Apr 12, 2012

Buriani Steven Kanumba: Kifo chako kimenifundisha jambo kubwa mno

Marehemu Steven Kanumba enzi za uhai wake

Steven Kanumba siku alipomtembelea Rais Kikwete
nyumbani kwake mjini Dodoma

WASANII mahiri wa filamu nchini wanazidi kupukutika, wasanii kama Mzee Jongo, Mzee Kipara, Mzee Pwagu, Pwaguzi, Mama Haambiliki na wengine. Lakini msiba wa hivi karibuni uliotokea Jumamosi ya tarehe 7 Aprili umeonekana kuwagusa na kuwashtua wengi sana, wafuatiliaji na wasio wafuatiliaji wa filamu, hasa kutokana na kifo cha ghafla cha kijana ambaye umaarufu wake ulikuwa ukizidi kupanda, na msanii mahiri wa filamu nchini, marehemu Steven Kanumba.

Umati uliojitokeza kuanzia siku kilipotangazwa kifo cha Kanumba hadi mazishi yake ni ushuhuda tosha kwamba tasnia ya filamu ni sekta yenye nguvu kubwa sana na kama ingetumiwa vizuri na serikali ingeweza kuchangia pato kubwa mno.

Niliapa kutokuwa mnafiki katika maisha yangu, na kwenye hili au kwenye jambo lolote linalogusa maisha yetu sitakuwa mnafiki, japo naamini kabisa kuwa haya ninayoyaandika hapa yanaweza kunigharimu kwa kuwa ninaotaka kuwafikishia ujumbe huu hawapendi kabisa kuambiwa ukweli.

Kwa kweli nilistushwa sana na msiba wa rafiki yangu Kanumba, nikiwa kati ya watu wa mwanzo kupata taarifa ya kifo chake mnamo saa tisa za usiku wa kuamkia Jumamosi, ingawa sikufika hospitali wakati mwili wa Kanumba ukipelekwa chumba cha maiti kwa kuwa mshtuko nilioupata ulinisababishia vidonda vya tumbo.

Nilitokea baadaye sana kwenye msiba nyumbani kwa marehemu baada ya kupata tiba iliyonipa nafuu japo kwa muda mfupi. Makala yangu ya leo hailengi kumzungumzia Kanumba jinsi nilivyomfahamu kama ambavyo wengi wamemzungumzia kwa kadri walivyoweza, bali nalenga katika kuangalia mustakabali wa tasnia ya filamu baada ya kile nilichokiona kilichotokana na kifo chake.

Waliomzungumzia marehemu Kanumba asilimia kubwa walikuwa wakimsema kwa mazuri, ama kinafiki kama ilivyo kawaida yetu ama kutoka moyoni, na wengine wakizusha tuhuma hizi na zile, ili mradi kila mmoja akijaribu kuonesha jinsi alivyomfahamu marehemu. Lakini tu yote hii imeonesha ni jinsi gani watu wengi wameguswa na msiba wa Kanumba kwa namna yao.

Kama ilivyo kawaida yetu, tayari kifo cha Kanumba kimeambatana na uvumi eti alikuwa Freemason na kwamba kuna masharti fulanifulani ameyakiuka na hivyo “ameuawa” kwa kukiuka mkataba wao! Kwangu mimi huu ni uzushi wa kupuuzwa, naheshimu taarifa za madaktari kuwa ndiyo taarifa rasmi na sababu za kifo cha rafiki yetu na kipenzi chetu Steven Charles Kanumba.

Katika taarifa ya awali ya madaktari ni kuwa Kanumba alipata mtikisiko wa Ubongo (Brain Concussion). Nikiwa mmoja wa watu waliopata nafasi ya kusomea fani ya utabibu sina shaka na hilo, ndiyo maana nakubaliana na taarifa ya madaktari. Brain Concussion hutokea baada ya ubongo kupata mshituko ama mtikisiko mkali wa ghafla na mara nyingi mtu hupoteza fahamu ingawa wengi huwa wanapona.

Katika msiba wa Kanumba nimeshuhudia mambo mengi na nimejifunza jambo kubwa ambalo kwangu ni elimu kubwa mno. Ni kama alivyotabiri mwenyewe kifo chake kwenye wimbo wake “Nakuinulia Macho Yangu” ambao baadhi ya mashairi yanasema kuwa:
“Nakuinulia macho yangu nitazame milima, msaada wangu baba utatoka wapi?... hata leo nikifa kila mtu atasifu na lake, ametutoka msaani wetu tuliyempenda sana, nani ataziba pengo lake, hata hao wanaonichukia, watabeba jeneza langu. Mwenzangu leo nipo hai twachekeana lakini rohoni ni vita kali, duniani tufurahie, furaha yetu hadi mbinguni, furaha ile ya milele. Sema na moyo wangu Bwana sema na maisha yangu mimi Kanumba, nitaridhika lini mimi masikini...”

Nimekuwa najiuliza, hivi tutaishi katika hali hii hadi lini? Wanatutumia kipindi cha kampeni lakini hawataki kuboresha miundombinu ya soko la sanaa ili kila msanii afaidi akiwa hai, sasa wameamua kututumia hata tukiaga dunia ili kurudisha umaarufu wao unaoporomoka! Ni lini wataacha tabia hii ya kutumia misiba ya wasanii maarufu kuwa ni sehemu ya kuuza sura? Hili kwangu si jambo la kufurahisha hata kidogo.

Jifikirie, msururu wote ule wa viongozi kwenda kwenye msiba wa Kanumba! Kama wangeamua kuivalia njuga tasnia hii na kutoa msaada wa kweli kwa kiwango hicho walichoonesha kwenye msiba, hivi wasanii wangekuwa kama walivyo leo? Kwa nini wasubiri tutumie nguvu nyingi kujipandisha kwenye umaarufu ili baadae wao wautumie unyonge wetu?

Viongozi kwenda kwenye msiba wa Kanumba na kutoa michango ya hela nyingi kwangu si tatizo, lakini pale viongozi wote wakuu wanapoacha kazi zao na kwenda msibani ni jambo linalotia shaka sana. Fikiria kiongozi, mkewe, familia yake wote wanakwenda kujazana kwenye msiba! Hivi walishindwa kuwakilishwa? Mbona tunaye Waziri mwenye dhamana ya Utamaduni, Vijana na Michezo ambaye angeweza kuiwakilisha serikali?

Isifikiriwe kuwa nasema haya labda sikumpenda marehemu Kanumba, la hasha! Marehemu alikuwa rafiki yangu mkubwa, lakini kama nilivyosema kuwa sipendi kuwa mnafiki. Kanumba keshatangulia, lakini vipi kuhusu wasanii waliobaki wanasaidiwaje kama hatutalisema hili? Na vipi kuhusu mustakabali wa tasnia nzima ya burudani?

Binafsi sikuona kabisa umuhimu wala haja ya viongozi wengi wa ngazi za juu kuacha shughuli nyingine nyeti za Taifa eti kwenda msibani, kusaini vitabu na kuhudhuria mazishi! Sawa Kanumba alikuwa msanii maarufu lakini si Kiongozi wa Serikali, hata Wawakilishi tu wa wakubwa wetu wangeweza kuwawakilisha vyema. Ina maana hatuna vipaumbele vyetu kama Taifa?

Msiba huu umenifundisha kuwa viongozi wa nchi hii hawana vipaumbele wala kazi za kufanya, wanaonekana bado wana ‘ujana’ ndani yao wakitafuta kitu kinachoitwa sifa bila kutazama maslahi ya taifa letu.

Ningewaona wa maana sana kama wangekuwa wamewasaidia wasanii kabla hawajarejea mavumbini. Hebu watazameni hawa wanaojiita wasambazaji wakubwa… Hivi tunajua kwamba marehemu Kanumba na wasanii wengine waliobaki hawachangii kabisa pato la taifa kwa sababu ya mambo ya kijanja janja yanayoendelea?

Majuzi kwenye mazishi ilinishangaza kusikia eti kiongozi anatamka kuwa wanataka sasa kulivalia njuga suala la uharamia (piracy) ili wasanii wafaidi jasho lao. Ina maana hili wamelijua leo? Hivi kweli wanaijua nguvu ya soko la filamu kabla hawajaivalia njuga piracy? Ni lini tutaacha kuongozwa kwa matamko ya viongozi ambayo mara zote yamekuwa hayatekelezwi? Kwa nini tusiweke misingi imara itakayosimamia soko letu bila kusubiri nani atafuata baada ya kanumba!

Hivi haki za wasanii wetu ziko wapi sasa? Nimekuwa nikilipigia kelele jambo hili kwenye makala zangu na hata kwenye vipindi vya televisheni ambavyo nimewahi kushiriki, nilifikia hatua ya kuishauri serikali yetu iutazame mfumo unaotumika Afrika Kusini kupitia chombo chao cha National Film and Video Foundation (NFVF) kama kweli wamekusudia kuisaidia tasnia ya filamu. Nikashauri tuwe na chombo chenye idara tano na nikazitaja, lakini hakuna kinachoendelea zaidi ya propaganda tu...

Soko la filamu nchini ni la mwenye nguvu ndiye anayepata huku serikali ikiwa haiambulii.Tazama hawana urithi wowote wafiwa, hizo milioni kumi walizopewa haziwasaidii katika kipindi chote bali ni za muda tu. Kazi nyingi alizozifanya marehemu hazitawasaidia, si za kwake kwani alishauza haki yake kwa hawa wanaojiita wasambazaji. Sijui viongozi wetu wanasemaje katika hili? Au kwa kuwa huo msiba ilikuwa ni nafasi ya pekee kuonekana na kuuza sura kwa watu wengi ndo tuone jinsi wanavyowajali wasanii? Hivi lini tutaacha unafiki?

Ni baadhi ya viongozi hawahawa wanaojitokeza leo kumsifu Kanumba na kusema wataipigania tasnia ya filamu ndiyo waliokuwa wakipalilia ugonvi wetu, ugomvi wa TAFF na Bongo Movies kwa kuwakubali wasiotambulika kisheria huku wakiwapatia misaada na kuwakataa wanaotambulika kisheria huku wasambazaji wakichukua haki zetu kirahisi!

Sikubaliani na wale wanaosema kuwa kifo cha Kanumba kimewafanya sasa viongozi wetu kuitazama tasnia ya filamu kwa macho mawilimawili na ndiyo mwanzo wa kufaidika kwa wasanii. Naamini kuwa tutafanikiwa tu pale tutakapoacha propaganda au kuchanganya siasa hata kwenye masuala ya msingi.

Naamini hata marehemu Kanumba atajisikia fahari huko aliko pale ambapo viongozi waliokuwa wakimsifu watakapoacha unafiki na kutenda wanachokihubiri. Kwangu mimi Kanumba ni kama nabii, moja ya sifa za manabii ni kutabiri vifo vyao.  Ukiacha wimbo ambao nimeshauelezea, Kanumba pia katika moja ya filamu zake za mwisho alizocheza imeonesha kutabiri kifo chake.

Filamu hiyo ya ‘Love is Power’ ambayo haijatoka, Kanumba ameigiza kujitolea figo kwa mke wake ambaye baadaye alikuja kumsaliti kwa kutoka nje ya ndoa na baada ya msanii huyo nyota kubaini uliibuka mzozo ambao ulisababisha kuwepo na ugomvi na mkewe lakini aliposukumwa na mkewe alianguka na kufa, jambo ambalo limetokea katika mazingira ya kifo chake halisi.

Na hata daktari ambaye alikuja kumtibu nyumbani kwake baada ya kuanguka majuzi kabla ya mauti kumkuta ndiye aliyeigiza katika filamu hiyo huku msanii ambaye pia amecheza kipande cha filamu kushuhudia kifo cha Kanumba ndiye huyo huyo majuzi aliifunua maiti yake kwenye jokofu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).

Buriani Steven Charles Kanumba, hakika kifo chako kimenifundisha jambo kubwa sana...

No comments: