Jun 24, 2011

Waziri Nchimbi, ni kweli wasanii hawapatani, sasa?

 Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, 
Emmanuel Nchimbi

Dilesh Solank, Mkurugenzi wa Steps Entertainment, 
wasambazaji wa filamu nchini wanaolalamikiwa 
kuasisi mgawanyiko wa wasanii

WIKI iliyopita, wasanii wa filamu walio chini ya mwamvuli wa Bongo Movie Club walizuru Bungeni Dodoma, walikocheza mechi ya kirafiki na timu ya wabunge, Bunge Sports Club. Ni katika hafla hiyo Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Emmanuel Nchimbi, alipokiri kuwepo matatizo ya kuelewana kwa wasanii wa filamu hapa nchini, hali ambayo inarudisha nyuma maendeleo ya sanaa.

Waziri Nchimbi aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na timu ya soka ya Bongo Movies Club baada ya kumalizika kwa mchezo wa kirafiki kati yake na timu ya Bunge Sports Club uliochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma, ambapo Bunge Sports Club iliifunga Bongo Movies Club 2-1.

Nchimbi aliwataka wasanii wa filamu kumaliza tofauti zao na kuwa na mshikamano na umoja ili waimarishe na kuboresha kazi zao za sanaa.

Ningependa kumkumbusha waziri akiwa kama mzazi (waziri mwenye dhamana) ana dhima ya kuondoa tatizo hilo ili kuleta mshikamano, kwa kuwa naamini kabisa kuwa anayajua matatizo yaliyopo, aliyajua kabla na akahakikishiwa siku alipokutana na wasanii wa maigizo katika ukumbi wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Mei 18, mwaka huu.

Naamini kuwa misuguano hii inawafanya wawekezaji walio tayari kuwekeza katika tasnia hii ya filamu kusita kwa sababu haya ni matatizo yanayoathiri sekta ya filamu kwa ujumla na kufanya utendaji kazi kuwa mbovu, ni matatizo ambayo hadi sasa hakuna juhudi zozote za makusudi zinazochukuliwa kuyatatua licha ya waziri kuthibitisha kuyajua. Ni matatizo yanayochangiwa kwa kiasi kikubwa na kutokuwepo malengo, kuwa na mipango mibovu na uchoyo usiokuwa wa lazima.

Napenda kumkumbusha waziri kuwa mgawanyiko huu unasababishwa na kutojiamini kwa watayarishaji wa filamu nchini ambao wamekosa kabisa mafunzo ya msingi ya namna ya kutengeneza kazi zao katika kiwango kinachokubalika. Hali hii imesababisha watayarishaji wengi wa filamu nchini kuwa wabinafsi na wanaowekeza kidogo na kutarajia wavune mara dufu.
Hii vurugumechi yote inatokana na soko letu kuparaganyika na watu walioko sokoni kujaribu tu kupata faida iliyo kubwa zaidi bila kuangalia upande wa pili unafaidikaje. Kwa maana hiyo, mgawanyiko unachochewa zaidi na uchoyo na ubinafsi.

Kutoelewana kwa wasanii ni mgawanyiko uliopo kati ya walio chini ya Bongo Movie Club, ambao wanafadhiliwa na msambazaji mkubwa wa filamu (Steps Entertainment) aliyelihodhi soko la filamu, na wale walio chini ya shirikisho la filamu Tanzania (Taff).

Waziri hakupaswa kushauri tu eti wasanii wakae ili kumaliza tofauti zao, kwani hali imefika ilipo kwa sababu maalum na bila serikali kuingilia kati hakuna kitakachofanikiwa. Serikali ina dhima ya kutatua msuguano huu kabla mambo hayajawa mabaya zaidi, na kuweka mazingira bora zaidi yenye mafanikio na haki.

Soko la filamu hapa nchini limejikita katika kanuni ya mwenye nguvu ndiye anayefaidi (Darwinism) kitu ambacho ni hatari kwa taifa, kwa sababu pia muundo wa soko letu umekuwa ukishusha hadhi ya utamaduni na sanaa zetu.

Serikali isiishie kutamka tu ikiwataka wasanii kuelewana wakati ikijua kiini cha matatizo hayo ni msambazaji kuwagawa wasanii, kitu kinachomsaidia kufanikiwa zaidi katika biashara yake.

Serikali ilipaswa kuwa wakala wa kusaidia masoko yaweze kufikia kwenye 'ubora' unaotakiwa na tumekuwa tukitegemea kuona serikali ikianzisha sera 'bora' na makini kwa kuanzisha chombo maalum chenye uwezo wa kuzitangaza kazi zetu. Kama haya yatafanyika hatutashuhudia migawanyiko miongoni mwa wasanii kwa kuwa wote watafikiwa na fursa hizi zitakazowafanya kuchapa kazi kwa bidii ili wafanikiwe.
Pia naendelea kusisitiza kuwa serikali lazima iirasimishe sekta hii ili kuongeza wigo wa ukusanyaji mapato kupitia tasnia ya filamu. Tuache siasa ambayo kwa kiasi kikubwa imeathiri mfumo mzima wa maisha yetu bila kujali ni nini tunapoteza.

Waziri afahamu kuwa sanaa na utamaduni ndivyo vitu vyenye mwitiko mkubwa kwa vipengele vya nafsi ya mwanadamu, na kwa maana hiyo, haviwezi kuachwa mikononi mwa wachache kuamua hatma yake ama kuuzwa na kununuliwa kama vile nyanya. Kuiachia sanaa mikononi mwa wenye pesa wachache ni sawa na kuusaliti utu tuliourithi wa sanaa.

Hivi waziri alipotoa ushauri hakujua kuwa alioongea nao (Bongo Movie Club) ndiyo waasisi wa mgawanyiko huu kwa maslahi ya wachache? Ni wao walioasisi shirikisho la filamu lililokuwa na mikakati ya kumbana msambazaji, na wamekuwa wa kwanza kulipinga baada ya kusainishwa mikataba na msambazaji huyohuyo inayowahakikishia mlo wa siku kadhaa.

Kwa taarifa tu waziri afahamu kuwa kauli yake kuwataka kuungana inapingwa na haohao, ambao wanatamka bayana kuwa Club yao ni kampuni kwa hiyo haihusiani kabisa na shirikisho la wasanii wa filamu Tanzania, na wala hawana mpango wa kujiunga na wasanii wengine, bali shirikisho linatakiwa kuwajua wanachama wake ambao ni vyama vya wasanii na si wasanii kama walivyo wao, Bongo movie Club.
Hao ambao waziri aliwashauri kuungana ndiyo wanaosisitiza kuwa jambo la muhimu kwa sasa kila mtu aangalie jinsi ya kujenga maisha yake kama ambavyo wao wanafanya na wala hawahitaji kushirikishwa kwa yeyote asiye na maslahi kwao!

Kauli hizi zinaashiria kujitenga na zinajenga mtafaruku mkubwa badala ya kuleta umoja ambao waziri anashauri uwepo. Umoja utapatikana wapi wakati mtu aliyekuwa mstari wa mbele kuhimiza umoja wa wasanii, kumbe tatizo lake lilikuwa njaa na alipohakikishiwa mkataba akawasahau aliowahimiza na hata kufikia hatua ya kuwabeza!

Hii inaonesha kuwa harakati nyingi za wasanii bila mkono wa serikali zina mashaka kwani mara nyingi wamekuwa wakianzisha harakati na kesho huzikana. Sioni sababu ya kuendeleza malumbano kwa sasa kwa kuwa yanayofanywa si kwa maslahi ya taifa bali ni ubinafsi tu unaowatawala wahusika. Walipaswa wakae pamoja wajenge tasnia hii, kwani kuyumba kwa tasnia hii kizazi kijacho kitawalilia wote.

Inashangaza kwa tasnia iliyosifiwa kwa mshikamano, pesa ndogo iwaweke katika makundi! Hivi wanapata muda wa kubadilishana mawazo na kunyooshana pale mmoja anapopinda, au ndiyo shaghalabaghala tu?

Kumbe hata ile falsafa ya wenye majina makubwa kuwa tayari kukutana na chipukizi ili kuwa kitu kimoja na kuleta chachu ilikuwa ndoto kutokana na njaa! Baada ya kusainishwa mikataba yenye kuwapatia uhakika japo wa kusukuma maisha kwa siku kadhaa yote hayo yamegeuka ndoto za alinacha!

Kwangu mimi mafanikio pekee ya soko letu ni kufanikiwa kurusha filamu zetu kwenye kituo cha Africa Magic, ambapo hapo awali filamu za Nollywood ndizo ziliteka ulingo huo. Kwa hilo mambo si mabaya, kwani Mtanzania popote alipo sasa anatambulika, japo kiwango bado si cha kuridhisha na subtitle zinatuangusha.

Aliyechangia mgawanyiko huu (Msambazaji) anajua fika kuwa endapo wasanii watakuwa na sauti moja itawasaidia katika mambo mengi, jambo ambalo litamfanya ashindwe kuwaibia. Na hadi sasa inaonekana wadau bado hawajang’amua, au kama wanajua basi kuendekeza njaa kunawaponza.

Kama hiyo haitoshi, wasanii haohao wamekuwa wakirudi nyuma hata pale wanaposhikwa mkono, kwani nimeweza kuhudhuria makongamano mbalimbali huku wengi wao wakishindwa kuitikia wito jambo linalowakatisha tamaa waandaaji.

Tasnia hii ina matatizo lukuki yanayopaswa kutafutiwa ufumbuzi ukiacha hili la mgawanyiko wa kujitakia, matatizo kama wizi wa kazi za wasanii (Piracy), ufumbuzi kwa wale wanaopenda kunakiri kazi za Nigeria na wanaotumia muziki wa wasanii wa muziki bila idhini yao.

Waziri alipaswa kuweka mikakati ya namna tutakavyoondokana na uchafu wa filamu zetu ambapo filamu za Kibongo zimekuwa na maadili mabovu yanayotokana na uvaazi vichupi kwa wasanii wa kike, uoneshaji wa matendo ya faragha mara kwa mara, script zenye kushabikia matendo maovu na yasiyofaa kwa jamii na kadhalika.

Alipaswa kuipa sapoti zaidi Bodi ya Filamu ihakikishe inadhibiti filamu zisizo na maadili na iwekwe sheria kali kwa yeyote atakayekiuka, kwani filamu zetu zimekuwa zikitia kinyaa. Filamu zetu nyingi hazibebi uhusika wenye ufanano na maisha/maadili ya Kitanzania.

Alipaswa kuangalia namna serikali itakavyowasaidia waongozaji na waandishi wa miongozo kwa kuwapatia warsha, semina na mafunzo ya muda mfupi kwenye taaluma zao kwani sinema zetu zinaonesha kuwepo ubunifu mdogo wa waongozaji, watengenezaji na waandishi wa miongozo ya filamu ambao umekuwa ukiwafanya muda mwingi wautumie kunakiri kazi za kigeni.

Pia alipaswa kuangalia namna wasanii watakavyoelimishwa kujua mikataba kwenye kazi zao. Wasanii wengi wamekuwa wakimlalamikia msambazaji kuwaibia wakati wamesainiana mikataba. Tatizo ni wasanii kusaini mikataba kwa uroho wa fedha bila kusoma mikataba husika. Je, ni nani wa kuwasimamia wasanii kuyajua haya na kuhakikisha kuwa mikataba inawanufaisha?

Tusiyaongee haya kisiasa bali tuchukue hatua sasa.

No comments: