May 8, 2012

Sajuki kwenda India leo


 Sadiki Juma Kilowoko (Sajuki) alivyo sasa

Sajuki wakati akiwa na afya njema

Msanii wa filamu nchini, Sadiki Juma Kilowoko (Sajuki) leo anasafirishwa kuelekea India kwa ajili ya matibabu baada ya kukamilika kwa asilimia kubwa ya michango iliyotolewa na wasanii na wadau mbalimbali wa tasnia ya filamu.

Msanii huyo ataongozana na watu wengine wawili katika safari yake hiyo. Zaidi ya Shilingi milioni 25 zilikuwa zikihitajika kwa ajili ya kumtibu msanii huyo ambapo pesa iliyopatikana ni milioni 16 pamoja na tiketi tatu za ndege. Hata hivyo michango mingine inazidi kuchangishwa na zitatumwa kwa ajili ya kuendelea na matibabu zaidi.

Akizungumza na wanahabari, Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania, Simon Mwakifamba alisema mbali na kushukuru kwa misaada iliyopatikana, alibainisha kuwa ugonjwa wa Sajuki umewafumbua macho na kuwafanya kama shirikisho kuwa na mikakati mipya ya
kuwasaidia wasanii wanachama wa shirikisho hilo.

Alisema kuwa kwa sasa shirikisho hilo limeingia makubaliano na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kuhakikisha kuwa wasanii wanajiunga na bima ya afya ambapo watakuwa wakichangia Sh 20,000 kila mwezi.

Alisema kuwa katika kuchangia fedha hizo wasanii pamoja na ndugu zao watatu watakuwa wakitibiwa ambapo aliwasihi wasanii kujitokeza kwa wingi kujiunga na shirikisho hilo.

“Najua wasanii wengi wanaishi maisha ya ujana na kushindwa kuangalia hatima ya uzee wao itakuwaje,” alisema.

Alisema, shirikisho limekubaliana na NSSF katika kuhakikisha kuwa wasanii wanaingia makubaliano ya mikopo ya nyumba. Sajuki anasumbuliwa na tatizo la uvimbe tumboni.

No comments: