May 22, 2012

Kwanini tuelendelee kuwa sekta ya 'kuganga njaa' tu?




Picha zote kwa hisani ya Mwewe

NILIANDIKA wakati wa msiba wa Kanumba kuwa umati wa watu waliojitokeza siku ya msiba wake ni ishara tosha kuwa sekta ya filamu nchini ni kubwa na yenye nguvu kubwa lakini iliyotelekezwa na serikali. Kama serikali itaamua kuzichukulia filamu kwa umakini mkubwa, ikaandaa sera na kuunda chombo maalum kitakachoshughulikia filamu mfano wa kile cha Afrika Kusini cha National Film and Video Foundation (NFVF), naamini kabisa zinaweza kuwa chanzo kikubwa na muhimu sana katika kujenga taifa na zinaweza kutumika kama jukwaa la kuchochea mijadala nchini kote.

Kupitia chombo chao cha NFVF Afrika Kusini wanajivunia ‘hazina’ za sekta ya filamu ya nchi hiyo kama Tsotsi, iliyoshinda tuzo ya Academy mwaka 2006, Yesterday, filamu nyingine iliyoshiriki tuzo za Oscar na iliyowahi kushinda katika tuzo mbalimbali za kimataifa, na U Carmen E Khayalitsha, iliyoshinda tuzo ya Golden Bear mwaka 2005 katika Tamasha la Filamu la Kimataifa la Berlin.

Muigizaji wa filamu ya Yesterday, Leleti Khumalo

Filamu ya Yesterday

Filamu ya Tsotsi iliyopata tuzo ya Oscar

Filamu hizi zimekuwa zikitia chachu na hamasa kwa watengenezaji wa filamu wa Afrika Kusini kuwa wabunifu na wenye kujali ubora. Vipi kuhusu sisi? Hivi serikali haidhani kuwa kuanzisha chombo cha aina hii kutasaidia kutufanya tuwe na kazi nzuri ambazo siku moja zinaweza kushinda tuzo katika matamasha makubwa na yanayoheshimika duniani?

Mbona hatujiulizi, sekta ya filamu Tanzania inatengeneza sinema nyingi mno zinazoifanya kushika nafasi ya tatu katika bara la Afrika, nyuma ya Nollywood (Nigeria na Ghana), lakini ni Afrika Kusini ambayo ina mafanikio makubwa kwenye sekta ya filamu. Kwa nini hatujiulizi kuwa sinema nyingi za bajeti kubwa na zenye mafanikio makubwa za kimataifa zimekuwa zikitengenezewa Afrika Kusini.
Nchi zilizoendelea kwenye sekta ya filamu duniani wanaitumia nchi hiyo kama eneo muhimu la kutengenezea sinema zao, ikiwa ni pamoja na Blood Diamond na Lord of War ambapo inaelezwa kuwa Lord of War imesaidia sana kutangaza maeneo tajiri ya Afrika Kusini.

Tuelewe kuwa hali ya kimafanikio ya Afrika Kusini haikuja hivihivi tu bali ilitokana na Serikali ya nchi hiyo kutambua kuwa sekta ya filamu ni sekta yenye nguvu na inayochangia kwa kiwango kikubwa ukuaji wa uchumi.

Kwa mujibu wa Idara ya Biashara na Viwanda, sekta ya burudani ya Afrika Kusini ina thamani ya karibu Randi bilioni 7.4, huku filamu na televisheni zikichangia zaidi ya Randi bilioni 5.8 katika shughuli za kiuchumi kila mwaka.

Ni wakati sasa tuamue kwa dhati kuandaa sera ya filamu, kuwa na chombo maalum cha filamu ili filamu zetu ziweze kututangaza vyema kimataifa, kuchangia pato katika taifa na kuvutia utalii. Bahati mbaya bado tasnia ya filamu nchini imezongwa na matatizo makubwa. Sekta hii inahitaji jitihada za kimtandao za ushawishi na utetezi. Hapana shaka jitihada hizi zikiwepo zitasaidia sana kuelekeza nguvu, kasi na ari zaidi iliyopo sasa katika jamii yetu kwenye maendeleo ya Sekta ya filamu.

Jambo linalouma zaidi ni kuona sekta ya filamu imekuwa ni sekta ya kujikimu tu, licha ya ukuaji wa haraka unaoonekana. Bado mavuno halisi katika kukuza pato la Taifa na hata watayarishaji walio wengi bado hawajafanikiwa kupata matokeo mazuri kiuchumi kupitia filamu.

Tasnia ya filamu ya Tanzania inaendelea kubakia kuwa aina ndogo ya sekta ambayo imekuwa mfano wa “kuganga njaa” ili mradi mkono uende kinywani, watayarishaji, wasanii na watendaji wengine wanabaki wakiwa wanaitumia sekta hii kujaribu kuweka mambo yao yaende sawa mezani, kwa maana ya kutafuta jinsi ya kujikimu tu. Bila jitihada za dhati sekta hii kamwe haitakuwa sekta endelevu ambayo taifa linaweza kujivunia.

Ingawa kumekuwepo juhudi nyingi kutoka kwa wadau mbalimbali kutaka sekta hii ikue na iweze kuleta tija, lakini juhudi hizo bado hazijaweza kutoa mavuno stahiki katika kile tunachoweza kuita pato linalotokana na uchumi wa kweli wa tasnia ya filamu.

Kwa nini sekta ya filamu iendelee kuwa sekta ya kuganga njaa? Hali hii itaisha lini? Hivi hatma ya wasanii kuishia kulipwa pesa kiduchu (peanuts) ambazo wala haziwasadii kujiendeleza bali zinasaidia kwa mlo wa siku chache tu ni ipi? Filamu ni chombo muhimu sana cha kijamii na kiutamaduni kwa ajili ya kujenga umoja miongoni mwa nchi hasa tunavyoelekea kwenye shirikisho la kisiasa la Afrika Mashariki.

Watazamaji wa Kitanzania kati ya wana-Afrika Mashariki wameonekana kuzipenda sana sinema zao pamoja na kuwepo kasoro nyingi na wamekuwa na hamasa kubwa. Kama zilivyo sinema za Nigeria ambazo alama yake kubwa ya kibiashara ni Kiingereza chao aina ya Pidgin, Kiswahili cha kisasa cha Tanzania kinazipa utambulisho wa kitaifa filamu zetu.

Kamwe hatutakiwi kukaa tu na kusema filamu ni burudani tu, hapana. Tunapaswa kuona filamu, mbali ya kuwa ni burudani lakini kama chombo maalum kwa ajili ya maendeleo ya taifa kwa sababu ndivyo imekuwa ikitumiwa na nchi nyingine zilizoendelea.

Changamoto ya kukosa ufahamu wa namna ya utengenezaji wa filamu kwa watayarishaji, wasanii wetu na watendaji wengine, uelewa mdogo wa wasanii, ukosefu wa miundo ya soko la kuuza kazi, tatizo kubwa la ukosefu wa mitaji ni mambo ambayo yanapaswa yabaki kuwa historia. Haipendezi kila siku tunapolia kuhusu mambo haya haya tu, wakati tuna mengo ya kufanya.

kwanini suala la mtaji liwe ni tatizo kubwa linaloumiza vichwa vya watayarishaji wa filamu kwa muda wote tangu Watanzania walipoanza kufanya filamu mpaka sasa? Tatizo la nchi hii ni nini hasa? Siku moja nilikuwa naongea na raia wawili wan chi jirani ambao walisema kuwa sekta ya filamu ndiyo fursa pekee ya Watanzania kujikwamua baada ya michezo mingine yote kuonekana tumeshindwa.

Kwa nini tasnia ya filamu ya Tanzania iendelee kuwa katika mparaganyiko mkubwa mno kutokana na ukosefu wa fedha? Kwa nini kikundi kidogo tu cha watu fulani mndicho kinachoachwa kulihodhi soko la filamu huku serikali ikiangalia na haifanyi jitihada zozote kunusuru hali hii?

Kwa takriban miaka 10 sasa kilio cha wasanii na watayarishaji wa filamu, mbali ya wizi wa kazi zao kimekuwa ni ukosefu wa mtaji wa kutengeneza filamu, ingawa mwezi Septemba 1998, ulianzishwa Mfuko wa Utamaduni na Serikali, ambao hata hivyo haukuwa na ufanisi kwa kuwa uligubikwa na matatizo lukuki.

Madhumuni makuu ya mfuko huo yalikuwa kuimarisha na kuiwezesha sekta ya Utamaduni (filamu zikiwemo) kuchangia kikamilifu katika mipango ya maendeleo ya uchumi wa Taifa kwa kuhamasisha jamii kujituma kufanya shughuli za utamaduni zenye kuchochea ubunifu, kuzingatia ubora wa bidhaa na huduma, kuongeza kipato katika kaya na kuhimiza ajira za kujitegemea.

Tangu mwaka 1998 ulipoanzishwa Mfuko, naweza kukiri kuwa Mawaziri wote waliopita Wizara ya Utamaduni wameshindwa kuandaa mkakati mzuri wa kusaidia upatikanaji wa pesa au kusaidia Mfuko kwa ajili ya watengeneza filamu kwa maendeleo ya Taifa, kwa sababu hakuna yeyote kati yao aliyeifahamu vizuri nguvu ya sekta ya filamu.

Pia kulikuwepo madai ya ufisadi au kutotumia pesa zilizotolewa na wahisani kwa ajili ya kuwawezesha wasanii na wadau wa utamaduni katika kufanikisha malengo. Walionufaika aidha walikuwa wanajuana na wahusika au ni ndugu, marafiki au maswahiba wa kibiashara. Sina uhakika katika hilo.

Tasnia ya filamu hapa nchini itaendelea kuwa sekta ya kuganga njaa kama hali itaachwa kama ilivyo. Ubunifu katika sekta ya burudani na sanaa - filamu - katika nchi hii umekuwa unakwazwa na ukosefu wa fedha jambo ambalo limekuwa ni tatizo kubwa katika jitihada za kukuza na kuendeleza sekta.

Ili tasnia ikue pande zote, serikali na sekta binafsi zinapaswa kuwa na sera nzuri, kinyume na ilivyo sasa ambapo hakuna sera ya filamu na wala hakuna anayefikiria kuipa kipaumbele tasnia hii. Hata hivyo, sekta hii imekuwa chanzo cha pato la mabilioni ya dola kwenye mabara mengine.

Tuanze sasa…

No comments: