Nov 24, 2010

Mwalimu Nyerere Film Festival kuwakomboa wasanii wetu

Simon Mwakifwamba akihojiwa na 
mtangazaji wa Clouds TV, Zamaradi Mtetema

INAONEKANA kuwa Shirikisho la filamu Tanzania lina mikakati kabambe ya kuikomboa tasnia ya filamu nchini dhidi ya changamoto mbalimbali zinazoikabili. Baadhi ya changamoto hizo ni kuwafanya wasanii wa Tanzania kuwa na maisha bora na pia kuwawezesha kufanya kazi zenye ubora na zinazokubalika ndani na nje ya nchi.

Mikakati hiyo ni pamoja na kuhakikisha sheria ya hakimiliki na hakishiriki inaangaliwa upya, kupambana na maharamia wa kazi za sanaa, kujenga mtandao mpana wa ushirikiano baina ya wadau, kuimarisha uongozi wa vyama mbalimbali vya wadau,
kupambana na unyonyaji dhidi ya wasanii, uvunjifu wa maadili na tabia chafu za wasanii wa filamu ambazo katika siku za hivi karibuni zimekuwa zikilalamikiwa sana na wadau kiasi cha kuacha maswali mengi juu ya hatma ya wasanii wa tasnia hiyo.

Simon Mwakifwamba, Rais Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) amekaririwa akisema kuwa shirikisho litakuwa linaendesha tamasha la filamu za Tanzania kila mwaka, na litafanyika kwa mara ya kwanza mwezi Februari mwakani, 2011.

Huu ni mwanzo mzuri kwa wasanii na wadau wa filamu hapa Tanzania kama wataamua kulitumia tamasha hilo kama kipimo halisi cha kutengeneza kazi nzuri zenye kuvutia na zenye kiwango kizuri na kuacha uvivu wa kufikiri.

Mwakifwamba alisema kuwa lengo la shirikisho ni kujaribu kukuza soko la kazi za filamu nchini na kukuza mahusiano ya kisekta kati ya wasanii wa Tanzania na wale wa nje ya nchi.

Tamasha hilo litapambwa na sinema ishirini za Kitanzania zilizofanya vizuri ndani na nje ya nchi, pamoja na burudani nyingine zikiwemo ngoma za asili, vichekesho, muziki na michezo mbalimbali.

Imeelezwa kuwa kutakuwa na tuzo ya sinema iliyopendwa na watazamaji au iliyofanya vizuri. Tuzo hiyo imepewa jina la “People's Choice Award”. Pia kutakuwepo tuzo nyingine zitakazoitwa “TAFF Special Awards”; kwa ajili ya kuwaenzi waasisi wa taifa hili, Mwalimu Nyerere na Mzee Rashid Kawawa kwa mchango wao katika maendeleo ya taifa na tasnia ya filamu nchini.

Tamasha hilo litafanyika kwa siku sita kuanzia tarehe 14 hadi 19, Februari, 2011 katika viwanja vya Leaders Club, Kinondoni.

Katika tamasha hilo, kabla ya maonesho ya siku husika kutatanguliwa na mafunzo kwa washiriki ambapo mada mbalimbali zinazohusu shughuli za filamu na maigizo zitatolewa na wakufunzi waliotayarishwa.

Naamini kama litatumika ipasavyo, shirikisho litajiweka kwenye nafasi nzuri ya kukuza tasnia hii, ingawa pia linapaswa kuandaa mikakati madhubuti ya kupambana na maadili machafu katika filamu, tabia za kukaa nusu uchi, kufanya mambo ya aibu, na kuweka kanuni za adhabu ambazo zitadhibiti maadili katika filamu na wasanii wake.

Mimi kama mmoja wa wanaharakati walioasisi utengenezwaji wa shirikisho nikiwa Katibu Mkuu wakati huo, nakumbuka kuwa harakati zilianza miaka kadhaa iliyopita lakini zilipata nguvu mwaka jana, hasa pale wadau walipoamua kushikamana kutokana na tukio la kusikitisha la kejeli na matusi kwa muigizaji wa filamu za Tanzania, Steven Kanumba. Ilikuwa ni baada ya kupata mwaliko wa kutembelea jumba la Big Brother, Afrika Kusini, mwaka jana.

Mengi yalisemwa kuhusu kilichotokea ndani ya onesho la 'Big Brother Africa Revolution'. Kanumba aliingia kwenye jumba hilo kama mmoja wa wasanii maarufu wanne wa Afrika waliokaa kwa saa 24, wala hakuwa mshiriki wa Big Brother. Yaliyotokea wote tunayajua.

Ushirikiano ulioneshwa pale Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere wakati Kanumba alipolakiwa na mamia ya wadau na mashabiki 'wazalendo' wachache, kitendo kilichomfanya kutokwa machozi ya furaha.

Baada ya hapo harakati ziliendelea kwa nguvu na kuwafanya wadau kuendelea kushikamana katika shughuli za kila siku. Tukio lingine ni la hivi karibuni kwenye harusi ya wasaii Thea (Ndubagwe Misayo) na Mike (Michael Sangu) ambapo wasanii walijitoa kwa hali na mali kufanikisha shughuli hiyo.

Shirikisho hili limeonekana kusaidia kwa kiasi fulani kuvunja baadhi ya tofauti zilizokuwepo kabla ingawa bado kuna kasoro kadhaa zinazopaswa kufanyiwa kazi.

Nawashauri wasanii na wadau wenzangu tusiishie kushirikiana kwenye harusi, Kitchen Party, Birthday Party, Bonanza na misiba tu, bali tushirikiane sana kwenye suala muhimu la uandaaji wa kazi za filamu. Jambo hili linapaswa lipewe kipaumbele badala ya kila mmoja kujifanyia kivyake kitu kinachochangia uwepo wa kazi duni. Kama ushirikiano katika kazi utapewa kipaumbele wadau kwa ujumla wake wanaweza kufaidika kwa kubadilishana ujuzi, na ubora wa filamu Tanzania utaweza kukua.

Jitihada hizi zinazofanywa na shirikisho la filamu zitasaidia kuinua sekta hii japo bado kuna kazi ngumu sana kuweza kufikia malengo. Sekta ya utengenezaji filamu haijaimarika sana humu nchini ikilinganishwa na mataifa mengine ya Afrika. Tanzania imekuwa soko kubwa la sinema feki kutoka Hollywood, Bollywood na Nollywood huku wasanii wa humu nchini wakiendelea kukabiliwa na changamoto chungu nzima katika fani hiyo.

2 comments:

Anonymous said...

Inapendeza sana kama shirikisho litafanikiwa kuyatekeleza hayo uliyoyaandika, hongera sana Hiluka

Anonymous said...

Mh, hivi kweli wataweza? Anyway time will tell!