Mar 2, 2016

LEONARDO DICAPRIO: Avumilia miaka 6 kushinda Tuzo ya Oscar


TUZO za Oscar (The Academy Awards), huwakilishwa kila mwaka na kampuni ya Academy of Motion Picture Arts and Sciences (Kifupi: AMPAS) kwa lengo la kutambulisha taaluma ya tasnia ya filamu, wakiwemo waongozaji, waigizaji, na watunzi wa filamu. Rasmi huwa sherehe za utoaji wa tuzo mbalimbali. Pia inasemekana kuwa ni miongoni mwa sherehe zinazotazamwa sana duniani mara tu sherehe hizo zinapoanza.

Katika Tuzo za mwaka huu mwigizaji nyota wa Hollywood, Leonardo DiCaprio, hatimaye amejishindia tuzo yake ya kwanza ya Oscar kwa uigizaji wake katika filamu ya ‘The Revenant’, baada ya kushindania tuzo hizo mara sita. Amekuwa mwigizaji bora kwenye Tuzo za 88 za Oscar.


Leonardo DiCaprio ni muigizaji wa Marekani ambaye alianza fani ya uigizaji akiwa mdogo kwenye televisheni. Mwaka 1989 alionekana kwenye kipindi cha ‘Lassie New’ na 1990 kwenye ‘Santa Barbara’ na pia mwaka huohuo aliigiza katika michezo ya vichekesho ya ‘Parenthood’ naGrowing Pains’ mwaka 1991, kabla ya kufanya filamu yake ya kwanza mwaka 1991, ya ‘Critters 3’.

Miaka miwili baadaye 1993, alicheza katika ‘This Boy’s Life’. Baadaye mwaka huohuo akacheza kama muigizaji msaidizi katika filamu ya ‘What’s Eating Gilbert Grape’, ambayo ilimwezesha kuteuliwa katika Tuzo ya Academy kama Muigizaji Bora Msaidizi. Mwaka 1995, DiCaprio alicheza kama mwandishi wa Marekani, Jim Carroll, katika filamu ya ‘The Basket Diaries’ na Mshairi wa Kifaransa, Arthur Rimbaud katikaTotal Eclipse’.

Mwaka uliofuata 1996 alicheza kama Romeo Montague katika filamu ya Romeo & Juliet ya Baz Luhrmann. Mwaka 1997 DiCaprio aliigiza pamoja na Kate Winslet katika filamu ya James Cameron ya Titanic. Filamu iliyokuwa na mapato ya juu sana duniani kote kwa mauzo ya teketi, na kumpa umaarufu mkubwa duniani.

Titanic ni filamu ya kusikitisha na ya mapenzi inayohusu kuzama kwa meli ya Titanic. Filamu hii iliongozwa, ikaandikwa, ikatayarishwa na kuhaririwa na James Cameron mnamo 1997. Wahusika wake ni Leonardo DiCaprio kama Jack Dawson na Kate Winslet kama Rose DeWitt Bukater. Wawili hawa wenye maisha tofauti walipendana walipokutana kwenye meli hii ambayo haikuwa na mwisho mwema.

Filamu hii ambayo ilikuwa itolewe mnamo 2 Julai 1997 lakini tarehe ikapelekwa mbele hadi 19 Desemba 1997. Ilipata mafanikio makubwa, kwa kushinda tuzo kumi na moja za Academy Awards. Pia alicheza sinema ya ‘Man in the Iron Mask’ mwaka 1998.

Kwa uigizaji wake, alipata Tuzo ya Muigizaji Bora wa Kiume wa MTV na uteuzi wake wa kwanza kwa Tuzo ya Golden Globe kama Muigizaji Bora - Motion Picture Drama.

Mwaka 2002, DiCaprio alicheza kama tapeli (con-artist) Frank Abagnale Jr. mpinzani wa Tom Hanks katika sinema iliyoongozwa na Steven Spielberg ya kihalifu inayoitwa ‘Catch Me If You Can’ na pia kuwa nyota katika sinema iliyoongozwa na Martin Scorsese ya ‘Gang of New York’. 

Alianzisha kampuni yake mwenyewe ya uzalishaji, Appian Way, mwaka 2004. Filamu mbili zilizofuata aliigiza kama nyota ambapo zote mbili ziliongozwa na Scorsese:Howard Hughes biopic The Aviator’ (2004) na ya kihalifu ‘The Departed’ (2006). Kwa uigizaji wake, DiCaprio alishinda tuzo ya Golden Globe kwa Muigizaji Bora – ‘Motion Picture Drama’ na kufanikiwa kuteuliwa kwa mara ya kwanza kwa ajili ya Tuzo ya Academy kama Muigizaji Bora. Na sinema ya kutisha ya vita vya kisiasa ya Blood Diamond mwaka 2006.

DiCaprio alitoa filamu ya makala (documentary) ya mazingira ‘The 11th Hour’ na ya vichekesho ya ‘Gardener of Eden’ mwaka 2007. Mwaka uliofuata, aliungana tena na Kate Winslet katika sinema ya ‘Revolutionary Road’ iliyoongozwa na Sam Mendes, na akaonekana katika sinema ya ‘Body of Lies’ iliyoongozwa na Ridley Scott. DiCaprio aliungana tena na Scorsese mwaka 2010 katika sinema ya kutisha ya kisaikolojia ya Shutter Island na pia akacheza kama nyota katika sinema iliyoongozwa na Christopher Nolan ya ‘Inception’.

Mwaka 2011, alimuigiza J. Edgar Hoover, mkurugenzi wa kwanza wa FBI. Mwaka uliofuata, alicheza muigizaji msaidizi katika sinema iliyoongozwa na Quentin Tarantino, ‘Django Unchained’. DiCaprio aliigiza katika filamu mbili zilizotokana na riwaya mwaka 2013; kwanza alionekana kama Jay Gatsby katika sinema iliyoongozwa na Luhrmann iliyotokana na riwaya ya F. Scott Fitzgerald ya ‘Great Gatsby’, na baadaye kama Jordan Belfort katika sinema ya ‘Wolf ya Wall Street’, iliyotokana na riwaya ya Belfort yenye jina kama hilo. Mwisho ilimwezesha kuteuliwa kwa mara ya tatu kuwania Tuzo za Academy kama Muigizaji Bora na Tuzo za Golden Globe kama Muigizaji Bora – ‘Motion Picture Musical or Comedy’

Jina lake kamili ni Leonardo Wilhelm DiCaprio, amezaliwa mnamo 11 Novemba 1974 katika eneo la Hollywood, California, ni mtoto pekee wa Irmelin (nee Indenbirken), mzaliwa wa Ujerumani ambaye ni katibu wa sheria, na George DiCaprio, msanii wa uchoraji (comic artist) na mtayarishaji na msambazaji wa vitabu vya Comic (hadithi za michoro). Baba yake DiCaprio ana asili ya kutoka ukoo wa Kitaliano (kutoka eneo la Naples) na Kijerumani (kutoka Bavaria).

Wazazi wa DiCaprio walikutana wakati wakisoma chuo na hatimaye wakahamia Los Angeles. Yeye aliitwa jina lake Leonardo kwa sababu mama yake alipokuwa mjamzito alikuwa akiuangalia sana mchoro wa Leonardo da Vinci katika makumbusho nchini Italia wakati DiCaprio aliporukaruka tumboni. Wazazi wake walitalikiana wakati DiCaprio alipokuwa na mwaka mmoja, na baadaye aliishi zaidi na mama yake. Waliishi katika vitongoji vya Los Angeles, kama vile Echo Park, na 1874 Hillhurst Avenue, wilaya ya Los Feliz (eneo ambalo baadaye lilibadilika kuwa maktaba za umma), wakati huo mama yake akifanya kazi kadhaa kwa ajili ya kujikimu yeye na mwanaye.

DiCaprio alisoma katika Shule ya Seeds Elementary (kwa sasa UCLA Lab School) na masomo ya sekondari katika shule ya John Marshall high School, mita chache tu, baada ya masomo Los Angeles Centre for Enriched Studies kwa miaka minne. Hata hivyo, aliacha shule akiwa shule ya sekondari katika mwaka wake wa tatu, hatimaye akapata stashahada. DiCaprio aliishi sehemu ya maisha yake ya utoto nchini Ujerumani kwa bibi na babu wa upande wa mama yake, Wilhelm na Helene. 


DiCaprio anaongea kidogo Kijerumani na Kitaliano.

No comments: