May 2, 2012

Tujifunze kutoka sekta ya filamu ya Afrika Kusini


Mtendaji Mkuu mpya wa Taasisi ya Taifa ya Filamu na Video 
(NFVF) nchini Afrika Kusini, Zamantungwa (Zama) Mkosi

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo nchini
Tanzania, Dk. Emmanuel Nchimbi

SIKU zote nimekuwa nikiwasihi wale wote wanaopenda maendeleo ya tasnia ya filamu nchini kuuangalia mfumo unaotumiwa na nchi ya Afrika Kusini ili kuiboresha sekta ya filamu nchini. Nadhani sasa ni muda muafaka kuliangalia kwa mapana yake, hasa kipindi hiki tunapojiandaa kuandika katiba mpya.

Sekta ya filamu ya Afrika Kusini ni moja ya sekta za filamu mahiri duniani, ni sekta inayokua na kuzidisha ushindani katika anga za kimataifa. Watengenezaji wa filamu wa ndani na wa nje wanatumia fursa mbalimbali zilizopo; maeneo ya kipekee - na gharama nafuu za uzalishaji kutokana na kiwango kizuri cha pesa ya nchi hiyo dhidi ya dola ya Kimarekani, ambacho hufanya kuwepo unafuu wa hadi asilimia 40 katika kutengeneza filamu Afrika Kusini kuliko Ulaya au Marekani na unafuu wa hadi asilimia 20 zaidi kuliko Australia.

Hazina kubwa katika taji la sekta ya filamu ya nchi hiyo ni Tsotsi, kazi ya Gavin Hood iliyoigiza kuhusu vijana waporaji wa Soweto, karibu na Johannesburg, ambayo imeshinda tuzo ya Academy katika kipengele cha filamu za lugha ya kigeni mwaka 2006. Filamu nyingine iliyoteuliwa kushiriki tuzo ya Oscar ni Yesterday, iliyochezwa na Leleti Khumalo, na ilishawahi kushinda katika tuzo mbalimbali za kimataifa, na U Carmen E Khayalitsha, iliyopigwa katika lugha ya Xhosa ambayo ilishinda tuzo ya Golden Bear mwaka 2005 katika Tamasha la Filamu la Kimataifa la Berlin, zimetia chachu kwa watengenezaji wa filamu wa Afrika Kusini kuwa wabunifu na wenye kujali ubora.

Kutokana na sifa hii, sinema nyingi za bajeti kubwa na zenye mafanikio makubwa za kimataifa zimekuwa zikitengenezewa humo, ikiwa ni pamoja na Blood Diamond iliyomshirikisha Leonardo DiCaprio na Lord of War, iliyomshirikisha Nicholas Cage akicheza kama muuza silaha duniani, Lord of War imesaidia kutangaza maeneo tajiri nchini Afrika Kusini – huku eneo la Cape Town likionekana kama maeneo tofauti 57 yaliyofanywa kuonekana kama maeneo katika Mashariki ya Kati, Afghanistan, Bolivia, Sierra Leone na kwingineko.

Hali hii haikuja hivihivi tu bali ilitokana na Serikali ya Afrika Kusini kutambua kuwa sekta ya filamu ni sekta yenye nguvu na inayochangia kwa kiwango kikubwa ukuaji wa uchumi. Ingawa mchango wa Afrika Kusini kwa pato kimataifa unasimama katika asilimia 0.4 tu, sekta ya filamu ndani ya Afrika Kusini inazidi kupata nguvu wakati wote.

Mwaka 1995, wakati nchi hiyo ilipoanza kutumika kama eneo muhimu kwa uzalishaji wa filamu na televisheni, sekta hiyo ilitoa ajira 4,000 nchini kote. Sasa imepanda hadi zaidi ya ajira 30,000, pamoja na ajira nyingine zaidi - na mapato – vikitengenezwa katika filamu - ikihusisha usafiri, malazi na chakula.

Kwa mujibu wa Idara ya Biashara na Viwanda, sekta ya burudani ya Afrika Kusini ina thamani ya karibu Randi bilioni 7.4, huku filamu na televisheni zikichangia zaidi ya Randi bilioni 5.8 katika shughuli za kiuchumi kila mwaka. Na kulingana na matokeo ya utafiti wa tathmini ya kiuchumi ya hivi karibuni uliosimamiwa na Tume ya Filamu ya Cape, sekta hiyo ina mapato ya moja kwa moja kila mwaka ya zaidi ya Randi bilioni 2.65 na huchangia mapato ya moja kwa moja kila mwaka ya zaidi ya Randi bilioni 3.5 ya pato la taifa la nchi hiyo (GDP).

Faida za ukuaji haraka wa sekta ya filamu ziko wazi, hasa linapokuja suala la kuingiza fedha za kigeni. Ushiriki katika uzalishaji na matokeo ya makampuni ya kimataifa katika uwekezaji wa moja kwa moja wa mamilioni ya randi katika uchumi.

Kufikia mafanikio hayo, Afrika Kusini iliingia mikataba ya ushirikiano katika uzalishaji filamu wa pamoja na nchi nne: Canada, Italia, Ujerumani na Uingereza. Hii inamaanisha kwamba ushirikiano wowote rasmi katika uzalishaji filamu unachukuliwa kama uzalishaji wa kitaifa kwa kila nchi mwenza iliyohusika katika uzalishaji, na hufanywa hivyo kwa faida au mipango kwa msaada wa kila nchi inayohusika. Afrika Kusini pia ina mkataba wa makubaliano ya filamu na India.

Serikali ya Afrika Kusini imekuwa ikisisitiza umuhimu wa filamu katika kujenga urithi wa nchi hiyo kwa kuwasimulia watu hadithi zao wenyewe, na imejiweka katika “kuwezesha udhibiti” kwa kuhimiza uzalishaji wa bidhaa za ndani.

Vyombo vya utangazaji vya Afrika Kusini vimekusudia kufikia lengo la kutoa kipaumbele kwa kazi huru za ndani, ambazo zimesababisha kuongezeka kwa mahitaji ya vipindi vya ndani. Zaidi ya tamthilia saba zinazorushwa kila siku Afrika Kusini zinazalishwa nchini humo.

Watengenezaji filamu wa kimataifa pia wanalengwa kwa Randi milioni 430, Studio za Filamu kama za Hollywood zinajengwa nje ya jiji la Cape Town. Wanahisa katika mradi wa Studio za Cape Town - zamani walijulikana kama Dreamworld - ni pamoja na Videovision, Sabido Investments, the Rico Trust, the Helderberg African Chamber of Commerce, na Taasisi ya biashara na uwekezaji ya Western Cape.

Serikali, kupitia Taasisi ya Taifa ya Filamu na Video (NFVF), Shirika la Maendeleo ya Viwanda na Idara ya Biashara na Viwanda, ni mwekezaji mkuu katika sekta ya filamu. Taasisi ya Taifa ya Filamu na Video husaidia katika upatikanaji wa fedha katika tasnia, kupromoti maendeleo ya watazamaji wa filamu na televisheni wa Afrika Kusini, kuendeleza vipaji na ujuzi katika nchi - kwa msisitizo maalum kwa makundi maalum - na kuwasaidia watengeneza filamu kuwakilisha na kuuza kazi zao kimataifa.

NFVF hutoa fedha kwa ajili ya uzalishaji wa filamu na makala (documentaries) kwa njia ya mikopo au ruzuku. Husaidia makampuni ya uzalishaji yanayomilikiwa na Waafrika Kusini, na hutoa kipaumbele kwa miradi au mashirika yanayoweka umuhimu wa kitaifa na mapendekezo ambayo yanasisitiza kazi za ndani na ambayo yana uwezeshaji au mafunzo.

Pia inagharamia fedha za elimu na mafunzo kwa njia ya masomo mbalimbali; kutoa tuzo za maendeleo; na misaada ya maombi ya fedha kwa ajili ya uuzaji na usambazaji, inaruhusu wazalishaji filamu wa kujitegemea na wasambazaji katika upatikanaji wa maeneo ya kuoneshea filamu na uzinduzi wa filamu. Mnamo Machi 2007, NFVF ilitoa kiasi cha Randi milioni 26 kama ruzuku.

Serikali kupitia Taasisi ya Maendeleo ya Fedha na Shirika la Maendeleo ya Viwanda (IDC) imekusudia kujenga sekta endelevu ya filamu ambayo ujuzi utasambaa kwa watu kutoka makundi yaliyokuwa chini ya ubaguzi wa rangi na "kazi za ndani" za filamu zinatengenezwa na kuangaliwa na Waafrika Kusini.

Misaada ya fedha kwa kawaida hutolewa katika mfumo wa mkopo. Ushiriki wake wa chini ni Randi million 1 na si zaidi ya asilimia 49 ya mradi. Mnamo Juni, 2008, IDC imewekeza zaidi ya Randi milioni 500 na kufadhili filamu zaidi ya 30 nchini humo.

Pia Idara ya Biashara na Viwanda (DTI) inatoa motisha maalum katika sekta ili kuhamasisha kazi za ndani pamoja na kuvutia uzalishaji wa kimataifa. DTI ilitangaza marekebisho ya motisha za uzalishaji filamu na vipindi vya televisheni mnamo Machi 2008, ikiondoa kizingiti na kufungua mlango kwa ajili ya filamu za bajeti ndogo kutoka kwa watengeneza filamu wanaoibukia.

Motisha ya fedha inatolewa katika Uzalishaji Filamu na vipindi vya Televisheni wa Afrika Kusini ili kusaidia uzalishaji wa bajeti angalau kwa Randi milioni 2.5 (takriban dola 310,000). Motisha inatolewa ikiwa na punguzo la asilimia 35 ya gharama kwa filamu na kipindi cha televisheni kwa Randi milioni 6 (dola 745,000) zilizotumika na asilimia 25 kwa salio la matumizi ya uzalishaji.

Motisha inayotolewa katika Maeneo ya uchukuaji picha za Filamu na Televisheni inalenga kuvutia filamu za nje za bajeti kubwa na vipindi vya televisheni. Inatoa punguzo la asilimia 15 kwa wazalishaji wa kigeni na Waafrika Kusini waliotumia angalau Randi milioni 12 (karibu dola za Marekani milioni 1.5). Miradi yote, imewekwa kufanya kazi hadi 2014.

Taasisi tatu za kikanda - Tume ya Filamu ya Cape, Tume ya Filamu ya Gauteng na Ofisi ya Filamu ya Durban - zimeanzishwa kusaidia kuitangaza miji yao kama maeneo muhimu ya uchukuaji picha za filamu na kujenga mazingira mazuri kwa watengeneza filamu.

Mipango ya msaada ya Tume ya Filamu ya Gauteng, kwa mfano, ni pamoja na kusaidia ufadhili na usimamizi wa fedha, na mazungumzo ya ushirikiano ya uzalishaj na miradi ya ushirikiano na utangazaji.

Kwenye suala la kodi; Huduma ya Mapato ya Afrika Kusini, katika Sehemu ya 24 F ya Sheria ya Kodi ya Mapato, hutoa ruzuku ya punguzo la gharama za uzalishaji wa filamu kwa mmiliki wa filamu. Haiunganishi makato yoyote katika gharama za uzalishaji, au posho yoyote inayohusiana na hicho, chini ya masharti yoyote ya Sheria ya Kodi ya Mapato, hutoa posho ya filamu badala yake. Sehemu ya 24 F pia inaeleza kwamba mmiliki wa filamu anaweza kukata posho ya filamu kutoka kwenye mapato yake.

No comments: