Apr 7, 2012

Msanii maarufu wa filamu Steven Kanumba hatunaye tena

Steven Kanumba (1984-2012)

Marehemu Kanumba akipelekwa chumba cha maiti

Elizabeth Michael (Lulu) anayehusishwa na kifo
cha Steven Kanumba

Zifuatazo ni picha za maombolezo:
Wasanii na wapenzi wa filamu wakiwa ndani ya fensi
ya nyumba aliyokuwa akiishi marehemu Kanumba

Wasanii mbalimbali wakiwa na simanzi nyumbani kwa
Steven Kanumba

Mwanamuziki H. Baba akiongea na waandishi wa habari
nyumbani kwa Steven Kanumba

Mohammed Mwikongi (Frank) akiongea kwa uchungu
kuhusu kifo cha Steven Kanumba

Mkurugenzi wa Global Publisher, Eric J. Shigongo
akiwasili nyumbani kwa Steven Kanumba

Mkurugenzi wa Aset, Asha Baraka akieleza masikitiko
yake kuhusiana na kifo cha Steven Kanumba

Ruge Mutahaba naye akielezea masikitiko yake kuhusiana
na kifo cha Steven Kanumba nyumbani kwa marehemu

Msanii maarufu wa filamu  nchini, Steven Kanumba, amefariki dunia ghafla usiku wa kuamkia leo baada ya kudondoka na kujingonga sehemu ya kisogo akiwa nyumbani kwake Vatican, Sinza jijini Dar es Salaam.

Tukio hilo limetokea majira ya saa 7 usiku wa kuamkia leo na taarifa za kudondoka kwa Kanumba zilitolewa na kijana anayeishi naye hapo nyumbani ajulikanaye kwa jina la Seti aliyemwita daktari kujaribu kuokoa maisha yake lakini alipofikishwa hospitali ya Muhimbili tayari alikuwa amekata roho.

Taarifa ambazo hazijathibitishwa ni kwamba Kanumba alianguka na kuumia kichwani baada ya mpenzi wake ambae anatajwa kuwa ni mwigizaji LULU (Elizabeth Michael) kumsukuma na kuanguka wakati wanagombana.
‘Inasemekana’ Kanumba wakati akijiandaa kutoka saa sita usiku aliingia bafuni kuoga, alipotoka alimkuta Lulu akiongea na mwanaume mwingine kwenye simu ndipo alipokasirika na ugomvi kuanza.

Mwili wa marehemu uko katika chumba cha kuhifadhia maiti hospitali ya Muhimbili. Habari zaidi zitawajia baadae.


Historia yake fupi:

Steven Charles Kanumbaa alizaliwa Januari 8, 1984 mkoani Shinyanga na amefariki Aprili 6, mwaka 2012. Elimu ya msingi alipata katika shule ya Bugoyi, Shinyanga na baadaye akajiunga na sekondari ya Mwadui, kabla ya kuhamia Dar Christian Seminary.

Baada ya kumaliza Kidato cha Nne hapo Dar Christian, Kanumba alijiunga na sekondari ya Jitegemee, Dar es Salaam kwa elimu ya Kidato cha Tano na Sita. Ni wakati huo akiwa Jitegemee Kanumba alianza shughuli za sanaa katika kundi la Kaole Sanaa Group la Magomeni, Dar es Salaam.

Baada ya kukomaa Kaole, Kanumba aliamua kuanzisha kampuni yake mwenyewe ya filamu na hadi anakutwa na umauti alikuwa mwigizaji anayefahamika Afrika nzima. Ameshirikiana na wasanii wakubwa duniani kama Ramsey Nouah wa Nigeria na amefanya kazi na mastaa wengine kadhaa wa Nigeria.

Miongoni mwa filamu ambazo alifanya ni Dar To Lagos, She is My Sister, Ancle JJ, Oprah, Tufani, Johari, Gharika, Baragumu, Sikitiko Langu, Dangerous Desire, Cross My Sin, Village Pastor, Family Tears na kadhalika.

Hivi karibuni, alikaririwa akisema atagombea Ubunge katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015. Kanumba atakumbukwa na wengi sana kwa ucheshi wake- upole na ushirikiano mzuri na wenzake katika kazi.

Kifo cha Kanumba ni pigo katika tasnia ya filamu Tanzania. Taifa limempoteza mtu ambaye alikwishaanza kuitangaza vema nchi kupitia sanaa hiyo na ambaye angetarajiwa kuitangaza zaidi katika anga za kimataifa zaidi kupitia sanaa hii.

Nigeria sasa wanajua Tanzania kupitia filamu. Nchi nyingi za Afrika zinajua sasa na hii sehemu ya kazi nzuri kwa Kanumba. Mwenyewe aliwahi kukaririwa alifika hadi Hollywood hadi Marekani, ambayo ni ‘makka’ ya wacheza filamu. Kwa sasa mwili wa marehemu upo katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam.

Tuzo:

-2011, Best Actor Of the Year - Bab Kubwa Magazine Awards
-2011, Best Movie Of the Year - Bab Kubwa Magazine Awards
-2011, The Best Film - Mini Ziff Film Awards
-2010, Best Male Actor - FilamuCentral Bora za 2010 Awards
-2010, Best Film Producer - FilamuCentral Bora za 2010 Awards
-2010, Best Actor – Clouds FM
-2010, Best Actor - Smiling Face Company
-2010, Certificate Of Appreciation - African Stars Entertainment (ASET)
-2008, Best Artist of the Year 2007/2008 - Federation of Artist in Tanzania, (Shiwata)
-2008, Honorary Award - Tanzania Film Vinara Awards

No comments: