Mar 30, 2016

Tunamisi burudani za majumba ya sinema

Watu wakiangalia sinema
LEO nimekumbuka mbali sana, hasa baada ya kupita sehemu na kuwasikia wanafunzi wa shule ya msingi (wenye miaka isiyozidi kumi), ambao wapenzi wa sinema, wakisimuliana na kubishana kuhusu kina Ray, Kanumba, Gabo nk. Ndipo nikakumbuka nilipokuwa katika umri huo tulikuwa pia tukisimuliana na kubishana kuhusu kina Amitabh Bachchan, Mithun Chakrabot, Amjad Khan, DharmendraSanjeev Kumar, Charlie Chaplin, nk.

Wakati huo hatukuwa na vituo vya televisheni kama leo. Vituo vya televisheni Tanzania Bara televisheni vimeanza mwanzoni mwa miaka ya 1990. Hadi 1996 kulikuwa na vituo vitatu tu vya CTN, DTV na ITV. Hata hivyo, televisheni imekuwapo Zanzibar tangu mwaka 1973.


Kipindi kile watu walikwenda kwenye majumba maalum ya sinema kuangalia sinema kwa wakati maalum na masharti maalum. Majumba haya yalikuwepo katika kila mji-makao makuu ya mkoa na baadaye katika wilaya, na idadi yake ilitegemea ukubwa wa mji.

Dar es Salaam kulikuwa na majumba kama Drive Inn (sasa kuna Ubalozi wa Marekani – hili lilikuwa ni eneo la watu matajiri zaidi, waliruhusiwa kuingia na magari yao kwenye ukumbi, watu wakikaa ndani ya magari na kuangalia filamu huku wakiburudika na vinywaji), Odeon (sasa kuna DTV/Channel Ten), New Chox (sasa kuna Continental Hotel), Empire (nadhani kuna makao makuu ya NMB), Avalon (lilianza kutumika na madhehebu ya kilokole kufanyia ibada zao, na sasa ni eneo la ofisi mbalimbali), Empress (zipo ofisi za BMT), na Cameo (sina uhakika linatumika kufanya nini kwa sasa).

Baadaye likaibuka jumba la Starlight (kuna hoteli ya Starlight), lililokuwa na uwezo wa kuingiza watu wengi sana. Na walalahoi pia walikuwa na mahali pa kwenda kutazama sinema, Amana Social Hall, eneo la Ilala.

Nakumbuka pale Drive Inn, ilikuwa kama huna pesa ya kuingilia, basi unaangalia sinema bubu – kwani mnalazimika kukaa nje na kutazama sinema kwa mbali lakini hamsikii sauti.

Tanga kulikuwa na Majestic, Novelty, Regal na Tanga Cinema. Mwanza kulikuwa na Liberty na Tivoli, Mji Kasoro Bahari kulikuwa na Shani na baadaye ikaja Sapna. Arusha ilikuwepo Metropolitan. Vivyo hivyo na miji mingine.

Enzi hizo (mimi nilikuwa kijana mdogo), kulikuwa na mabingwa wa kusimulia sinema hata kama mliiona wote, basi mtaanza kusimuliana tena na tena, hata kama kimombo hukijui, utasimulia yote waliyokuwa wanasema kwenye hiyo sinema. Wakati wa sinema yenyewe watu watapiga makelele, “angalia nyuma wewe… Jamaa anataka kukuua!” Au pale Drive Inn kwa nje, jamaa anakusimulia utadhani anasikia vile!

Ilikuwa raha mustarehe, enzi hizo tukiwa wadogo basi ikatokea kama kuna sinema maarufu mjini wenzako wanaweza kukusimulia mwanzo hadi mwisho bila kukosea (na kuongezea chumvi kidogo) ingawa hawajaiona ila wamesimuliwa. Ama kweli siku hazigandi!

Kwa sasa ukiwaona watu (hasa Dar es Salaam) wakiingia kuangalia sinema pale Century Cinemax–Mlimani City, Cineplex–Quality Centre, au Century Cinemax–Oysterbay, unaweza kudhani kuwa huu ni utamaduni mpya. Kumbe kabla na baada ya Uhuru kwenda Sinema ilikuwa ni jambo la kawaida na kitu kilichoweza kukuletea mapenzi na heshima kubwa kwa familia yako, rafiki au mpenzi wako, kwa wakati ule.

Hivi sasa katika ulimwengu huu wa utandawazi na soko huria, hasa baada ya ujio wa televisheni nchini, majumba ya sinema yamefungwa kutokana na kukosa wateja – sijui nani kasema mkiwa na televisheni nyumbani basi majumba ya sinema si muhimu? Badala yake majumba ya sinema yamehamia kwenye nyumba zetu na vichochoroni kulikochipuka mabanda ya kuonesha video kama uyoga ambayo siyo rasmi.

Kiukweli hii ni kumbukumbu nzuri na ya kuuzunisha, maana enzi hizo kweli ilikuwa jambo la tunu sana kwa mtoto au hata mtu mzima kupelekwa sinema. Kwanza halikuwa jambo rahisi kwa mtu tu asiye na ubavu kupata tiketi, hasa pale filamu ikiwa ni mpya na waigizaji wakiwa ni maarufu.

Nakumbuka walanguzi wa tiketi za sinema walikuwa wakimaliza kulangua pale New Chox Cinema, walikuwa wakikimbilia Avalon Cinema, halafu sasa tiketi zilikuwa zikiuzwa nusu, kisha zilizobakia wale Wahindi wakiwapa watu wao na kuziuza kwa bei ya juu.

Pale Empire nako wakimaliza kuuza, walikuwa wakienda Empress. Ila jumba ambalo vijana wengi wakilipenda ni jumba la Empire kwa sababu walikuwa wakionesha sinema nyingi za Hollywood, na waendeshaji walikuwa na tabia ya kuongeza sauti hasa wakati wa mapigano, ili kuwakoleza watazamaji.

Majumba ya Cameo na Odeon hasa yalikuwa maarufu kwa sinema za Kihindi, wakifuatiwa na New Chox Cinema na Avalon na Empress, halafu ndio Empire. Kule Drive Inn Cinema wakazi wa Msasani wengi walikuwa wakijazana nje ya ukuta na kutazama sinema japokuwa hawakuweza kusikia sauti lakini wengi wakiridhika na hiyo hali. Ilikuwa mnakaa nje ya ukuta na kununua karanga na juice, mnatafuta tofali na box chakavu kisha mnakaa kuangalia movie!

Vijana leo wanaweza kushangaa wakisikia kuwa hata Wimbo wa Taifa ulikuwa ukipigwa kabla ya onesho, ila baadaye sana ikaja kuondolewa kwa sababu ilisemekana kuwa hakukuwa na heshima, sababu wengine walikuwa ni walevi na hawakuwa wakisimama wima pale Wimbo wa Taifa unapopigwa.

Hii biashara ya majumba ya sinema ilianza kudorora vilipoanza vituo vya TV na kushamili kwa biashara ya video na maktaba za kukodisha video. Wengi walikuja kupendelea kukodisha kanda za video kuliko kwenda kwenye majumba ya sinema kwa sababu kwanza ilikuwa ghali kwa mtu mwenye familia, kugharamia watu zaidi ya wanne, pili filamu zenyewe nyingi zilikuwa baadaye zikirudiwa rudiwa.

Enzi za hayo majumba kwenda kuangalia filamu kama Dracula, ilikuwa ishu, wengi walikuwa wakitishika kuiangalia hiyo filamu, lakini siku hizi kutokana na utaalam na watu kuzoea kuangalia sinema zenye ‘special effect’ nyingi, imeifanya sinema kama Dracula isitishe tena. Yaani kwa kizazi cha ‘dot.com’, hii sinema si lolote si chochote, ndo kwanza inaboa tu.

Hata kwa wale waliokuwa hawana uwezo wa kwenda kwenye majumba ya sinema, bado waliinjoi kusikiliza michezo na vichekesho vya redioni kama Mahoka, na vichekesho vya Pwagu na Pwaguzi vikirushwa na Redio Tanzania, hakuna shaka kuwa hawa jamaa walikuwa vinara wa vichekesho kwa jinsi walivyoweza kupangilia vituko vyao japo tulisikia sauti tu bila kuwaona.

Hizo zilikuwa siku, ukijua leo kuna mchezo wa redio saa tatu na nusu usiku basi hubanduki redioni uwasikie kina marehemu Kipara, Rajab Hatia, Hamisi Tajiri, Zena Dilip, Ally Keto nk.

Na kwa waliokwenda kwenye kumbi mbalimbali hasa hapa Dar es Salaam na miji mikubwa walikutana na vikundi vya sanaa kama Kibisa, Muungano, Mandela, Bima, vikundi vya Jeshi nk. kwa kweli hawakukosa kufurahia vichekesho vya kina King Majuto, Branco Minyugu, Bartholomew Milulu na wengineo.


Dah… kweli siku hazigandi!

No comments: