo ya watazamaji.

Uingereza pia ilijikuta ikishindwa kutambua maisha na tamaduni za Kiafrika. Kitengo cha sinema cha kikoloni “CFU” walikuwa wakichukulia kila kitu cha Kiafrika kama ushirikina na kubaki nyuma ya wakati. Walikuwa wakilinganisha kila kitu cha Ulaya katika mazingira ya Kiafrika, kana kwamba walitaka kuua kabisa mila na desturi za Kiafrika ili kuanzisha tamaduni za Ulaya (Rouch, uk. 392).

Kutokana na ubabe, ubaguzi na kutoyaona hayo, vitengo vya filamu havikuweza kutoa mafunzo fasaha kwa Waafrika ili kuwafanya waweze kutengeneza kazi zao katika kiwango kilichokubalika. Kama Waafrika wangeweza kujitengenezea kazi zao kwa usahihi, “CFU” isingehitajika tena kwa kazi hizo.

Baadaye Uingereza ililitambua hilo na ndiyo maana waliamua kuachia ngazi katika miaka ya mwanzo ya hamsini hasa kutokana na mwanzo wa vuguvugu la nchi nyingi za Kiafrika kuanza kudai uhuru. Ikumbukwe kuwa, Serikali katika koloni la Tanganyika ilikuwa imeanzisha rasmi kitengo cha filamu mwaka 1948.

Ilipofika mwanzoni mwa miaka ya 1950, tayari kulikuwa na vitengo vya filamu vya kudumu katika Afrika Mashariki. Hapa Tanganyika (Tanzania) kitengo hicho kiliweza kutengeneza sinema kumi na sita (zote za miaka ya 1950) za ukulima wa pamba. Ni katika kipindi hicho mzee Rashid Mfaume Kawawa alipopata nafasi ya kuwa mmoja wa waigizaji wa filamu wa mwanzo wa Kitanzania na kufungua njia kwa Watanzania wengine.

Kadri uhuru kwa nchi za Afrika Mashariki ulivyokuwa ukikaribia, ndivyo pesa za Serikali za Kikoloni Afrika Mashariki zilivyokuwa zikihitajika zaidi kwa mahitaji mengine na hivyo kujikuta vitengo vya sinema kwa nchi hizi vikitelekezwa, ingawa baadhi yake vilikuja kufufuka baada ya nchi kupata uhuru. Mwaka 1955 “CFU” ilitoa tamko kwamba imepata mafanikio makubwa kwa kufikia lengo kwa kile walichokusudia: yaani kutoa elimu ya utengenezaji wa sinema kwa Waafrika.

Makoloni yote yaliombwa kugharamia kazi za sinema zao badala ya kutegemea pesa kutoka Uingereza. Ndipo “CFU” ilipoamua kubadili jina lake na kuitwa “Overseas Film and Television Centre”. CFU ikiwa haitaki tena kujihusisha na uandaaji wa sinema kwenye makoloni, bali ilitumika kama makao makuu ya uratibu wa vitengo huru vya utengenezaji sinema kwenye makoloni yote na kutoa mafunzo kwa waandaaji wa sinema na televisheni.

Pia ilitumika kama kituo maalum cha mauzo ya vifaa vya sinema (film equipments) kwa Waafrika na mahala pa kufanyia uhariri (post-production) wa kazi za Waafrika. Kwa maneno mengine, Uingereza ilijivua kabisa mzigo wa kugharamia sekta ya sinema kwenye makoloni yake. Sera hii pia ilikuwa ni ishara ya matayarisho kwa makoloni yake kupatiwa uhuru ili yaweze kuendeleza kazi zao.

Mabadiliko haya ya kisera yalikuja kwa sababu Uingereza ilijua fika kuwa wakati wowote makoloni hayo yangekuwa huru (Rouch, uk. 390).

Kitengo cha filamu katika Tanganyika kilirithiwa na Serikali ya Tanganyika baada ya uhuru na kupewa jukumu la kuhifadhi matukio muhimu ya Serikali. Kampuni ya Filamu Tanzania (TFC) ilianzishwa rasmi mwaka 1968. Ilitoa filamu za matukio kwa ajili ya mashirika ya umma na kumiliki studio ya kurekodi kwa ajili ya kuhifadhi kazi za muziki wa bendi na kwaya.

Filamu ndefu za wananchi zilizotengenezwa na Kampuni ya Filamu Tanzania ni pamoja na: “Fimbo ya Mnyonge (1974)”, “Arusi ya Mariam (1984)” zilizoongozwa na Ron Mulvihill na Marehemu Nganyoma Ng’oge, na “Yomba Yomba (1985)” ya Martin Mhando.
Sinema nyingine ni pamoja na “Mama Matumaini (1986)” iliyotengenezwa kwa ushirikiano wa Watanzania na Marekani, sinema hii ilipata tuzo katika tamasha la FESPACO mjini Ouagadougou mwaka 1987. “Maangamizi (1996)” iliyoongozwa na Ron Mulvihill akishirikiana na Martin Mhando pia ilioneshwa kwenye tamasha la “FESPACO” mwaka 1997, na baadaye ikashinda tuzo ya sinema bora “Golden Dhow Award” kwenye tamasha la kwanza la Filamu la Kimataifa la Nchi za Jahazi, Zanzibar (ZIFF) mwaka 1998. Pia sinema hii ilitoa muigizaji bora wa kike, Prof. Amandina Lihamba.

Sinema nyingine ni “Neema” ya Geoffrey Mhagama ilishinda tuzo kwenye Tamasha la Filamu la Kimataifa la Nchi za Jahazi, Zanzibar (ZIFF) mwaka 2000.

Miaka michache baadaye, sinema ya “Tumaini (2004)” iliyoandaliwa na kuongozwa na Beatrix Mugishagwe (Abantu Vision) ambayo picha zake zilipigwa Muleba, Bukoba mjini na Mwanza ilipata tuzo za UNICEF kwenye Tamasha la Filamu la Kimataifa la Nchi za Jahazi, Zanzibar (ZIFF).

Hizo ni baadhi ya kazi za Kitanzania zilizopata mafanikio makubwa katika sekta ya filamu.

Ikumbukwe kuwa kutokea na kuibuka kwa maendeleo ya haraka ya tasnia za televisheni na video kuliiua Kampuni ya Filamu Tanzania (TFC) kwa kuwa haikuwavutia tena wananchi. Taasisi ya Vielelezo (Audio Visual Institute AVI”) iliyoanzishwa mwaka 1974 ilichukua nafasi ya Kampuni ya Filamu lakini iliendelea kufanya kazi ya Kitengo cha Hifadhi ya Kumbukumbu cha Serikali. Hata hivyo AVI pia ilijaribu kutengeneza filamu za matukio za kielimu ambazo zilitumika shuleni na katika taasisi nyingine za mafunzo.

Pia Taasisi hiyo ya Vielelezo ilirithiwa na Televisheni ya Taifa (TvT) ambayo baadaye ilibadilishwa na kuwa Shirika la Utangazaji la Tanzania (TBC).

Itaendele

No comments: