Dec 24, 2010

Vita ya wakoloni dhidi ya utamaduni wetu

Ramani ya bara la Afrika
 Moja ya sanaa za Kiafrika

HISTORIA ya ukoloni katika Bara la Afrika, inaonyesha jinsi walivyojitahidi kuua utamaduni wa Waafrika na kuwajenga katika misingi ya utamaduni wa kizungu. Katika baadhi ya makoloni, ubora wa Mwafrika ulipimwa kwa kiasi ambacho alikuwa amejengeka katika utamaduni huo.

Baadhi ya Waafrika waliweza hata kupewa uraia wa nchi za wakoloni kutokana na vile walivyokuwa wamejiimarisha katika  ‘ustaarabu’ wa wakoloni. Mchakato wa elimu haukuwa na maana tu ya kuwapatia Waafrika maarifa na ujuzi, bali pia ilikuwa ni fursa ya kuwaondoa katika utamaduni wao na kuwajenga katika utamaduni wa kizungu.Ndiyo chanzo cha baadhi ya Waafrika kuitwa wazungu weusi, ikiwa ni taswira ya jinsi walivyobobea na kubobeka katika utamaduni wa kizungu. Wakoloni walifanya hivyo ili kuua fahari, heshima, utu, mshikamano na umoja wa watawaliwa.

Tulipopata uhuru, jitihada kubwa zilifanywa ili kufufua na kukuza utamaduni wetu wa Kiafrika. Hili lilikuwa na kipaumbele cha juu katika nchi zetu zote mara zilipopata uhuru. Mantiki yake ilitokana na imani ile ile kuwa roho ya jamii au taifa ni utamaduni wake.

Katika kujenga heshima, fahari, umoja na uzalendo wa wananchi hatua hii ilionekana kuwa na umuhimu wa pekee. Nchi nyingi, Tanzania ikiwa mojawapo, ziliunda wizara maalumu za kusimamia, kufufua, kukuza na kuendeleza utamaduni wa asili. Tanzania na nchi nyingine nyingi, pia zilianzisha asasi kwa ajili ya kushughulikia kwa kina maeneo maalumu.

Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita), lilianzishwa mwaka 1967, miaka sita baada ya uhuru, kwa ajili ya kukuza Kiswahili ili kiwe lugha inayoweza kutumiwa katika nyanja zote za jamii, utawala, elimu, mafunzo na biashara.

Miaka minane baadaye, Serikali ya Tanzania ilianzisha Baraza la Sanaa la Taifa na Baraza la Muziki la Taifa, ambayo yaliunganishwa mwaka 1984 kuwa Baraza la Sanaa la Taifa la sasa (Basata). Madhumuni ya Basata na mabaraza yaliyolitangulia ni kufufua, kuendeleza na kukuza sanaa za asili za Watanzania.

Aidha, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilianzisha masomo ya sanaa tangu mwaka 1966. Mwaka 1973, mafunzo ya sanaa kwa walimu wa shule za msingi yalianzishwa katika Chuo cha Ualimu Chang’ombe, Dar es Salaam na baadaye kuhamishiwa katika Chuo cha Ualimu Butimba Mwanza.

Chuo cha Sanaa Bagamoyo, sasa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni (TaSUBa), kilianzishwa mwaka 1981 kwa lengo la kutoa mafunzo kwa wasanii. Wizara inayohusika na utamaduni nayo imekuwa na kitengo kwa ajili ya kutafiti, kuhifadhi na kuhimiza mila na desturi za Watanzania. Aidha, mwaka 1985 serikali ilianzisha matamasha na mashindano ya fani mbalimbali za utamaduni kuanzia ngazi ya wilaya, mkoa, kanda hadi taifa.

Kwa upande wa siasa, tunakumbuka jitihada kubwa iliyofanywa na chama cha TANU katika kuhimiza maendeleo ya utamaduni wetu. Enzi zake, TANU kilikuwa na idara maalumu ya kushughulikia mambo ya utamaduni. Kilitoa maazimio mengi juu ya ukuzaji wa utamaduni, hususan katika Mkutano Mkuu wa 15 na wa 16.

Mwaka 1976, TANU kilitoa tamko maalumu kuhusu utamaduni. Tamko hili lilikuwa la kisera na liliweka bayana misingi ya shughuli za utamaduni nchini. Azimio la Arusha nalo, pamoja na mambo mengine, lilihimiza suala zima la kujitegemea kama taifa.

Mwelekeo huu ulikuwa na msukumo mkubwa katika kukuza utamaduni wetu, maana kujitegema ni pamoja na kujenga utamaduni wa asili ya taifa letu. Bila kujijenga katika utamaduni wetu wenyewe, ni vigumu kujenga fikra na utashi wa kujitegemea katika maeneo mengine ya jamii na uchumi.

Jitihada hizi hazikuwa haba na ulikuwa mwelekeo sahihi. Mwamko wa utamaduni katika miaka ya 1960 hadi 1980 ulikuwa mkubwa kweli kweli kuanzia shule za msingi, sekondari, vyuoni, mijini na vijijini. Kiwango cha ubunifu katika sanaa kilikuwa kikubwa. Wasanii walipambana katika kubuni kazi mpya, siyo katika kuiga kazi za wengine.

Pamoja na msukumo huu mkubwa wa maendeleo ya utamaduni, inaelekea wasomi wetu waliokuwa wamekabidhiwa madaraka ya kuendesha shughuli za serikali hawakubadilika. Hawakuleta madhara makubwa kwa sababu walikosa nafasi ya kutosha kuweza “kufanya vitu vyao”. Ni wakati huu, Hayati Mzee Rashidi Kawawa na viongozi wenzake wazalendo walianza kuwasema wasomi wa aina hii kuwa “wana kasumba”.  Kauli hii na nyinginezo zilikuwa na lengo la kuhimiza uzalendo na upenzi kwa utamaduni wa taifa letu.

Mwishoni mwa miaka ya 1980, hali ya uchumi wa nchi ilipodorora, Serikali ilianzisha programu mbalimbali kwa ajili ya kukabili hali hiyo. Mipango kadhaa ya kurekebisha uchumi iliandaliwa. Mipango ya Kurekebisha Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na Mashirika ya Umma ilianza kutekelezwa. Programu zote hizi zilikuwa na lengo la kupunguza matumizi ya Serikali na “kuongeza ufanisi”.

Iliyoathirika zaidi ilikuwa sekta ya utamaduni. Idara ya utamaduni katika ngazi ya mkoa ilifutwa na wilayani idara ikadhoofishwa na kubaki jina tu. Kwa jumla mgawo wa bajeti ya serikali kwenda sekta ya utamaduni ilipungua sana. Matokeo yake ni kwamba shughuli nyingi za utamaduni zilisitishwa. Matamasha, mashindano ya sanaa, maonyesho makubwa yote yakatoweka. Asasi kama Bakita na Basata pia zilidorora; kasi na ufanisi wa utendaji wake ulishuka sana.

Jambo jingine kubwa lilotokea wakati huu ni kubuniwa na kutangazwa kwa sera ya uchumi huria na uchumi wa soko. Hili lilifungulia milango kwa utamaduni wa kigeni na kushamiri kwa kinachoitwa muziki wa kizazi kipya. Kina Mlimani Park, Msondo Ngoma, kina Komandoo Hamza Kalala, ambao wamekuwa wakijitahidi kuweka muziki wa Kitanzania kwenye ramani ya dunia, sasa wamebaki majina tu.

Zipo dalili, hasa katika Awamu hii ya Nne ya uongozi wa nchi yetu kuwa sekta ya utamaduni imeanza kupewa umuhimu katika mipango ya Serikali. Imeanza kuongezewa mgawo wa bajeti na kujengewa miundombinu muhimu. Hata hivyo, siku hizi tunawauliza TaSUBa, Makumbusho ya Taifa na Basata, “Majumba yenu mazuri ya maonyesho ya sanaa za jukwaani na ufundi yamekamilika, mtaonyesha nini humo ndani?”

Bado kuna changamoto na matatizo mengi. Bila kupambana na changamoto na matatizo hayo, ongezeko la bajeti ya utamaduni na miundombinu maridhawa kwenye asasi za Serikali za usimamizi na ukuzaji wa shughuli za utamaduni halitaleta tija inayotarajiwa. 

Habari hii ilichapwa kwenye gazeti la Mwananchi na iliandikwa na Rashid Masimbi. pia inapatikana kwenye tovuti hii; http://www.mwananchi.co.tz

No comments: