Jun 8, 2011

Waziri Mponda ataka filamu ziwe somo la Malaria

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda

Muongozaji wa Filamu ya Chumo, Jordan Riber (katikati) 
akitoa maelezo juu ya Filamu hiyo. Kushoto ni baba yake 
ambaye pia ni mtengenezaji wa filamu, John Riber.

Baadhi ya washiriki wa sinema hiyo

 Baadhi ya wadau waliofika kwenye uzinduzi wa filamu hiyo

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda amewataka wadau wa filamu na burudani nchini kutumia sanaa katika kuelimisha jamii kuhusu ugonjwa wa Malaria. Mponda amesema hayo baada ya uzinduzi wa filamu ya Chumo yenye dakika 45 inayoelimisha jamii kuhusu ugonjwa wa Malaria pamoja na kutoa suluhisho katika kupambana na ugonjwa huo.

Mponda alisema kuwa anatambua mchango wa sanaa katika kuelimisha jamii na kuongeza kuwa kupitia sanaa wanajamii wanaweza kuelimika kirahisi zaidi na kuepuka uwezekano wa kupata ugonjwa huo.


Filamu hiyo imeandaliwa na John Riber wa kampuni ya Media for Development International Tanzania (MFDI) na kuongozwa na Jordan Riber, imewashirikisha wasanii mbalimbali wakiwemo Yusuph Mlela, Hussein Mkiety, Jokate Mwegelo na Jafarai Makati.

Filamu hiyo imetengenezewa katika eneo la Kimbiji lililopo Kigamboni na imechukua siku 16 kutengenezwa ambapo mazingira yaliyotumika ni ya ufukweni zaidi.

Stori katika filamu hiyo; Jokate ameigiza kama mtoto wa mvuvi aitwaye Amina ambapo alikuwa na uhusiano na kijana mvuvi aliyekuwa hana uwezo kifedha na kujikuta akipata ujauzito na alitumia muda wake mwingi kujikinga na Malaria ili asihatarishe maisha yake.

Naye Meneja wa mipango wa mradi wa uelimishaji wa ugonjwa wa Malaria (Commit), Waziri Nyoni alisema kuwa filamu hiyo itaanza kuoneshwa bure katika vijiji vyote nchi nzima ikiwa ni pamoja na kuuzwa kupitia kampuni ya usambazaji ya Steps.

Alisema kuwa filamu hiyo inaitwa Chumo kwa kuwa kuna kampeni mpya ya Malaria inayotarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni. Naye Mkurugenzi wa Masoko wa Benki ya Stanbic, Abdala Singano alisema kuwa benki hiyo imedhamini filamu hiyo kwa Sh milioni 15 kwa kuwa inatambua mchango wa filamu katika kuelimisha jamii.

Wadhamini wengine ni John Hopkins Bloomberg School of Public Health Center na kituo cha Mawasiliano na Mipango kwa ufadhili wa Mpango wa Malaria wa Rais wa Marekani kupitia USAID.

No comments: