Apr 17, 2012

Rambirambi za msiba wa Kanumba zachachuliwa

Steven Charles Kanumba, enzi za uhai wake

Waigizaji wa filamu nchini, Mahsen Awadh (Cheni) 
na Issa Mussa (Claude) kwenye msiba wa Kanumba.
Claude ndiye aliyekuwa mwekahazina wa kamati
ya mazishi ya Kanumba

Wananchi wakimuaga Kanumba kwenye viwanja 
vya Leaders Club

Uongozi wa Bongo Movie uliohusika na uratibu wa shughuli za mazishi ikiwemo michango katika msiba wa msanii Steven Kanumba, umeingia kwenye kashfa nzito. Kwa mujibu wa chanzo cha uhakika kutoka ndani ya familia ya Kanumba, kamati hiyo imedaiwa kufanya uchakachuaji wa michango hiyo inayokadiriwa kuwa mamilioni ya fedha, achilia mbali vitu kadhaa, yakiwemo magunia 32 ya mchele.

Inasemekana kuwa, dalili za hali hiyo zilianza kujitokeza mapema kabisa pale mwanandugu mmoja alipoenguliwa kwenye kamati hiyo, kwa kile kinachoelezwa, kamati hiyo kufanya jukumu hilo kwa uhuru zaidi.

Dalili nyingine, ni kitendo cha wajumbe wa Kamati hiyo kutoweka baada ya mazishi hadi walipofika nyumbani kwa marehemu Alhamisi usiku.

Kwamba, pamoja na mambo mengine, kwenye kikao kilichofanyika siku hiyo kati
ya wanandugu na kamati hiyo, Mama Kanumba amezuiwa kuzungumzia suala la michango.

“Mama Kanumba ametakiwa asiseme lolote kwa Waandishi wa Habari kuhusu michango… kaelezwa kama atafanya hivyo, huenda asipate kitu kabisa,” alisema ndugu huyo.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, Kamati hiyo imetoa onyo hilo kwa vile tangu kwisha kwa maziko ya Kanumba, wamekuwa wakipata usumbufu wa simu watu kuulizia kilichokusanywa na kilichobaki.

Chanzo hicho kimedokeza kuwa, baada ya kamati hiyo kukutana na wanafamilia kwa mara ya kwanza baada ya ukimya mrefu, ilisema michango yote ni shilingi milioni 51. Kati ya fedha hizo, gharama za mazishi ni shilingi mil 48 huku kukiwa na deni la shilingi milioni 2 za ukarabati wa barabara ya Leaders kutokana na uharibifu uliofanywa na waombolezaji.

Chanzo hicho kimedokeza kuwa, walipohoji fedha zilizochangwa kupitia M-pesa kupitia namba ambayo ilitangazwa, walielezwa ilipatikana sh 20,000 tu. Inasemwa, kiasi hicho ni kiduchu mno kwa sababu mashabiki wa Kanumba wa Mwanza pekee, walichanga sh 300,000.

Pia imesemwa kulikuwa na gunia 32 za mchele zilizotolewa na msamaria, hazijulikani zilipokwenda.
“Licha ya kutolewa gunia 32 za mchele, hazijulikani zipo wapi… fikiria hata mfiwa, anakosa hata gunia moja la kwenda kuanzia maisha mapya bila mwanaye,” kilidokeza chanzo hicho.

Ilipoulizwa kwa nini hawakuweka ndugu kwenye kamati hiyo tangu mapema, walisema alikuwemo, lakini akaenguliwa kwa kwa zengwe. Uratibu wa msiba huo ulikuwa chini ya Kamati iliyokuwa chini ya Gabriel Mtitu na wajumbe kama Vincent Kigosi (Ray), Issa Mussa (Cloud), Steven Nyerere, Happiness Magese, William Mtitu, Jacob Steven (JB) na wengineo.

No comments: