Jun 15, 2011

FILAMU ZA BONGO: Sumu mbaya iliyopandikizwa kuhusu sinema za Part 1 na 2

 Naomi Part 1

Naomi part 2

NAUHUSUDU sana mkoa wa Tanga, mkoa wanakotoka magwiji wa filamu waliothubutu kuandaa filamu miaka ya tisini japo mazingira yalikuwa magumu; ingawa filamu iliyowazindua wengi ni 'Girlfriend' (2002) chini ya uongozaji wa George Otieno “Tyson”, lakini ni filamu ya 'Shamba Kubwa' (1995) iliyotungwa na kuongozwa na Mwl. Kassim Al Siagi wa Tanga ndiyo iliyofungua milango ya filamu za kibiashara hapa nchini.

Kipindi kile teknolojia ilikuwa bado ndogo na vituo vya televisheni ndo kwanza vilikuwa vimeanza. Wakati huo kulikuwa na vituo vya ITV na CTN tu ambavyo hata hivyo vilirusha matangazo yake hapahapa jijini Dar es Salaam.

Shamba Kubwa’ ndiyo filamu iliyowaibua wasanii ambao baadaye wamekuwa mahiri katika ulimwengu wa filamu, kama Hassan Master, Jimmy Master, Kaini na Amina Mwinyi, ni filamu iliyoteka wengi kwa wakati ule japo teknolojia ilikuwa bado ndogo sana ukilinganisha na hivi sasa.

Baadaye zilifuatia sinema nyingine kama ‘Love Story Tanganyika na Unguja (1998)' ya Amri Bawji, ‘Kifo Haramu’ ya Jimmy Master, ‘Dunia Hadaa (2000)' ya Mwl. Kassim Al Siagi, na ‘Augua (2002)' ya Amri Bawji iliyodhaminiwa na Mfuko wa Utamaduni. Magwiji hawa wote wanatokea Tanga.

Ikumbukwe kwamba filamu hizi zilitengenezwa katika mfumo wa VHS (analogy), na hata uhariri wake ulitumia akili zaidi kutokana na teknolojia ya wakati huo kuwa ya kiwango kidogo, lakini zilivutia sana kutokana na maudhui na msuko mzuri wa hadithi.

Hata zilipoibuka filamu za Girlfriend, Sabrina, Masaa 24, na nyingine nyingi zilizofuata baada ya hapo, bado watu waliburudika japo zilikuwa na makosa ya hapa na pale ya kiufundi, msuko wa hadithi na maudhui, lakini hata siku moja watazamaji hawakudai uwepo wa part 2 kwa sinema hizo.

Nikiri kwamba soko la filamu lilikuwa likikua vizuri na kuleta ufanisi, lakini kitendo kilichofanywa na msambazaji wa filamu nchini, Steps Entertainment, kuwalazimisha watayarishaji wa filamu kutengeneza sinema yenye sehemu mbili au zaidi hata kama hadithi hairuhusu, kwa kweli si cha haki na kunazidi kuididimiza tasnia hii kwa maana ya kupungua ubora wa kazi husika.

Kitendo hiki pia humlazimisha msanii kuigiza awamu ya pili ya filamu (kwa pesa ileile) hata kama hakuwa na lengo la kuigiza sehemu hiyo, jambo hili linatafsiriwa kama kuendelea kuwanyonya wasanii kupitia kazi zao kwa malipo kiduchu wanayowalipa.

Nina mfano hai uliomtokea mtayarishaji wa filamu nchini, Hamisi Kibari, anayejulikana sana kwa filamu zake za 'Usiku wa Taabu', ‘Usikose Kwenye Mazishi Yangu’ na 'Mtoto wa RPC' ambaye kwa sasa anajiandaa kutoa filamu nyingine inayoitwa 'Naomi'. Kibari aliitengeneza filamu ya Naomi ikiwa katika sehemu moja tu, baada ya kuridhishwa na script iliyopitiwa na wataalam kadhaa na kuonekana kuwa ni nzuri.

Baada ya kukamilisha kazi hiyo aliipeleka kwa msambazaji (Steps), ambaye aliipitia na timu yake, waliisifia sana lakini wakamshauri kuwa kama anataka waisambaze lazima aangalie uwezekano wa kuirefusha kwa kutovikata vipande (scenes) mapema, bali aviache viendelee kwa zaidi ya dakika tano, aongezee establishing shots nyingi na kuweka flashback ndefu ili angalau filamu iwe ndefu kwa ajili ya kuikata sehemu mbili, jambo ambalo Kibari hakukubaliana nalo kwa kuhofia kuharibu mtiririko wa stori.

Baadaye Kibari aliamua kufanya utafiti kuhusu faida na hasara ya filamu hizi za part 1 na 2 kwa kumfuata msambazaji mwingine, ambaye alimweleza kuwa watazamaji wengi na hata wauzaji wa filamu wa rejareja wamekuwa wakizikacha filamu zisizokuwa na sehemu mbili na husubiri hadi sehemu ya pili itakapotoka ndipo wanunue, jambo ambalo limekuwa likisababisha hasara kwa watayarishaji wa filamu zisizokuwa na sehemu mbili.

Kulazimisha sinema iwe na namba moja na mbili kunasababisha kuoneshwa kipande (scene) kimoja cha mtu kwa zaidi ya dakika tano akifanya tukio moja, mfano mtu anatoka kuoga anaingia chumbani, kisha anaaza kupaka mafuta, anavaa nguo, anachana nywele na kupaka vipodozi! Yote yakiwa yanafanywa kwa zaidi ya dakika tano! Jambo hili limekuwa linavuruga lengo la sinema ambalo ni kuwaburudisha na kuwaelimisha watazamaji kama ilivyo dhana nzima ya filamu na ugizaji, na badala yake limekuwa likiwakera.

Utoaji wa filamu ya part 1 na 2 ni sumu mbaya sana iliyopandikizwa kwa watazamaji wa filamu ambao wamekuwa wakiamini kununua sinema yoyote isiyokuwa na part 1 na 2 ni kuibiwa, na imekuwa kama jeraha kubwa lililogeuka kuwa gonjwa sugu mfano wa saratani. Hivi sasa tunashuhudia filamu zisizo na ubora zikijitokeza kila uchao kwa sababu ya kulazimisha utengenezaji wa sehemu mbili kinyume na taaluma ya filamu.

Watayarishaji wengi wa filamu wanaopeleka kazi zao Steps, hata kama zina ubora hujikuta wakikataliwa kwa sababu tu hazina sehemu mbili, kitu ambacho ni unyanyasaji, hujuma kwa soko la filamu na hakizingatii taaluma (professionalism).

Kwa sasa imekuwa ni jambo la kawaida kwa filamu moja kuigawa na kuwa na sehemu zaidi ya moja na kubatizwa jina la part 1 na kuendelea hata kama zitafika mia ni jukumu la mtayarishaji wa filamu husika, na ukiuliza utaambiwa kuwa wasambazaji wanapambana na maharamia wa kazi za wasanii, wakigawa wanasababisha wezi hawa kupungua, jambo ambalo sidhani kama lina ukweli wowote.
Kilichofanywa hapa ni kiini macho tu na wizi, kupunguza bei ya DVD hadi 1,500/- na kuigawa filamu mara mbili au zaidi, ambapo mtazamaji anayehitaji kuiangalia filamu yote humlazimu kununua DVD nyingi (sehemu ya filamu zote) ambazo zimegawanywa, na hujikuta akizinunua kwa bei kubwa zaidi tofauti na inavyosemwa kuwa bei imeshushwa. Kama lengo ni kupambana na uharamia wa filamu basi kwa mtindo huu watakuwa wamechemsha, kwa kuwa filamu bandia bado ni gharama nafuu.

Kimsingi ugawaji wa filamu katika sehemu zaidi ya moja unamnufaisha zaidi msambazaji na wala si mtumiaji ambaye amejengewa dhana ya kwamba sinema isiyokuwa na sehemu mbili haifai na anaibiwa pesa zake. Filamu ya Part 1 na 2 ni sawa na filamu moja yenye dakika 70 hadi 90, na ukiangalia kitaalamu zaidi utagundua kuwa ndani ya filamu hiyo kuna filamu fupi sana isiyozidi dakika 20, kwa kuwa vipande vingi ni vile ambavyo kitaalam vinaitwa
establishing shots, flashbacks ndefu, na matukio marefu yasiyo na maana kabisa.

Utengenezaji wa filamu ya part 1 na 2 ni njia ya kuwaibia watazamaji kijanja bila kutoa jasho. Mbona filamu za Kihindi ni ndefu sana lakini hazina part 1 na 2? Ila kutokana na msisimko wa visa, msuko mzuri wa stori zao na nyimbo (nachi) utajikuta umemaliza filamu bila kuulizia part 2.

Kitaalam kuna neno linaloitwa ‘serialization’, yaani muendelezo wa visa kuhusiana na mhusika fulani au hadithi husika. Mfano mzuri ni filamu za God Father, Da Vinci Code, Harry Porter na kadhalika. Pia kuna sinema kama The Princess Diary, ambayo ina sehemu mbili lakini zilizopangiliwa vizuri kiasi kwamba huhitaji kupata sehemu zote ili kuijua stori, kila sehemu inatosha kukuburudisha bila msada wa sehemu ya pili, japo ya pili ni kama muendelezo wa sehemu ya kwanza.

Kibari ameamua kutoa filamu ya Naomi ambayo licha ya kuwa na sehemu mbili lakini kila sehemu ina stori inayojitegemea, yenye maudhui na visa tofauti kumhusu binti anayeitwa Naomi ili kumpa burudani mtazamaji, jambo ambalo limezingatia taaluma husika.

Wananchi na wanunuzi wa sinema za Bongo wanapaswa kufahamu kuwa kununua filamu za part 1 na 2 ambazo kimsingi zilipaswa kuwa sehemu moja tu ya filamu ni kuibiwa.

No comments: