Apr 25, 2012

Ni nini kitatusaidia kufikia mafanikio ya soko la filamu?


Ukurasa wa facebook unaweza kutumika kutangaza sinema

Pia unaweza kutumia ukurasa katika mtandao wa Youtube

TASNIA ya filamu nchini ni sawa na mtoto yatima lakini hali hii isiwe sababu ya kutufanya kulipua kazi zetu, bali tunapaswa kuangalia namna iliyo nzuri itakayotuwezesha kuboresha kazi zetu na kufanikiwa katika soko la ndani na hata nje ya Tanzania. Nimewahi kudokeza katika siku za nyuma kuhusu vigezo muhimu viwili vinavyoweza kutuongoza katika dhana nzima ya mafanikio hasa tunapolifikiria soko la filamu: Maudhui/Mahitaji ya Watazamaji na Jukwaa la Uwasilishaji.

Tunapaswa kwanza kuwaelewa watazamaji wetu kabla ya kufanya chochote, kwani ni hatua muhimu sana katika mchakato wa biashara ya filamu.
Tunapaswa kubainisha maudhui ya kazi zetu ili yaendane na matarajio yao. Kama hatuwezi kuambatanisha maudhui yetu yaende sambamba na mtazamo wa watazamaji, basi, filamu zetu zitaendelea kupuuzwa na tutaendelea kuwa watu wa kulalamika.

Kama mtayarishaji wa filamu, suala la kwanza anatakiwa kuwajengea msingi watazamaji katika maudhui aliyoyakusudia, akielewa kwamba anaweza kuwa bosi kwenye kampuni yake; LAKINI ANACHOKIFANYA SI KWA AJILI YAKE! NI KWA AJILI YA WATAZAMAJI NA HADITHI ZAO!

Kwa miaka kadhaa, sekta ya filamu Tanzania imeshuhudia utofauti mkubwa kati ya maudhui katika hadithi zetu na kile watazamaji wanachokihitaji, na matokeo yake yameendelea kuyumbisha mikakati ya soko na sera za usambazaji. Watazamaji wamekuwa wakinunua kazi zetu si kwa kuwa wanazipenda, hasha, bali kwa kuwa hawana mbadala. Tusitegemee hali hii kuendelea kutubeba siku zote, tunapaswa sasa kuzingatia suala la maudhui ambayo lazima yahusishwe moja kwa moja na mahitaji ya watazamaji ili kuwe na nafasi ya mafanikio kwenye soko.

Maudhui yanayofaa katika kizazi cha leo ni yale yanayokwenda sambamba na watazamaji ndani ya akili zao na kuihusisha jamii moja kwa moja. Kitu ambacho mtayarishaji/ mwandishi anapaswa kujua kuhusu watazamaji wake ni muhimu sana kwa mafanikio katika biashara ya usambazaji. Kujenga maudhui bila uelewa mkubwa na ufafanuzi kwa walengwa, ni kama kufunga safari ya kwenda mahali bila kufikiria jinsi ya kufika huko. Kama maudhui tunayoandaa hayakushikamana na aina ya maisha au matarajio ya watazamaji wetu, ni dhahiri tunawapoteza.

Watayarishaji wa filamu wayafahamu kwanza makundi ya watazamaji wetu, na kundi la kwanza la watazamaji wa filamu zetu ni la akina mama wa nyumbani, wafanyakazi wa ndani, na vijana wasio na ajira. Kundi la pili ni la watazamaji linalotokana na matokeo ya moja kwa moja ya vituo kama Africa Magic kuonesha filamu kwenye familia za watu wa tabaka la kati na la juu wenye uelewa mpana.

Na bila shaka kuna kundi la tatu linalotokana na watazamaji Watanzania walio nje ya nchi na Waafrika (wanaojua au kukipenda Kiswahili) katika bara la Afrika na maeneo waliko. Ni muhimu kuelewa kwamba kila moja ya makundi haya ya watazamaji yana muundo na mawazo ambayo ni tofauti sana na kundi jingine.

Katika utazamaji filamu zetu, kuna dhana ambayo huendana na mitazamo ya watazamaji (matamanio, maadili, na mtazamo wa mtu binafsi kulingana na uzoefu wake katika kuangalia kazi mbalimbali) na vitu hivi huathiri namna watazamaji wanavyohusiana na dunia inayowazunguka, ikiwa ni pamoja na maudhui.

Kabla hadithi zetu hazijawafikia watazamaji, tayari mtazamaji atakuwa na picha ya kipi anataka kukiamini na kama hadithi zetu zimeandaliwa katika mtazamo mzuri, mtu wa aina hiyo huamini na hununua kazi bila kusita kama ilivyo kwa kazi za wenzetu. Kama hadithi itaifikia jamii ya watazamaji ambao mtazamo wao utalingana na visa vyetu, wigo wake utapanuka, watu watapeana taarifa kwa njia ya neno kwa neno (ambayo ni njia ya ufanisi zaidi kwa mkakati wa soko) na hujenga nidhamu ya utazamaji wa filamu.

Vizuri tu kama, tutaambatanisha ubora wa kiufundi wa filamu zetu uendane na ubora wa watazamaji wetu waliouzoea. Tusidanganyane, watazamaji wa leo wameelevuka na wanaujua ubora wanaouhitaji, hivyo tusitegemee kuendelea kufanya biashara - kwa mfano, kuwapa filamu yenye kiwango hafifu watazamaji ambao wamezoea kuangalia sinema za kigeni, ambazo zimetengenezwa kwa kiwango cha juu cha ubora.

Pia tusisahau kuwa watazamaji wetu wanahitaji majukwaa ya habari kama wanavyojali kuangalia maudhui. Falsafa hii ni muhimu wakati tunaposhughulikia maudhui yanayowafaa watazamaji. Jukwaa la uwasilishaji katika dunia ya kisasa ya filamu haliishii tu kwenye kazi ya usambazaji, linakwenda ndani zaidi ya kile hasa soko la filamu lilivyo leo. Jukwaa litasaidia kuwasilisha mawazo kwa watu katika njia itakayojumuisha mitazamo yao.

Ufanisi katika uwasilishaji unachangia utoaji haki ya kuchagua; kuyaleta maudhui kwa watazamaji katika dunia yao wenyewe. Kulingana na uwezo mkubwa wa soko la Tanzania kama litawezeshwa (ndani na nje ya bara la Afrika), jukwaa muafaka litamfanikisha kwa urahisi mtengenezaji wa filamu kuendana na ushindani wa soko.

Mustakabali wa biashara ya usambazaji wa filamu na masoko Tanzania unatokana na watazamaji vijana. Watoaji filamu wanatakiwa kuandaa kwa uangalifu takwimu ya watazamaji na kukutana nao katika dunia yao.

Katika hatua hii itakuwa vizuri pia kuuchunguza mfumo wa usambazaji ili kupata ufumbuzi wa kutangaza na kusambaza ambao umesaidia kurekebisha tasnia katika nchi nyingine, ili uigwe katika sekta ya filamu Tanzania. Filamu ni bidhaa, kama zilivyo bidhaa nyingine, kuzitangaza na kuzisambaza ni vitu vyenye umuhimu sawa.

Lazima tuweke mkakati wa kujitangaza kwenye mitandao ya intaneti. Hii itaongeza mipaka katika utekelezaji wa kampeni ya kuzitangaza kazi.
Lakini tuna tatizo kubwa hapa kwetu kwamba Tanzania bado haina kiwango kikubwa cha watu wanaotumia intaneti ukilinganisha na nchi zingine katika Afrika, ni asilimia ndogo sana ya wananchi wanaotumia mtandao.

Ili tuweze kupiga hatua kwenye suala hili tunahitaji nguvu kubwa kuielimisha jamii faida za kutumia mitandao ya jamii inayoweza kusaidia utoaji habari za filamu na kujenga jamii yenye wafuasi, na humo, mijadala inaweza kujadilika, kipengele muhimu kabisa cha kuleta ufahamu au kampeni ya kujitangaza.

Hayo ni maeneo ambayo watu wanaotembelea wanaweza kupata habari zaidi, kushiriki katika mijadala, kujiunga na majarida, na kubadilishana ujuzi na mawazo na watu wengine, kwa lengo la kupanua wigo mkubwa wa watazamaji.
Katika miaka michache iliyopita, mitandao imesaidia sana kufanya uwepo wa gharama nafuu katika kutangaza na kuuza kazi kwa watengeneza filamu na hata kwa studio. Katika baadhi ya nchi zilizoendelea, ni nadra na kosa kubwa kutokuwa na wavuti (website) ya kutangaza filamu kabla haijaoneshwa kwenye majumba ya sinema.

Hii inawapa mashabiki fursa ya kupata habari kuhusu maudhui/hadithi, wasifu wa waigizaji, na kuchangia maoni yao na matamanio yao katika filamu na husaidia kuenea kwa taarifa au tetesi za filamu. Mbali na kuwa na wavuti ya kujitolea, kuweka filamu zetu kwenye mitandao ya kijamii iliyopo ni njia nyingine nzuri ya kuongeza jamii ya watazamaji/wafuatiliaji wa filamu.

Siku hizi, facebook, Twitter, Youtube ni njia nzuri za kujitangaza kwa haraka, kama watayarishaji lazima tuangalie namna ya kuongeza wavuti zetu na kuongeza matangazo na taarifa zetu muhimu. Matangazo ya kulipia kwenye televisheni, radio, magazeti, majarida, na majarida ya kitaaluma (professional journals) ni muhimu pia.

Pia tuhakikishe tunaziingiza filamu zetu kwenye matamasha ya filamu ili zionekane. Kuzionesha filamu kwenye matamasha ya filamu ni jambo zuri sana ambalo linaweza kusaidia kuongeza wigo wa taarifa. Matamasha ya filamu husaidia kueneza taarifa miongoni mwa wakosoaji wa filamu na watazamaji, na inaweza kuongeza umaarufu wa filamu na watazamaji kuwa wengi kama mapitio yake yalikuwa ya kuvutia.

Wakati sisi tukiendelea kukaa katika ulimwengu wetu wa 'uvivu wa fikra' sehemu nyingine ya dunia inasonga mbele kwa kasi zaidi kuliko tunavyodhani.
Pamoja na ongezeko kubwa la idadi ya mitandao na kunyonya filamu (film downloads) ambapo mauzo na usambazaji wa DVD na video yanaendana na mahitaji ya teknolojia yatabadilisha mkondo wa mapato, watengeneza filamu wataweza kupanua njia yao ya wigo wa usambazaji kwa idadi kubwa ya watazamaji, hasa vijana, ambao wameonekana kuwa na msisimko mkubwa na teknolojia hii.

Kumbuka kuwa: Hivi sasa, mipango ipo njiani kwa nchi kuhama kutoka matangazo ya kizamani ya Analogia ya televisheni kwenda kwenye mfumo mpya wa digitali – kunakoongeza mahitaji makubwa ya vituo vya televisheni; hii inatoa nafasi kubwa ya kuingia.

Alamsiki…

No comments: